Sunday, 2 November 2014

Maalim Seif: Mabadiliko katika nchi huletwa na vijana


Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu Zanzibar wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad (hayupo pichani) katika kongamano lililo andaliwa na Jumuiya yaq Vijana ya CUF (JUVICUF) katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani.

Na Nassor Khamis.
Vijana wa vyuo vikuu nchini wametakiwa kuwa mstari mbele katika kuleta mabadiliko Zanzibar hasa katika Nyanja za za kiuchumi na kijamii kutokana na nafasi walionayo katika jamii.


Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizungumza na wawakilishi kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu Zanzibar kwenye Kongamano lililoandaliwa na Jumuia ya Vijana wa chama hicho (JUVICUF)  katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.


Kongamano hilo lililoandaliwa kueleza nafasi ya wasomi vijana katika mabadiliko na maendeleo ya jamii Maalim Seif alisema vijana wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko iwapo wataamua kutumia taaluma zao kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na taifa.


Alisema kuwa, mabadiliko katika nchi nyingi duniani huletwa na vijana wakiongozwa na wasomi wa fani mbalimbali hivyo na Zanzibar vijana wana nafasi ya kuleta mabadiliko hayo kutokana na asilimia 65 ya Wazanzibari kuwa ni vijana.


“Nchingi duniani vijana ndio walioleta mabadiliko kutokana nafasi zao hata Uingereza kabla ya kuitwala Zanzibar kwa mara ya kwanza walimtuma kijana mwenye umri chini ya miaka 20 kuiendesha Zanzibar na alifanikiwa” alisema Maalim Seif.


“Nahata Ujarumani nao walimtuma kijana wao Kall Peters Barani Afrika kuingia mikataba ya ukweli na uwongo na Machifu na hatimae Ujarumani kupata maendeleo, na nyinyi vijana munayo nafasi ya kuleta mabadiliko hapa Zanzibar” aliongeza Maalim Seif.


Maalim Seif alisema historia inayonesha harakati zinazosimamiwa na kuongozwa na vijana mara zote hupata mafanikio makubwa na ndio maana hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliongoza vyema TANU hadi kuleta Uhuru wakati huo ambapo alikuwa ni kijana shababi.


Alieleza kuwa mbali na Mwalimu, hata Waziri Mkuu Mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim alipewa Ubalozi nchini Misri na marehemu Mzee Karume akiwa na umri wa miaka 22 na alifanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa, mbali na yeye (Maalim Seif) pamoja na vijana wengine ndani ya CCM ambao waliweza kukitikisa chama hicho na kuleta mabadiliko makubwa wakiwa vijana.


Pia aliwataka vijana hao kuwa mstari wa mbele katika kuipinga katiba inayopendekezwa kutokana kuwa na maslahi na CCM badala ya wanachi na haiwakilishi maoni ya Watanzania pia haiinufaishi Zanzibar katika Muungano.


Alisema kuwa jambo kubwa lililopo mbele hususan kwa vijana ni kuipinga rasimu ya katiba inayopendekezwa pamoja na kujiandaa kuing’oa CCM madarakani ifikapo 2015.


 “Vijana wasomi nyinyi ndio wenye maamuzi kwa nchi yenu, mkiamua mnataka kitu gani ndicho kitakacho kuwa, tushirikiane kupiga kampeni ya Hapana kwa Katiba inayopendekezwa yenye maslahi na CCM na sio ya wananchi”, amehimiza Maalim Seif.


Maalim seif ambae pia ni Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema anafurahishwa kuona vijana wa Zanzibar wako mstari mbele katika kutetea hadhi na maslahi ya nchi yao kuliko wazee huku kasi ya vijana kudai mamlaka Zanzibar ikizidi kuimarika.


Alisema kuwa kuipigia kura ya ya ndio Katiba inayopendekezwa ni kuhalalisha Muungano usio na uhalali tokea kuasisiwa kwake kutokana na kukosa ridhaa ya Wazanzibari kupitia Baraza la Mapinduzi la wakati huo.


Licha ya kuuhalalalisha muunagano huo pia ni kuzidi kuikandamiza Zanzibar kutokana na Katiba hiyo haikuzingatia maslahi ya Zanzibar.


Akiizungumzia katiba inayopendekezwa Maalim Seif alisema enadapo katiba hiyo itapitishwa kwa njia yoyote hile italeta mgogoro wa kikatiba kati ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hile ya Zanzibar kutokana na kugongana kwa baadhi ya vifungu ndani ya katiba hizo.


Alisema kuwa mgogoro huo utasababisha kufanywa kwa mabadiliko katika ya Zanzibar jambo ambalo halitowezekana kutokana masharti ya katiba hiyo kuhitaji theluthi mbili ya watakaokubali kufanya mabadiliko na wawakilisha wa CUF hawatokuwa tayari kufanya mabadiliko hayo.


Akizungumza katika Komangamano hilo Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Mh, Ismail Jussa Ladu alisema wimbi la Mageuzi linaloikumba Zainzibar haliwezi kuzuilika kutokana na Wazanzibari wote kudai mamlaka kamili ya nchi yao na atakae jaribu kulizuia hatofanikiwa.


Aidha alielezea kusikitishwa kwake na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliokuwa wakitetea hadhi ya Zanzibar katika baraza la Wawakilishi na badala yake kugeuka kwa kuendelea kuikndamiza Zanzibar karika Bunge Maalum la Katiba.


Alisema Wazanzibari hawawezi kukubali kuporwa heshima na hadhi ya nchi yao ambayo kwa miaka mingi nyuma imekuwepo, hadi kufikia hatua ya kuwa ni Himaya (Empire), lakini heshima hiyo imkuwa ikifutwa kidogo kidogo hadi sasa kuelekea kuwa Zanzibar ni kama vile Manispaa tu.


Nae Makamo Mwenyekiti wa Jumuia ya Vijana CUF taifa Nd, Yussuf Kaiza Makame alisema huu si wakati tena wa vijana wa vyuo vikuu kukubali vitisho vya aina yoyote vikiwemo kukosa ajira baada ya kumaliza masomo yao badala yake wawe mstari wa mbele katika kutetea hadhi ya nchi yao.


“Sasa umefika wakati kwa vijana wasomi wa vyuo vikuu kupigania maslahi na hadhi ya nchi yao katika muungano na huu si wakati wa kutishana tena” alisema Nd, Kaiza.


Mapema katika risala yao wanafuzi wa vyuo vikuu mbalimbali Zanzibar iliyosomwa na Hafidh Ali Hafidh walisema walifarijika baada ya Rais Kikwete kuitisha mchakato wa Katiba mpya kwa kuona ni wakati muafaka kwa Zanzibar kupata haki zake katika Muungano na baadae wamefadhaishwa baada ya yaliyotokea kwenye Bunge Maalum la Katiba.


Walisema kuwa Bunge Maalum la Katiba wamepitisha Katiba kinyume na matarajio ya Wananchi wengi wa Tanzania kwa kupitisha mfumo wa serikali mbili katika muundo wa Muungano bada la ya hule wa serikali tatu uliopendekezwa na Wananchi.


Walisema kwamba kitendo walichokifanya wana CCM ni uhalifu mkubwa na ni ubaguzi mkubwa ambao hawakubaliani nao na Katiba wanayoipendekeza haifai na wao watakuwa mstari wa mbele kuendesha kampeni ya Hapana.


Hafidh alisema kwa Katiba inayopendekezwa hatma ya Zanzibar imewekwa katika Kuti Kavu na sasa inadhihirika wazi wapo baadhi ya watu wanataka Zanzibar ifutike kabisa katika ramani ya Dunia, jambo ambalo Wazanzibari wazalendo hawatalikubali.


“Wenzetu hawa wamezowea vya kunyonga kamwe vyakuchinja hawaviwezi, tutaitetea Zanzibar kwa vyovyote itakavyo kuwa, tutapita kila kona kuhamasisha vijana waikatae Katiba hiyo inayojali maslahi ya wachache”, wamesema katika risala hiyo.


Katika Kongamano hilo vijana wapatao 380 kutoka vyuo vikuu mbalimbali na taasisi za elimu ya juu Zanzibar walijiunga na Chama cha Wanachi CUF na kupewa kadi za uanachama hapohapo na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad.

No comments:

Post a Comment