Tuesday, 4 November 2014

Makonda ajitetea

Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Paul Makonda anayeshutumiwa kuchafua hali ya hewa kwenye kongamano la katiba
Wakati wanasiasa na mitandao ya kijamii ikimlaani Katibu wa uhamasihaji wa Jumuia ya Vija CCM (UVCCM) Paul Makonda, kiongozi huyo jana aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema hakumpiga Jaji Warioba, bali alikuwa akimwokoa katika vurugu hizo.

Makonda alisema baada ya vurugu hizo kutokea, aliamua kumwokoa Mjumbe wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, Amon Mpanju na Jaji Warioba ili wasijeruhiwe kwenye vurugu hizo. Picha zilizochapishwa jana zilimwonyesha Makonda akiwa amemshika Jaji Warioba.

“Nilipoingia ukumbini nilikwenda kukaa jirani na Mpanju, baada ya kutokea vurugu nikaona ni lazima nimwokoe kwa sababu ya ulemavu wake wa kutokuona. Jaji Warioba alituona na akanisogelea akaniambia nisimwache Mpanju asije akapata matatizo. Kwa hiyo nikawa niko karibu na Mpanju na Warioba ili kuhakikisha kuwa wanakuwa salama.”

“Warioba ni kama baba yangu, kamwe siwezi kunyanyua mkono wangu na kumpiga, nitakuwa ninajitafutia matatizo, huu ni mchezo mchafu unaochezwa na baadhi ya wanasiasa wenye lengo la kunichafua.

“Leo (jana) asubuhi Warioba amenipigia simu akinipa pole kwa vurugu hizo, nami nikampa pole kwa yote yaliyotokea jana, sasa inakuwaje mtu uliyempiga halafu akakupigia simu ya kukupa pole?” alisema Makonda.

Hata hivyo, Jaji Warioba hakupatikana jana kuzungumzia nini hasa kilitokea kati yake na kada huyo wa CCM ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bunge la Katiba.

CUF kulinda midahalo
Chama cha Wananchi (CUF) kimelaani kitendo cha kufanyiwa vurugu kwa Waziri Mkuu mstaafu wa jamhuri ya Muungani wa Tanzania Jaji Joseph Sinde katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation juu ya Katiba inayopendekezwa katika ukupi wa Hoteli Ubungo Plaza jijini Dar es salam juzi.

Mbali ya kulaani kitendo hicho, kimekwenda mbali na kikisema kinachukua dhamana ya kuilinda midahalo yote itakayomhusu Jaji Warioba, waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko Katiba na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), kwa nia njema ya kutoa elimu ya uraia juu ya Katiba Inayopendekezwa.

Taarifa ya Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Abdul Kambaya ilisema chama hicho kimeamua kuchukua dhamana hiyo kwa kuwa polisi wameshindwa kutekeleza wajibu wao.

“Jaji Warioba ni kiongozi wa Taifa hili, hivyo kwa namna yoyote ile hawezi kudhalilishwa huku CUF kama wadau wa mambo ya siasa na elimu ya uraia tukiwa kimya,” ilisema taarifa hiyo ya Kambaya.

Kauli ya Polisi
Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba alisema bado viongozi wastaafu wanapatiwa ulinzi wa kutosha lakini hakutaka kufafanua zaidi vigezo vinavyoangaliwa kwa kile alichoeleza kuwa ni sababu za kiusalama,” alisema.

Mwaka 2009 Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi alipigwa kibao shavuni alipokuwa akihutubia katika Baraza la Maulid.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema watu kadhaa ambao hata hivyo hakuwataja kwa majina wala idadi, walihojiwa ili kujua chanzo cha vurugu hizo na kuwa uchunguzi unaendelea.

Chanzo: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment