Thursday, 5 May 2016

Hapa Kazi tu yamkera Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
KAULI mbiu ya serikali ya Rais John Magufuli ya hapa kazi tu imedaiwa kuwa imeongeza vitendo vya kikandamizaji kila mahali nchini.


Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki na Waziri kivuli wa Wizara ya Katiba na sheria amesema kauli mbiu hiyo imeleta ukandamizaji katika baadhi ya maeneo hata kule ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kilikataliwa.

Alitolea mfano wa vitendo hivyo vilijitokeza katika jiji la Tanga ambako CCM ilikataliwa na wananchi lakini ilitumia ghilba na mabavu ya kila aina kuhakikisha inanyakuwa umeya wa jiji hilo.

Kutokana na ukandamizaji huo wa CCM, viongozi mbalimbali na madiwani waliochaguliwa na wananchi wanakabiliwa na mashtaka ya kutengenezwa kwa sababu tu ya kukataa kwao kutawaliwa na watu ambao hawakupata ridhaa ya wananchi.

Amefananisha kitendo hicho na kile na kilicho tokea Halmashauri ya Kilombero ambako mbunge halali wa jimbo hilo alitolewa kwa nguvu na polisi ili CCM iliyokataliwa na wananchi kwenye kura iweze kushinda nafasi ya mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo.

Amesema katika jiji la Dar es Salaam na Halmashauri zake licha ya serikali kuwa na nguvu nyingi lakini wananchi na viongozi wao walifanikiwa kutetea maamuzi ya wapiga kura na kuzuia ubakaji wa kidemokrasia kwa kuweka mameya wa chama kilichotawala kwa nguvu ya wananchi kwenye uchaguzi.

“haijalishi kwamba mawaziri hawa si mamlaka yao ya kinidhamu kwa utumishi wa umma na kama tulivyo onyesha wala hawajakamilisha majukumu yoyote ya kisheria sasa mawaziri wanafukuza au kusimamisha au kuwahamisha watumishi walio chini yao wakiulizwa hujibu hapa kazi tu”Lissu amesema.

Aidha amesema wakuu wa mikoa nao wanatumbua majipu kwa kuwasimamisha wakurugenzi wa halmashauri za serikali za mitaa na watumishi wengine wa serikali za mitaa bila kujali kuwa hawana mamlaka yoyote ya kisheria kwa kufanya hivyo wakiulizwa hukimbilia kujificha katika kauli mbiu hiyo ya kikandamizaji.

Alionya kuwa serikali ya Magufuli imekumbatia dhana ya kunyamazisha upinzani dhidi yake na kunyima uhuru wa vyombo vya habari na kudhihirisha hilo imeanza kuingilia uhuru wa mahakama kwa njia ya ajabu ambayo ni dalili ya moja kwa moja nchi kuingia kwenye udikekta kwa kauli mbiu ya hapa kazi tu.
CHANZO: MWANAHALISI ONLINE

No comments:

Post a Comment