Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wakiwa kwenye kikao cha Bunge hilo Mjini Dodoma |
Kaimu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda alisema jana: “Mawaziri
na manaibu ambao ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walioko mjini
Dodoma wanapokuwa na safari za kikazi huaga kwa Waziri Mkuu lakini jambo
la kushangaza ni kuendelea kulipwa posho wakati hawapo.”
Alisema hali hiyo husababisha Bunge hilo kuendelea kuwalipa posho
kupitia akaunti zao za benki lakini wakiwa hawapo Mjini Dodoma.
Mwakagenda alisema mawaziri hao wanapotoka kwenda kwenye shughuli
mbalimbali za kiserikali nako hulipwa posho.
“Haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma, mawaziri na manaibu
wanalipwa posho hata wanapokuwa nje ya Bunge Maalumu la Katiba,
wanaposafiri pia wanalipwa posho na Serikali,” alisema Mwakagenda.
Alisema pamoja na kwamba Ofisi Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba
imeonyesha kubana mianya kwa wajumbe kusaini bila kufanya kazi, bado
kuna ufujaji wa fedha eneo la mawaziri.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema
ruhusa za kutoka nje ya Dodoma hutolewa na Mwenyekiti wa Bunge hilo,
Samuel Sitta na kwamba wasiohudhuria huwa hawalipwi.
“Tunalipa wajumbe wanaohudhuria bungeni, kama hilo linatendeka lazima
nilifuatilie. Ninachosema kama kuna waziri amelipwa na hayupo itabidi
aturejeshee hiyo fedha. Lakini hili tatizo ni gumu kwa sababu mtu
analipwa na tunajua yupo kumbe pengine hajaingia katika vikao,” alisema.
Alisema kanuni za Bunge hilo zinataka mjumbe anapoondoka aombe ruhusa kwa Mwenyekiti wa Bunge na nakala kwa Katibu.
“Wakicopy (wakinakili) kwangu mimi nawaorodhesha nampelekea mhasibu,
tukikaribia kulipa namwambia hawa hawapo, kwa hiyo mtu siku ambazo
anaomba ruhusa hata kama anaumwa hatumlipi, labda awe amelazwa hospitali
ambaye tunamlipa half (nusu),” alisema.
Hata hivyo, alisema tatizo linalowapa shida kiutendaji ni kwa wale
wasioaga wanapotoka nje ya Dodoma na kwamba hilo atalifuatilia kwa
kuangalia orodha za mahudhurio kwenye vikao.
Mahudhurio hafifu
Kuhusu mahudhurio Hamad alikiri kwamba hilo ni tatizo kutokana na
baadhi ya wajumbe kutokuwa makini na kwamba mahudhurio hafifu yanaathiri
uendeshaji wa vikao hivyo.
“Kama leo nilikwenda katika kamati nikawaambia kama haupo ni haupo
tu, wengine wakasema unajua wengine walikuwa wanaumwa, nikawaambia mimi
najua hiyo ni luck of seriousness tu (kukosekana kwa umakini), hakuna
lingine. Wakanitaka niombe radhi lakini mimi nikawaambia wala siombi
radhi… Umakini mdogo… Unakuta wengine wanajadili na wengine wanaathiri
kura kwa uzembe tu, nafikiri kama kila mtu angekwenda katika vikao
tusingekuwa na shida.”
Mwakagenda alisema katika wiki mbili zilizopita, mahudhurio yamekuwa madogo katika vikao vya kamati za Bunge.
Alisema Bunge hilo limesema wajumbe 441 wanahudhuria vikao hivyo
lakini uchunguzi wa Jukata umeonyesha baadhi yao wamekuwa wakisaini tu
kitabu cha mahudhurio.
Mwakagenda alisema uchunguzi huo ulionyesha kwamba wajumbe 100 hawahudhurii kwenye kamati.
Aidha, alisema kitendo cha Bunge hilo kuendelea kupokea maoni ya
makundi mbalimbali ya kijamii ni kwenda kinyume na Sheria ya Mabadiliko
ya Kifungu namba 9 (1) ambacho alisema kinaeleza kwamba kazi ya
kukusanya maoni ni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment