|
Rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta |
Na Joseph Mihangwa.
KWA miaka minne mfululizo kati ya
mwaka 1962 na 1965, nchi zote nne za Afrika Mashariki asilia, kwa maana ya
Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar, zilikumbwa na kiwewe pamoja na hofu ya
ushawishi wa itikadi za Kikomunisti katika kipindi ambacho dunia ilikuwa
ikijijenga kwa misingi ya vita baridi kati ya nchi za kibepari za Magharibi
zikiongozwa na Marekani, na nchi za Kikomunisti/Kisoshalisti za Mashariki,
zikiongozwa na Urusi na China.
Mapema mwaka 1961, vita hivi vilikuwa vimejidhihirisha kwa uwazi zaidi nchini
Congo (sasa DRC) ambapo mgongano wa kambi hizo mbili ulipelekea kupinduliwa kwa
serikali mpya ya Waziri Mkuu mwenye mrengo mkali wa siasa za Kikomunisti,
Patrice Emery Lumumba, kisha kuuawa kwa amri ya Shirika la Kijasusi la Marekani
(CIA) na Kapteni (baadaye Jenerali) Joseph Desire Mobutu (baadaye Mobutu
Sesesseko Kuku Ng’bendu wa Zabanga) kuchukua madaraka.
Zanzibar ilihofiwa zaidi kugeuka mlango na kitovu cha Ukomunisti Afrika
Mashariki kupitia mwanaharakati wa itikadi hiyo, Abdulrahman Mohamed Babu tangu
miaka ya 1950 akiwa Katibu Mkuu wa Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP)
kilichokuwa na uhusiano wa harakati za ukombozi na China, Cuba, Misri, Algeria
na Urusi na ambaye baadaye alijiengua kutoka chama hicho na kuanzisha chama cha
Umma Party (UP) mwaka 1963.
Ni chama hicho ambacho kwa sehemu kubwa makada wake walishiriki kupanga na
kuratibu Mapinduzi ya umwagaji damu ya Januari 12, 1964 yaliyotokea visiwani
Zanzibar.
Harakati za Babu na makada wenzake kuona Zanzibar inatawaliwa kwa sera na
itikadi za Kikomunisti kufuatia Mapinduzi, zilitia hofu nchi za magharibi na
kuipa Zanzibar jina la “Cuba ya Afrika”, zikaanza kuchukua tahadhari juu ya
kujijenga haraka kwa Ukomunisti sehemu hii ya Afrika.
Mkakati wa kwanza wa nchi hizo, hususani, Marekani na Uingereza, kwa kumtumia
Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ulikuwa ni kuundwa kwa
Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF) ambamo Zanzibar ya Kikomunisti ingeweza
kumezwa isifurukute.
Mazungumzo ya kuunda EAF yaliposhindwa na mradi huo kusambaratika mjini
Nairobi, Aprili 10, 1964, Marekani na Uingereza zilichukua mkakati mwingine
uliobuniwa na aliyekuwa Balozi wa Uingereza nchini Kenya, William Attwood,
ulioitwa “Zanzibar Action Plan” (ZAP) wa kuivamia Zanzibar kijeshi, mkakati
uliomshtua Mwalimu kwa kuhofia vita vya kimataifa kupiganiwa mlangoni mwa Tanganyika.
Ni Attwood aliyepewa jukumu la kuandaa mpango wa uvamizi huo, na baada ya
kuonana na Rais Jomo Kenyatta wa Kenya, aliripoti Washington akisema, “Kenyatta
ameonesha kukubali mpango huu iwapo tu Nyerere na Obote wataridhia hatua hiyo.
Amenithibitishia atakutana na Nyerere, Obote na Karume hivi karibuni
kuzungumzia suala la Zanzibar”.
Ili kuepusha vita hivyo, Mwalimu alibuni “Shirikisho” tofauti na lile la EAF;
safari hii alibuni Shirikisho (Muungano) kati ya Tanganyika na Zanzibar kwa
madhumuni yaleyale ya kukabiliana na Ukomunisti kwa njia ya Zanzibar ya
Wakomunisti kumezwa ndani ya tumbo la Tanganyika.
Aprili 18, 1964, Mwalimu alimruhusu Waziri wake wa Ulinzi na Mambo ya Nje,
Oscar Kambona, kumjulisha Balozi wa Marekani nchini Tanganyika, William Leonhardt,
juu ya Muungano uliotarajiwa, naye akaitaarifu Washington siku hiyohiyo
akisema, “Kuzorota kwa hali na kuongezeka kwa ushawishi wa Babu na Wakomunisti
Visiwani Zanzibar kumefanya Tanganyika ione umuhimu wa kuunda Shirikisho na
Zanzibar ili visiwa hivi visiende kwa Wakomunisti wa China – CHICOMMS”.
Haya yakiendelea, Makamanda wa Vikosi vya Uingereza, I.S. Stockwell wa Jeshi la
Anga la Uingereza (RAF) Afrika Mashariki, na I. H. Freeland wa Jeshi la Nchi
Kavu (Infantry), tayari walikuwa wametoa amri ya pamoja (Joint Instruction) kwa
Vikosi vyao, Namba 2/64 tayari kwa uvamizi.
Siku nne baadaye, Aprili 22, 1964, Mkataba (Hati ya Muungano) ukatiwa sahihi
kati ya Karume na Nyerere mjini Unguja, na Muungano kutangazwa rasmi, Aprili
26, 1964 na hivyo Nyerere kuweza kuepusha “janga” la vita na kwa Ukomunisti
kushika hatamu Afrika Mashariki.
Haya yakitokea nchini Tanganyika na Zanzibar, na nchini Kenya iliyowahi kuwa
koloni la Uingereza tofauti na Tanganyika, Ukomunisti uliendelea kunyemelea
chini kwa chini na kupanga Mapinduzi kwa staili tofauti na iliyotumika
Zanzibar.
Alipofungua Chuo cha Kumbukumbu ya Patrice Lumumba (Lumumba Institute) mjini
Nairobi siku na baada ya kuapishwa kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya,
Desemba 12, 1964, Rais Jomo Kenyatta hakujua kwamba chuo alichokuwa akifungua
ulikuwa ni mpango uliosukwa kwa makini kuja kumpindua.
Akifungua chuo hicho, kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 20, barabara ya Thika,
akiwa katikati ya Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo, Bildadi Kagia; mke wa Rais, Mama
Ngina na Makamu wa Rais wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga; Rais Kenyatta
alifahamishwa madhumuni ya chuo hicho yalikuwa ni kutoa elimu kwa makada wa
chama tawala (KANU) kwa lengo la kuimarisha na kueneza moyo wa “Harambee”
katika ujenzi wa taifa hilo kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Pengine Bango la shaba langoni mwa chuo lilielezea mengi zaidi kuliko yale
aliyoelezwa Kenyatta wakati wa ufunguzi, lilisomeka: “Chuo hiki ni kwa
kumbukumbu ya hayati Patrice Lumumba, mwanaharakati mzalendo aliyefia mikononi
mwa mabeberu na mawakala wao kwa kupigania uhuru wa kweli wa Kiafrika kisiasa,
kiuchumi na ‘kiujamaa’ barani Afrika”.
Lakini Mkenya mmoja mzalendo na mwanaharakati; Makamu wa Rais, kwa jina la
“Jaramogi” Oginga Odinga, alijua siri nyingine kubwa zaidi juu ya chuo hicho,
ya “kuingiza nchini itikadi na Mapinduzi ya Kikomunisti nchini Kenya” kwa
mlango wa nyuma bila serikali kujua na hatimaye kufanya Mapinduzi.
Na kwanini utawala wa Kenyatta, ulioegemea zaidi kwenye sera na itikadi za
Ulaya Magharibi, haukuweza kutambua hilo kutokana na mazingira; kwa kuanzia na
Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo, Bildadi Kagia, aliyepata elimu na mafunzo ya
kiharakati nchi za Kikomunisti (Urusi, China, Czechoslavukia) na aliyefahamika
kwa misimamo yake ya Kikomunisti nchini Kenya, sawa tu na alivyokuwa
Abdulrahman Babu, Zanzibar?.
Na lile bango langoni, je, halikuwashtua? Kwa nchi ya kibepari (Kenya), ambayo
Rais wake alitamani hata iwe “huru” lakini isiwe Jamhuri, ibakie daima chini ya
Malkia, kama zilivyo Canada, Australia, au New Zealand; kwa kusomeka kumtukuza
Lumumba, hayati Mkomunisti wa kutupa, na kulaani “ubeberu” na badala yake
kutukuza “ujamaa” ndani ya nchi ya kibepari?.
Huenda pengine ni kwa sababu Kenyatta na serikali yake walimuamini sana Oginga
kwa kila alilofanya kwa Kenya, lakini kwa hili la kupanga Mapinduzi alikwenda
mbali zaidi.
Aliwaza Ujamaa kabla ya Nyerere
Kenya ilipata madaraka ya ndani Juni 1, 1963 ambapo Waziri Mkuu Jomo Kenyatta
aliteua Mawaziri 13 wa serikali yake huku Oginga Odinga akiwa Waziri wa Mambo
ya Ndani.
Desemba 12, 1963 bendera ya Uingereza, “Union Jack” ilishushwa na bendera ya
Kenya huru ikapepea kuashiria tamati ya utawala wa miaka 68 wa Uingereza,
kuelekea Jamhuri chini ya chama tawala “Kenya African National Union” – KANU,
Kenyatta akiwa Rais wa chama na Odinga makamu wake.
Mwezi Juni 1964, Kenyatta alihudhuria Mkutano wa Nchi za Madola nchini London
na aliporejea alikuta fukuto la Usoshalisti ndani ya chama na serikali
likiongozwa na Odinga pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu, Bildadi Kagia,
wakitaka sera mpya juu ya umiliki Ardhi na Elimu.
Harakati hizi ziliiweka pabaya serikali ya Kenyatta hata kulazimika kuweka sera
na kuridhia sera ya “Ujamaa” kupitia “Session Paper No. 10” yenye dhana juu ya
“African Socialism and its Application to Planning in Kenya” kama “Ujamaa wa
Kiafrika na matumizi yake katika Mipango nchini Kenya”, na kuchapishwa Mei 4,
1965.
Kufikia mwaka 1965, “Ujamaa” wa Odinga ulikuwa umeigawa jamii ya Kenya na
kupelekea kuuawa kwa kupigwa risasi kwa mtetezi wa “Ujamaa” na mwanasiasa
machachari kupitia KANU, Pio Gama Pinto. Ndiyo kusema, Odinga aliwaza Ujamaa
kabla ya Mwalimu kuandika Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea
mwaka 1967.
Hali ilipokuwa si shwari tena ndani ya KANU, Kenyatta aliona njia pekee ya
kuzima “Ujamaa” ilikuwa ni kumwondolea Odinga wadhifa wa Makamu Rais wa KANU,
kwa kuanzisha nafasi za Makamu Rais wa KANU wa Majimbo ambapo kwa Jimbo la
Mashariki aliteuliwa Bw. Jeremiah Nyagali; Magharibi, Bw. James Masakhala;
Nairobi, Bw. Mwai Kibaki; Pwani, Bw. Ronald Ngala, na Bonde la Ufa, Bw. Daniel
Arap Moi huku Tom Mboya aliyekuwa wakala na kuwadi mkubwa wa Shirika la Ujasusi
la Marekani (CIA) nchini Kenya akichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa KANU.
Kuona hivyo, Odinga alijiuzulu kutoka KANU, Aprili, 1966, na kuunda Chama cha
Kenya Peoples’ Union” (KPU); na Mei 1966, akachapisha sera ya chama chake
kuhusu Ardhi, Elimu na “Ujamaa”.
Julai 3, 1969, pale Tom Mboya alipouawa kwa kupigwa risasi na kufuatiwa na
kuzuka kwa ghasia mjini Kisumu, KPU kilipigwa marufuku na Odinga kutiwa kizuizini.
Mkakati wa Mapinduzi ulivyosukwa
Mkakati wa kuangusha Serikali ya Kenyatta kupitia chama tawala – “KANU”,
ulibuniwa na Oginga mwenyewe kwa ushirikiano na “Wakomunisti” wenzake ndani na
nje ya KANU, kama ambavyo tu Babu na Wakomunisti wenzake Zanzibar, walivyoasisi
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kwa kushirikiana na “Wakomunisti” ndani ya Chama
tawala – Afro-Shirazi Party (ASP) bila Rais Abeid Amani Karume kujua.
Eneo la ekari 20 za chuo kilipojengwa lilinunuliwa na Oginga mwenyewe na ujenzi
kukamilika kwa kasi ya ajabu ya miezi mitano tu na kugharimu pauni za Uingereza
27,000, huku sehemu kubwa ya fedha ikitolewa na nchi za Kikomunisti na Odinga
kupewa na serikali jukumu na uhuru wote wa kuratibu ujenzi na uendeshaji wa
Chuo.
Na ndiye pia aliyekuwa na mamlaka ya kuteua Bodi ya Chuo iliyokuwa na
“Wakomunisti” wa Kikenya wa kutupa, wakiwamo, Bildadi Kagia (Mwenyekiti), Pio
Gama Pinto (aliyeuawa kwa msaada wa CIA), J. Thuo, S. Nzioki, J. Wanyonyi,
Profesa Munoru, Ochieng Oneko na S. Othigo Othieno.
Wengine walikuwa ni Kungu Karumba, Frederick Kubai; F. Oluande, Paul Ngei na
Joseph Murumbi ambaye CIA lilimtumia bila mafanikio, kuhakikisha kwamba EAF
linaundwa na Zanzibar inamezwa ndani ya Shirikisho hilo, wakati huo akiwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya.
Menejimenti ya Chuo iliongozwa na Mwana Sayansi ya Siasa mahiri na Mkomunisti,
Mathew Mutiso na Naibu wake, mwanaharakati aliyepata mafunzo nchini
Czechoslovakia, Wanguhu Ng’ang’a. Odinga alileta pia wahadhiri wawili kutoka
Urusi, Mabwana Alex Zidravomyslov na Andrei Bogdanov, kufundisha somo la
Misingi ya Ujamaa.
Masomo yaliyofundishwa karibu yote yalikuwa ya mrengo wa “Ujamaa”, na
yalichaguliwa kwa umakini mkubwa: Historia ya Mifumo ya Siasa, Afrika kuelekea
Ujamaa, Kiswahili, Uhasibu na Maisha ya Jomo Kenyatta.
Machi 4,1965., Odinga alipokea misaada mbalimbali kutoka nchi za Kikomunisti
Czechoslovakia, Yugoslavia, Ujerumani Mashariki na China, ikiwa ni pamoja na
gari la senema, vitabu na mablanketi.
Ukweli, mradi huu ulianza kwa kishindo na nguvu kubwa, nyuma yake kukiwa na
Warusi na Wachina kwa kificho kwa lengo la kumwezesha Odinga kunyakua madaraka
kupitia chama cha KANU.
Wanafunzi wa kwanza 114 waliripoti chuoni, Machi 4, 1965 wakiwamo Wenyeviti,
Makatibu na Wahasibu wa KANU wa Wilaya, ambapo wanafunzi 84 wa kwanza walifuzu
mafunzo Juni 30, 1965 na kurejea sehemu za kazi.
Wiki mbili baadaye, kikosi cha wahitimu hao kiliongoza “Mapinduzi” kwa kuutimua
uongozi mzima wa KANU, Makao Makuu na kuwabakiza Kenyatta na Odinga pekee bila
kujua ambacho kingefuatia. Lakini, Oginga na Wakomunisti wenzake walijua
kilicholengwa.
Nyuma ya “Mapinduzi” haya alikuwamo raia wa China, Wang Te Mi, aliyesafiri hadi
Kenya kwa kificho kama Mwandishi wa Habari kwa kutumia Pasi ya Kibalozi. Wang
alitumika kama askari wa kujitolea wakati wa vita ya Korea (1954) na kupanda
cheo kufikia Meja.
Mwingine alikuwa raia wa Afrika Kusini, Mkomunisti wa kutupa aliyekuwa
akifundisha chuo cha “Duke of Gloucester” mjini Nairobi, Hosea Jaffe, na
wengine nyuma ya pazia.
Ni Balozi wa Uingereza, William Attwood, kupitia kile kile alichokiita
“vyanzo”, aliyegundua kilichotokea, kilichokuwa kikiendelea na kilichotarajiwa
Makao Makuu ya KANU. Haraka haraka “akamujuza” aliyekuwa Waziri wa Mipango ya
Uchumi na Wakala mkubwa wa CIA nchini Kenya, Tom Mboya ambaye naye aliunguruma
bungeni kutaka serikali ichukue hatua za haraka kudhibiti hali.
Kuanzia hapo, serikali ilikazia jicho chuo hicho huku serikali ya Uingereza
ikitishia kuvunja uhusiano na Kenya, na Marekani ikitishia kuiadhibu nchi hiyo
ambapo Mei 5, 1965, serikali ya Kenya iliwafukuza wahadhiri hao wawili wa
Kirusi chuoni hapo.
Hatua hii ya serikali, chini ya jicho kali la Uingereza na Marekani, iliepusha
mapinduzi nchini Kenya mithili ya yaliyotokea Zanzibar kabla ya hapo.