Kamati hiyo inaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu na makamu wake ni Waziri wa Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, huku ikiwa imesheheni vigogo wengine
wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Viongozi wengine katika kamati hiyo ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uhusiano na Uratibu), William Lukuvi, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
Wamo pia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk
Seif Rashid, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Jana asubuhi, Mwalimu na Profesa Mbarawa walifika
mbele ya waandishi wa habari katika Hoteli ya St Gasper wakiwa
wameambatana na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa
Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy.
Lengo la mwenyekiti na makamu wake lilikuwa ni
kumbana Keissy ili akanushe taarifa aliyoitoa juzi kwenye moja ya
televisheni kwamba kamati hiyo inaongoza kwa kuvunja kanuni hasa katika
suala la akidi ya vikao kutotimia.
Sinema ilivyoanza
Walipofika mbele ya waandishi wa habari, Keissy
alipewa fursa ili akanushe taarifa yake, lakini alibadili mada na kuanza
kuzungumzia masuala ya muundo wa Serikali na Bunge, huku akisema yeye
ni muumini wa serikali tatu na siyo mambo ya serikali mbili
zinazopendekezwa na wengi kutoka katika chama chake.
Kauli hiyo iliwashtua Mwalimu na Profesa Mbarawa ambao walianza kumkatisha ili asiendelee.
“Keissy sikukuitia mambo hayo, huu ni mkutano
wangu, naomba ukanushe nilichokuitia, hayo utazungumza baadaye tafadhali
sana,” alisema Mwalimu.
Wakati huo Profesa Mbarawa na waandishi wa habari
waliokuwapo walivunjika mbavu kwa vicheko, huku yeye akiendelea
kusisitiza kwamba ni muumini wa Tanganyika.
Wakati akisema hayo, Profesa Mbarawa naye
aliingilia kati na kumtaka Keissy kueleza kilichompeleka hapo huku
akimtaka aache kelele za kupotosha wananchi kwa kuwa anachosema siyo
kweli.
Alipopewa nafasi ya kuzungumzia jambo hilo, Keissy alisema:
“Jana (juzi), mimi nilihesabu mara mbili nikaona Zanzibar hawajatimia
lakini kumbe mmoja nilimfanya akawa mtu wa Tanganyika, kwa hilo
nilighafilika, lakini mle ndani mambo siyo mazuri,” alisema Keissy.
Kabla hajaendelea Mwalimu alidakia na kumtaka
anyamaze kimya kwa kuwa huo haukuwa mkutano wake, ili yeye (Mwalimu)
aendelee kueleza mambo yaliyojiri ndani ya kamati.
“Jamani waandishi si mnaona amekanusha, huu ni
mkutano wangu na yeye sitaki azungumze mambo ya mle ndani kwa kuwa
msemaji ni mimi au makamu wangu au mtu yeyote atakayeteuliwa na
mwenyekiti, sasa tunaendelea,” alisema Mwalimu.
Mara baada ya Mwalimu kutoa taarifa ya kamati yake
kwa waandishi wa habari na kumaliza kujibu maswali, alinong’ona na
Profesa Mbarawa na hapo wakampa nafasi Keissy ili azungumze kwa ufupi
mambo yake lakini palepale mbele yao.
Kauli za Keissy
Akitumia fursa hiyo, Keissy alisema: “Kuna mambo
yanafanywa mle ndani ambayo mimi na wenzangu wengine tunalazimishwa,
hatukubaliani nayo likiwamo suala la kuizika Serikali ya Tanganyika
wakati wa upande wa pili (Zanzibar) wanapewa nafasi na kunufaika na
rasilimali za nchi hii, ndugu zangu huu ni uonevu.”
Alisema uonevu huo umekuwa mkubwa kwa wabunge wa
Tanzania Bara ukilinganisha na wenzao wa Zanzibar ambao alisema wanakula
fedha nyingi za bure ilihali hawafanyi kazi za Tanganyika.
“Ndugu zangu, hapa tusidanganyane, we fikiria watu
zaidi ya 50 wanatoka kule Zanzibar na kuja kutuamulia mambo yetu, hii
si halali hata kidogo. Haiwezekani mtu wa Zanzibar akaja kuzungumzia
masuala ya Nkasi wakati hayajui,” alisema.
Alisema kuwa msimamo wake siku zote ni serikali
tatu na kwamba hatayumbishwa na vitisho au jambo la aina yoyote hata
kukiwa na kulazimishwa.
Mbunge huyo alisema kuwa kutakuwa na urahisi wa
kuongoza Serikali kama Tanganyika itapewa hadhi yake kuliko ilivyo sasa
kwa serikali mbili zinazopigiwa upatu.
Kwa mapendekezo yake alisema ni vyema likawepo
Bunge la Tanganyika, Bunge la Zanzibar na kisha miongoni mwa wabunge
hao, wachaguliwe wachache kuunda Bunge la Muungano.
Aliendelea kusisitiza kuwa wabunge kutoka Zanzibar
wanawanyonya wenzao wa Tanzania Bara kwa kila kitu kauli ambayo
ilionekana kumkera Profesa Mbarawa na kuamua kumkatisha asiendelee
kuzungumza.
Wakati akiendelea kuzungumza, viongozi hao walimkatisha tena na
kumwambia akubali waondoke pamoja kuendelea na vikao vya kamati. Baada
ya hapo, Mwalimu na Profesa Mbarawa walinyanyuka na kuanza kuondoka,
lakini Keissy alisimama na kuendelea kuzungumza na waandishi wa habari.
Baada ya kuona anaendelea, Profesa Mbarawa alirudi
na kumshika mkono Kessy huku akisema; “Mheshimiwa Keissy twende bwana,
maana ukimwacha huku huyu atazungumza mambo mengi.”
Wakati akiondoka eneo hilo, Keissy alipaza sauti
akiwaambia waandishi wa habari: “Angalieni tunavyodhibitiwa, lakini
msimamo ni huo wala sitayumba ngoja tukaendelee lakini mimi ndiyo mtoa
habari namba moja.”
Msimamo wa serikali tatu ni wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) waliosusia Bunge.
CHANZO: MWANANCHI.
CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment