Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein. |
Na Enzi T. Aboud – Imechapwa 25 April 2016
MZIMU wa ubaguzi kwa misingi ya rangi,
mtu alikotoka, kuzaliwa na uchama wa vyama mfu vya kale, vya upinzani;
Hizbu (ZNP) na chama cha watu wa Unguja na Pemba (ZPPP), sasa
unakitafuna Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.
Baadhi ya makada wa CCM na wazee
mashuhuri wa chama hicho wamesisitiza kukisafisha chama chao, lakini
wakiwa na chembe za ubaguzi zinaoonekana dhahiri.
Katika kutekeleza zoezi hilo, makada hao
wameapa kuwaondoka ndani ya chama wanachama wanaowaita “wasaliti,” ambao
wanahusishwa, kwa njia moja ama nyingine na vyama hivyo vya upinzani.
Ma-Hizbu na Ma-CUF, kama wanavyoitwa
ndani ya chama hicho, wanatuhumiwa kukihujumu na pia kuihujumu serikali
yake ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Serikali hiyo iliyoundwa hivi karibuni
kwa mbinde na kususiwa na CUF na vyama vingine, imo katika majaribio
makubwa ya kiuongozi kutokana na kutengwa na vyama vyote hivyo vya
upinzani.
Kama hilo halitoshi, Rais Ali Mohamed
Shein amenyooshewa kidole na baadhi ya makada wa CCM wenye msimamo mkali
kwa hatua yake ya kumteuwa Hamad Rashid, kiongozi wa chama kidogo cha
upinzani (ADC) kuwa waziri wa kilimo. Pia rais huyo aliwateua viongozi
wawili wengine; Said Soud wa chama cha wakulima (AFP) na Juma Khatibu wa
chama cha Tadea, ambao wamewateuliwa kuwa mawaziri wasiokuwa na wizara
maalum.
Makada hao wa CCM wanapingana waziwazi na
uteuzi huo wa viongozi wa upinzani, wakidai kuwa hawatamsaidia rais
kutokana na misimamo yao ya kupinga sera za CCM na Mapinduzi ya Zanzibar
ya 1964.
Wamebainisha kuwa Hamad Rashid alifukuzwa
CCM miaka ya 80 pamoja na wenzake saba, akiwemo Maalim Seif Sharif
Hamad walipobainika kuwa hawakubaliani na sera za CCM na muundo wa
Muungano wa serikali mbili.
Pia viongozi hao walituhumiwa kujikita
zaidi katika siasa za upinzani za kuitetea Zanzibar kupata hati zake
ndani ya Muungano na kuwa mamlaka kamili.
Aidha, Rais Shein analalamikiwa kwamba
hakufanya uchunguzi wa kina au washauri wake hawakumpa ushauri ipasavyo
katika hatua za mwanzo kabla ya kufanya uteuzi wa mawaziri wa serikali
yake mpya.
Inaelezwa kwamba CCM Zanzibar
imekasirishwa na uteuzi wa Moulding Castico kuwa waziri kwa maelezo ya
kutokuwa mzaliwa wa Zanzibar na siyo raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Imedaiwa kuwa Moulding ni raia wa
kuzaliwa nchini Zambia ambaye aliwahi kuolewa na hayati Joseph Castico,
Mzanzibari aliyefariki dunia miaka ya 90 na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa
mila, utamaduni na sanaa katika wizara iliyokuwa ya habari wakati wa
utawala wa Rais (mstaafu) Dk. Salmin Amour na Dk. Amani Karume.
Katka mazingira hayo ya siasa za majungu,
chuki za ubaguzi na kutuhumiana kwa mambo yasiyokuwa na tija ndani ya
CCM, imethibitika kuwa hali hiyo ya udhaifu imeanza kuzoeleka na kuota
mizizi.
Mbali na Moulding Castico kutiliwa shaka
kwa kutuhumiwa kuwa siyo raia wa Tanzania, pia mwingine aliyenyooshewa
kidole kwa tuhuma kama hizo ni spika mpya wa Baraza la Wawakilisha,
Zubeir Ali Maulid.
Huyu anatuhumiwa kwamba siyo raia wa Tanzania, bali ni mzaliwa wa Uganda.
Kushuka na kupanda kwa Moulding Castico
katika ulingo wa siasa Visiwani, kumetokana na mazingira ya majungu ya
kisiasa na kupanda kwake kumetokana na ushiriki wake mzuri katika
harakati za kijamii hasa za kuwapigania wanawake na uwezo wake wa
kisiasa.
Kwa mara ya kwanza Moulding Castico
aliteuliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na baadaye
kuteuliwa kuwa Katibu wa Mkoa wa Arusha.
Nafasi nyingine alizowahi kushika katika
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mkurugenzi katika wizara iliyokuwa
ya habari, mila na utamaduni wakati wa uongozi wa Dk. Salmin Amour,
ingawa uteuzi wake ulitenguliwa baada ya kubainika kwamba hakuwa
Mzanzibari na hakuwa raia wa Tanzania. Kwa miaka yote hiyo aliyoishi
Zanzibar alikuwa ni mke wa hayati Joseph Costico aliyekuwa Zanzibar na
raia wa Tanzania wa kuzaliwa.
Imekuwa ni kawaida kwa Zanzibar kuwapokea
wageni na kuweza kuishi nchini bila kufuatiliwa kisheria na hata
kufikia kushika nafasi za juu katika uongozi wa chama cha siasa hata
katika nafasi za uongozi katika Serikali.
Utamaduni huu wa kutojali kuwahakiki
wageni wanapoingia Visiwani, hasa wale wanaotoka nchi za jirani za
Afrika Mashariki kama vile Kenya, Uganda, Zambia na Malawi, imekuwa ni
jambo la mazoea.
Mwanya huo umekuwa ukitumiwa miaka mingi,
hata baadhi ya viongozi wa kundi la kamati ya watu kumi na nne (14)
waliofanya Mapinduzi mwaka 1964, yaliongozwa na John Okello aliyejivika
cheo cha Field Marshall, alibainika kuwa ni raia wa Uganda.
Aidha, mjumbe mwingine wa kamati hiyo alikuwa Egunas Injin, raia ya Kenya.
Wakati CCM Zanzibar kinaishi kwa hofu ya
mzimu wa chama cha kale, kilichokufa cha ASP, CCM Bara inasumbuliwa na
hofu inayotokana na Katiba mbovu ya Muungano, inayozua maswali mengi
kuliko majibu kuhusiana na uhalali wa Muungano wenyewe na namna ya kutoa
fursa kwa vyama vyengine vya upinzani kwa upande wa Zanzibar.
Swali linakuja hapa- “je kama chama cha
CUF kingeshinda uchaguzi wa mwaka jana wa Oktoba 25 na kiongozi wa Chama
hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Rais wa Zanzibar na Dk. John
Magufuli kuwa Rais wa Tanzania, hali ya kisiasa ingekuwaje kwa vyama
viwili tofauti kutawala sehemu mbili tofauti ya Tanzania?
Kinachoonekana sasa Wazanzibari bado
wanabaguana kwa misingi ya vyama vya siasa vilivyo hai vya CCM na CUF na
vyama mfu vya ASP, ZNP na ZPPP.
Fikra hovyo za makada wa CCM zilizojikita
katika ndoto hewa za kurudi utawala wa sultani wa kiarabu nazo pia
zinajumuisha matatizo ya kudumu ya kisiasa yasiyoweza kutatuka.
Hii pia imeonekana katika siasa
zilizojitokeza na kuvunjwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo
inahusishwa na utawala wa kisultani.
Njia pekee ya kuondokana na mzimu wa
vyama mfu katika utawala wa Zanzibar na katika siasa za mfumo wa vyama
vingi ndani ya visiwa hivyo ni kufanya juhudi za kurudisha maelewano wa
vyama vikubwa hivi viwili vya CUF na CCM na kutoa wigo mpana wa kugawana
madaraka.
Lakini juhudi hizo zitaweza kufanikiwa
pale tu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa Rais Magufuli
kuziangaza upya haki za Zanzibar na kuwajali Wazanzibari katika
kusimamia uhuru na haki ya Zanzibar
No comments:
Post a Comment