Joseph Mihangwa
Joseph Mihangwa
Joseph Mihangwa
|
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiteta jambo na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa. |
Na Joseph Mihangwa.
KATIKA sehemu ya kwanza ya makala
haya wiki iliyopita, tuliona namna kampuni tata ya Meremeta “ilivyoingia”
nchini kwa ubunifu wa vigogo wa serikali na Benki Kuu na hatimaye kuchota
kijanja mabilioni ya fedha na “kutoweka” kwa “kusindikizwa” na vigogo hao hao
wa serikali.
Utata huo, kama tu ulivyokuwa utata wa kampuni ya Richmond iliyochota mabilioni
ya fedha kwa mfumo unaofanana, ulitokana na madai ya kampuni hiyo kusajiliwa
nchini Uingereza na madai mengine ya kusajiliwa nchini mwetu na kwa kisingizio
cha kufanya kazi kwa mwavuli wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na hivyo
kujengewa mazingira ya kuhitaji usiri wa kiusalama ili isiguswe kwa utapeli huo
na hujuma kwa nchi.
Baada ya kukomba dhahabu yote huko Buhemba na Buhemba Kusini, Nyamongo na
Magunga, mwaka 2006, Meremeta ilitangazwa kuwa ilikuwa inafanya kazi kwa hasara
na ikaundwa tume ya serikali ya watu watano, kuchunguza matatizo ya kampuni
hiyo.
Wazito na waheshimiwa waliokuwa katika Tume hiyo, ni Daudi Balali – Gavana wa
BoT na Mwenyekiti wa Tume; Gray Mgonja, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,
na Patrick Rutabanzibwa, wakati huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.
Wengine walikuwa ni Mabwana Vincent Mrisho, Katibu Mkuu, Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa; Andrew Chenge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Bwana
Michael G. Garner, kama mshauri huru wa tume, ambaye alikuwa pia ndiye Mshauri
wa Benki ya Nedbank, yenye uhusiano na kampuni ya Nedcor Trade Service,
iliyochota bilioni 155/- kutoka Benki Kuu katika mazingira ya kutatanisha.
Tume hiyo ilipendekeza kusitishwa kwa shughuli za kampuni ya Meremeta za
kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, jukumu ambalo tayari
ilikwishalitelekeza tangu mwaka 2003, na kujiingiza katika uchimbaji na umiliki
wa migodi.
Tume ilipendekeza pia kuanzishwa kwa kampuni mpya yenye jukumu la kusimamia na
kuendesha Mgodi wa Buhemba yenye kumilikiwa na serikali kwa asilimia 100. Kwa
lugha nyingine ni kwamba, baada ya kung’atuka kwa Meremeta, serikali iliamua
kusimamia yenyewe mradi huo wa dhahabu kupitia chombo au taasisi teule.
Na kwa uzito wa mapendekezo ya tume hiyo ya Balali, Meremeta ilifilisiwa,
ambapo mali na madeni yake yalichukuliwa na kampuni mpya ya “Tangold,”
inayodaiwa kumilikiwa na serikali kwa asilimia 100. Na ingawa Meremeta
([halisi) ilifungwa rasmi mwaka 2006 nchini Uingereza, shughuli zake hazikukoma
nchini Tanzania wakati huo, kama tutakavyoona baadaye katika makala haya.
Hapa kuna utata mwingine, kwamba kumbukumbu zinaonesha kuwa kampuni ya Tangold
ilianzishwa katika Visiwa vya Mauritius, Aprili 4, 2005; na kupewa Leseni ya
Biashara Aprili 8, 2005 kama kampuni binafsi. Lakini kumbukumbu zingine
zinaonesha kuwa, Tangold ilifungua Akaunti ya Benki Namba 011103024852, Tawi la
Corporate Drive la NBC, Dar es Salaam, Januari 1, 2003; kabla hata Tume ya Balali
na wenzake haijaundwa kutatua tatizo la Meremeta.
Taarifa zingine zimeonesha zaidi kuwa kampuni hiyo ni ya kigeni iliyosajiliwa
nchini Mauritius na kupewa leseni nchini Tanzania, Februari 20, 2005 kama Tawi
la Kampuni ya kigeni; na ilianza kupatiwa fedha na BoT Agosti 1, 2005 kwa kazi
isiyojulikana.
Je, ina maana kwamba Tangold ilikuwapo nchini Tanzania kabla ya kuanzishwa
nchini Mauritius mwaka 2005, au ni aina fulani tu ya usanii? Hata kama
ilikuwapo, iliwezaje kufungua akaunti benki, Januari 1, 2003 ambayo ilikuwa
Sikukuu ya Kitaifa ya Mwaka mpya?
Kama ilikuwapo, kwa nini tume ilipendekeza kuundwa kwa kampuni ambayo tayari
ilikuwapo? Nini tofauti kati ya Tangold iliyofungua akaunti Januari 2003, na
Tangold iliyosajiliwa Mauritius April 4, 2005 kurithi Meremeta?
Ingawa mapendekezo ya tume na tamko la serikali yalikuwa kwamba kampuni hiyo
mpya (Tangold) imilikiwe kwa asilimia 100 na serikali, utekelezaji wake ulikuwa
ni kinyume chake; ambapo inaelekea wajumbe wa tume iliyoundwa kuchunguza
matatizo ya Meremeta, ndio waliogeuzwa kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo mpya.
Hao wanatajwa (kwa baadhi majina yao kuongezwa herufi moja ya katikati), kuwa
ni Daudi Balali, Gray S. Mgonja, Andrew Chenge, Patrick J. W. Rutabanzibwa na
Vicent F. Mrisho.
Inawezekana, kwa mtazamo wa enzi hizo na kwa kusudi hilo, kwamba hao watano
ndio walikuwa serikali yenyewe; lakini kifungu cha saba (7) cha Katiba ya
Kampuni ya Tangold kinatibua dhana yote hiyo, kinaposema, “Wenye hisa ya
kampuni wanaweza kurithisha hisa zao kwa ndugu zao”.
Je, ni kweli Tangold ilikuwa inamilikiwa na serikali kwa asilimia 100 kama
ilivyopendekeza Tume ya Balali na pia kwa mujibu wa tamko la serikali? Ni ndugu
wapi hao wa serikali (kama kweli serikali ina ndugu!) waliostahili kurithishwa
hisa za serikali?.
Haya ni maswali magumu, na tunashawishika kuamini kwamba, Tangold haikumilikiwa
na serikali kwa asilimia 100 kama tulivyoambiwa bali ilikuwa kampuni binafsi
iliyorithishwa mali za Kampuni ya Meremeta.
Wakati matatizo ya Meremeta yakiendelea na wakati huohuo tayari mapendekezo ya
Tume ya Balali ya watu watano yakiwa yameanza kufanyiwa kazi, Machi 18, 2004,
iliundwa kampuni nyingine iitwayo “Deep Green Finance” (DGF) ambayo madhumuni
na shughuli zake hazijafahamika vizuri mpaka sasa.
Wakurugenzi wa DGF walikuwa ni Mark Ross Weston wa New Zealand; Antón Taljaard
wa Afrika Kusini, na Rudolf Van Schalkwyk, pia wa Afrika Kusini.
Wanahisa wa DGF walitajwa kuwa ni Protase R. G. Ishengoma, Stella Ndikimi wa
Kampuni ya uwakili ya IMMA, ya jijini Dar es Salaam; Benki ya Nedbank Africa
Investment Ltd ya Afrika Kusini (ambayo Mshauri wake, Bwana Michael G. Garner,
ndiye pia aliyekuwa mshauri huru wa Tume ya watu watano, iliyochunguza matatizo
ya Meremeta na kupendekeza kuundwa kwa Tangold), na kampuni ya SBM Nedcor
Holdings, ambayo haijafahamika bado, kama ina uhusiano wowote na kampuni ya
Nedcor Trade Service, iliyolipwa na BoT malipo tata ya zaidi ya Sh. 155bn/= kwa
niaba ya Meremeta.
Wakurugenzi hao watatu wa Deep Green Finance, pia ndio waliokuwa maafisa wa
NedBank; na jina la Deep Green limetumiwa mara nyingi na NedBank katika miradi
yake ya kijamii.
Haifahamiki pia ni kwa vipi na kwa njia ipi, Watanzania pekee wawili, Protase
Ishengoma na Stella Ndikimi, walitembelewa na ngekewa ya kununua hisa za
kampuni yenye kumilikiwa na wageni kama hii (DGF); na kama ni kweli
inavyodaiwa, kwamba hatimaye walichukua hisa (kwa njia ya kuhamishia au
kununua) katika Nedbank Ltd na Nedbank Africa Investments, Aprili 15, 2004.
Kama ilivyokuwa kwa kampuni ya Tangold, iliyofungua akaunti siku ya sikukuu ya
mwaka mpya; ndivyo ilivyokuwa pia kwa kampuni ya Deep Green Finance,
iliyofungua akaunti Benki ya NBC, Na. 011103024840, Tawi hilo hilo la Corporate
Drive; safari hii ilikuwa sikukuu (ya mapunziko) ya Mei Mosi, 2004.
Kuna utata kuhusu utoaji wa namba za akaunti za benki hiyo, kwamba akaunti ya
Tangold, Namba 011103024852, iliyofunguliwa Januari 1, 2003, ni kubwa (kwa
akaunti 12 zaidi), ikilinganishwa na akaunti Namba 01110302840 ya Deep Green
Finance, iliyofunguliwa zaidi ya mwaka mmoja baadaye, Mei 1, 2004.
Je, ni utaratibu wa NBC kutoa namba za akaunti kuanzia na namba za juu, kushuka
chini? Kama sivyo, basi kuna uwalakini unaotufanya tuamini kwamba kulikuwa na
mchezo mchafu, ikizingatiwa pia kwamba akaunti zote mbili zilifunguliwa siku za
mapumziko ya Sikukuu za Kitaifa.
Toka Mei 1, 2004 akaunti ya Tangold ilipofunguliwa, hadi Julai 31, 2005 (zaidi
ya mwaka mmoja), hapakuwa na shughuli za DGF zilizoingiza fedha katika akaunti
hiyo, hadi Agosti 1, 2005 ilipoanza kupokea mabilioni ya fedha kutoka ama benki
Kuu, Deep Green Finance au Tangold, kwenda ama Deep Green Finance, Tangold,
Meremeta, IMMA Advocates au kusikojulikana.
Wakati tunaelezwa kwamba Tangold ilianzishwa April 5, 2005 na kupewa leseni ya
biashara April 8, 2005 kuchukua nafasi ya Meremeta, na mali na madeni ya
Meremeta kuhamishiwa au kuchukuliwa na kampuni mpya, kwa maana kwamba Meremeta
ilikuwa imefilisiwa na kufungwa.
Lakini kumbukumbu zinaonesha kwamba, Oktoba 12, 2005, jumla ya Shs.
1,690,500,000 zilihamishwa kutoka Tangold kwenda kampuni (mfu?) ya Meremeta; na
vivyo hivyo Novemba 23, (Tshs. 555,300,048/=) na Desemba 12 kiasi cha Shs.
551,060,000. Iliwezekanaje Meremeta kulipwa fedha hizo wakati
ilikwishafilisiwa? Nani aliifufua?
Kwa kifupi, kati ya Agosti 1, 2005 na Desemba 21, 2006, jumla ya Sh. 32bn/=
zilihamishwa kutoka Benki Kuu kwenda Deep Green Finance na Tangold; mbali na
zile zilizopelekwa kusikojulikana.
Tunashawishika kuamini kwamba Deep Green Finance iliundwa kurahisisha na
kuhakikisha utoroshaji wa fedha za Meremeta na Tangold kwenda nje ya nchi na si
kwa sababu nyingine yoyote ile.
Baada ya purukushani hizo, na kuonekana kwamba mradi wa Tangold hauwezi
kuendelea, serikali iliuza haki za mgodi huo kwa kampuni ya “Rand Gold” ya
Afrika Kusini, kwa bei ya chini ya soko, na kusababisha hasara ya dola za
Kimarekani milioni 100; na pia kulipa dola miliono 132 pamoja na adhabu na
riba, kutokana na Serikali (BOT) kudhamini wakopaji/wawekezaji waliofilisika na
kutupa mzigo kwa serikali kuyalipa.
Purukushani hii, toka kuundwa kwa kampuni ya Meremeta, hadi kuundwa na
kufilisika kwa kampuni ya Tangold, licha ya kuruhusu uporaji mkubwa wa
mabilioni ya fedha na rasilimali zetu, ilisababisha pia hasara ya jumla ya dola
za Kimarekani milioni 232, sawa na Shs. 232bn/= wakati huo, kwa njia ya
kifisadi.
Serikali ya Awamu ya Tatu, ya Rais Mkapa ilifanya malipo hayo Oktoba 2005,
mwezi mmoja tu kabla ya kumaliza muda wake wa kuwa madarakani.
Na ndivyo hivyo awamu hiyo ya tatu ilivyolipa pia kwa malipo tata ya kashfa ya
EPA, 133bn/= mwishoni mwa Oktoba 2010. Na vivyo hivyo Serikali ya awamu ya nne
ilivyolipa malipo tata ya 326bn/= kutoka akaunti ua “Tegeta Escrow” kwa kuporwa
na Kampuni ya PAP, miezi kadhaa kabla ya kumaliza kipindi chake.
Utamaduni huu wa kupora dakika za mwisho kwa watawala utadumu hadi lini?.