Wanachama wa Chama cha Wananchi CUF wakimsikiliza Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho , Mh, Juma Duni Haji (hayupo pichani) katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Amani kwa mabata. |
Suala la wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliokuwa kwenye ibada ya Hijja katika miji ya Makka na Madina chini Saudi Arabia, kupigia kura rasimu ya katiba inayopendekezwa na Bunge hilo sikweli.
Hayo yalielezwa na Makamo mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF taifa Mh, Juma Duni Haji wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho katika viwanja vya Amani kwa mabata wilaya ya Magharibi Unguja.
Mh, Duni ambaye pia ni Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alisema, kulingana na hali ilivyokuwa katika ibada ya hijja ni vigumu kwa wajumbe hao kupiga kura kwa njia yoyote kutokana na muda wote kuwa katika ibada.
“Suala la kupigwa kura kwa njia ya mtandao ni uongo kwani hakuna hata mtu mmoja aliyepiga kura kutokana na muda wote kuwa katika ibada” alisema Mh, Duni.
“Mimi nilikuweko wakati tupo katika mabanda yetu mahujaji nilimuuliza mmoja wa wajumbe vipi ndio utapigia kura katiba hapa” aliongezaMh. Duni.
Pia alisema kuwa licha ya mahujaji hao kushindwa kupiga kura kwa njia ya mtandao, hakuna afisa yoyote aliyeweza kuendesha zoezi la upigaji kura kutokana na kutokuruhusiwa kuingia kwa mtu yoyote asiyekuwa mwenye kufanya ibada hiyo ya hijja.
Aidha amesema kuwa kutoka na mahujaji hao kutokupiga kura na wengine waliyoikata hadharani theluthi mbili ya wazanzibari ya kupitisha katiba inayo pendekezwa haikutimia.
Akizungumzia Katiba inayopendekezwa alisema, katiba hiyo haina maslahi kwa Zanzibar kwani Katiba inayopendekezwa inafuta utambulisho wa Zanzibar pamoja na kuinyima Zanzibar mamlaka yake ya kujiendesha wenyewe.
Alisema kuwa baadhi ya vipengele vinavyoonyesha kuipa mamlaka Zanzibar ni sawa na kupewa kitu kwa mlango wa mbele na kisha kunyang’anywa kwa mlango wa nyuma kwani vipengele hivyo vipo chini ya mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vipengele hivyo amevitaja kuwa ni pamoja na Zanzibar kujenga mashirikiano na mashirika ya kimataifa pamoja na uwezo wa kukopa fedha kutoka taasisi mbali mbali za kifedha hadi ipate udhamini kutoka kwa Serikali ya Muungano.
“Eti wanasema sasa Zanzibar inaweza kukopa pamoja na kujiunga na mashirika ya kimataifa baada yakupata udhamini ikiwa huo udhamini haukutolewa pamepatikana kitu hapo?” alihoji Mh, Duni.
Pia alisema kuwa kutokana katiba mpya inayopendekezwa kubainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atachaguliwa kwa kupata zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote ni vigumu kwa Mzanzibari yoyote kushika wadhifa huo kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura walioko Tanzania Bara.
Alisema kuwa ili kupata uhalali wa Rais wa Muungano, Katiba inayopendekezwa iweke kifungu kinacho onesha kiwango maalum cha kura kutoka kwa wapiga kura wa pande zote za Muungano.
Mh. Duni pia alizungumzia vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji unaofanywa na jeshi la polisi kwa watuhumiwa makosa ya ugaidi huku viongozi wa serikali wakikaa kimya, ni kushindwa kusimamia haki za wananchi wanaowaongoza.
Akitolea mfano wa vitendo vya udhalilishaji kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali yaliyowahi kufanyika huko nyuma askari waliofanya vitendo hivyo walichukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufukuzwa kazi.
Amesema kuwa wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza wa Jamhuri Muungano wa Tanzani vitendo vya udhalilishaji wa watuhumiwa waliokuwa mahabusu jijini Mwanza Mwalimu Nyerere aliwawajibisha maafisa wa jeshi la polisi kwa kuwafukuza kazi huku aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani wakati huo Mzee Ali Hassan Mwinyi kulazimika kujiuzulu wadhifa wake.
“leo wanakuja raia mahakamani wanaonesha suruali zinavyovuja chini kutokana na vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa na Polisi wewe husemi kitu Rais gani wewe” alisema Mh. Duni.
Aidha mh, Duni ametaka sheria zilizotungwa zifuatwe kama inavyostahiki pamoja na kuheshimiwa na watu wote.
Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mh, Nassor Ahmed Mazruy alisema kifungu cha thalathini na nne cha sheria ya mabadiliko ya katiba inayosema kuwa katiba inayopendekezwa itapitishwa kwa zaidi ya asilimia hamsini ya kila upande kimelenga kuchakachua kura za maoni ya kupitishwa kwa katiba hiyo.
Alisema kuwa kifungu hicho pia kinawataka Wazanzibari walioko Tanzania Bara kupiga kura upande wa Zanzibar jambo ambalo haliingia akilini na ina lengo la kuvuruga idadi ya wazanzibari ili waweze kupitisha katiba hiyo.
Aidha alisema kuwa chama cha CUF pamoja na vyama vyengine vya upinzani vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA kwa pamoja wamesaini mkataba wenye lengp la kushirikaiana katika chaguzi mbalimbali ukiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa lengo la kuindoa CCM madarakani.
Mapema Mjumbe wa Baraza kuu la Uongozi la CUF Taifa ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Ole Mh, Hamad Massoud Hamad amewataka wanachama wa chama hicho kujiweka tayari kwa uchaguzi mkuu ujao kwa lengo la kuiondoa CCM madarakani.
Amesema kuwa uchaguzi unaofuata chama cha CUF hakitofanya makosa kama chaguzi zilizopita kwa kukubali matokeo yasiyo halali yanayo tangazwa na tume ya uchaguzi Zanzibar kwa kutoa ushindi usiostahiki kwa CCM.
“Uchaguzi wa safari hii CUF haifanyi makosa kama yaliyopita viongozi wa juu tayari wameshajiandaa na nyinyi wananchi jiandaeni tuhakikishe tunaing’oa madarakani CCM ifikapo mwakani” alisema Mh, Hamad huku akishangiriwa na wanachama waliohudhuria mkutano huo.
No comments:
Post a Comment