Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika Mwalimu Julius K Nyerere na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Abeid Aman Karume wakisaini hati za makubaliano ya Muungano wa Tanzania. |
Na Ally Mohammed.
APRILI 26, mwaka huu 2016, Tanzania
imetimiza miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ni hatua kubwa na ni jambo la kupendeza kuona tunasherehekea kitu
kilichotufanya tukawa wamoja.
Pamoja na umoja wetu huu tunaojivunia sasa, ni jambo la kawaida kuona minyukano, vituko na mabishano kila inapokaribia uchaguzi na hata baada ya uchaguzi hapa Zanzibar.
Ule msemo wa kuna maisha baada ya uchaguzi kwa Zanzibar nimeushuhudia siku za mwisho wakati wa uongozi wa Rais Amani Abeid Karume na mwanzoni tu mwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoshirikisha vyama vya CCM na CUF.
Huu mnyukano wa CCM na CUF na tangu zama za ZNP, ZPPP na ASP nini hasa kilichopo ni Zanzibar kujiogopa au kuogopwa?
Mandhari nzuri na fukwe, pia upepo wa marashi ya karafuu sicho haswa kinapelekea kutokuwa na muelekeo wa kustawi kwa demokrasia katika visiwa hivi kwani kila mmoja kwa uwezo wake anayo fursa ya kutembelea fukwe kuanzia Kizimkazi mpaka Nungwi bila ya bughudha yeyote ile. Na hii inanasibishwa na msemo adhimu wa “Zanzibar ni njema atakae na aje”.
Kwenye siku za kuelekea Mapinduzi ya Januari 12, 1964, kulikuwa na tetesi kuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na Kassim Hanga, kuwa na mpango wa kuangusha Serikali ya Zanzibar.
Lakini, Rais wa Tanganyika wakati huo, Julius Nyerere pamoja na Nchi za Magharibi walikuwa na hofu kwamba Zanzibar ingefanikisha mapinduzi hayo ingeweza kuwa “Cuba ya Afrika” na kwa vile ipo karibu na Tanganyika, ilizidi kumtia hofu Nyerere.
Nyerere alianza kuona kitisho hicho na kuamua kuwashawishi Milton Obote na Jomo Kenyatta kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki ili kujiweka salama na kitisho cha Zanzibar.
Wakati Nyerere akiiona Zanzibar kama balaa lijalo, Marekani nao kwa upande wao waliiona Zanzibar kama kizingiti kikubwa maana ilishaanza kuelekea kwa China, Urusi na Cuba kwenye siasa za Ukomunisti na hivyo Marekani kuona jinsi itavyokuwa na upungufu wa uwezo katika ukanda huu.
Tishio hilo la Zanzibar kwa Marekani lilizidi kuhanikiza na kumshawishi Nyerere afanye Muungano na Zanzibar ili kuimeza na kupunguza kitisho hicho.
Pia tusisahau kuwa kwa wakati huo, Zanzibar ilikuwa ni nchi yenye uchumi mkubwa kuliko Tanganyika na hivyo kuweka tishio hilo kuwa la kweli katika pande zote.
Sababu nyingi zilizosababisha Muungano wakati huo hazipo tena na sasa kuna sababu mpya na zenye misingi ya wananchi wenyewe wa Zanzibar na Tanganyika pia.
Tumeanza kusikia wananchi wakidai Muungano wa Serikali Tatu, Muungano wa Mkataba, Mamlaka Kamili, Kero za Muungano, Kura ya Maoni kuhusu uhalali wa Muungano wenyewe na jambo kubwa la Mabadiliko ya Katiba.
Pia tumeshuhudia viongozi mbalimbali wa SMZ kutoka CCM wakieleza kwa namna tofauti kuwa hawawezi kuishi bila ya Muungano na kuwa Zanzibar haiwezi kusimama yenyewe bila ya Muungano.
Hoja zao nyingi zimejawa na woga na pia hazina ushahidi wowote wa hayo wayasemayo.
Kwa mfano, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliandika makala ndefu katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015 na kueleza wasiwasi kama huo na kunasibisha matukio ya kumwagiwa tindikali kwa wasichana wawili raia wa Uingereza, uwepo wa kikundi cha Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu (Uamsho) kuwa ni miongoni mwa dalili hizo za kuelekea kwenye ugaidi ikiwa CUF watashinda Zanzibar.
Hayo yote na mengineyo ni sehemu ya woga kwa vile hakuna kesi hata moja ya ugaidi ambayo imehukumiwa na kuthibitishwa tuhuma zake.
Watuhumiwa 14 wa kesi ya ugaidi kutoka Zanzibar bado wapo rumande kwa zaidi ya miaka miwili huku upande wa mashtaka ukiwa haujakamilisha upelelezi wa mashtaka yao.
Zanzibar haijawahi kuwa na tatizo la udini, tangu enzi na dahari kwani Zanzibar kuna makanisa makubwa makubwa na yenye historia ndefu sana, mfano wa makanisa ya Mbweni, Kizimbani, Chachani na Mkunazini.
Hakuna kumbukumbu zozote au mahala popote pale kwenye taarifa za kupigwa au kuuawa mtu kwa kubaguliwa katika misingi ya dini yake.
Moja ya mnasaba wa kauli za woga kwa kisingizo cha udini inaweza kuwa hoja ya Padri Evarist Mushi kuuliwa kwa kupigwa risasi hapa Zanzibar na kisha kukamatwa watu ingawa mpaka leo hii mtuhumiwa hajatiwa hatiani na sheria kufuata mkondo wake na yupo nje akiendelea na shughuli zake, wengi walihusisha kukamatwa kwake na sababu za kisiasa.
Mtiririko wa matukio ya kila namna ya kutegwa mabomu na miripuko isiyoua, uchomwaji moto wa baadhi ya nyumba za wananchi, nyumba za ibada na maskani za vyama vya siasa ni baadhi ya matukio ambayo mpaka leo hii hakuna hata moja lililothibitishwa kimahakama na watuhumiwa wake kuhukumiwa.
Hii inaleta tafsiri mbili kubwa kuwa Jeshi la Polisi lina uwezo mdogo ama linatumika kisiasa na huenda lipo nyuma ya matukio haya ama inawajua hakika waliofanya na haiwachukulii hatua.
Tangu mwaka 1995 wakati uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliporejeshwa, wafuasi ambao wamekikamatwa mara zote ni wale wa vyama vya upinzani hususani CUF.
Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla katika hili la Muungano kumekuwa na maneno mengi yanayolenga kuleta hofu ambayo yanatolewa na baadhi ya viongozi wakubwa tu kusema maneno ambayo hata hayana mantiki.
Je, bila ya Muungano Wazanzibari wasingeoa Tanganyika au kuolewa Tanganyika?
Hoja hii ya kuoa na kuolewa ni hoja dhaifu sana kwa sababu Wazanzibari wamechanganya damu na mataifa ambayo hata mnasaba nayo hatuna na wala sio kwa dhana ya Muungano.
Jengine wanachochea hofu kuwa Muungano ukivunjika basi Wazanzibari watahama Tanganyika na kurudi kwao ili tu mtu mwenye mali au familia aone ni jambo haliwezakani.
Pia tumesikia wabunge kadhaa wakisema ukivunjwa Muungano basi mchele wa Mbeya itakuwa ndiyo mwisho kufika visiwani. Kwamba moja ya faida ya Muungano ni kwa Wazanzibari kula mchele wa Mbeya!
Huu Muungano una faida nyingi sana na kutoa fursa kubwa sana kwa pande zote, kwa muda wake na sababu zilizowekwa na kuuasisi mwaka Aprili 26, 1964 hazipo tena leo inapaswa kuangaliwa upya mfumo na matakwa yake kwa kizazi cha leo na kijacho.
Ukisema tumeunganika kwa sababu za kihistoria basi Zanzibar ilipaswa kuungana na Uingereza, Oman, Yemen, India pia kwa vile hao wamefika mwanzo Zanzibar na wana historia ndefu zaidi na Zanzibar kuliko Tanganyika.
Pili ukisema kwa sababu ya muingiliano wa kidamu, Zanzibar ilipaswa pia iungane na Kenya kwa ndugu zao walioko Lamu, Malindi na Mombasa.
Pengine pia Zanzibar ilitakiwa iwe na Muungano na Commoro. Kuna vitabu vimewahi kumnukuu Nyerere akisema kwamba angetamani visiwa vya Zanzibar viwe mbali sana na Tanganyika. Kwamba kama angeweza, angeweza kuvisukuma mbali baharini. Inawezekana vipi mtu atamani kumsukuma ndugu yake mbali kiasi hicho?
Kauli nyingine yenye utata ni ile iliyowahi kutolewa na Balozi Ali Karume kuwa “Sultan Jamshid alikuwa mtawala wa Kigeni Zanzibar”. Hii inaleta taabu kidogo kuilewa kwani kati ya Ali Karume na Jamshid nani ni mgeni hapa Zanzibar?
Sultan Jamshid kaburi la babu yake Sayyid Said bin Sultan lipo Zanzibar wakati kaburi la babu yake Ali Karume, Amani Karume, halipo Zanzibar. Ukitaka kujua kuhusu hili, pitia kitabu cha Ibrahim Noor Sharif Tanzania na Propaganda za Udini.
Yaliyowakuta akina Kassim Hanga, Abdulrahman Babu, Saleh Sadalla, Amani Thani, Khamis Ubwa na wengine yanafanana na yanayowakuta Uamsho leo pamoja na viongozi wa CUF na wengineo nje ya CCM.
Tumeona wengi wa hao waliopo CCM wanatetea muungano huu wakiwa wapo kwenye vyeo tu na kulinda tonge zao.
Wengi wakitolewa kwenye mfumo au kustaafu nao akili zao hurudi na kuona mapungufu makubwa ya Muungano huu.
Zanzibar tuliona Baraza la Wawakilishi kuogopa maazimio yao wenyewe waliyoyapitisha kama mapendekezo katika mchakato wa katiba mpya na kwenda kushikana uchawi Dodoma kwa akina Pandu Ameir Kificho na Marehemu Awadh Salmin.
Hapa ndipo unapoona kujiogopa kwa Zanzibar yenyewe kwa upande mmoja na pia kushikana kwake kunavyoleta woga kwa watu nje ya Zanzibar.
Hapo utaona kuwa mpaka leo Muungano unaishi kwa dhana kubwa ya woga. Marekani waliiogopa Zanzibar ila si kweli kuwa wanaiogopa leo tena.
Tanganyika bado wanaiogopa Zanzibar ukisikiliza kauli za viongozi mbalimbali hasa wa upande wa CCM.
Na pia woga umewajaa Wazanzibari wenyewe ndani ya CCM kuona hawawezi bila ya Muungano huu hivi ulivyo.
Ukiyapima manufaa ya Muungano huu ya miaka 50 hayamithiliki zaidi ya dhana zilizojengwa na ambazo hukosa majibu muhimu ya kisheria ama kijamii.
Kwa mfano je, Tanganyika imeenda wapi baada ya Muungano?
Aboud Jumbe alipopeleka hoja yake hakujibiwa ila alifanyiwa jambo binafsi na kuvuliwa nyadhifa zote pale Dodoma.
Seif Shariff na AMAHURU hawakujibiwa hoja zao na mwisho walifukuzwa na kufungwa.
Mfululizo wa matukio haya unalenga kuwa hapa kinachofichwa ni nini?
Muungano kwa sasa unasimama kwenye misingi mibovu ambayo kila mmoja anajiuliza maswali mengi yasiyo majibu.
Tunaposherehekea kutimiza miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wakati pia wa kuangalia namna bora tunaweza kuwa na Muungano ambao utakuwa na mizania sawa kwa washirika wote wa Muungano huu.
No comments:
Post a Comment