Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. |
Na Ahmed Rajab
UONGOZI ni dhamana. Ni dhamana kubwa
na nzito mtu kujitwika nayo au hata kutwikwa nayo. Mzigo wa uongozi unazidi
kuwa mzito uongozi huo unapokuwa uongozi wa taifa. Hili ni wazi, na halina
shaka, isipokuwa kwa wasiotaka kulijuwa.
Dhamana nayo ina majukumu yake. Na majukumu hayo yanazidi kuwa nyeti dhamana hiyo inapokuwa ni dhamana ya kuliongoza dola, watu wa hilo dola, yaani wananchi, na rasilmali zake ambazo kwa hakika huwa ni rasilmali za hao wananchi.
Kuna wenye kuhoji kwamba aliyesimamia utawala wa awamu ya nne anastahiki ashitakiwe kwa matumizi mabaya ya madaraka aliyokuwa nayo.
Wanayataja mambo mawili makuu: la kwanza, ufisadi uliokithiri na la pili, kuporwa kwa haki za Wazanzibari kutokana na kufutwa kwa uchaguzi uliokuwa huru na wa haki wa Oktoba 2015.
Madai yote hayo mawili ni mazito.
Wenye kuyatoa wanaendelea kuhoji kwamba kwa kutochukua hatua imara kupambana na ufisadi Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwezesha pawepo nafasi kubwa iliyowaruhusu wezi kuiba mali ya serikali.
Wakati huo huo nafasi hiyo au mazingira hayo yamewawezesha watumishi wa serikali waendeshe mambo ovyo ovyo.
Kuendesha mambo ovyo ovyo, kienyeji, kwa kujizingatia “sisi kwa sisi” tu bila ya kuwajali wananchi walio wengi kumekuwa na athari zake. Athari hizo ni ovu na nyingi.
Miongoni mwazo ni kuzusha hali zinazoupalilia ufisadi wa kisiasa na wa kiuchumi, kuzusha hali au mazingira yasiyoweza tena kuudhibiti ubadhirifu wa fedha za umma. Na ni hali hizo hizo zinazoiruhusu serikali iwe inatoa mikopo kiholela, mikopo inayowafaidisha zaidi wanasiasa na watumishi wakuu wa serikali.
Kwa jumla kuna ushahidi mkubwa wenye kuonyesha na kuthibitisha jinsi ufisadi ulivyojengeka nchini, hususan katika awamu ya nne, kwa ubia uliozidi kufanikishwa baina ya wanasiasa, mafisadi katika sekta ya binafsi na watumishi wakuu wa serikali.
Hili ni jengo la ufisadi lililojengeka juu ya misingi iliyochimbwa na kusimamishwa na wanasiasa wa chama kinachotawala.
Chama hicho kimekumbwa na ugonjwa uleule uliovikumba vyama vilivyopigania uhuru katika nchi nyingi za Kiafrika. Huu ni ugonjwa wa kuamini kwamba ni vyama hivyo tu vyenye haki ya kutawala na viongozi wa vyama hivyo tu ndio wenye haki ya kuitwa watawala.
Wakishaitwa watawala, wakavikalia viti vya utawala huanza kujiona kuwa wao ndio serikali na serikali ndio dola.
Kwa hivyo, kwa kuwa wao wanajiona kuwa ndio serikali basi mantiki yao inawafanya waamini kwamba wao pia ndio dola. Siyo tu kwamba dola ni lao wao peke yao lakini wao ndio hasa dola. Wao ndio dola na dola ndio wao. Ndiyo maana wanalisarifu dola watakavyo. Chambilecho Joseph Mihangwa wanaligeuza dola kuwa “shamba la bibi”.
Kwa hakika, makala ya Mihangwa katika matoleo mawili yaliyopita ya gazeti hili pamoja na makala ya ukurasa wa mbele wa toleo la wiki iliyopita chini ya kichwa cha maneno “Nchi ilivyotafunwa mbele ya Kikwete” ni makala ambayo kila Mtanzania anapaswa ayasome.
Makala yote hayo matatu yanatoa mwanga kuonyesha jinsi utawala wa awamu ya nne ulivyokithiri si katika ufisadi tu bali pia kwa uzembe katika uendeshaji wa serikali.
Ukishayasoma makala hayo hutokuwa na shaka yo yote kwamba Rais wa awamu ya nne ni mtu anayetakiwa afikishwe mahakamani ila Katiba tuliyo nayo huenda ikamkinga. Juu ya hayo, kuna wenye kusema kwamba kwa Magufuli chochote kinaweza kuzuka na kwamba hata ile haramu ya Zanzibar inaweza ikawarejea wenyewe.
Hata hivyo licha ya Magufuli na ayafanyayo, si wengi wenye matumaini hayo. Hoja yao kubwa ni kwamba hakuna wa kuaminiwa, na kuaminika, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Yeyote yule anayeibuka akawa na ujasiri wa kuwaambia kweli watawala kwamba wako uchi na wanahitaji wajistiri huambiwa kuwa ni msaliti na haini. Jaza yao huwa ni kudhalilishwa na kugandamizwa. Na wenye kuwagandamiza huwa ni wale wale waliokuwa wakipigania haki na usawa wakati wa kupambana na ukoloni. Mfumo wa kisiasa wa aina hiyo haukubali abadan kuruhusu pawepo na mfumo mbadala.
Hayo si mageni katika historia ya ulimwengu. Tangu Mapinduzi ya Ufaransa (1789 hadi 1799), mara nyingi wakombozi wa nchi mbali mbali wamekuwa wakigeuka na kuwa wagandamizi. Waliokuwa wakionewa wakawa ndio wenye kujitutumua kuwaonea wengine. Na wakionea na wakiwaumiza watu kwa kuzikanyaga haki zao za binadamu hawadhani kuwa wanawajibika kuwaomba radhi wananchi.
Hii ndiyo moja ya sababu zinazowafanya baadhi ya watu katika nchi za Kiafrika wawe wanahoji kimwehu kwamba bora kutawaliwa na wakoloni kushinda kutawaliwa na Waafrika wenzetu. Hoja yao kubwa ni kwamba kimsingi maisha yao ya kawaida hayakubadilika tangu enzi za ukoloni. Wanasema hawaoni tofauti kubwa kwa namna wanavyotawaliwa sasa na walipokuwa wakitawaliwa na wakoloni.
Sababu ya hayo ni kwamba hawa watawala wetu wa leo wamerithi mengi kutoka kwa wakoloni. Wamerithi sera na hata namna ya kufikiri, namna ya kuyatumia madaraka waliyo nayo na namna ya utendaji kazi wao. Wanayakumbatia na kuyapakata madaraka kama ni yao wao watawala peke yao bila ya kuwashirikisha wengi wa wananchi.
Mambo ya ufisadi hayako kwetu tu lakini wenzetu nao pia wanayo ila wao wameweza kuzitumia nguvu za umma kupambana nayo. Wameweza pia kuzitumia taasisi za kidemokrasia kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa. Tuchukulie mifano ya nchi kadhaa za Amerika ya Kati na Amerika ya Kusini.
Sheria katika baadhi ya nchi hizo zinaruhusu marais wastaafu na hata wa sasa wafikishwe mahakamani. Hivi karibuni marais wawili wastaafu wa Honduras na El Salvador walishtakiwa kwa ufisadi.
Serikali ya Rais mstaafu wa Honduras Rafael Leonardo Callejas ilifanya mengi katika ustawi wa jamii lakini mafanikio hayo hayakuweza kumkinga Callejas asishtakiwe. Alikabiliwa na mashtaka saba ya ufisadi alioufanya wakati wa muhula wake wa urais (Januari 1990 hadi Januari 1994). Nchini Honduras, Rais ana muhula mmoja tu wa kutawala wa miaka minne.
Mnamo 2005, Bunge la Honduras liliibatilisha sheria iliyokuwa ikiwakinga Marais wastaafu wasishtakiwe. Sheria hiyo ilipobatilishwa Callejas mwenyewe, kwa hiyari yake, alijipeleka mahakamani na akafunguliwa kesi kwa mashtaka yote yaliyomkabili. Alifanyiwa kesi na halafu Mahakama ikamwachia huru baada ya kuona kwamba hakuwa na hatia.
Halafu Desemba mwaka jana alishtakiwa na Mahakama ya Marekani kwa kuhusika na kashfa ya ufisadi ya Shirikisho la Soka la FIFA wakati alipokuwa mkuu wa Shirikisho la Soka la nchi yake.
Siku kadhaa baada ya kushtakiwa Callejas mwenyewe akenda Marekani ambako alitiwa mbaroni na siku chache baadaye aliachiwa na Mahakama kwa dhamana. Mwezi uliopita alikiri kwamba alikuwa na hatia ya kupokea hongo ya dola za Marekani 500, 000 mwaka 2012, fedha ambazo alikuwa azile yeye na afisa mwengine.
Nchini El Salvador hakimu mmoja alimuamuru Rais mstaafu Francisco Flores ashtakiwe kwa tuhuma za kuziingiza katika akaunti yake binafsi na akaunti ya chama chake dola za Marekani milioni 15 wakati alipokuwa Rais baina ya 1999 na 2004. Fedha hizo zilizokuwa zimechangwa zilikusudiwa waathirika kwa zilzala iliyotokea nchini humo.
Halafu kuna RaisOtto Pérez Molina wa Guatemala aliyechaguliwa Rais 2012 na aliyelazimika kujiuzulu urais Septemba mwaka jana baada ya kukabiliwa na mashtaka ya ufisadi. Molina hivi sasa yuko jela pamoja na aliyekuwa makamu wake. Wote wawili wanakabiliwa na mashtaka ya ulaji rushwa.
Yaliyomkuta Molina ni mara ya mwanzo kumkuta Rais aliye madarakani tangu mfumo wa demokrasia ushamiri katika nchi za Amerika ya Kusini.
Na kuna ya Brazil ambako Rais mstaafu Luiz Inácio Lula da Silva ameshtakiwa wakati uchunguzi ukifanywa kuhusu shutuma za kashfa ya ufisadi zinazoikabili kampuni ya Petrobras, ambayo ni kampuni ya mafuta yenye kumilikiwa na serikali ya Brazil.
Shutuma hizo zinazomkabili Lula ni kitisho kwa mrithi wake Rais Dilma Rousseff ambaye anayumbayumba kisiasa kwa vile Bunge limo katika mchakato wa kumshtaki kwa kutumia vibaya madaraka. Lula anasema shtuma zote hizo ni njama za kisiasa zinazopikwa na maadui wao wa kisiasa.
Kote huko katika eneo la nchi za Amerika ya Kusini Marais siku hizi wanahaha. Wananchi wa huko wakitiwa nguvu na jumuiya za kiraia, zisizo za kiserikali, wamekuwa wakipiga kelele na kuzishinikiza serikali zichukuwe hatua dhidi ya ufisadi na dhidi ya wakubwa wao wenye kushutumiwa kwa mashtaka ya ufisadi.
Rais mstaafu wa Panama Ricardo Martinelli naye anakabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu wa fedha za umma, njama za kuwafanyia ujasusi mahasimu wake wa kisiasa na mashtaka mingine ya ufisadi. Kwa amekimbilia Florida, Marekani, lakini Mahakama Kuu ya Panama imetoa amri akamatwe na arudishwe kwao kupandishwa kizimb
Huku kwetu Kikwete anaweza akaponea chupuchupu. Kwa hali ilivyo, Katiba ndiyo imekuwa kinga yake wakati alipokuwa Rais na sasa baada ya kuuacha urais. Si Katiba peke yake lakini ana kinga nyingine — ule moyo wa kulindana walio nao watawala wetu.
Kwa hivyo, hata kama patakuweko na kipengele cha sheria au mwanya wa kisheria utaoweza kumfanya ashtakiwe kutakuwako na huo moyo wa wakubwa kulindana ambao huenda ukakoroga mambo. Wakubwa wanaweza kufanya hivyo kwa sababu hawaitii maanani demokrasia na wamezoea kuubeza mfumo huo.
Kutokana na hayo ni kheri tuwe na demokrasia ya kibwanyenye kushinda kukosekana demokrasia ya yo yote. Angalau katika mfumo huu wa demokrasia ya kiini macho viongozi wanaweza wakawajibishwa kwa ufisadi wao.
No comments:
Post a Comment