Rais Jakaya Mrisho Kikwete. |
Miongoni mwa watu walihojiwa, pamoja na kukubaliana na uamuzi huo wa
kutafuta mwafaka, suala la Bunge kuendelea na vikao kabla ya maridhiano
hayo limeendelea kuiweka Katiba Mpya njiapanda.
Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles
Kibodya amesema, “Tusiogope kuingia gharama kuanza upya mchakato wa
kupata Katiba Mpya iwapo hakutapatikana maridhiano. Tunatakiwa kujifunza
kuanzia hapo.”
Kibodya alisema ni ngumu kwa Ukawa kuridhia mambo yatakayopigiwa kura
kwa sababu mengi waliyapinga na ndiyo ilikuwa sababu ya umoja huo
kususia vikao vya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu.
“Katiba ni ya nchi, si mali ya vyama vya siasa, hivyo maridhiano ni
muhimu. Kikubwa wakati wa utungaji wa Katiba ni lazima yawepo maridhiano
ya kisiasa. Rais Kikwete anatakiwa kutumia hekima katika mkutano huo na
washiriki wote kwa ujumla waondoe vichwani mwao kwamba sisi ‘tumeshinda
na wao wameshindwa’.
Alisema pamoja na mambo mengine, ni bora mchakato wa kuandika Katiba
Mpya ukachukua muda mrefu na gharama kubwa lakini makundi yote
yakakubaliana, tofauti na ilivyo sasa kwa baadhi ya watu kwenda
mahakamani na hii inaonyesha kuwa kuna tatizo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema, “Mkutano huo una umuhimu mkubwa,
ila ushauri wangu ni kuhakikisha kuwa pande zote zinakubaliana na kuwa
kitu kimoja.” Dk Makulilo alisema kama washiriki wa mkutano huo
watafikia mwafaka, makubaliano yao yanatakiwa kutoingilia utaratibu wa
Bunge la Katiba wa kupiga kura kupitisha kifungu kwa kifungu, vinginevyo
itakuwa ni kuingilia masuala ya kisheria.
“Katika hili napendekeza kuwa kitakachokubaliwa kitumike katika hatua
zinazoendelea za kupata Katiba Mpya. Unajua mchakato ukiendelea kama
ulivyo sasa bila mwafaka kupatikana Rasimu ya Katiba inaweza kukataliwa
na wananchi katika kura ya maoni. Kwa sasa watu wanapinga mambo mengi
yanayoendelea katika Bunge la Katiba,” alisema Makulilo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Ali Said alisema hatua
ya Rais Kikwete kukutana na makundi yaliyosusia kikao cha Bunge la
Katiba ni mwafaka lakini kwanza Bunge hilo liahirishwe ili kupisha
mazungumzo hayo.
Awadh ambaye alikuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema
kitendo cha Bunge hilo kuendelea huku kukiwa na kikao cha kutafuta
usuluhishi ni sawa na mtu anayejenga nyumba katika kiwanja chenye
mgogoro.
“Kama umekubaliana na mwenzio kwamba tutakula chakula baada ya
kumaliza mazungumzo, si sahihi mmoja aendelee kula mwingine akisubiri
mazungumzo na ndicho wanachokifanya wajumbe wa Bunge la Katiba,” alisema
na kuongeza kuwa Bunge hilo limepoteza dira na mwelekeo kutokana na
viongozi wake kuanza kufanya kazi ya kukusanya maoni ambayo
ilikwishafanywa na tume, kitendo alichosema kinaonyesha kuwa wameshindwa
kuelewa mamlaka na majukumu ya chombo hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui alisema licha ya uamuzi wa Rais Kikwete kuchelewa, mazungumzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa vile ndiyo yatakayosaidia kupata Katiba Mpya yenye maridhiano.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui alisema licha ya uamuzi wa Rais Kikwete kuchelewa, mazungumzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa vile ndiyo yatakayosaidia kupata Katiba Mpya yenye maridhiano.
Mazrui alisema CUF itashiriki katika mazungumzo hayo ambayo yanasimamiwa na TCD chini ya Mwenyekiti wake, John Cheyo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai alisema uamuzi wa
Rais Kikwete ndiyo msimamo wa CCM uliofikiwa katika kikao cha Kamati Kuu
kuwa juhudi ziendelee kufanyika za kutafuta mwafaka ili Kundi la Ukawa
lirejee bungeni.
“Hatua hii ni muhimu, Katiba tunayoitafuta ina manufaa kwa wananchi
wa pande zote mbili za Muungano na lazima tupate Katiba itakayosukuma
mbele maendeleo ya wananchi wote,” alisema Vuai.
Katika hatua nyingine, Baadhi ya wananchi wilayani Monduli wamekiomba
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kufungua kesi kuzuia
uongozi wa Bunge la Katiba kuendelea kuvunja sheria kwa kukusanya maoni
ya makundi mbalimbali ya wananchi.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na LHRC, wananchi
hao walisema kitendo hicho ni kinyume cha Kifungu cha 25 cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba kinachoelezea kazi na majukumu ya Bunge hilo.
“Kisheria, kazi na jukumu la kisheria la Bunge la Katiba ni kujadili
na kupitisha Rasimu ya Katiba baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi,” alisema Thomas Mbwambo.
Mkazi mwingine, Eric Ngwijo alihoji uhalali wa kura za maoni kwenye
Katiba itakayopitishwa na Bunge Maalumu ambayo viongozi wake wanavunja
sheria kwa kupuuza maoni na mapendekezo ya wananchi yaliyo katika
rasimu.
Katika siku za karibuni, uongozi wa Bunge Maalumu umekuwa ukikutana
na kupokea mapendekezo na maoni kutoka makundi na watu mbalimbali kwa
kile unachodai ni kuingiza mawazo mapya yasiyokuwamo kwenye rasimu.
Ofisa Mfawidhi wa LHRC Kanda ya Arusha, Shilinde Ngalula aliwahimiza
wananchi kushiriki mchakato wa Katiba Mpya na kuwataka wajumbe wa Bunge
hilo kuheshimu misingi ya mawazo na maoni ya wananchi.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment