Thursday, 5 May 2016

Nyerere na “ujechaji” wa haki za umma


Mwalimu Julius K Nyerere.

Na Ahmed Rajab
“UKWELI ni kama kalio (tako), kila mtu anaukalia wake.”
Kama sikosei maneno hayo yaliwahi kutamkwa na Lech Walesa, kiongozi wa zamani wa wafanyakazi wa Poland aliyewahi kuwa Rais wa nchi yake (1990-1995) na ambaye siku hizi amestaafu.

Sasa nimekumbuka.
Nina hakika matamshi hayo yalikuwa yake Walesa.Nilikutana nayo nilipokuwa nikimsoma mwandishi aliye mwananchi mwenzake aitwaye Mariusz Szczygieł.

Kauli hiyo kuhusu ukweli inaweza ikawa na ufafanuzi mrefu na maelezo mapana na ya kina. Hata hivyo, naamini unaweza ukayakunja maelezo ya kauli hiyo.

Muhtasari wa maelezo ya kauli hiyo utakuwa kwamba kila mtu anauona ukweli kwa jinsi macho yake yaonavyo, kwa mtazamo wake.

Hayo yanaweza yakawa kweli kwa mambo fulani lakini sidhani, kwa mfano, kama unaweza usiku ukauita mchana au mchana ukauita usiku.

Huwezi ukionyeshwa paka ukasema kuwa huyo ni bata. Ukisema hivyo kwa kuamini basi wanaokusikiliza watasema kwamba labda umepungukiwa na sukurubu mbili tatu kichwani mwako.

Wala sidhani kama unaweza haramu ukaiita halali au halali ukaiita haramu.
Tukifuata mantiki ile kadhia ya Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ya kuufuta uchaguzi mkuu uliofanywa Zanzibar Oktoba 2015, na yaliyofuatia baadaye, haiwezi kuelezewa vingine isipokuwa kwamba kilikuwa kitendo cha ubakwaji wa demokrasia.

Kilikuwa kitendo kilichowapokonya wananchi haki yao na uhuru wao wa kumchagua wamtakaye. Hicho kikiwa ni kigezo muhimu katika mfumo wa demokrasia.

Hoja zote zimekwishatolewa kuwafahamisha watawala wabakaji wa demokrasia kwamba walichofanya ni dhuluma. Ni wizi kwa hivyo ni kosa la jinai.Ni kwenda kinyume na utu kwa hivyo si kitendo cha kiungwana.
Ni ushenzi.
Ni uhuni.

Ni ubabe wa kisiasa ambao unatumiwa kwa faida ya wachache katika jamii wenye lengo la kudumisha utawala wao.

Yote yanayopaswa kusemwa yamekwishasemwa kuhusu uharamia huo wa kisiasa. Watawala wameaswa na walio ndani ya nchi pamoja na walio nje ya nchi lakini bado hawataki kusikia. Wakiambiwa kweli wanakuwa kama waliolishwa shubiri; hutema papo hapo.

Juu ya yote yaliyotokea kuna funzo tulilolipata. Kadhia hiyo imedhihirisha namna ambavyo serikali ya dola iliyo dhaifu na inayokandamiza inavyoukaba, tena kwa urahisi, uhuru wa kisiasa wa wananchi na hivyo kuzidi kuwakandamiza.

Jengine lililojitokeza ni jinsi serikali ya aina hiyo inavyounda taasisi zenye dosari ambazo hufanywa makusudi ziwe na dosari ili ziweze kuyakidhi matakwa ya watawala wasio na nia ya kuyaacha madaraka.

Miongoni mwa taasisi hizo ni tume ya uchaguzi, uteuzi wake na muundo wake pamoja na mahakama na vyombo vya kulinda amani kama jeshi la polisi.

Serikali hizo huwa na uwezo wa kufanya hivyo zinapoachiwa kujifanyia zitakavyo bila ya kuwajibishwa au hata kuwekewa mipaka.

Hasara wanayoipata wananchi huwa haisemeki.Wanapokuwa wanapokonywa haki zao wanakuwa pia wanaporwa fursa ya kutamani. Hii nahisi ni hasara kubwa.

Ni dhara kwa sababu wananchi walio katika upinzani wasipokuwa makini na wakikosa viongozi madhubuti wanaweza wakavunjika moyo.

Wanaweza wakaacha kuwa na matumaini kwamba hali zao zinaweza kubadilika kwa kupatikana mageuzi ya utawala.

Mpaka sasa haionyeshi kwamba wapinzani wa Zanzibar wamefikia hali hiyo.
Kweli tangu uchaguzi wa Oktoba mwaka jana ubatilishwe wamekuwa wakiishi chini ya wingu la huzuni la kupokonywa ushindi wao lakini inatia moyo kuwaona bado wakiwa na matumaini.
Inavyoonyesha ni kwamba wanaamini ya kuwa giza la usiku halidumu milele.

Lililo muhimu hapa ni kwamba bado wana imani na viongozi wao na hawakujiingiza katika vitendo vya uvunjaji sheria na vya kuchafua amani licha ya kuchokozwa na mahasimu zao wa kisiasa.

Moja ya maswali yanayoulizwa na baadhi ya wenye kuzifuatilia siasa za michuano ya kisiasa visiwani Zanzibar ni iwapo yaliyozuka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana yalikuwa mambo ya kutarajiwa.

Kufutwa kwa uchaguzi mzima ulikuwa ni mpango wa kusudi uliokuwa umepangwa tangu awali au ulikuwa ni matokeo ya ajali ya kisiasa baada viongozi wa CCM kutanabahi kwamba ushindi haukuelekea kuwa wao?

Ushahidi uliopo unaonyesha kwamba ubakwaji wa demokrasia visiwani Zanzibar ni mkakati uliopangwa muda mrefu na viongozi wa chama kinachotawala.

Itakumbukwa kwamba wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu wa 2000 aliyekuwa siku hizo Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Salmin Amour, alisema kadamnasi kwamba “ushindi lazima uwe wa CCM.”

Kujitakia ushindi si dhambi.
Lakini kilichoashiria shari ni pale Salmini alipoongeza kusema kwamba wakati wa upigaji kura yeye atakuwa nyumbani “lakini mambo yakizidi nitaingia uwanjani. Nasema waziwazi kama mambo hayaendi vizuri tunataka kushindwa basi nitaingia uwanjani bila ya hodi, tena khiyari yenu. Mkinikamata, mkinifunga lakini uhuru wangu uko hatarini.

Kwa hilo sina subira wala sina sumile…”
Kauli hiyo aliitoa Salmini mwaka mmoja baada ya kufariki dunia Mwalimu Julius Nyerere, muasisi mkuu wa CCM na mwenyekiti wake wa mwanzo (1977 hadi 1985).

Nyerere alikuwa na uzoefu wa mifumo tofauti ya kisiasa. Alipozivaa kwanza siasa nchini Tanganyika hapakuwako vyama vya siasa, halafu palikuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa, mfumo ulioendelea kwa muda baada ya nchi hiyo kupata uhuru 1961.

Baadaye Nyerere aliupiga marufuku mfumo huo na akakihalalisha chama kimoja tu, Tanganyika African National Union (TANU).

Tanganyika ilipoungana na Zanzibar 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila mojawapo ya nchi hizo mbili ilikuwa na chama chake kimoja tu kilichokuwa halali.

TANU kilikuwa kwa upande wa Tanganyika na Afro-Shirazi Party (ASP) ndiyo iliyokuwa ikitawala Zanzibar.

Hali hiyo iliendelea hadi 1977 vyama hivyo viwili vilipoungana na kukizaa CCM.
Chama hicho siyo tu kwamba kina uzito mkubwa Tanzania lakini pia ni chama kilicho kwenye madaraka kwa muda mrefu kushinda chama kingine chochote cha siasa barani Afrika.

Tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urejeshwe Tanzania 1992 chama cha CCM kilizidi kujizatiti na kuandaa mikakati ya kuhakikisha ya kuwa madaraka hayakiponyoki. Kimeshinda chaguzi zote tano zilizofanywa kitaifa 1995, 2000, 2005, 2010 na wa 2015.

Juu ya hayo kumekuwako na shutuma kwamba CCM hakikuweza kupata ushindi wa halali visiwani Zanzibar na kwamba, kwa ufupi, ushindi wake huko daima umekuwa wa “kulazimishwa”.

Hata ushindi wake huko Bara nao pia umetiwa walakini katika uchaguzi wa mwaka jana.
Jambo moja lisilo na ubishi ni kwamba CCM ni chama chenye uwezo mkubwa wa kung’ang’ania madaraka.Kina magunia chungu mbovu yaliyojaa mbinu za kutumiwa ili kiweze kuendelea kutawala.

Baadhi ya mbinu hizo ni za halali na nyingine ni za haramu. Sitoshangaa ikiwa hizo za haramu ndizo nyingi.

Mbinu hizo zitakuwa zinakwenda sambamba na mfumo mzima wa utawala nchini.
Swali jengine la kujiuliza ni nini ungekuwa msimamo wa Nyerere kuhusu ubakwaji wa demokrasia Zanzibar? Angeliungama na wahuni wa kisiasa wa chama chake na kuhalalisha kilicho haramu?

Nadhani kwa hili angeliwaacha mkono. Kwa namna mambo yalivyokuwa yanakwenda ndani ya CCM katika siku za mwisho za uhai wake alikwishabaini kwamba hapakuwa na ugumu wa CCM kushindwa.

Yeye mwenyewe alikwishatamka kwamba angeweza kukiacha mkono chama hicho kwa kuwa kilikwishaanza kuoza.

Nyerere amewahi kufanya makosa mengi lakini kuhusu suala hilio ninaamini kwamba asingelikubali kuruhusu jina lake lichafuliwe kwa kuhusishwa na uamuzi ambao nina hakika angeliuelezea kuwa wa kijinga.

Nimewahi kusoma hivi karibuni jinsi jamaa fulani huko Afrika ya Kusini walivyoligeuza jina “Zuma” na kulifanya liwe kitenzi.

Wamefanya hivyo kwa sababu jina la Jacob Zuma, Rais wa Afrika ya Kusini, linanuka katika duru nyingi nchini humo kwa vile linahusishwa na shutuma za ufisadi wa aina kwa aina, toka wa kiuchumi (ulaji rushwa) na wa kisiasa (matumizi mabaya ya madaraka ya urais) pamoja na kashfa nyingine ambazo kheri tuzifunikie kombo.

Kwa hivyo, ni dhambi “kumzuma” mwenzako.
Unaweza kufikiri kuwa dhihaka kama hizi za kugeuza majina ya wakubwa na kuyafanya vitenzi ni mizaha ya kustawisha soga barazani au kwenye vijiwe lakini kwa kweli mizaha ya aina hiyo husambaza ujumbe mzito katika jamii. Huwa ni dhihaka zenye falsafa kubwa.

Sema sijui katika uonevu uliopita Zanzibar wakati wa uchaguzi wa Oktoba 2015 ni yupi mwenye kustahiki kupewa “hishma” kama hiyo ya jina lake kugeuzwa na kuwa kitenzi. Katika muktadha huo wa kudhulumu tuligeuze jina la Jecha Salim Jecha, aliyetumiwa kutekeleza dhulma hiyo?
Au tuligeuze jina la aliyemtuma, Dk. Ali Mohamed Shein?

Ikiwa Sule amemdhulumu Athumani tuseme Sule “amemjecha” Athumani au Sule “amemshein” Athumani?

Au vitenzi vyote hivyo viwili (“kujecha” na “kushein”) vinaweza kutumiwa kuwa na maana hiyohiyo moja ya kudhulumu au kuonea au kupokonya haki za watu, kutegemea na andasa za mtumizi wa kitenzi kinachohusika.

No comments:

Post a Comment