Sunday, 12 October 2014

Maalim Seif: Katiba inayopendekezwa inainyima mamlaka Zanzibar

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda Maiti Zanzibar.
Na Nassor Khamis.
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kupiga kura ya hapana kwa Rasimu ya katiba inayopendekezwa kutokana na kutozingatia maslahi ya Zanzibar.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda maiti mjini Unguja.

Akivizungumzia baadhi ya vifungu Maalim Seif amesema katiba inayo pendekezwa imepunguza mamlaka zaidi ya Zanzibar tofauti na ilivyoelezwa na wanaounga mkono katiba hiyo.

Amesema kuwa katiba inayopendekezwa imetoa mamlaka zaidi kwa Serikali ya Muungano kwa kusema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja yenye mamlaka kamili hivyo kuinyang’anya Zanzibar mamlaka iliyo nayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar toleo la 2010.

Maalim Seif amesema kuwa Katiba ya Zanzibar inampa uwezo Rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika Mikoa na maeneo mengine ya kiutawala ambapo kwa sasa mamlaka hayo yamewekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha amesema kuwa rasimu hiyo bado haijatoa uhuru kwa Zanzibar kushirikiana na Mashirika na Jumuiya za kikanda pamoja na Kimataifa kutokana na mashirika hayo kutoa uwanachama kwa nchi zenye mamlaka kamili ya kiuongozi jambo ambalo kwa Zanzibar bado halijapatikana.

“Shirika kama la Chakula duniani, UNESCO na mashirika mengine hatoi uanachama kwa nchi ambazo hazina mamlaka ya kujiendesha wenyewe na kwa Katiba hii inaqyopendekezwa bado Zanzibar haijapata mamlaka kamili” alisema Maalim Seif.

Aidha amesema kuwa Rasimu iliyotolewa na Tume ya jaji Warioba ilipunguza idadi ya mambo ya Muungano kutoka 22 hadi kufikia saba badala yake Rasimu inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba imeyaongeza kutoka saba hadi 14.

Pia amesema kuwa Rasimu inayopendekezwa bado imeifanya Ta nganyika kuendelea kuvaa koti la Muungano kutokna na mambo yake yasiyokuwa ya Muungano kuendelea kusimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia amesema kuwa katiba inayo pendekezwa imekosa uhalali wa kisheria kutokana na kutopatikana kwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar waliyoinga mkono rasimu hiyo wakati wa upigaji wa kura.

Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba Yahya Khamis Hamad wajumbe waliopiga kura ya ndio hawakufikia theluthi mbili badala yake matokeo yaliyotangazwa yalikuwa na lengo la kuipitisha rasimu hiyo kinguvu kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi.

Aidha amesema kuwa endapo katiba inayopendekezwa itapitshwa itasababisha mgogoro wa kikatiba kutokana na na katiba hiyo kukinzana na katiba ya Zanzbar hivyo kulazimisha kufanyiwa marekebisho katiba ya Zanzibar jambo ambalo halitawezekana.

Amesema kuwa ili kuifanyia marekebisho katiba ya Zanzibar kutahitajika theluthi mbili ya Wajuumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunga mkono ambapo wajumbe watokanao na chama cha CUF hawatakubali jambo hilo kutokea.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Mh, Nassor Ahmed Mazrouy amewataka Wazanzibar kuikataa katiba inayo pendekezwa pamoja na kuwakataa Wabunge na Wawakilishi wote waliopiga kura ya ndio kwa katiba inayo pendekezwa.

Naye Mjumbe wa kamati ya maridhiano Mansour Yussuf Himid amesema kuwa ataendelea kuitetea Zanzibar ipate mamlaka yake kamili hivyo ataendelea kupingana na mfumo wa Muungano wa CCM uliojaa ukatili dhidi ya Wanzibari.

Alisema kuwa kwa mujibu wa vitabu vya dini mbali mbali vinaeleza kila nafsi itaonja mauti je wao wanaogopa nini kilichobakia ni kuingia mitaani kuwambia Wazanzibar wasikubali kuipitisha katiba hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Maridhiano Zanzibar,Mzee Nassor moyo alisema kuwa Wazanzibar waliungana na Tanganyika kwa hiari yao hivyo hakuna mtu yeyote wa kuwalazimisha kufanya mambo yanayokwenda kinyume na matakwa ya Wazanzibar.

Mapema mkurugenzi wa habari na uenezi wa CUF, Salim Abdallah Bimani alisema kuwa rasimu inayopendekezwa sio ya wazanzibar na haitofika Zanzibar bali itaishia Kisiwa cha Chumbe .

Na aliwataka wazanzibari kuungana pamoja na kuikataa kwa nguvu zote rasimu ya Chenge na wenzake kwani imekuja kuangamiza Zanzibar.

Sunday, 28 September 2014

Mahakama ya Kadhi yalitafuna Bunge

Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakiwa Bungeni mjini Dodoma. PICHA YA MAKTABA
Suala la Mahakama ya Kadhi limechafua hali ya hewa bungeni mjini Dodoma baada ya wajumbe Waislamu kutishia kupiga kura ya hapana kama halitaingizwa katika Rasimu inayopendekezwa.

Wakati Waislamu wakishikilia msimamo huo, wajumbe ambao ni Wakristo nao wamejipanga kupiga kura ya hapana endapo Mahakama ya Kadhi itaingizwa katika Katiba inayopendekezwa.

Dalili za mpasuko huo zilianza kujitokeza jana asubuhi baada ya mjumbe mmoja, Jaku Ayub Hashim kuwasha kipaza sauti akitaka kuzungumza akisema ana jambo muhimu.

“Mheshimiwa tangu jana (juzi) ulisema utanipa nafasi ya mwanzo nizungumze,” alisema Jaku, lakini Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu alimtaka aketi chini na suala lake limesikika.

Suluhu akaendelea kuwapa wajumbe wengine kuendelea kuchangia na baadaye alimpa Jaku muda wa dakika saba ili kuwasilisha kile alichotaka kukizungumza ndani ya Bunge hilo.

Jaku alisema walipendekeza kifungu kinachotaka uamuzi unaohusu ndoa, talaka na mirathi iliyoamuliwa kwa misingi ya dini ingizwe kwenye Katiba inayopendekeza lakini hakimo.

“Ni kitu kidogo kabisa tuliomba kiongezwe lakini cha kusikitisha kikundi cha sanaa kimeingizwa. Mimi binafsi yangu sitaunga mkono wala mguu wala sitaipigia kura hii,” alisema Jaku.

Suluhu akamweleza kuwa angalizo lake limechukuliwa, na uongozi wa Bunge pamoja na kamati ya Uandishi wanajitahidi kuingiza kila kitu kinachowezekana, lakini kwa misingi na sheria za nchi.

Baadaye Sheikh Masoud Jongo alipopewa nafasi ya kuchangia, naye alitahadharisha kuwa mambo yaliyopendekezwa na Waislamu yasipoingizwa kama ilivyo kwa sasa, hawatakuwa tayari kwa lolote.

“Msimamo wetu sisi Waislamu kama mambo yetu tuliyoleta katika mapendekezo hayataingizwa, basi yatabomokea hapa na hatutakuwa tayari tena,” alisema Sheikh Jongo, kauli iliyowashtua wajumbe.

Akihitimisha majadiliano hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge alisema kamati yake imefanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kwa masilahi ya Watanzania.

Akiahirisha Bunge, Suluhu alisema kesho Bunge litaanza kwa kupitia baadhi ya mambo yaliyoibuka katika uhakiki kisha kupitisha azimio la upigaji wa kura. Kura zitapigwa kati ya kesho hadi Oktoba 2.

Baada ya kuahirishwa kwa Bunge, Sheikh mwingine, Hamid Jongo alimwendea Askofu mstaafu Donald Mtetemela na kumkumbatia, kisha kumvuta pembeni na kisha kuteta kwa dakika tano.

Katika viwanja vya Bunge, hali ilikuwa tete kwani kulikuwa na makundi tofauti tofauti ya Wakristo na Waislamu kila moja likijadili na kutafakari suala la Mahakama ya Kadhi kuingizwa kwenye Katiba.

Mjumbe wa kundi la 201 Dk Aley Nassoro alisema kuwa suala la Mahakama ya Kadhi lisipoingizwa katika Katiba inayopendekezwa, atakuwa wa kwanza kuhamasisha wenzake ili wagome kupiga kura.

Dk Nassoro alisema Waislamu wamechoka kudanganywa kwani tangu kipindi cha kampeni za mwaka 2010, waliahidiwa kuwa jambo hilo lingeshughulikiwa mapema lakini watawala wamekuwa kimya.

“Hii Katiba itakuwa ni mbovu kuliko ile ya mwaka 1977 na italeta migongano baada ya miezi sita tu tangu kuzinduliwa. Bora iachwe kwani mambo mengi ya msingi kwa Wazanzibari yameachwa,”alisema.

Akiwa viwanja vya Bunge Askofu Mtetemela alionekana akishauriana na wajumbe mbalimbali na baadaye alisema analaani kauli hizo na kusema kuwa hazilengi kujenga nchi badala yake zinabomoa.

“Kinachotakiwa ni amani, sasa tukianza kutishiana mambo hayatakwenda maana na sisi Wakristo tutataka mambo yetu yaingizwe humo, tunachohitaji ni amani na si vinginevyo,” alisema Mtetemela.

Askofu Mtetemela alisema kikubwa kinachotakiwa kwa wajumbe ni maridhiano na isiwe vitisho kwa kuwa walianza pamoja hivyo wanapaswa kumaliza pamoja.

Aliitaka Kamati ya Uandishi kutoingiza kabisa jambo hilo katika Katiba na akasema hali ikifikia hapo itasababisha mgogoro wa kimasilahi kwa kila mtu kudai haki yake ndani ya Katiba.

Hata hivyo, aliitaka Serikali kutunga sheria za kutambua uamuzi wa Waislamu wa ndoa, mirathi na umiliki wa rasilimali kwa Waislamu ili yakubaliwe kwenye sheria siyo kwenye Katiba.

Mjumbe mwingine wa Bunge hilo, John Cheyo, alitaka Watanzania kuendelea kuheshimu Katiba ambayo imeweka wazi kuwa Serikali haina dini bali wananchi wake ndiyo wenye dini.

“Kwa sababu ukienda njia hiyo hakuna atakayeshinda. Na sisi Wakristo tuseme bila ‘Canon Law’ (Sheria za Kanisa) hakuna hatupigi kura, tutafika wapi? Ndiyo maana tuliyatenganisha haya mambo,”alisema.

Wakati makundi hayo yakiwa na msimamo tofauti, jana katika viwanja hivyo vya Bunge walisikika Waislamu wakihamasishana kwamba kama ikifika kesho hakuna Mahakama ya Kadhi wasusie Bunge.

Suala la Mahakama ya Kadhi, linaonekana kuwapasua kichwa wajumbe wa Kamati ya Uongozi ambayo juzi na jana zilikutana kutafuta njia ya kulinusuru Bunge hilo na mpasuko huo mkubwa.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe walipendekeza kuitishwa kwa Kamati ya Maridhiano ili kutafuta njia bora itakayonusuru Katiba Mpya kukwama kesho.

CHANZO: MWANANCHI

Saturday, 27 September 2014

Majambazi wapora milioni 30.6 wajeruhi Polisi, Mfanyabiashara

Sajenti Hija Hassan Hija akipatiwa huduma ya kwanza katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mara baada ya kujeruhiwa kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni mjambazi maeneo ya Mlandege.
Na Tatu Makame, Laylat Khalfan
WATU wawili akiwamo askari mmoja wamenusurika kifo baada ya kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, waliofanikiwa kupora mfuko wa fedha unaosadikiwa kuwa na zaidi ya shilingi milioni 30.

Tukio hilo, lilitokea jana mchana majira ya 8:30 katika Mtaaa wa Mlandege Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo majambazi hao walimvamia mmoja wa wafanya biashara wa Mchele hapa nchini aliyetambulika kwa jina la Salum Issa Suleiman (50), Mkaazi wa Baghani Mjini Unguja ,, ambaye walimpora mfuko wake wa fedha hizo wakati akiwa njiani kuzipeleka benki.

Mfanyabiashara wakati akiwa njiani alijikuta akizingirwa na mojaya gari ndogo na kuanzakushambuliwa kwa risasi ambazo zilimjeruhi sehemu zake za miguuni na ghafla kuanguka na ndipo majambazi hao walipowezakufanikiwa kumpora fedha hizo.

Wakati tukio hilo likitokea mmoja wa askari  polisi wa Kituo cha Malindi Sajenti Hija Hassan Hija, alijaribu kupambana namabambazi hao, lakini alishindwa kufanikiwa baada na yeye kujeruhiwa sehemu ya mkononi na mguuni kutokana kushambuliwa kwa risasi.

Wakizungumza na gazeti hili, waathirika wa tukio hilo,  Mfanya biashara Salum alisema, wakati alipokuwa akielekea maeneo ya Benki hiyo  ndipo ilipotokea gari ndogo mbele yake na kumnadia mwizi na hapo ndipo walipompiga risasi ya mguu wa kulia na kumnyang’anya fedha hizo na kuondoka nazo .

Kwa upande wake askari Hija alisema, alipofika maeneo hayo ndipo alipomkuta Mfanyabiashara huyo akiwa katika harakati za kujinasua na  hali  na ndipo askari huyo alipokwenda kumuokoa lakini na yeye alishambuliwa na majambazi hao na kufanikiwa kuondoka na kitita hicho cha fedha zamfanyabiashara huyo,

Hata hivyo,  majeruhi hao bado wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali kuu ya Mnazi mmoja na hali zao walieleza kuwa zinaendelea vizuri.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi,  Mkadam Khamis Mkadam, alisema ni kweli tukio hilo limetokea  na aliyeporwa fedha hizo ni  Mfanyabiashara   wa Mchele katika maeneo ya Bandarini ambae alikuwa akielekea katika Benki ya PBZ tawi la Mlandege.

Alisema mfanyabiashara huyo alikuwa na fedha zenye thamani ya shilling milioni 30,6,00,000, ambazo ni mali ya tajiri wake anafahamika  kwa jina la Yussuf Mohamed, ambazo alikuwa anakwenda kuziweka katika Benki hiyo.

Hata hivyo, Kamanda Mkadam, alitoa wito kwa Wananchi wakati wanapokwenda kuweka pesa kuacha kwenda kwa miguu na kuwatumia askari kwani askari wapo kwa ajili yao ili kuimarisha usalama wa raia.

Shirika la UNFPA Yakabidhi magari ya Wagonjwa Zanzibar.

Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Rashid Seif wakati akilijaribu moja ya gari hilo zilizotolewa na UNFPA katika hafla ilizofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Na RAMADHANI ALI /MAELEZO ZANZIBAR

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) limekabidhi  msaada wa magari manne ya Ambulance  kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar ambayo yatatumika katika Hospitali nne.

Mwakilishi wa UNFPA Tanzania  Dkt. Natalia Kanem alimkabidhi Waziri wa Afya Rashid Seif Suleiman magari hayo katika sherehe zilizofanyika   Wizarani Mnazimmoja.

Dkt. Natalia alitaka  magari hayo yatumike kwa uangalifu ili  kufikia malengo ya millennia  ya kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto wanaozaliwa hasa katika maeneo ya vijijini.

Alisema moja ya sababu inayopelekea vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga ni tatizo la usafiri ambalo linachangiwa na uwezo mdogo wa baadhi ya familia hasa katika maeneo ya vijijini.

Aliongeza kuwa  msaada huo ni  sehemu ya Mpango maalum wa Shirika la Umoja wa  Mataifa  ulioanza  mwaka 2011 na kumalizika Juni 2015  ambao  huenda ukaendelea hadi mwaka 2016 kusadia  masuala ya Afya na Lishe.

Amesema  mpango huo wa miaka minne  ambao unahusisha maeneo  makuu saba unaendeshwa kwa pamoja na Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa  ambayo ni WHO, UNFPA, UNICEF na WFPA.

Mwakilishi huyo wa UNFPA amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Jakaya Mrisho Kkwete na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Muhamed Sheina kwa juhudi kubwa wanazochukua katika kuimarisha huduma za  mama wajawazito na watoto wachanga.

Aliesema UN inathamini juhudi hizo na  juhudi za kuimarisha uchumi hivyo aliahidi  kuwa wataendelea  kuunga mkono kuhakikisha mama wajawazito na watoto wanaozaliwa wanaendelea kuishi katika mazingira yaliyo  salama.

Waziri wa Afya  Rashid Seif Suleiman, alilishukuru Shirika la UNFPA kwa misaada mbali mbali inayotoa kwa Wizara hiyo  na ameahidi kuwa magari hayo yatatumika katika malengo yaliyokusudiwa.

Amekiri kuwa tatizo la usafiri kwa  mama wajawazito Zanzibar limekuwa likiwasumbua wananchi wengi na inafikia wakati akinamama hujifungua wakiwa kwenye gari  wakati wa kupelekwa Hospitali ambazo hazina stara wala hazifai kwa kazi hiyo.

Alieleza matarajio  yake kuwa tatizo hilo kwa sasa litapungua kwa kiasi kikubwa baada ya kupatiwa msaada huo ambao umekuja wakati muwafaka ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaelekeza juhudi zake kuimarisha  huduma za afya mijini na vijijini.

Gari hazo za ambulance ambazo zitapelekwa katika Hospitali ya Kivunge, Mwembeladu, Mkoani na Micheweni zimegharimu shilingi milioni 245,000,000 za kitanzania.

CHANZO: ZANZINEWS.

Sitta apokea meseji za matusi

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh. Samuel Sitta.
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta amesema anapokea meseji za simu zaidi ya 50 kwa siku za kumtukana na kusisitiza ataendelea kupambana kuhakikisha Katiba inayopendekezwa inapatikana.

Sitta alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana wakati akielezea kutoridhishwa kwake na kile alichodai ni namna hukumu ya kesi iliyofunguliwa na Saed Kubenea inavyopotoshwa na wanaomchukia.

“Kuna baadhi ya vyombo vya habari wananichukia mimi binafsi. Wasichanganye chuki hizo na mchakato wa Bunge Maalumu,” alisema Sitta na kuongeza;

“Mimi napokea matusi kila siku. Meseji zisizopungua 50 viongozi wa Chadema wameweka namba zangu katika tovuti nitukanwe kila siku hilo mimi niko tayari na mnaniona niko safi tu wala sihangaiki nalo.”

“Lakini sasa Bunge Maalumu ni chombo cha kikatiba,  kiko tofauti na mwenyekiti wake. Huwezi kuliadhibu Bunge Maalumu kwa sababu hupendi sura ya mwenyekiti wake,” alisema.

Sitta alienda mbali zaidi na kusema, “Kwa hiyo wale wanaoendeleza hayo mapambano tuendelee na tutaendelea kupambana, lakini kazi ya Bunge Maalumu itaendelea na ndugu zangu Watanzania mjue tunaandaa Katiba safi na rafiki kwa wananchi na itapatikana.”

Sitta alisema baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo ya kesi ya Kubenea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kumekuwa na tafsiri alizosema ni potofu.

Baada ya maelezo hayo alimpa ruksa AG, Jaji Frederick Werema kutoa ufafanuzi.

Jaji Werema alisema Mahakama Kuu, katika kutafsiri kifungu cha 25(1) (2) inakiri kwamba kuna tofauti kati ya kifungu kilichoandikwa Kiswahili na kile kilichoandikwa Kiingereza.

Alisema Mahakama Kuu katika hukumu hiyo imesema mamlaka ya kuandika Katiba Mpya ina maana ni mamlaka ya kuandika na kupitisha katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

CHANZO: MWANANCHI.

Jaji Warioba: Tutakutana mtaani

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 19 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dar es Salaam jana.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya mageuzi.

Akiyataja mambo hayo muhimu ambayo ni maadili ya viongozi wa umma,  madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na muungano. “Tutakutana mtaani. Tume tutaendelea kutetea rasimu yetu na wao wawaeleze wananchi kwa nini wameondoa maoni yao yaliyokuwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba,” aliongeza kwa ufafanuzi Jaji Warioba.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema rasimu hiyo inatofautiana kwa kiasi kikubwa na rasimu iliyotolewa na tume hiyo Desemba mwaka jana.

“Sina hakika kama tutapata Katiba Mpya labda Katiba iliyoboreshwa. Rasimu au Katiba itakayopendekezwa na Bunge Maalumu haitapigiwa kura hadi 2016. Sina hakika kama kura hiyo itapigwa kwa kuwa hakuna maridhiano hasa kuhusu muungano,  rasimu hiyo itaanza kupingwa tangu siku ya kutolewa kwake,” alisema.

Aliongeza, “Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka kesho Katiba Mpya itakuwa agenda, na agenda hiyo inaweza kuigawa nchi. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mwaka 2016 badala ya kupiga kura mchakato ukaanza upya.”

Jumatano wiki hii Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge aliwasilisha rasimu hiyo bungeni na kueleza kuwa kamati yake imefuta ibara 28 zilizokuwa katika rasimu ya Jaji Warioba na kuacha ibara 47, kuongeza ibara 42 na kurekebisha ibara 186.

Alisema rasimu hiyo ina sura mpya mbili ambazo ni Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi, Maliasili na Mazingira ambayo haikuwekwa katika rasimu ya Warioba kwa kuwa si mambo ya muungano.

Rasimu hiyo ilirejesha muundo wa Serikali mbili kama ilivyo sasa na kutupilia mbali muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.

Huku akiwa makini, Jaji Warioba ambaye alitumia saa 1:02 kufafanua umuhimu wa mambo manne yaliyoachwa katika rasimu iliyotolewa na Bunge la Katiba, alisema hivi sasa wajumbe wa Bunge la Katiba wana msemo wao kuwa “Warioba ni shida”, kufafanua kuwa watakapomaliza vikao vya Bunge hilo Oktoba 4, mwaka huu na kurejea mtaani walipo wananchi ndiyo watajua nani ni ‘shida’, kati yake na wao.

Akizungumzia kitendo cha Bunge hilo kubadili kanuni ili kuruhusu wajumbe wake kupiga kura za kupitisha rasimu hiyo kwa baruapepe (e-mail) na nukushi (fax) wakiwa nje ya nchi, Jaji Warioba alisema, “Utaratibu huu hauwezi kutuletea Katiba ya maridhiano. Hata mimi nimeanza kukata tamaa.”

Huku akishangiliwa kila mara na mamia ya watu waliohudhuria kongamano hilo, wakiwamo wasomi na baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema kila mjumbe wa tume hiyo alikuwa na mawazo yake juu ya Katiba, lakini waliweka kando mawazo yao baada ya kusikia kauli za Watanzania juu ya Katiba wanayoitaka.

Katika maadhimisho hayo,  Jaji Warioba pia alizindua kitabu cha marehemu Dk Sengondo Mvungi kiitwacho ‘Mvungi anapumua Katiba’. Dk Mvungi  aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Katiba na mmoja wa waanzilishi wa LHRC, alifariki dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini alikopelekwa kutibiwa baada ya kujeruhiwa na majambazi akiwa nyumbani kwake.

Maadili ya Viongozi wa umma
Kuhusu maadili ya viongozi wa umma alisema, “Wananchi walitoa maoni mazito kuhusu maadili ndani ya jamii na maadili ya viongozi. Kutokana na maoni ya wananchi Tume iliimarisha misingi mikuu ya taifa iliyo katika Utangulizi wa Rasimu. Misingi iliyo katika katiba ya sasa ni uhuru, haki, udugu na amani.”

Alisema kutokana na maoni ya wananchi misingi mipya iliongezwa ambayo ni;  utu, usawa, umoja na mshikamano na kwamba wananchi pia walipendekeza tunu za taifa ziwekwe kwenye katiba ambazo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa (Kiswahili ).

“Bunge Maalumu limeondoa uadilifu, uzalendo, umoja, uwazi, na uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za taifa na kuziweka kwenye misingi ya utawala bora. Kila Mtanzania anatakiwa awe mzalendo, kila Mtanzania anatakiwa kuwa mwadilifu, kila Mtanzania anatakiwa aenzi umoja. Inakuwaje mambo haya yahusu utawala tu?” alihoji.

Alisema tunu za taifa ndiyo msingi wa utamaduni na maadili ya taifa, kwamba mwelekeo wa taifa utategemea jinsi wananchi wanavyoenzi misingi mikuu na tunu.

Aliponda kitendo cha Bunge la Katiba kutoweka miiko ya uongozi kwenye Katiba wakati kila siku viongozi wanalalamika juu ya rushwa na ufisadi, pamoja na fedha za umma kuwekwa kwenye akaunti za benki nje ya nchi.

“Katika bara la Afrika, nchi kama Afrika Kusini, Namibia na Kenya zimeweka misingi ya maadili na miiko katika Katiba. Hapa kwetu sheria tulizonazo haziwezi kupambana na rushwa na ufisadi. Sijui kwa nini Bunge la Katiba wameondoa hili,” alisema.

Madaraka ya Wananchi
Jaji Warioba alipinga kitendo cha Bunge la Katiba kuondoa kipengele cha wananchi kuwa na madaraka ya kumwondoa mbunge wao kama hawaridhishwi na uwakilishi wake bungeni, mbunge kutokuwa waziri ili aweze kuwawakilisha vizuri na ukomo wa mbunge kuwa vipindi vitatu .

“Bunge lina kanuni za kuwawajibisha wabunge na wananchi nao wanapenda kuwa na madaraka hayo. Vyama vya siasa vina madaraka ya kuwaondoa wabunge wao katikati ya kipindi. Wananchi nao wanataka watumie madaraka yao,” alisema.

Mgawanyo wa madaraka
Akizungumzia mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya Bunge, Serikali na Mahakama, alisema pendekezo lao la kumwondoa rais na mawaziri kutoka kwenye Bunge linakataliwa kwa sababu nchi imezoea mfumo wa kibunge kama ilivyo kwa nchi nyingi za jumuiya ya madola.

“Siyo kweli kwamba mfumo wetu ni wa kibunge. Kwenye mfumo wa kibunge mkuu wa nchi hana madaraka ya utendaji. Madaraka hayo yako mikononi mwa Waziri Mkuu ambaye ni mbunge. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Uingereza, India, Canada, Australia, New Zealand,” alisema.

Akitolea mfano mwingiliano huo alisema wakati wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, bunge lilitunga sheria lakini baadaye Rais alifanya mazungumzo na watu nje ya bunge na baadaye bunge likalazimika kubadili uamuzi.

 “Tanzania ina mfumo wa urais ambapo rais ni mkuu wa nchi, mtendaji mkuu na amiri jeshi mkuu. Rais na mawaziri wake kuwa sehemu ya bunge ni kuchanganya mamlaka. Hali hii inafanya Serikali kuingilia mamlaka ya bunge na pia bunge kuingilia mamlaka ya Serikali,” alisema.

Aliongeza, “Nchi nyingi zimebadili Katiba zao ili kutenganisha madaraka ya mihimili. Jirani zetu wa Msumbiji na Kenya wamefanya hivyo. Kenya imefanya hivyo na sababu zao zinafanana kabisa na zile ambazo wananchi wa Tanzania walitoa.”

Muungano
Huku akitaja kero 20 za muungano, 11 za Zanzibar na 10 za Tanzania Bara zilizotajwa na wananchi wakati wa kukusanya maoni, Jaji Warioba alisema, “Ingawa Rasimu ya Bunge Maalumu limerudisha madaraka ya rais kuigawa nchi hiyo peke yake haitoshi. Mambo haya ni magumu kubadilika kwa upande wa Zanzibar.”

Aliongeza kuwa ili kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar ni lazima mabadiliko yapitishwe kwa theluthi mbili au zaidi ya Wawakilishi.

CHANZO: MWANANCHI.

Friday, 26 September 2014

Balozi Seif akanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti la Mtanzania

2. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo m bali mbali nchini hapo katika Ukumbi wa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.
Na Othman Khamis OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekanusha Habari  iliyochapishwa katika Gazeti litolewalo  kila siku la Mtanzania iliyotolewa siku ya Jumatano ya tarehe 24 Septemba, 2014 likiwa na  Kichwa cha Maneno kisemacho

“SIRI ZAVUJA ZA AG ZANZIBAR KUJIUZULU “.
Kanusho hilo limetolewa na Makamu  wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa Vyombo mbali mbali vya Habari katika Ukumbi wa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.

Balozi Seif  alisema Serikali inakanusha suala la sintofamu lililoandikwa na gazeti hilo ambayo imedai kwamba Viongozi wa juu wa CCM walikutana kwa dharura na kuazimia kufukuzwa kazi kwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ  kwa kile walichodai kwamba amekisaliti Chama cha Mapinduzi

Alifahamisha kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatakiwi kuwa muumini wa Chama chochote cha siasa na ndio maana hata vikao vya chama hatakiwi kuhudhuria.  Hivyo uteuzi wa Kiongozi huyo anayesimamia masuala ya kisheria hufanywa na Rais wa Zanzibar ambae ndie mwenye maamuzi ya kumuweka na kumuondoa.


Akigusia hoja 17 za Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alizotaka ziingizwe katika Katiba Balozi Seif alisema suala hilo ni kweli na Mjumbe huyo alitakiwa aziwasilishe katika Kamati jambo ambalo alilitekeleza.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziar alielezea faraja yake kutokana na masuala hayo kuingizwa katika Rasimu ya Katiba ambapo hadi sasa Hoja 4 kati ya hoja hizo 17 bado zinafanyiwa kazi.

Alieleza kwamba kuchaguliwa kwa Mjumbe katika Kamati na kukataa kuhudhuria kama alivyofanya Mwanasheria Mkuu huyo wa SMZ ni maamuzi yake binafsi kwa vile hakuna ulazima wa mjumbe kuchaguliwa huko ikaonekana kama kifungo ingawa atakuwa na wajibu wa kuendelea kufanya kazi katika kamati hadi mwisho wake.

Balozi Seif alisema kwamba Mh.Othman Masoud alitakiwa ashiriki katika kamati kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wa Zanzibar.

Alisema hata hivyo kutokuwemo kwake katika kamati sio kikwazo cha kupatikana kwa rasima ya katiba, kwa vile waliokuwamo ndani ya kamati kwa upande wa Zanzibar walitosheleza kuiwakilisha Zanzibar kikamilifu.

Akigusia upotoshaji mwengine ulioandikwa na gazeti hilo la Mtanzania juu ya masuala 17 aliyotaka Mwanasheria Mkuu wa SMZ yaingizwe katika Rasimu ya Katiba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Taarifa hiyo si ya kweli kabisa.

Balozi Seif alisema Mawaziri wa Chama cha Wanachi {CUF } hawamo katika Bunge Maalum la Katiba sasa inakuaje washiriki kuchangia masuala ambayo wao kama sehemu ya { Umoja wa Katiba ya Watanzania } UKAWA hawakubaliani na kuendelea kwa Bunge hilo.

“Wapo baadhi ya waandishi wa Habari hawafahamu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendeshwa katika Mfumo wa Umoja wa Kitaifa ulioundwa na Vyama vya CCM na CUF na kama inavyoeleweka CUF hawamo ndani ya Bunge hilo sasa itakuaje washiriki kuchangia masuala hayo? “ Aliuliza Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba suala hilo liliripotiwa sambamba na upotoshaji mwengine wa gazetui hilo la mwanasheria huyo kuwasiliana na Rais wa Zanzibar alisema ni uzushi mtupu usio na maana.

Alisema Mh. Othman Masoud kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wowote na uwezo wa kuwasiliana na Rais au Makamu wa Pili wa Rais kwa mashauriano ya jambo lolote analoona linafaa.

Balozi Seif alithibitisha wazi kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati anaamua kujiuzulu wadhifa wa Ujumbe wa Kamati ya Uandishi Rais wa Zanzibar Dr. Shein alikuwa nje ya Nchi kwa kiziara rasmi ya Kiserikali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi pamoja na Chama cha Mapinduzi bado kinawaamini wana Habari wa vyombo vyote, hivyo amewaomba waandhishi kujiepusha na tabia ya kuzusha baadhi ya mambo ambayo hayana ukweli wowote.

Balozi Seif aliwataka Wana Habari wote Nchini kujitahidi kutumia kalamu zao vyema kwa kuwaelimisha wananchi masuala ya ukweli badala ya kuwapotosha kwa kuwalisha mambo ya kubabaisha.

Akijibu baadhi ya maswali ya wana Habari hao Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitegemei kuchukuwa hatua yoyote ya kisheriaadhidi ya Gazeti hilo. Lakini ikauomba Uongozi wa Gazeti hilo kuzingatia maadili ili kuendelea kutoa Habari zenye usahihi.

Wakati mwengine tunaelewa kwamba kalamu za waandishi huwaponyoka wakati wanapoandika Habari zao. Lakini kuponyoka huko kusiwe ndio muendelezo wa uchapishaji wa Habari zisizo na nuchunguzi “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameiasa mitandao ya kijamii kujiepusha na tabia ya kuendeleza vitisho wanavyovielekeza kwa wajumbe wa Kamati za Bunge Maalum la Katiba hasa kutoka Zanzibar kwa visingizio vya kuizamisha Zanzibar.

Balozi Seif alisema kilichofanyika na kuendelea kufanywa na Kamati hizo chini ya Bunge hilo ni kutekeleza jukumu walilokabidhiwa na watanzania na inapaswa kuheshimiwa na kila Mwanadaamu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wajumbe wa Kamati hizo kwamba Serikali kupitia vyombo vya Dola vitazingatia usalama wao na vitakuwa tayari wakati wowote kumchukulia hatua za kisheria mtu ye yote atakayetishia maisha ya wananchi wakiwemo wajumbe hao.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed aliwaeleza Wanahabari hao wa vyombo mbali mbali Nchini kwamba Katiba ni mchakato ambao masuala yote yanafanyiwa uhakiki wa kina.

Mh. Aboud alifahamisha kwamba suala lolote zito linalohusu mambo ya Muungano haliwezi kutekelezwa bila ya kuhusishwa viongozi na wataalamu wa pande zote mbili.