Wednesday, 27 August 2014

Hoja ya Maalim Seif kupokezana urais yawa ‘ngumu kumeza’

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi Waandishi wa Habari
Dar/Dodoma. Kauli ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kuhusu haja ya kupokezana nafasi ya urais kati ya Bara na Visiwani imekuwa ‘ngumu kumeza’ kwa wanasiasa walio wengi.

Baadhi ya wanasiasa wakiwamo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wasomi wengine waliozungumza na waandishi wetu wamepinga kauli hiyo wakieleza kuwa suala hilo halitawezekana kwa sababu linaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa katika jamii.

Mwanasiasa pekee aliyeonyesha kuiunga mkono kauli hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema jambo hilo linazungumzika kwa sababu huwezi kuwa na nchi mbili zilizoungana lakini nchi moja pekee ndiyo inayotoa rais mara zote.

“Miaka ya nyuma utaratibu huu ulikuwapo lakini baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka, CCM wakauondoa. Kitendo cha rais kutoka Tanzania Bara kila baada ya miaka 10, ndicho chanzo cha Zanzibar kubadili Katiba yao na kuifanya nchi hiyo kuwa na mamlaka kamili yasiyoweza kuingiliwa na rais wa Muungano,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema mfumo wa kubadilishana urais, utaleta mgawanyiko kwa makundi na maeneo mengine ya nchi kudai kuwa na zamu ya urais.

“Hatuwezi kwenda katika mfumo huo. Utasababisha kugawanyika kwa sababu ukishasema hivyo watatokea Waunguja nao watadai, Wakaskazini, Waislamu na Wakristo nao watadai,” alisema.

Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, alisema utaratibu huo unaweza kuleta matatizo kwa vyama katika kumpata mgombea mwenye sifa.

Alitolea mfano katika uchaguzi uliopita ambao Dk Slaa alipata mgombea mwenza ambaye hatoshi upande wa Zanzibar.

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Profesa Abdul Sheriff alisema utaratibu huo utaleta maana iwapo kuna muundo wa serikali tatu na si wa serikali mbili.

“Kwa sasa rais anachaguliwa na upande wenye watu wengi ambao ni Bara kwani wazi atashughulika na mambo ya Serikali ya Tanzania Bara na si ya Muungano,” alisema.

Mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti alisema suala hilo ni zuri na analiunga mkono iwapo nchi inakwenda katika muundo wa serikali moja. “Kama tunataka kutekeleza chini ya mundo wa serikali mbili ni lazima tubadilishe mambo mengi kwanza,” alisema.

Kimiti alisema zamani iliwezekana kwa sababu nchi ilikuwa katika mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Mbunge wa Dole (CCM), Sylvester Mabumba alisema rais anatakiwa atokane na uwezo, sifa, uadilifu, hekima na jinsi alivyo na upendo kwa wapigakura wake, badala ya eneo anakotoka.

“Kama ni zamu ya upande Tanzania Bara na tumekosa mtu ambaye ana sifa na uwezo tunafanyaje na tumeshajiwekea utaratibu huo?” alihoji Mabumba. “Maalim Seif ni mwanasiasa mzoefu na aliyebobea na pia ni msomi katika eneo la siasa angefanya uchambuzi, vinginevyo atasababisha mgongano katika jamii,” alisema.

Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM –Bara, Pius Msekwa alisema, “Sioni tatizo lolote kwa sababu uongozi huwa haubadilishwi kama mtu anavyobadilisha shati. Unajua mkiamua kupeana zamu ni dalili za kutoaminiana.”

Huku akimtolea mfano Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Msekwa alisema rais huyo alitokea Zanzibar na alipatikana kwa sababu kwa wakati huo alionekana anafaa na si kwa sababu alikuwa akitokea upande huo wa Muungano.

“Jiulizeni kama mnapotaka kubadilisha ili kila upande utoe rais kila baada ya miaka 10 mnataka kurekebisha jambo gani? Mbona kwa sasa hakuna tatizo lolote, binafsi naunga mkono utaratibu wa sasa.”

“Ndani ya CCM majina ya wagombea urais hupendekezwa na hatimaye kubaki jina moja na huo utaratibu hutumika katika vyama vingine, sasa ukifanyika uchaguzi anayeamua nani awe rais ni Watanzania wenyewe bila kujali huyu wa huku na huyu wa kule,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Agustine Mrema alisema: “Tukipitisha kisheria ya suala hili tutajiletea matatizo makubwa. Anatakiwa kutizamwa mtu mwenye vigezo kwa wakati huo kama ilivyokuwa kwa Mwinyi. Jambo hili lisiwe lazima, bali yatazamwe mahitaji ya wakati husika.”

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura alisema: “Hakuna sheria inayosema nchi mbili zikiungana lazima rais atoke kila upande wa muungano kila baada ya miaka fulani. Binafsi sioni kama jambo hili ni tatizo kwa sababu nchi hizi zinaweza kukubaliana tu tena kwa mazungumzo ya kawaida kabisa.”

Rwechungura alisema ingawa Zanzibar wanaweza kuhoji kuwa udogo wa nchi yao ndiyo sababu ya kutokutoa rais wa muungano, lakini hata kama wakipewa fursa hiyo haiwezi kuwa dawa ya kuondoa kero za muungano zilizopo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema tatizo lililopo ni muundo wa muungano na si mzozo wa nani atoe rais na nani asitoe.

“Lazima mkubaliane muundo wa muungano na mgawanyo wa mamlaka ya serikali baina ya pande mbili za muungano. Rasimu ya Katiba ya sasa haisemi lolote juu ya jambo hili na lingeweza kujadiliwa ila kama unavyoona mchakato wa Katiba nao umeingia dosari,” alisema.

CHANZO: MWANANCH.

No comments:

Post a Comment