Jaji Joseph Sinde Warioba akitolewa nje ya ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salam baada ya kuzuka kwa vurugu katika ukumbi huo jana. |
MDAHALO wa kujadili Katiba inayopendekezwa ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, jana ulivunjika baada ya kutokea vurugu ambako Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipigwa vibao shingoni na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa CCM.
Hali hiyo ilijitokeza kwenye Hoteli ya Blue Pearl iliyopo Ubungo Dar es Salaam, baada ya kuvunjika mdahalo huo uliokuwa umehudhuriwa na mamia ya watu, wengi wao wakiwa vijana.
Baada ya vurugu hizo, waandaji waliamua kuwatoa nje ya ukumbi wasemaji wa mdahalo huo akiwamo Warioba, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Mwesiga Baregu.
Wengine waliokuwa wazungumze kwenye mdahalo huo ni Humphrey Polepole na Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadhi Said, ambao wote walikuwa wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Warioba, aliyewahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, alipigwa vibao viwili shingoni alipofika kwenye mlango kuu wa kutoka ukumbini ambako kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu. Wakati huo, Warioba na viongozi wenzake walikuwa wakitolewa nje ya ukumbi huo.
Hatua hiyo ilifanya mlinzi wake na baadhi ya watu waliokuwa wakimtoa kiongozi huyo waongeze mwendo na kumkimbiza kiongozi huyo wa taifa kwenye chumba maalumu cha wageni wa heshima (VIP lounge), kilichoko ndani ya hoteli hiyo.
Wakati Warioba akipigwa vibao, miongoni mwa watu waliokuwa karibu nyuna yake ni Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM, Paul Makonda.
Kwa sababu hiyo, baadhi ya vijana walichangia kumpiga kada huyo wa UVCCM aliyekuwa amevalia shati jeupe, huku wakimzuia kuingia kwenye chumba cha VIP ambako Jaji Warioba alikuwa amepelekwa.
Kufanikiwa kwa vijana hao kumzuia Makonda kuingia kwenye chumba hicho, kulitoa fursa ya kuendelea kupigwa hadi alipoponyoka na kukimbilia katika ofisi moja katika jengo hilo na kujifungia.
Baada ya kujificha katika chumba hicho, vijana hao waliitana na kuhamasishana ili wavunje mlango huo na kumtoa Makonda.
Hata hivyo baada kufanikiwa kuvunja mlango huo, vijana hao hawakumuona Makonda hadi walinzi wa hoteli hiyo na askari kanzu walipofika hapo na kuwafukuza.
Vurugu zilivyoanza
Vurugu katika mdahalo huo zilianza muda mfupi kabla ya Jaji Warioba aliyekuwa msemaji wa kwanza, kumaliza hotuba yake.
Baada ya kumaliza kuichambua Katiba inayopendekezwa, Jaji Warioba alisema katika kuitetae katiba hiyo, baadhi ya watu wamekuwa wakimtumia Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere kuunga mkono hoja zao.
“Tunatumia jina la Mwalimu ili kuunga mkono hoja zetu wakati mwingine ninajiuliza hivi tunatumia Mwalimu yuleyule ama…
“Mwalimu amekufa akisema hajaona hata sehemu ya kutia koma katika Azimio la Arusha, kuna watu waliwahi kumletea Mwalimu barua wakimwambia afungue akaunti nje ya nchi ndiyo fedha zake zitakuwa salama… Mwalimu siyo tu alikataa lakini alitangaza kila kitu hadharani.
“Leo Mwalimu angekuwapo angekubali watu wafungue akaunti nje ya nchi, angekubali watu wapewe zawadi wakae nazo… nikasema huyo wao siyo Mwalimu, Mwalimu alikuwa ni mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi mgumu hata unaomhusu yeye,” alisema Warioba.
Vijana na mabango
Baada ya maneno hayo, baadhi ya vijana takriban 20, walisimama na kunyanyua juu mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali wa kumtukana Jaji Warioba na mengine yakisifu Katiba inayopendekezwa.
Kitendo hicho kilifanya baadhi ya watu kujaribu kuwakalisha chini huku wengine wakichana mabango hayo hali iliyozusha vurugu.
Wakati wote huo Jaji Warioba alikuwa amesimama akijaribu kuwasihi watu hao kukaa chini, lakini hali hiyo ilionekana kutozaa matunda.
Baada ya muda vijana hao walijitenga pembeni karibu na jukwaa kuu huku wakiwa na mabango yao, wakiimba nyimbo mbalimbali za CCM.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu watoke ukumbini huku wengine wakiwa wanarudi kuketi kwenye viti vyao.
Wakati vurugu hizo zikiendelea, Profesa Kabudi na Butiku kwa nyakati tofauti, walionekana wakimtaka Makonda kuwatuliza vijana hao wa CCM ambao alidaiwa yeye yeye ndiye aliwaingiza katika ukumbi huo.
Wakati viongozi wakimtaka Makonda kufanya hayo, vijana wengine walionekana kumvuta Makonda wakitaka kumpiga hali iliyomlazima kumtumia kama kinga, Amon Mpanju, ambaye alikuwa Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba akiwakilisha kundi la walemavu.
Hali iliendelea hivyo hadi baadhi ya vijana waliokuwa wamekaa walipohamasishana na kuwapiga wale waliokuwa na mabango, kwa kutumia viti hali iliyofanya wakimbie na kutoka nje ya ukumbi huo.
Baada ya vijana hao kutoka nje, hali iliwageukia Makonda na Mpanju ambao baada ya kuona hali imekuwa tete, walikimbilia kwenye jukwaa kuu na kukaa karibu na Jaji Warioba.
Huku hali ikiwa bado ya taharuki, viongozi hao (Warioba na wenzake) waliamua kutoka nje ya ukumbi na ndipo zahama ya kupigwa vibao kwa Jaji Warioba ilipojitokeza.
Butiku: Hii ni siku ya aibu
Baada ya vurugu hizo kuisha Jaji Warioba hakurejea na badala yake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisimama na kuiita siku ya aibu kwa Watanzania.
Alisema tukio la vurugu ndani ya ukumbi wa mdahalo huo limeshuhudiwa na Watanzania nchi nzima.
“Baadhi ya wahuni waliofanya tukio hilo tunawatambua hivyo katika mikutano yetu ijayo hatutawaruhusu kushuhudia midahalo yetu,” alisema.
Butiku alisema kuwa tukio hilo halitakuwa mwisho wa kuendelea kwa midahalo ya taasisi iliyopangwa kufanyika Mwanza, Mbeya, Zanzibar na Tanga.
Jaji Warioba apata watetezi
Akizungumzia kadhia iliyotokea katika mkutano huo, mmoja wa waliohudhuria mdahalo huo, Halfan Said, alisema amesikitishwa na fujo zilizofanywa na vijana wa CCM waliofikia hatua ya kumpiga Jaji Warioba.
“Warioba kama raia mwingine wa kawaida anayo haki ya kutoa maoni yake na yanastahili kuheshimiwa na pia hakustahili kufanyiwa vurugu aliyofanyiwa na vijana hawa wa CCM ambao wameshindwa kuheshimu hata madaraka aliyowahi kuitumikia nchi hii na chama chake,” alisema.
Rudovick Mosha alisema kuonekana kwa kada wa CCM, Paul Makonda, kunaonyesha dhahiri chama hicho kilikuwa nyuma ya mpango huo mchafu wa kumfanyia vurugu Jaji Warioba katika mdahalo huo.
Katibu Mkuu wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP-Tanzania), Alphonce Lusako, alisema amesikitishwa kwa tukio la vijana wa CCM kushindwa kusikiliza hoja na badala yake kufanya vurugu.
“Inatubidi vijana nchini tufikie mahali tukatae kutumika na kusema kuwa imetosha kutumika tuweze kusonga mbele kuepusha yaliyotokea,” alisema Lusako.
Naye Pius Mchulu alisema kumpinga Jaji Warioba ni kuukomaza na kuboresha ujinga na umasikini kwa wanyonge.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya, alitoa onyo kwa kundi lililofanya tukio hilo lenye nia ya kunyamazisha sauti za watu kuwa watakuwa wamejitafutia anguko.
“Suala la kusema na kusikilizwa ndiyo demokrasia na unapozuia mwisho hautakuwa mbali kwani Mungu anawaona na mwisho wa maovu yao unakaribia.
“Aliyeandaa tukio hilo la vurugu kwa Jaji Warioba atakutana na upanga wa Mungu na hata baki salama,” alisema Nkya.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema tukio hilo limedhihirisha kwamba dola inazama kwa kuwa mbinu wanazotumia kwa sasa ni dhaifu zilizowahi kutumiwa zamani na madikteta.
Katika vurugu hizo za kurushiana viti, mwandishi wa BBC, Arnold Kayanda alijikuta akipigwa kichwani na kiti.
Mabango, nyimbo zatawala
Baadhi ya mabango ya karatasi waliyosimama nayo vijana wa CCM yalikuwa na ujumbe uliosomeka: “Katiba inayopendekezwa tumepokea na tunaiunga mkono”, “Katiba hii tumeiona, tumeielewa na tunaikubali”. Mabango mengine yalikuwa na ujumbe wa matusi kwa Jaji Warioba.
Vijana hao ambao hata hivyo hawakuwa wengi katika ukumbi huo walianza kusikika wakiimba nyimbo za CCM kwa maneno ya ‘CCM nambari wani’.
Mmoja wa vijana hao alikataa kutaja jina lake lakini alisikika akisema kuwa, “tumechoka kudanganywa na Jaji Warioba.”
Wakati zilipozuka vurugu hizo na watu wakaanza kutoka nje, polisi walikuwa wakipiga risasi hewani nje ya ukumbi lakini hawakuingia ndani kuzuia vurugu hizo.
CHANZO: MTANZANIA
No comments:
Post a Comment