Amesema haiwezekani ziwepo nchi mbili zilizoungana
halafu kila akichaguliwa rais awe anatokea upande mmoja tu wa muungano,
huku upande mwingine ukiambulia kutoa makamu wa rais.
Mbali na hilo, Maalim Seif pia ametaja sifa tano
za rais ajaye huku akisisitiza kuwa kigezo si umri, bali uwezo wake wa
kufanya kazi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili Dar es Salaam, Maalim Seif alisema: “Kama ni muungano wa nchi mbili
lazima kuwe na mfumo ambao tutajua kwamba kipindi hiki rais ametokea
Zanzibar, basi kipindi kingine rais atatoka Bara.”
Tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na
kuzaliwa Tanzania mwaka 1964, Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi ndiye pekee ambaye alitokea
Zanzibar. Aliongoza kati ya mwaka 1985-1995.
Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama
inaweza kutumika Tanzania Bara, kwa umakini Maalim Seif alisema, “Hilo
ndilo suluhisho kutokana na mivutano iliyopo Tanzania Bara. Serikali hii
inaunganisha vipaji vya watu ambao wanafanya kazi kwa pamoja.”
Sifa za rais
Huku akiwa makini na kuonyesha msisitizo wa ishara
za mikono, Maalim Seif alisema: “Kwanza rais awe na uwezo wa
kuunganisha wananchi kwa sababu ni wa Watanzania wote, kuanzia
waliompigia kura na ambao hawakumpigia kura. Asiwe na upendeleo.”
Alisema mtu akishakuwa rais lazima aweke masilahi ya chama chake pembeni na awatumikie wananchi wote.
“Pili, rais anatakiwa kuwa karibu na wananchi kwa
sababu sifa za kiongozi mzuri ni kujua hali halisi ya wale unaowaongoza,
huwezi kujua hali halisi maisha ya wananchi kama hauko karibu nao,”
alisema.
Akitaja sifa ya tatu huku akicheka, Maalim Seif
alisema rais ni lazima awe na uamuzi na kuhakikisha kuwa anawabana watu
aliowateua.
“Simaanishi rais awe dikteta. Rais unaweza kuwa na
baraza lako la mawaziri lakini lazima uwe na malengo yako. Mawaziri
wako unawaeleza wazi kwamba katika sekta fulani unataka jambo fulani
lifanikiwe, jambo hilo linapendekezwa na kujadiliwa katika kikao cha
mawaziri na hatimaye kupitishwa.”
Alisema rais ni lazima ajue kuwa jambo fulani lina manufaa au
halina manufaa na akichukua uamuzi hatakiwi kuyumba, bali kuusimamia
mpaka mwisho.
“Nne, rais anatakiwa kuwa na msimamo na akubali
kushaurika. Licha ya kuwa Katiba inaeleza kuwa rais ni mtu mwenye uamuzi
wa mwisho lakini ni lazima awe mtu anayekubali kushaurika,” alisema.
Akitaja sifa ya tano, Maalim Seif alisema urais ni
taasisi, hivyo rais ni lazima akubali kuisimamia taasisi hiyo... “Rais
anatakiwa kutambua kuwa kuna Bunge, Mahakama na Serikali na kila mhimili
unatakiwa kufanya kazi bila kuingiliwa. Ukiwa na taasisi imara hata
kama utakuwa na rais asiye na uwezo mambo yatakwenda tu.”
Maalim Seif alisema nchi kama Marekani kila mtu anaweza kuwa rais na mambo yakaenda vizuri kutokana na kuwa na taasisi imara.
Umri wa urais
“Unajua idadi kubwa ya Watanzania ni vijana na pia
lazima tujue kuwa vijana wa sasa ni tofauti na ‘vijana’ sisi.
Tunahitaji mtu mzoefu. Tusitazame ujana au uzee. Inatakiwa aangaliwe mtu
mwenye uwezo wa kuongoza watu. Tunataka rais akiwa kijana asipinge
mawazo ya wazee na akiwa mzee lazima ajue matatizo ya sasa ya vijana.”
Huku akitolea mfano wa China, Maalim Seif alisema
nchi hiyo licha ya kurekebisha masuala mengi ya uongozi mpaka sasa, Rais
na Waziri Mkuu wake ni lazima wawe wa umri zaidi ya miaka 50.
“Unajua wakati mwingine vijana wanakuwa na jazba.
Ukiwa rais hautakiwi kutawaliwa na jazba na unatakiwa kuwa na busara,
hekima na utaalamu,” alisema.
Alivyomtolea nje Sitta
Katika hatua nyingine, Maalim Seif ameeleza namna
viongozi wa Serikali ya Umoja ya Kitaifa Zanzibar, walivyojitahidi
kuunusuru mchakato wa Katiba Mpya, huku akisisitiza kuwa sasa umefikia
pabaya na ni busara tu ndizo zinazoweza kuunusuru.
Alisema aliwahi kumkatalia Mwenyekiti wa Bunge
Maalumu la Katiba, Samuel Sitta alipomfuata kutaka ushauri wake ili
kunusuru mchakato huo kwa kuwa taratibu na kanuni za Bunge Maalumu
zimevunjwa makusudi.
Alisema alimtaka Sitta kuheshimu maoni ya wajumbe
wa Ukawa wanaotokana na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ambao
walisusia vikao vya Bunge la Katiba, wakishinikiza ijadiliwe Rasimu ya
Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Mwenyekiti (Sitta) alinifuata na kuomba busara zangu katika
jambo hili lakini nikamwambia kama busara hazikutumika ni vigumu
kuzipata tena busara hizo.
Lakini maoni yangu yakawa ni yaleyale ya
kukubaliana na Ukawa ili kuona jinsi ya kupokea mawazo yao kuliko
kulazimisha kuendelea na mchakato eti kwa sababu Ukawa ni wachache.”
Maalim Seif anaamini kuwa kuandika Katiba ni jambo
la maridhiano hivyo hata watu wachache nao wana haki ya msingi katika
suala hilo na wanawawakilisha wengi.
“Hiyo ilikuwa hatua ya kwanza iliyofanyika. Hatua
ya pili ni sisi viongozi wa Zanzibar, mimi, Dk Shein (Ali Mohamed, Rais
wa Zanzibar) na Balozi Seif Ali Iddi (Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar),
tulikaa kujadili jinsi ya kusaidia jambo hili lakini hatimaye likaibuka
suala la serikali mbili au tatu na hatukupata mwafaka,” alisema.
Kuhusu nafasi ya Rais Jakaya Kikwete, huku
akicheka, Maalim Seif alisema yupo tayari kukutana naye kama akiombwa
wazungumze kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
Alipoulizwa kwa nini yeye asimtafute, alijibu:
“Sasa nikianza mimi kumtafuta Rais Kikwete wakati tayari nimeanza
kuzungumza na wenzangu, Dk Shein na Balozi Seif, nitaonekana kama
ninatapatapa.”
Hata hivyo, Maalim Seif alisema Rais Kikwete ndiye
mtu pekee anayeweza kunusuru mchakato wa Katiba kwa sababu awali
aliaminika na watu wote kwa tabia yake ya kukutana na makundi mbalimbali
kila yalipokuwa yanatofautiana.
“Kilichotokea sasa ni Rais kukubali kushawishiwa
na chama chake. Mwanzo kanuni zilitungwa kwamba rais atalizindua Bunge
halafu atafuata Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (Jaji
Warioba) kuwasilisha Rasimu. Wao wakabadilisha na kulazimisha aanze
Warioba na kutaka kumpa saa moja tu ya kuzungumza,” alisema.
Alihoji: “Mtu aliyetembea Tanzania nzima kukusanya
maoni ya wananchi unataka kumpa saa moja kuwasilisha rasimu, halafu
anakuja Wako (Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Kenya, Amos) unampa siku
nzima.”
Alisema suala hilo liliibua mvutano mkali na
kusababisha wapinzani kutishia kugoma na baadaye suluhu ikapatikana
kwamba Jaji Warioba apewe saa nne kuwasilisha Rasimu, lakini awe wa
kwanza na Rais Kikwete afuate.
“Rais haikuwa jukumu lake kupinga alichokisema
Warioba. Nakumbuka alivyozungumza na Baraza la Vyama vya Siasa
alinifurahisha kwa sababu alizungumza kama Rais wa nchi na hakuegemea
upande wowote na alisema wazi kwamba tusidhani wingi ndiyo utapitisha
Katiba na kwamba Katiba ni maridhiano,” alisema.
Huku akicheka alisema: “Sijui ni nini kilitokea.
Rais alifungua Bunge na kuchukua moja kwa moja msimamo wa chama chake na
kuanzia hapo ndipo mambo yalipoanza kuharibika. Bado Rais anayo
opportunity (fursa) kwa sababu Ukawa wanachotaka ni kuhakikishiwa kuwa
wanakwenda katika Bunge kujadili Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.”
CHANZO: MWANANCHI.
Alipoulizwa kama Katiba Mpya itaweza kupatikana kama Ukawa
wataendelea kususia vikao vya Bunge hilo, alisema jambo hilo
halitawezekana kwa sababu haitapatikana theluthi mbili ya wajumbe kutoka
Zanzibar kwa ajili ya kupiga kura ya kufanya uamuzi.
“Ndiyo maana nikasema tunatakiwa kuwa na rais wa
Watanzania wote akatazame hoja kama za Ukawa ili kuona kama zina msingi
wowote maana kama hoja zisingekuwa za msingi, Ukawa wasingetoka,”
alisema.
Alisema kuwa rais ni mtu mzima, si lazima awaombe
radhi Watanzania, bali anaweza kutoa lugha nzuri na watu wakamwelewa
kuwa aliteleza katika hotuba yake ya kulifungua Bunge la Katiba.
Kuhusu Ukawa kuachiana majimbo katika Uchaguzi
Mkuu mwaka 2015 alisema, uamuzi wa mwisho bado haujachukuliwa lakini
maoni yaliyopo ni Ukawa kuendelea hata baada ya mchakato wa Katiba.
“Kwanza tunaangalia jinsi tutakavyoweza
kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu unaokuja, lakini hili nataka liwekewe
mikakati yake kwa sababu huko nyuma tulishajaribu lakini tukaachana
njiani, sasa hatutaki hayo yatokee. Tuliachana njiani kwa sababu
hatukujiandaa vizuri.”
CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment