Mwalimu Julius K Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume |
Na Othman Miraji
Watanzania wanaadhimisha miaka 52 ya
Muungano wao wa Tanganyika na Zanzibar. Hongera. Siku 104 nyuma kutoka sasa
Watanzania pia waliadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Namshukuru
Mwenyezi Mungu kwamba nimeshuhudia kwa macho yangu matukio hayo mawili makubwa
ya kihistoria na maendeleo yake hadi leo. Kwangu mimi matukeo hayo mawili
yamefungamana. Bila ya kutokea Mapinduzi ya Zanzibar (12.01.1964) sifikiri
kwamba tungekuwa na Muungano huu wa Tanzania tunaouadhimisha. Japokuwa Hayati
Mwalimu Nyerere (Muasisi wa Muungano pamoja na Hayati Mzee Karume) aliwahi
kunukuliwa akisema kwamba hata kama Chama cha Afro-Shirazi, ASP, cha Zanzibar
kingeingia madarakani kwa njia za kikatiba na si kwa njia ya mapinduzi, Muungano
bado ungefanyika. Mimi sina hakika.
Kwa sisi wanafunzi wachache wa
Kizanzibari (ungeweza kuihesabu idadi yetu kwa vidole vya mikono miwili)
tuliokuwa tukisoma wakati huo katika Shule ya Sekondari ya Aga Khan (sasa
Tambaza ) mjini Dar es Salaam, habari ya Mapinduzi ya serikali yaliotokea
Zanzibar Januari 12, 1964 yalitufikia kwa mshangao mkubwa. Akili zetu za ujana
wakati huo zilivurugika kutokana na habari hiyo, japokuwa kila wakati
tulitakiwa na wazee wetu tujielekeze zaidi katika masomo na si katika siasa za
mivutano zilizotawala nyumbani wakati huo. Ilipopita miaka ndipo wengi wetu
tulipotambua kwamba Mapinduzi hayo yalifungamana pia na siasa kubwa zaidi
kuliko vimo vyetu vichanga vya utoto. Mwishowe tuligundua kwamba kumbe wadau
katika Mapinduzi hayo walikuwa si Wazanzibari peke yao.
Na pale Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ulipoundwa, Aprili 26, 1964 baadae ndipo kila mmoja wetu alipogundua
kwa ghafla kwamba mnamo siku moja tu amegeuka kutoka kuwa raia wa Jamhuri ya
Watu wa Zanzibar na kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Pia kwamba Zanzibar haitokuwa tena na kiti chake katika Umoja wa Mataifa,
lakini kutoka wakati huo itawakilishwa na kiti kimoja cha taifa jipya lenye
jina la Tanzania. Tuligundua baadae pia kwamba wadau wa Muungano walikuwa ni
wengi, yakiwemo madola mkuu yaliokuwa yakisuguana katika Vita Baridi baina ya
kambi ya kibepari ya Magharibi na ya kikoministi ya Mashariki. Madola hayo
yalisaka kila njia ili kuwa na ushawishi katika uchoraji wa ramani ya njia
itakayopitia Tanzania katika siku za mbele.Yalikuweko maslahi kadhaa
yaliopingana ndani ya Muungano huo. Kujiuliza masuali mengi wakati huo kulikuwa
hakuna faida. Kwa vyovyote Muungano ulishaundwa, hamna litakaloweza
kuubadilisha ukweli huo. Baadhi yetu tulijiuliza mbona mambo yalikwenda fasta
fasta, kasi ilikuwa kubwa mno? Tulijijibu wenyewe kwamba kulikuwa hakuna wakati
wa kudurusu nini kilichoamuliwa jana, hakuna wakati wa kuulizana na
kushauriana. Kwanini? Sijui.
Licha ya kwamba kila mmoja wetu
baada ya kumaliza shule alielekea njia yake- baadhi walienda vyuo vikuu na
wengine kutafuta ajira- nilishangaa kwamba katika shule za madaraja yote na pia
katika vyuo vya juu katika pande zote mbili za Muungano hakujatolewa elimu juu
ya Muungano. Si tu wanafunzi katika masomo yao ya historia na elimu ya uraia,
lakini pia Watanzania, kwa ujumla, hawakupewa maarifa na kuelemishwa kwa undani
juu ya Muungano wao, faida zake na sabababu zilizopelekea uundwe. Nilishangaa
pia kuona vipi Muungano huo ulivyofanywa kuwa zaidi mali ya viogozi badala ya
kuwa mali halali ya wananchi wote wa pande mbili. Lakini nilijitosheleza kwamba
Muungano wa watu wa pande mbili hizo ulikuweko kwa miaka na dahari, na
hautavunjika, ila tu huu wa sasa umesadifu kuandikwa karatasini na wanasiasa.
Katika miaka ya sitini tulikuwa
tunaishi wakati wa Vuguvugu la Mwamko wa Afrika, tukivutiwa na tunu za Afrika
ilioyoungana. Viongozi wetu waliotuongoza kuelekea ukombozi, akina Nkurumah wa
Ghana, Jamal Abdel Nasser wa Misri, Julius Nyerere wa Tanganyika na Jomo
Kenyatta wa Kenya walituambia kwamba Afrika ili iweze kusikika vilivyo na kuwa
na nguvu katika jukwaa la kimataifa lazima nchi za Afrika ziungane. Nkurumah
alienda mbali kutaka Afrika ilio na serikali, bunge, jeshi na rais mmoja.
Mwalimu Nyerere alimtahadharisha mkuu huyo wa Ghana na kumwambia aste aste,
polepole. Kwanza tuanze na Muungano wa nchi zilioko katika mkoa mmoja mmoja.
Baadhi ya vijana wa wakati huo walivutiwa na Muungano wa Tanzania, kama kianzio
cha ndoto ya kuwa na Muungano wa Afrika nzima. Hawajajali kwamba matayarisho
yake hayajawa ya kutosha na kwamba wananchi wa pande hizo mbili hawakushauriwa
kabla. Hata baadhi ya mawaziri wa huko Zanzibar walikuwa hawana taarifa hadi
siku za mwisho kabla ya kutiwa saini Mkataba wa Muungano. Kwa vijana hao,
lakini, lengo ndilo lilikuwa muhimu zaidi kuliko njia za kupita kulifikia lengo
lenyewe.
Hadi miaka ya karibuni (baada ya
kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa) ilikuwa mwiko kuzungumzia juu ya suala
la Muungano na manung’uniko ( yaliyoitwa “Kero”) juu ya Muungano huo yalifichwa
chini ya mkeka. Mara nyingi kero hizo zilisikika zaidi kutoka upande wa
Zanzibar kuliko wa Tanganyika. Ni kawaida yule anayehisi anapoteza zaidi ndiye
anayelalamika zaidi. Huenda kwa mujibu wa tarakimu za kifedha ikaonekana upande
mmoja unabeba mzigo mkubwa zaidi kuliko vile inavostahiki au inapunjwa zaidi
kuliko inavostahiki. Lakini kwa vile kunakosekana uwazi na kwamba Muungano
umekuwa ukiendeshwa kwa kuoneana muhali na kienyeji kuliko kuwa wa kisayansi na
wa kitarakimu, ni rahisi kwa kila upande kudai kwamba unaonewa na si kwamba
unaonea.
Muungano wa Tanzania haujajengeka
kwa nguvu za tarakimu na za kifedha, lakini, kama walivyosema waasisi wake,
kutokana na udugu wa kihistoria wa watu wake. Ni Muungano wa Damu ambao si
rahisi kuvunjika kwa sababu za kifedha. Muhimu zaidi ikumbukwe kwamba ni
Zanzibar iliyowachia mamlaka yake ya juu kabisa ya kiutawala na utambulisho
wake wa kimatifa, mambo ambayo kabisa mtu hawezi kuyatathmini kwa vipimo vya
fedha na tarakimu.
Japokuwa hapo awali Mkataba wa
Muungano ulitaka taasisi mbili za kutunga sheria- Bunge kwa upande wa
Tanganyika na Baraza la Mapinduzi kwa upande wa Zanzibar- mwishowe ziidhinishe
ibara ziliomo ndani ya Mkataba huo, kuna watu wanaodai kwamba kwa upande wa
Zanzibar jambo hilo halijafanyika. Hivyo kuna wanasheria wa masuala ya katiba
wanaouwekea alama ya kuuliza uhalali wa Mkataba huo. Lakini hayo, baada ya
kupita miaka 52 ya Muungano na kama Wajerumani wanavyosema, hiyo ni theluji
ilionyesha jana. Imeshayayuka. Au kwa msemo wa Kiswahili: Yaliopita si ndwele,
tugange yajayo. Mkataba wa Muungano ulitaja mambo 11 tu yawe masuala ya
Muungano, lakini sasa yameengezwa na kufikia 23. Hiyo ni kusema mamlaka ya
Zanzibar ndani ya Muungano yamezidi kufifia.
Tume ya Marehemu Jaji Francis
Nyalali iliyochunguza mwaka 1991 juu ya utayarifu wa Watanzania kama wanautaka
mfufo wa vyama vingi vya siasa ilitaka utaratibu wa sasa wa kuwa na serikali
mbili- ya Muungano na ya Zanzibar- ubadilishwe na uwe wa Shirikisho. Tume hiyo
ilikubali kwamba kuna matataizo ndani ya Muungano na ikasema ingekuwa busara
kero kuhusu Muungano huo zisikilizwe na zitafutiwa ufumbuzi. Lakini walitokea
watu waliosema kwamba mfumo wa Shirikisho utafungua njia kwa Muungano wenyewe
kuvunjika. Kuna watu walioamini na bado wanaamini kwamba Mapinduzi ya Zanzibar
yasingedumu hadi leo bila ya kuweko Muungano.
Udhaifu ninaouona mimi ni kwamba
Watanzania wa pande zote mbili za Muungano hawajaelezewa kinagaubaga sababu za
kuunganishwa hapo April 1964. Inasemekana Hayati Mzee Karume wa Zanzibar
alilikubali wazo la Muungano kutoka kwa Hayati Mwalimu Nyerere wa Tanganyika
kama njia kwa serikali mpya ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na ulinzi dhidi ya
jaribio lolote la wapinga mapinduzi wa ndani na nje ya Zanzibar kutaka
kuipindua serikali yake.
Ndani ya Baraza la Mapinduzi la
Zanzibar kulikuweko pia watu waliokuwa wanafuata siasa za mrengo wa kikoministi
na wa shoto ambao Mzee Karume inadaiwa alihisi wangeweza kutishia uongozi wake.
Lakini watafiti wengine wanahoji
kwamba kulikuweko mbinyo mkubwa kutoka nchi za Magharibi, hasa kutoka Marekani,
ili Mapinduzi ya Zanzibar yadhibitiwe kwa vile yalionekana kuwa ni ya hatari na
huenda yangeeneza ushawishi wa Wakominsiti na wa nchi za Kambi ya Mashariki katika
eneo zima la Mashariki ya Afrika. Wamarekani hawajataka kucheza bahati nasibu
na halafu washindwe na kuiona Zanzibar inageuka kuwa „ Cuba ya Afrika
Mashariki“. Wao waliiona Jamhuri ya kimapinduzi ya Watu wa Zanzibar kuwa ati ni
kibaraka wa madola ya Mashariki, hivyo kwa wao Wamarekani Muungano wa
Tanganyika ( iliokuwa wakati huo inasaidiwa sana na nchi za Magharibi) na
Zanzibar ni njia bora ya kuzuwia kusambaa hatari ya ukoministi.
Haijapita miaka, Mapinduzi ya
Zanzibar yaligeuka na yalianza „kuwatafuna watoto wake“ yenyewe, licha ya
wapinzani wake wa asili. Hofu ilienea Visiwani na kuna watu waliopotea bila ya
kujulikana hatima zao hadi leo. Wazanzibari wengi walikimbilia Tanzania Bara
kunusuru maisha yao au wakihofia kwamba wangewekwa vizuizini. Baadhi ya wale
waliofukuzwa makazini Zanzibar waliweza kujipatia ajira Bara na wengine kwenda
ng’ambo. Serikali ya Muungano mjini Dar es Salaam ilijua fika nini kilichokuwa
kinatendeka Zanzibar, lakini wachambuzi wanasema wakuu wa Bara hawajataka
kujiingiza katika mambo ya ndani ya Visiwani. Walihofia wasije kuwakasirisha
wakuu wa huko Zanzibar. Yote huenda ni kuulinda Muungano usipate mtikisiko na
labda kuvunjika. Na hasa inavyosemekana kwamba katika miezi ya mwisho kabla ya
kuuawa Hayati Mzee Karume uhusiano baina yake na Hayati Mwalimu Nyerere ulikuwa
si wa uchangamfu mkubwa kama ulivyokuwa hapo mwanzo.
Malengo makubwa ya Mapinduzi ya
Zanzibar ambayo Chama cha Afro Shirazi yalijivunia nayo – kuondosha ubaguzi wa
makabila na wa rangi, kuhakikisha kuna huduma za kijamii kwa watu wote,
kutokomeza umaskini, kutoa bure huduma muhimu za kijami za elimu, afya pamoja
na maji – yalianza kusahauliwa polepole. Badala yake viongozi walijikusanyia
mali na kuwa kama masultani wepya, huku uhuru wa raia wa kutoa maoni ukibanwa.
Wahakiki wanasema kwamba Mzee Hayati
Karume aliposaini Mkataba wa Muungano alifikiri Tanganyika na Zanzibar
zinaingia katika Mfumo wa Shirikisho la nchi mbili zitakazokuwa na mamlaka
mengi, tena sawa, kila moja katika mambo yake ya ndani, na mambo machache yawe
ya Muungano. Kabla ya nchi zote za Afrika Mashariki kuwa huru, wazo la kuundwa
Shirikisho la Afrika Mashariki baada ya uhuru lilikuweko na kupigiwa upatu
sana. Inafikiriwa na baadhi ya watu kwamba kiongozi huyo wa Zanzibar wakati huo
hajafikiria kwamba Muungano huo utakuwa kama huu wa sasa ambao unaweka mamlaka
mengi sana kwa serikali ya Muungano. Utaratibu wa serikali ya Tanganyika kuwa
ni ileile ya Muungano ulikusudiwa uwe kwa muda mfupi sana, labda mwaka mmoja,
hadi pale katiba mpya ya kudumu ya Muungano itakapotungwa. Lakini hadi leo
mfumo huu ungaliko, bado unaendelea, ikiwa ni miaka 52 tangu kuanzishwa
Muungano. Hoja iliotolewa kwa miaka mingi kutoka upande wa Zanzibar ni kwamba
hakuna msingi wowote wa kusema kwamba Tanganyika imepoteza utambulisho wake
ndani ya Muungano huu. Kwa hakika Tanganyika imevaa joho la Muungano na
imejipanua kimamlaka. Ni mamlaka ya Zanzibar, kama inavotajwa katika Mkataba wa
Muungano, ndio ya kulindwa na kuendelezwa ili kwamba, kama alivosema Hayati
Mwalimu Nyerere mara kadhaa, kusiweko dhana kwamba Tanganyika ilio kubwa na
yenye rasilimali nyingi zaidi “imeimeza” Zanzibar ilio ndogo kieneo na kwa
idadi ya wakaazi.
Ukweli ni kwamba kila miaka
ilivyoenda utambulisho wa Zanzibar ndani ya Muungano, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni,
unapungua. Hilo ni jambao ambalo Wazanzibari wengi linawasumbua hata kufikia
hadi wengi wao sasa wanataka mfumo wa serikali tatu kama Tume ya Katiba Mpya ya
Jaji Warioba ilivyopendekeza miaka miwili ilopita. Katika uchunguzi wake, tume
hiyo imegundu kwamba zaidi ya asilimia 60 ya Wazanzibar wanataka Muungano wa
Mkataba baina ya Tanganyika na Zanzibar.
Wazanzibari wanalikumbuka baraza la
mawaziri la mwanzo la serikali ya Muungano hapo mwaka 1964, chini ya Hayati
Mwalimu Nyerere kama rais. Lilikuwa na mawaziri 20 ( akiwemo mwanasheria mkuu
wa kutoka upande wa Bara asiyekuwa na kura). Kati yao 13 walikuwa wanatokea
Bara (Nyerere, Kawawa, Kambona, Munanka, Maswanya, Mgonja, Shaba, Eliofoo,
Jamal, Bryceson, Tewa, Sijaona na Lusinde) na 7 walitokea Zanzibar (Karume,
Jumbe, Hanga, Idriss Abdulwakili, Babu, Hasnu Makame na Hassan N. Moyo).
Linganisha na baraza la Mawaziri la sasa chini ya Rais Magufuli ambalo lina
mawaziri 23 (pamoja na mwanasheria mkuu wa serikali kutoka Bara asiyekuwa na
kura) . Lina Wazanzibari wanne tu (Makamo wa rais Bi Samia Suluhu, Dk. Shein –
kutokana na mamlaka aliyokuwa nayo kama rais wa Zanzibar – Dk. Hussein Mwinyi
na Profesa Makame Mbarawa.
Tangu kuweko Muungano hakuna
Mzanzibari aliyewahi kushika nafasi za juu katika taasisi za Muungano kama
Benki Kuu, jeshi au polisi. Kuna idadi ndogo sana ya Wazanzibari wanaofanya
kazi katika balozi za Tanzania nchi za nje na pia sehemu ya Zanzibar katika
michango inayopata Tanzania kama misaada, mikopo au ruzuku kutoka nchi na
taasisi za nje ni haba mno. Ilipokataliwa Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya
Kiislamu Duniani, OIC, kwa kuambiwa kwamba masuala ya mambo ya kigeni na
ushirikiano wa kimataifa yako chini ya serikali ya Muungano, Wazanzibari wengi
walihuzunishwa. Mfumo wa serikali ya Muungano wa utozaji na ukusanyaji kodi
umelaumiwa mara kadhaa na wafanya biashara wa Zanzibar kwamba unawaonea,
hautilii maanani kwamba uchumi wa Zanzibar ni wa kivisiwa, tafauti na ule wa
Bara.
Hadi mwaka 1992 ulipoingia mfumo wa
vyama vingi vya kisiasa, maoni yeyote yaliyohoji au kuonesha kutoridhika na
mfumo wa Muungano uliokuweko yalinyamazishwa. Lakini watu waliendelea kuelezea
maoni yao na kutaka kuchangia katika kutunga mustakbali mwema wa Muungano wao.
Marais wa Zanzibar waliopita, Mzee Jumbe, Dr. Salmin Amour na pia Dr. Amani
Karume hawajawa na wakati rahisi pale walipokuwa wanasimama kidete kabisa
kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano. Mara kadhaa maalalamiko
aliyokuwa akiyatoa aliyekuwa makamo rais wa kwanza wa Zanzibar, Maalim Seif
Shariff, juu ya kupunjwa Zanzibar katika faida za Muungano yamekuwa yakibezwa
kutokana tu na maslahi ya kichama badala ya kushughulikiwa.
Zanzibar inahitaji iuangalie
uhusiano wake namna ulivyo na Tanzania Bara kwani unatoa sura kwamba Tanganyika
ndio mlinzi wa serikali ya Zanzibar kwa vyovyote vile, bila ya kujali nini
kinatokea ndani kwenyewe Visiwani. Maadam chama tawala cha CCM kinabakia
madarakani katika pande zote mbili za Muungano. Maono ya CCM tangu kuundwa
kwake kuelekea Zanzibar yamekuwa kuwekea uzito zaidi suala la usalama katika
visiwa hivyo kuliko lile la maendeleo.
Zanzibar imeshindwa kutamba na
kuingia kwa njia huru katika mikataba ya kiuchumi na kifedha bila ya ridhaa ya
serikali ya Muungano. Haiwezi kufurukuta na kuwa na siasa zake huru juu ya
mambo ya fedha na sarafu zinaoambatana na mikakati yake ya maendeleo, kwa vile
masuala hayo ni ya Muungano. Siasa zozote mbovu za Benki Kuu ya Tanzania
zinaumiza moja kwa moja uchumi wa Zanzibar. Kugharimia urari wa malipo huko
Bara kunaiumiza pia Zanzibar- ughali wa maisha kupanda na kuweko mriupuko wa
bei za bidhaa.
Ukitizama uzoefu wa Miungano katika
sehemu nyingine za dunia ni kwamba pale Muungano unapokuwa baina ya nchi kubwa
na nchi ndogo kunakuweko kila wakati hofu ya nchi ndogo „kumezwa“ na nchi
kubwa. Miungano kama hiyo iliojengeka kwa hofu kutoka upande mmoja haijadumu,
imevunjika. Mifano mizuri ni ile iliokuweko baina ya Misri na Syria na kuundwa
Muungano wa Jamhuri ya Kiarabu baina ya mwaka 1958-1961. Wasyria walihiyari
kujitoa kutoka Muungano huo kwa vile waliona hatamu na nyadhifa nyingi za juu
katika serikali ya Muungano zilikamatwa na Wamisri.
Shirikisho la Senegambia ambalo
lilikuwa baina ya Senegal na Gambia, nchi mbili huko Afrika Magharibi, lilikufa
mwaka wa 1989 baada ya kudumu miaka saba tu. Gambia ilikataa kuwa na mfumo wa
serikali ya Muungano ikihofia kumezwa na Senegal ilio kubwa kieneo na kwa idadi
ya wakaazi. Pia tusiusahau Muungano wa Kisoviet (Urusi) baina Russia na Jamhuri
nyingine za Kisoviet na ambao ulisambaratika mwaka 1999 baada ya kuweko kwa
karibu miaka 80. Waeritrea wilikataa kubakia ndani ya Ethiopia na walikamata
bunduki kupigana dhidi ya majeshi ya Ethiopia ili kuikomboa nchi yao baada ya
kukaliwa kwa zaidi ya miaka 20. Watu wa nchi ndogo ya Timor Mashariki huko
Kusini Mashariki ya Asia baada ya Mreno kuondoka nchini mwao mwaka 1975
hawajakubali ukoloni huo nafasi yake ichukuliwe na ukoloni wa nchi kubwa jirani
ya Indonesia. Walipigana hadi walipopata uhuru mwaka 2002. Wasahara Magharibi
huko Afrika Kusini wanapigana, hawataki kulikubali takwa la Morocco kwamba nchi
yao iwe sehemu ya miliki ya Ufalme wa Morocco.
Baadhi ya wakati huzushwa suala kama
Tanganyika au Zanzibar zitamudu kuishi kila moja peke yake bila ya Muungano.
Suala hilo hasa linaelekezwa zaidi kwa Zanzibar kama inaweza kuishi bila ya
Tanganyika. Tanganyika inaweza sana, ukiangalia uchumi wake mkubwa. Lakini
haitopenda kuwa na jirani ambaye hatabiriki, hajulikani atakuwa vipi baada ya
kuvunjika Muungano. Hiyo ndio maana Rais aliyepita wa Muungano, Jakaya Kikwete,
alimwambia wazi hivi karibuni katibu mkuu wa Chama cha Upinzani cha CUF, Maalim
Seif Shariff, kwamba CCM inahofia kwamba pindi Maalim Seif Shariff atakuwa rais
wa Zanzibar basi atauvunja
Muugano. Hilo Maalim Seif Shariff
amelikataa moja kwa moja, na kusisitiza kwamba yeye ni muumini wa Muungano,
lakini Muungano anaoutaka ni ule wa haki. Anasema Muungano wa sasa unaibana
Zanzibar na anakumbusha msemo wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee
Karume, kwamba Muungano ni kama koti. Usishange mtu anapotaka kulivua pale
linapombana sana na kushindwa kupumua. Maalim Seif Shariff anashikilia kwamba
yeye ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa urais wa Zanzibar wa Oktoba mwaka jana
na ambao ulivunjwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.
Wazanzibari wengi sana hawana wazo
la kuuvunja Muungano. Vivyohivyo walivyo Watanganyika wengi. Wengi wao
hawajawahi kuishi katika nchi nyingine isipokuwa hii ya sasa yenye jina la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawaijui ile Zanzibar kabla ya 1964.
Vivyohivyo kwa Watanganyika. Ni wachache walio hai wanaijuwa Tanganyika. Suali
linazushwa kila wakati ikiwa Muungano huu ni mzuri na wenye manufaa mbona nchi
nyingine za jirani hazijavutiwa nao? Tukumbuke kwamba Muungano huo ulisadifu
kufanyika katika wakati ambao viongozi waliouasisi walihitajiana. Na ingekuwa
si wakati huo na matukeo yaliozunguka wakati huo, kama vile kutokea Mapinduzi
ya Zanzibar na uhasama wa madola makuu uliokuweko wakati huo wa Vita Baridi,
sidhani kwamba ingewezekana kuwa na Muungano wa Tanzania wa aina hii. Suala la
Muungano wa damu, japokuwa ni muhimu, lakini ni la pembeni.
Licha ya yote hayo, inafaa pia
tuachane na ile ambayo imekuwa dhana potofu hadi miaka ya karibuni kwamba
kuhoji mambo fulani yanayofanyika ndani ya Muungano- ambayo hayatimizi lile
lengo mama la awali la usawa baina ya pande mbili- ni uhaini, kukosa uzalendo
au sawa na kuupinga Muungano wenyewe. Suala la kuhoji mambo ya yanayofanyika
kuhusu Muungano, kuudadisi na kuudurusu baada ya kila muda ni jambo linaloupa
afya Muungano pamoja na hewa mpya ya kupumua nayo kila wakati. Muungano ni
zoezi endelevu na kila inapohitajika kuufanyia marekebisho au mabadiliko ni
sahihi kabisa kufanya hivyo. Siasa za mkwamo hazisaidii. Watu wasigope kuja na
ubunifu mpya kuhusu Muungano wao. Wakati mwingine woga ni mbaya zaidi kuliko
yale magonjwa ya hatari sana kwa mwanadamu. Katika mchezo wa mpira inabidi
wakati mwingine ubadilishe mbinu (tactics ) za mchezo ili ushinde. Vilevile kwa
Watanzania juu ya Muungano wao.
Muungano mzuri na ulio wa amani ni
ule unaowapa watu wote wa pande zote za Muungano haki ya kuchangia na
kujiamilia mustakbali wao tangu kutoka ngazi za chini kabisa hadi juu kabisa.
Chachu nyingine inayojenga Muungano imara ni kuheshimiwa haki za binadamu kwa
raia wote ndani ya Muungano, raia wawe huru kuchagua mfumo wa kisiasa
wanaoutaka na viongozi gani wanataka wawaongoze kwa ajili ya maendeleo yao ya
kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
Kwa vyovyote, kwamba Muungano wao
umefikia miaka 52, licha ya matatizo yote, ni jambo la fahari kwa Watanzania.
Wana kila haki ya kujivunia. Wamezipiku nchi nyingi zilizojaribu kufanya hivyo
na zikashindwa njiani. Watanganyika na Wazanzibari kwa pamoja wamethibitisha
kwamba mara nyingine “kupepesuka si kuanguka”. Happy Birthday Muungano.
No comments:
Post a Comment