Thursday, 28 August 2014

Tigo kushirikiana na SMZ katika uwekezaji wa mawasiliano.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Tigo yenye makao Makuu yake Nchini Sweeden Bwana Arthur Basting akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Jengo la Msekwa ndani ya Viunga vya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.
Na Othman Khamis Ame

Kampuni ya Mitandao ya simu za Mkononi ya Tigo imejitolea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye sekta ya uwekezaji katika masuala ya mitandao ya mawasiliano sambamba na kusaidia huduma za Kijamii kwa wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo yenye Makao Makuu yake Mjini Stokholmes Nchini Sweeden Bwana Arthur Basting alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake katika Jengo la Msekwa ndani ya Viunga vya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.

Bwana Arthur Basting ambae anasimamia Kampuni Tigo Barani Afrika alisema Uongozi wa Taasisi hiyo imejikita kutoa ushirikiano huo ikizingatia zaidi umuhimu wa mawasiliano ya Teknolojia yaliopo hivi sasa Ulimwenguni kote.

Bwana Arthur alisema Uongozi wa Kampuni ya Tigo unafurahia kuona kwamba Teknolojia ya Mawasiliano kupitia simu za Mikononi hivi sasa imeenea na kupokelewa vyema na wananchi wa Bara la Afrika.

Alisema kutokana na hatua hiyo Uongozi wa Taasisi hiyo umefikiria kuongeza kuhuduma zake mara dufu ndani ya Bara la Afrika ili kuona sekta ya  mawasiliano inaendelea kutoa huduma katika masuala ya kijamii na uchumi.

Bwana Arthur alifahamisha kwamba  mfumo ulioanzishwa na Kampuni hiyo wa huduma za kusafirisha fedha kupitia mtandao wa Simu za Kiganjani umeleta faraja kwa watu mbali mbali ukionyesha mafanikio makubwa ya kupunguka kwa unyang’anyi na wizi wa fedha baina ya watu au hata taasisi.

Naye Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Tigo Hapa Tanzania Bibi Sylvia Balwire alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Kampuni hiyo tayari imeanza mipango maalum ya kusaidia huduma za Kijamii katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

Bibi Sylvia alisema Wataalamu wa Tigo hivi sasa wako katika hatua za mwisho kukamilisha mipango ya kusaidia uendelezaji wa mradi wa kilimo cha Mwani Kisiwani Pemba.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliuomba Uongozi wa Kampuni ya Tigo kushirikiana na Kampuni ya Zantel katika kuona huduma za mitandao ya mawasiliano inazidi kuimarika.

Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa Kampuni hiyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari wakati wowote kutoa ushirikiano wa karibu ili kuongeza nguvu zitakazoiwezesha Kampuni hiyo kutekeleza malengo iliyojipangia.


Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliusharui Uongozi huo kuongeza nguvu zake zaidi katika kusaidia miradi ya Kijamii ambayo bado inaonekana haijawa na nguvu za kujiendesha yenyewe.

“ Hadi wakati huu tunaozungumza zipo skuli zetu nyingi hazijawa na vikalio, huduma za maabara na Maktaba, hata vifaa katika vituo vyetu vya Afya. Uwepo wenu kama wawekezaji unaweza pia kuyaangalia maeneo hayo muhimu kwa ustawi wa Jamii yetu “. Alisema Balozi Seif.

Balozi Seif alitoa mifano ya miradi hiyo ambayo inaweza kuongezewa nguvu na Kampuni hiyo ya Tigo kuwa ni pamoja na huduma za afya, Kilimo pamoja na Elimu.

Mkutano wa JK, Ukawa ni kishindo

Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kutaka kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge kupitia muungano wao wa Kituo cha Demokrasia (TCD), umeibua mjadala katika sehemu mbalimbali nchini huku wasomi na wanasiasa wakitoa angalizo.

Miongoni mwa watu walihojiwa, pamoja na kukubaliana na uamuzi huo wa kutafuta mwafaka, suala la Bunge kuendelea na vikao kabla ya maridhiano hayo limeendelea kuiweka Katiba Mpya njiapanda.

Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Kibodya amesema, “Tusiogope kuingia gharama kuanza upya mchakato wa kupata Katiba Mpya iwapo hakutapatikana maridhiano. Tunatakiwa kujifunza kuanzia hapo.”

Kibodya alisema ni ngumu kwa Ukawa kuridhia mambo yatakayopigiwa kura kwa sababu mengi waliyapinga na ndiyo ilikuwa sababu ya umoja huo kususia vikao vya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu.

“Katiba ni ya nchi, si mali ya vyama vya siasa, hivyo maridhiano ni muhimu. Kikubwa wakati wa utungaji wa Katiba ni lazima yawepo maridhiano ya kisiasa. Rais Kikwete anatakiwa kutumia hekima katika mkutano huo na washiriki wote kwa ujumla waondoe vichwani mwao kwamba sisi ‘tumeshinda na wao wameshindwa’.

Alisema pamoja na mambo mengine, ni bora mchakato wa kuandika Katiba Mpya ukachukua muda mrefu na gharama kubwa lakini makundi yote yakakubaliana, tofauti na ilivyo sasa kwa baadhi ya watu kwenda mahakamani na hii inaonyesha kuwa kuna tatizo.

Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema, “Mkutano huo una umuhimu mkubwa, ila ushauri wangu ni kuhakikisha kuwa pande zote zinakubaliana na kuwa kitu kimoja.” Dk Makulilo alisema kama washiriki wa mkutano huo watafikia mwafaka, makubaliano yao yanatakiwa kutoingilia utaratibu wa Bunge la Katiba wa kupiga kura kupitisha kifungu kwa kifungu, vinginevyo itakuwa ni kuingilia masuala ya kisheria.

“Katika hili napendekeza kuwa kitakachokubaliwa kitumike katika hatua zinazoendelea za kupata Katiba Mpya. Unajua mchakato ukiendelea kama ulivyo sasa bila mwafaka kupatikana Rasimu ya Katiba inaweza kukataliwa na wananchi katika kura ya maoni. Kwa sasa watu wanapinga mambo mengi yanayoendelea katika Bunge la Katiba,” alisema Makulilo.

Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Ali Said alisema hatua ya Rais Kikwete kukutana na makundi yaliyosusia kikao cha Bunge la Katiba ni mwafaka lakini kwanza Bunge hilo liahirishwe ili kupisha mazungumzo hayo.

Awadh ambaye alikuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema kitendo cha Bunge hilo kuendelea huku kukiwa na kikao cha kutafuta usuluhishi ni sawa na mtu anayejenga nyumba katika kiwanja chenye mgogoro.

“Kama umekubaliana na mwenzio kwamba tutakula chakula baada ya kumaliza mazungumzo, si sahihi mmoja aendelee kula mwingine akisubiri mazungumzo na ndicho wanachokifanya wajumbe wa Bunge la Katiba,” alisema na kuongeza kuwa Bunge hilo limepoteza dira na mwelekeo kutokana na viongozi wake kuanza kufanya kazi ya kukusanya maoni ambayo ilikwishafanywa na tume, kitendo alichosema kinaonyesha kuwa wameshindwa kuelewa mamlaka na majukumu ya chombo hicho.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui alisema licha ya uamuzi wa Rais Kikwete kuchelewa, mazungumzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa vile ndiyo yatakayosaidia kupata Katiba Mpya yenye maridhiano.

Mazrui alisema CUF itashiriki katika mazungumzo hayo ambayo yanasimamiwa na TCD chini ya Mwenyekiti wake, John Cheyo.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai alisema uamuzi wa Rais Kikwete ndiyo msimamo wa CCM uliofikiwa katika kikao cha Kamati Kuu kuwa juhudi ziendelee kufanyika za kutafuta mwafaka ili Kundi la Ukawa lirejee bungeni.

“Hatua hii ni muhimu, Katiba tunayoitafuta ina manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano na lazima tupate Katiba itakayosukuma mbele maendeleo ya wananchi wote,” alisema Vuai.

Katika hatua nyingine, Baadhi ya wananchi wilayani Monduli wamekiomba Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kufungua kesi kuzuia uongozi wa Bunge la Katiba kuendelea kuvunja sheria kwa kukusanya maoni ya makundi mbalimbali ya wananchi.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na LHRC, wananchi hao walisema kitendo hicho ni kinyume cha Kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinachoelezea kazi na majukumu ya Bunge hilo.

“Kisheria, kazi na jukumu la kisheria la Bunge la Katiba ni kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi,” alisema Thomas Mbwambo.

Mkazi mwingine, Eric Ngwijo alihoji uhalali wa kura za maoni kwenye Katiba itakayopitishwa na Bunge Maalumu ambayo viongozi wake wanavunja sheria kwa kupuuza maoni na mapendekezo ya wananchi yaliyo katika rasimu.

Katika siku za karibuni, uongozi wa Bunge Maalumu umekuwa ukikutana na kupokea mapendekezo na maoni kutoka makundi na watu mbalimbali kwa kile unachodai ni kuingiza mawazo mapya yasiyokuwamo kwenye rasimu.

Ofisa Mfawidhi wa LHRC Kanda ya Arusha, Shilinde Ngalula aliwahimiza wananchi kushiriki mchakato wa Katiba Mpya na kuwataka wajumbe wa Bunge hilo kuheshimu misingi ya mawazo na maoni ya wananchi.

MWANANCHI

Tuhuma nzito kwa mawaziri

Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wakiwa kwenye kikao cha Bunge hilo Mjini Dodoma
Dar na Dodoma. Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limedai kuwa baadhi ya mawaziri na manaibu wao wamekuwa wakilipwa posho za kuhudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katiba hata wanapokuwa hawapo bungeni.

Kaimu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda alisema jana: “Mawaziri na manaibu ambao ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walioko mjini Dodoma wanapokuwa na safari za kikazi huaga kwa Waziri Mkuu lakini jambo la kushangaza ni kuendelea kulipwa posho wakati hawapo.”

Alisema hali hiyo husababisha Bunge hilo kuendelea kuwalipa posho kupitia akaunti zao za benki lakini wakiwa hawapo Mjini Dodoma. Mwakagenda alisema mawaziri hao wanapotoka kwenda kwenye shughuli mbalimbali za kiserikali nako hulipwa posho.

“Haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma, mawaziri na manaibu wanalipwa posho hata wanapokuwa nje ya Bunge Maalumu la Katiba, wanaposafiri pia wanalipwa posho na Serikali,” alisema Mwakagenda.

Alisema pamoja na kwamba Ofisi Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba imeonyesha kubana mianya kwa wajumbe kusaini bila kufanya kazi, bado kuna ufujaji wa fedha eneo la mawaziri.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema ruhusa za kutoka nje ya Dodoma hutolewa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta na kwamba wasiohudhuria huwa hawalipwi.

“Tunalipa wajumbe wanaohudhuria bungeni, kama hilo linatendeka lazima nilifuatilie. Ninachosema kama kuna waziri amelipwa na hayupo itabidi aturejeshee hiyo fedha. Lakini hili tatizo ni gumu kwa sababu mtu analipwa na tunajua yupo kumbe pengine hajaingia katika vikao,” alisema.

Alisema kanuni za Bunge hilo zinataka mjumbe anapoondoka aombe ruhusa kwa Mwenyekiti wa Bunge na nakala kwa Katibu.

“Wakicopy (wakinakili) kwangu mimi nawaorodhesha nampelekea mhasibu, tukikaribia kulipa namwambia hawa hawapo, kwa hiyo mtu siku ambazo anaomba ruhusa hata kama anaumwa hatumlipi, labda awe amelazwa hospitali ambaye tunamlipa half (nusu),” alisema.

Hata hivyo, alisema tatizo linalowapa shida kiutendaji ni kwa wale wasioaga wanapotoka nje ya Dodoma na kwamba hilo atalifuatilia kwa kuangalia orodha za mahudhurio kwenye vikao.

Mahudhurio hafifu
Kuhusu mahudhurio Hamad alikiri kwamba hilo ni tatizo kutokana na baadhi ya wajumbe kutokuwa makini na kwamba mahudhurio hafifu yanaathiri uendeshaji wa vikao hivyo.

“Kama leo nilikwenda katika kamati nikawaambia kama haupo ni haupo tu, wengine wakasema unajua wengine walikuwa wanaumwa, nikawaambia mimi najua hiyo ni luck of seriousness tu (kukosekana kwa umakini), hakuna lingine. Wakanitaka niombe radhi lakini mimi nikawaambia wala siombi radhi… Umakini mdogo… Unakuta wengine wanajadili na wengine wanaathiri kura kwa uzembe tu, nafikiri kama kila mtu angekwenda katika vikao tusingekuwa na shida.”

Mwakagenda alisema katika wiki mbili zilizopita, mahudhurio yamekuwa madogo katika vikao vya kamati za Bunge.

Alisema Bunge hilo limesema wajumbe 441 wanahudhuria vikao hivyo lakini uchunguzi wa Jukata umeonyesha baadhi yao wamekuwa wakisaini tu kitabu cha mahudhurio.

Mwakagenda alisema uchunguzi huo ulionyesha kwamba wajumbe 100 hawahudhurii kwenye kamati.
Aidha, alisema kitendo cha Bunge hilo kuendelea kupokea maoni ya makundi mbalimbali ya kijamii ni kwenda kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Kifungu namba 9 (1) ambacho alisema kinaeleza kwamba kazi ya kukusanya maoni ni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

MWANANCHI

Wednesday, 27 August 2014

Vifaa vya ebola kufungwa mipakani

Madaktari wakimuhudumia Mgonjwa wa Ebola
Dar es Salaam. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatarajia kufunga vifaa vya kupimia joto (Thermal Scanner) katika mipaka ya nchi ili kudhibiti kuenea ugonjwa wa ebola ambao umeelezwa umeingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Juzi, Waziri wa Afya DRC, Felix Kabange Numbi alikaririwa akisema ebola imeingia nchini humo na watu wawili walioambukizwa, wamefariki dunia katika Jimbo la Eguator, Kaskazini Magharibi wa nchi hiyo.

Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Dharura na Maafa wa wizara hiyo, Dk Elias Kwesi alisema baada ya kufunga vipima joto kwenye viwanja vya ndege, hivi karibuni wataanza kufunga kwenye mipaka.

“Vifaa hivyo tayari tumeshafunga kwenye viwanja vya ndege kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza na Mbeya,” alisema.

“Unajua baada ya kupata taarifa za kuingia kwa ugonjwa wa ebola Kongo, tumeona mbinu za kujikinga zinatakiwa kuwa za hali ya juu, hivyo tumeamua kufunga Thermal Scanner kwenye mipaka yote,” alisema Kwesi.

Alisema vifaa mbalimbali vikiwamo vya kujikinga vimesambazwa kwenye mikoa yote na wataalamu wa afya wanaendelea kuelimishwa kuhusu ugonjwa huo.

DRC inakuwa nchi ya tano barani Afrika kukumbwa na mlipuko huo ambao hadi sasa umeua zaidi ya watu 1,427 Magharibi mwa Afrika.

Nchi nyingine za Afrika zilizokumbwa na ugonjwa huo ni Liberia, Nigeria na Sierra Leone na Guinea.

Hoja ya Maalim Seif kupokezana urais yawa ‘ngumu kumeza’

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi Waandishi wa Habari
Dar/Dodoma. Kauli ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kuhusu haja ya kupokezana nafasi ya urais kati ya Bara na Visiwani imekuwa ‘ngumu kumeza’ kwa wanasiasa walio wengi.

Baadhi ya wanasiasa wakiwamo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wasomi wengine waliozungumza na waandishi wetu wamepinga kauli hiyo wakieleza kuwa suala hilo halitawezekana kwa sababu linaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa katika jamii.

Mwanasiasa pekee aliyeonyesha kuiunga mkono kauli hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema jambo hilo linazungumzika kwa sababu huwezi kuwa na nchi mbili zilizoungana lakini nchi moja pekee ndiyo inayotoa rais mara zote.

“Miaka ya nyuma utaratibu huu ulikuwapo lakini baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka, CCM wakauondoa. Kitendo cha rais kutoka Tanzania Bara kila baada ya miaka 10, ndicho chanzo cha Zanzibar kubadili Katiba yao na kuifanya nchi hiyo kuwa na mamlaka kamili yasiyoweza kuingiliwa na rais wa Muungano,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema mfumo wa kubadilishana urais, utaleta mgawanyiko kwa makundi na maeneo mengine ya nchi kudai kuwa na zamu ya urais.

“Hatuwezi kwenda katika mfumo huo. Utasababisha kugawanyika kwa sababu ukishasema hivyo watatokea Waunguja nao watadai, Wakaskazini, Waislamu na Wakristo nao watadai,” alisema.

Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, alisema utaratibu huo unaweza kuleta matatizo kwa vyama katika kumpata mgombea mwenye sifa.

Alitolea mfano katika uchaguzi uliopita ambao Dk Slaa alipata mgombea mwenza ambaye hatoshi upande wa Zanzibar.

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Profesa Abdul Sheriff alisema utaratibu huo utaleta maana iwapo kuna muundo wa serikali tatu na si wa serikali mbili.

“Kwa sasa rais anachaguliwa na upande wenye watu wengi ambao ni Bara kwani wazi atashughulika na mambo ya Serikali ya Tanzania Bara na si ya Muungano,” alisema.

Mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti alisema suala hilo ni zuri na analiunga mkono iwapo nchi inakwenda katika muundo wa serikali moja. “Kama tunataka kutekeleza chini ya mundo wa serikali mbili ni lazima tubadilishe mambo mengi kwanza,” alisema.

Kimiti alisema zamani iliwezekana kwa sababu nchi ilikuwa katika mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Mbunge wa Dole (CCM), Sylvester Mabumba alisema rais anatakiwa atokane na uwezo, sifa, uadilifu, hekima na jinsi alivyo na upendo kwa wapigakura wake, badala ya eneo anakotoka.

“Kama ni zamu ya upande Tanzania Bara na tumekosa mtu ambaye ana sifa na uwezo tunafanyaje na tumeshajiwekea utaratibu huo?” alihoji Mabumba. “Maalim Seif ni mwanasiasa mzoefu na aliyebobea na pia ni msomi katika eneo la siasa angefanya uchambuzi, vinginevyo atasababisha mgongano katika jamii,” alisema.

Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM –Bara, Pius Msekwa alisema, “Sioni tatizo lolote kwa sababu uongozi huwa haubadilishwi kama mtu anavyobadilisha shati. Unajua mkiamua kupeana zamu ni dalili za kutoaminiana.”

Huku akimtolea mfano Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Msekwa alisema rais huyo alitokea Zanzibar na alipatikana kwa sababu kwa wakati huo alionekana anafaa na si kwa sababu alikuwa akitokea upande huo wa Muungano.

“Jiulizeni kama mnapotaka kubadilisha ili kila upande utoe rais kila baada ya miaka 10 mnataka kurekebisha jambo gani? Mbona kwa sasa hakuna tatizo lolote, binafsi naunga mkono utaratibu wa sasa.”

“Ndani ya CCM majina ya wagombea urais hupendekezwa na hatimaye kubaki jina moja na huo utaratibu hutumika katika vyama vingine, sasa ukifanyika uchaguzi anayeamua nani awe rais ni Watanzania wenyewe bila kujali huyu wa huku na huyu wa kule,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Agustine Mrema alisema: “Tukipitisha kisheria ya suala hili tutajiletea matatizo makubwa. Anatakiwa kutizamwa mtu mwenye vigezo kwa wakati huo kama ilivyokuwa kwa Mwinyi. Jambo hili lisiwe lazima, bali yatazamwe mahitaji ya wakati husika.”

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura alisema: “Hakuna sheria inayosema nchi mbili zikiungana lazima rais atoke kila upande wa muungano kila baada ya miaka fulani. Binafsi sioni kama jambo hili ni tatizo kwa sababu nchi hizi zinaweza kukubaliana tu tena kwa mazungumzo ya kawaida kabisa.”

Rwechungura alisema ingawa Zanzibar wanaweza kuhoji kuwa udogo wa nchi yao ndiyo sababu ya kutokutoa rais wa muungano, lakini hata kama wakipewa fursa hiyo haiwezi kuwa dawa ya kuondoa kero za muungano zilizopo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema tatizo lililopo ni muundo wa muungano na si mzozo wa nani atoe rais na nani asitoe.

“Lazima mkubaliane muundo wa muungano na mgawanyo wa mamlaka ya serikali baina ya pande mbili za muungano. Rasimu ya Katiba ya sasa haisemi lolote juu ya jambo hili na lingeweza kujadiliwa ila kama unavyoona mchakato wa Katiba nao umeingia dosari,” alisema.

CHANZO: MWANANCH.

Posho za Bunge kaa la moto

Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wakiwa Bungeni.
OFISI ya Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, imetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu kuchelewa kwa malipo ya posho za wajumbe wa Bunge hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkurugenzi wa Habari na Itifaki wa Bunge Maalumu, Jossey Mwakasiyuka, alisema ofisi ya Bunge hilo imekerwa na baadhi ya vyombo vya habari kuchapisha taarifa hizo.

Alisema taarifa hizo ni za upotoshaji na zina lengo la kuwadhalilisha wajumbe na kuwafanya waonekane wenye kuishi na kufanya kazi kwa kutegemea posho wanazolipwa.

“Ni vema ikaeleweka kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu wote ni watu wenye nafasi zao katika jamii na ni wenye kazi au shughuli zao mahususi zinazowaingizia kipato, na kwamba ujumbe wa Bunge Maalumu ni nafasi ya muda tu ya kutimiza jukumu la kuliandalia taifa Katiba mpya,” alisema

Mwakasyuka.
Alisema si vizuri kwa vyombo vya habari kuwadhalilisha wajumbe hao kwa njia yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo kunawavunja moyo na kuwafanya washindwe kuifanya kazi yao vizuri kama ilivyotarajiwa na wananchi.

“Ni vyema ikaeleweka kwamba malipo ya posho yanafuata taratibu za fedha za umma na yanapita kwenye mchakato maalumu unaojumuisha kupata orodha za mahudhurio ya wajumbe kwenye kikao, upatikanaji wa fedha toka Hazina na upatikanaji wa fedha toka benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku kadhaa hadi kukamilika,” alisema Mwakasyuka.

Kutokana na hali hiyo, Mwakasyuka aliwataka wanahabari kuzingatia maadili na kanuni za uandishi wa habari zinazotolewa katika vikao vya Bunge Maalumu.

“Kumbukeni kuwa wajibu wenu ni kuhabarisha umma na sio kupotosha umma na hata kuleta usumbufu kwa jamii kutokana na uandishi usio makini,” alisema.

CHANZO: MTANZANIA.

Kikwete uso kwa uso na Ukawa

Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Dodoma/Dar. Wakati wowote wiki hii, Rais Jakaya Kikwete anatarajia kukutana na viongozi wa Vyama vya Siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ili kuzungumzia mchakato wa Katiba.

Katika mkutano huo, Rais Kikwete atakutaka ‘kiaina’ na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF.

Aprili 16, mwaka huu wajumbe wa Ukawa na baadhi kutoka Kundi la 201, walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM kutaka kuingiza mfumo wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa katika Rasimu.

TCD inaundwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni ambavyo ni CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP, huku vyama visivyo na uwakilishi bungeni vikiwakilishwa na UPDP kinachoongozwa na Fahmi Dovutwa.

Jana, kwa nyakati tofauti wenyeviti wenza wa Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR Mageuzi), walisema wako tayari kukutana na Rais, ila msimamo wao wa kutaka ijadiliwe rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa Ukawa kuomba wakutane na Rais Kikwete kwa ajili ya kujadiliana namna bora ya kuendesha mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni Dodoma jana, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alisema Rais atafanya kikao hicho wakati wowote ndani ya wiki hii na kwamba viongozi wa vyama wakiwamo wa Ukawa, wamethibitisha kushiriki.

Cheyo alisema, katika kikao walichokutana Dar es Salaam Agosti 23, wanachama wa TCD walikubaliana kwamba upo umuhimu wa kukutana na Rais Kikwete kwa mazungumzo na maridhiano.

Kukutana kwa viongozi hao, kunakuja huku wajumbe wa Bunge Maalumu wakiwa wamemaliza kujadili sura zote 15 zilizokuwa zimesalia na tayari baadhi ya kamati zimemaliza kupiga kura wakisubiri kuingia bungeni Septemba 2 kwa kazi ya kupigia kura sura kwa sura.

Kuhusu viongozi wa Ukawa, alisema wanazo taarifa na baadhi yao walikuwapo katika kikao cha kujadili kukutana na kiongozi huyo wa nchi, hivyo akasema lazima watashiriki wakati wowote wakiitwa.

Lipumba
Akizungumzia mkutano huo na Rais, Profesa Lipumba alisema: “Tunakutana na Rais Kikwete kwa sababu sisi ni wanachama wa TCD.” Alipoulizwa juu ya msimamo wa Ukawa, alisema lengo ni kutafuta mwafaka ili mchakato wa kupata Katiba Mpya uendeshwe kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.

“Kikubwa tunachokitaka ni maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Warioba kuheshimiwa na siyo kuchukuliwa maoni mengine kama inavyofanyika sasa huko bungeni,” alisema Profesa Lipumba.

Mbowe
Mbowe alisema Katiba Mpya ni kwa masilahi ya Watanzania wote na Taifa lao, hivyo inapotokea mikutano kama hiyo na kwa hali ilivyo sasa, hakuna mtu mwenye nia njema atakayekataa kushiriki. Kikubwa ni kwamba hatuwezi kubadili msimamo wetu na huo ndiyo ukweli,” alisema.

Kuhusu Bunge hilo kupokea maoni ya makundi mbalimbali wakati tayari ukusanyaji wa maoni umeshafanywa na Tume ya Jaji Warioba, Mbowe alisema, “Ndiyo maana tulisusia vikao vya Bunge la Katiba, nadhani sasa Watanzania wamejua kwa nini tulitoka nje.”

Mbowe alisema kuwa mchakato wa Katiba unaendeshwa kwa mujibu wa sheria, lakini hivi sasa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta analiendesha Bunge hilo kinyume na sheria hiyo... “Ukusanyaji wa maoni unaofanyika sasa ni fedheha kwa CCM na Serikali, ni utoto na aibu wa CCM. Kwa sasa Ukawa tumetulia tunatazama hali inavyokwenda na tuna mipango yetu ambayo tunapanga. Kama hali ikiendelea kuwa hivi tutachukua uamuzi mgumu ili dunia nzima ijue.”

James Mbatia
Alisema wako tayari kukutana na Rais Kikwete kwa ushauriano kwa sababu suala la maridhiano ni la msingi na viongozi wote wa TCD walikubaliana Agosti 23.

“Mwaliko tumeupata na tutashiriki. Bunge linaweza kuendelea kwa taratibu zake za kisheria, lakini suala la mashauriano, lazima tukae tuangalie ni jinsi gani Taifa letu linaweza likavuka kwa maridhiano kwa amani na utulivu,” alisema.

Kauli ya Ikulu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu alisema Rais Kikwete yuko tayari kukutana na viongozi wa vyama vya siasa muda wowote... “Wao wafuate utaratibu tu, Rais hawezi kukataa kukutana nao na hilo amekuwa akilisema mara nyingi tu.”

Monday, 25 August 2014

Maalim Seif: Zanzibar,Bara zipokezane urais

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi wa gazeti la Mwananchi walioongozwa na Mhariri Mtendaji, Frank Sanga (wa tatu kulia) walipomfanyia mahojiano maalumu kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, hivi karibuni
Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kwa mfumo wa muungano uliopo, ni vyema kila upande ukawa unatoa rais kila baada ya miaka 10.

Amesema haiwezekani ziwepo nchi mbili zilizoungana halafu kila akichaguliwa rais awe anatokea upande mmoja tu wa muungano, huku upande mwingine ukiambulia kutoa makamu wa rais.

Mbali na hilo, Maalim Seif pia ametaja sifa tano za rais ajaye huku akisisitiza kuwa kigezo si umri, bali uwezo wake wa kufanya kazi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili Dar es Salaam, Maalim Seif alisema: “Kama ni muungano wa nchi mbili lazima kuwe na mfumo ambao tutajua kwamba kipindi hiki rais ametokea Zanzibar, basi kipindi kingine rais atatoka Bara.”

Tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na kuzaliwa Tanzania mwaka 1964, Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi ndiye pekee ambaye alitokea Zanzibar. Aliongoza kati ya mwaka 1985-1995.

Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama inaweza kutumika Tanzania Bara, kwa umakini Maalim Seif alisema, “Hilo ndilo suluhisho kutokana na mivutano iliyopo Tanzania Bara. Serikali hii inaunganisha vipaji vya watu ambao wanafanya kazi kwa pamoja.”

Sifa za rais
Huku akiwa makini na kuonyesha msisitizo wa ishara za mikono, Maalim Seif alisema: “Kwanza rais awe na uwezo wa kuunganisha wananchi kwa sababu ni wa Watanzania wote, kuanzia waliompigia kura na ambao hawakumpigia kura. Asiwe na upendeleo.”

Alisema mtu akishakuwa rais lazima aweke masilahi ya chama chake pembeni na awatumikie wananchi wote.

“Pili, rais anatakiwa kuwa karibu na wananchi kwa sababu sifa za kiongozi mzuri ni kujua hali halisi ya wale unaowaongoza, huwezi kujua hali halisi maisha ya wananchi kama hauko karibu nao,” alisema.

Akitaja sifa ya tatu huku akicheka, Maalim Seif alisema rais ni lazima awe na uamuzi na kuhakikisha kuwa anawabana watu aliowateua.

“Simaanishi rais awe dikteta. Rais unaweza kuwa na baraza lako la mawaziri lakini lazima uwe na malengo yako. Mawaziri wako unawaeleza wazi kwamba katika sekta fulani unataka jambo fulani lifanikiwe, jambo hilo linapendekezwa na kujadiliwa katika kikao cha mawaziri na hatimaye kupitishwa.”

Alisema rais ni lazima ajue kuwa jambo fulani lina manufaa au halina manufaa na akichukua uamuzi hatakiwi kuyumba, bali kuusimamia mpaka mwisho.

“Nne, rais anatakiwa kuwa na msimamo na akubali kushaurika. Licha ya kuwa Katiba inaeleza kuwa rais ni mtu mwenye uamuzi wa mwisho lakini ni lazima awe mtu anayekubali kushaurika,” alisema.

Akitaja sifa ya tano, Maalim Seif alisema urais ni taasisi, hivyo rais ni lazima akubali kuisimamia taasisi hiyo... “Rais anatakiwa kutambua kuwa kuna Bunge, Mahakama na Serikali na kila mhimili unatakiwa kufanya kazi bila kuingiliwa. Ukiwa na taasisi imara hata kama utakuwa na rais asiye na uwezo mambo yatakwenda tu.”

Maalim Seif alisema nchi kama Marekani kila mtu anaweza kuwa rais na mambo yakaenda vizuri kutokana na kuwa na taasisi imara.

Umri wa urais
“Unajua idadi kubwa ya Watanzania ni vijana na pia lazima tujue kuwa vijana wa sasa ni tofauti na ‘vijana’ sisi. Tunahitaji mtu mzoefu. Tusitazame ujana au uzee. Inatakiwa aangaliwe mtu mwenye uwezo wa kuongoza watu. Tunataka rais akiwa kijana asipinge mawazo ya wazee na akiwa mzee lazima ajue matatizo ya sasa ya vijana.”

Huku akitolea mfano wa China, Maalim Seif alisema nchi hiyo licha ya kurekebisha masuala mengi ya uongozi mpaka sasa, Rais na Waziri Mkuu wake ni lazima wawe wa umri zaidi ya miaka 50.

“Unajua wakati mwingine vijana wanakuwa na jazba. Ukiwa rais hautakiwi kutawaliwa na jazba na unatakiwa kuwa na busara, hekima na utaalamu,” alisema.

Alivyomtolea nje Sitta
Katika hatua nyingine, Maalim Seif ameeleza namna viongozi wa Serikali ya Umoja ya Kitaifa Zanzibar, walivyojitahidi kuunusuru mchakato wa Katiba Mpya, huku akisisitiza kuwa sasa umefikia pabaya na ni busara tu ndizo zinazoweza kuunusuru.

Alisema aliwahi kumkatalia Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta alipomfuata kutaka ushauri wake ili kunusuru mchakato huo kwa kuwa taratibu na kanuni za Bunge Maalumu zimevunjwa makusudi.

Alisema alimtaka Sitta kuheshimu maoni ya wajumbe wa Ukawa wanaotokana na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ambao walisusia vikao vya Bunge la Katiba, wakishinikiza ijadiliwe Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Mwenyekiti (Sitta) alinifuata na kuomba busara zangu katika jambo hili lakini nikamwambia kama busara hazikutumika ni vigumu kuzipata tena busara hizo.

Lakini maoni yangu yakawa ni yaleyale ya kukubaliana na Ukawa ili kuona jinsi ya kupokea mawazo yao kuliko kulazimisha kuendelea na mchakato eti kwa sababu Ukawa ni wachache.”

Maalim Seif anaamini kuwa kuandika Katiba ni jambo la maridhiano hivyo hata watu wachache nao wana haki ya msingi katika suala hilo na wanawawakilisha wengi.

“Hiyo ilikuwa hatua ya kwanza iliyofanyika. Hatua ya pili ni sisi viongozi wa Zanzibar, mimi, Dk Shein (Ali Mohamed, Rais wa Zanzibar) na Balozi Seif Ali Iddi (Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar), tulikaa kujadili jinsi ya kusaidia jambo hili lakini hatimaye likaibuka suala la serikali mbili au tatu na hatukupata mwafaka,” alisema.

Kuhusu nafasi ya Rais Jakaya Kikwete, huku akicheka, Maalim Seif alisema yupo tayari kukutana naye kama akiombwa wazungumze kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.

Alipoulizwa kwa nini yeye asimtafute, alijibu: “Sasa nikianza mimi kumtafuta Rais Kikwete wakati tayari nimeanza kuzungumza na wenzangu, Dk Shein na Balozi Seif,  nitaonekana kama ninatapatapa.”

Hata hivyo, Maalim Seif alisema Rais Kikwete ndiye mtu pekee anayeweza kunusuru mchakato wa Katiba kwa sababu awali aliaminika na watu wote kwa tabia yake ya kukutana na makundi mbalimbali kila yalipokuwa yanatofautiana.

“Kilichotokea sasa ni Rais kukubali kushawishiwa na chama chake. Mwanzo kanuni zilitungwa kwamba rais atalizindua Bunge halafu atafuata Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (Jaji Warioba) kuwasilisha Rasimu. Wao wakabadilisha na kulazimisha aanze Warioba na kutaka kumpa saa moja tu ya kuzungumza,” alisema.

Alihoji: “Mtu aliyetembea Tanzania nzima kukusanya maoni ya wananchi unataka kumpa saa moja kuwasilisha rasimu,  halafu anakuja Wako (Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Kenya, Amos) unampa siku nzima.”

Alisema suala hilo liliibua mvutano mkali na kusababisha wapinzani kutishia kugoma na baadaye suluhu ikapatikana kwamba Jaji Warioba apewe saa nne kuwasilisha Rasimu, lakini awe wa kwanza na Rais Kikwete afuate.

“Rais haikuwa jukumu lake kupinga alichokisema Warioba. Nakumbuka alivyozungumza na Baraza la Vyama vya Siasa alinifurahisha kwa sababu alizungumza kama Rais wa nchi na hakuegemea upande wowote na alisema wazi kwamba tusidhani wingi ndiyo utapitisha Katiba na kwamba Katiba ni maridhiano,” alisema.

Huku akicheka alisema: “Sijui ni nini kilitokea. Rais alifungua Bunge na kuchukua moja kwa moja msimamo wa chama chake na kuanzia hapo ndipo mambo yalipoanza kuharibika. Bado Rais anayo opportunity (fursa) kwa sababu Ukawa wanachotaka ni kuhakikishiwa kuwa wanakwenda katika Bunge kujadili Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.”

Alipoulizwa kama Katiba Mpya itaweza kupatikana kama Ukawa wataendelea kususia vikao vya Bunge hilo, alisema jambo hilo halitawezekana kwa sababu haitapatikana theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar kwa ajili ya kupiga kura ya kufanya uamuzi.

“Ndiyo maana nikasema tunatakiwa kuwa na rais wa Watanzania wote akatazame hoja kama za Ukawa ili kuona kama zina msingi wowote maana kama hoja zisingekuwa za msingi, Ukawa wasingetoka,” alisema.

Alisema kuwa rais ni mtu mzima, si lazima awaombe radhi Watanzania, bali anaweza kutoa lugha nzuri na watu wakamwelewa kuwa aliteleza katika hotuba yake ya kulifungua Bunge la Katiba.

Kuhusu Ukawa kuachiana majimbo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 alisema, uamuzi wa mwisho bado haujachukuliwa lakini maoni yaliyopo ni Ukawa kuendelea hata baada ya mchakato wa Katiba.

“Kwanza tunaangalia jinsi tutakavyoweza kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu unaokuja, lakini hili nataka liwekewe mikakati yake kwa sababu huko nyuma tulishajaribu lakini tukaachana njiani, sasa hatutaki hayo yatokee. Tuliachana njiani kwa sababu hatukujiandaa vizuri.”

CHANZO: MWANANCHI.

Friday, 22 August 2014

Watuhumiwa ugaidi wachafua hali ya hewa kortini

Watuhumiwa wa kesi ya ugaidi, akiwamo Sheikh Farid Hadi Ahmed (kushoto), wakitoka kwenye chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es alam.
KIONGOZI wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed (43), ametoa shutuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi akidai kuwa limewafanyia ukatili kwa kuwapiga, hali inayowafanya baadhi yao wajisaidie damu.

Sheikh Farid alitoa madai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa, wakati kesi ya tuhuma za ugaidi inayowakabili ilipokuwa ikitajwa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Njike, alidai kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi haujakamilika na wanaomba hati ya kuwachukua washtakiwa saba, akiwamo Sheikh Farid kwa ajili ya mahojiano.

Hakimu Riwa alikubali maombi hayo na kuahirisha kesi hadi Septemba 3, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Hali hiyo ilisababisha washtakiwa kuomba kutoa maelezo yao.

“Mheshimiwa wametuomba kwenda kutuhoji tena, mara ya kwanza tulipohojiwa, polisi hawakutumia ustaarabu wala ubinadamu, ni ushenzi na ukatili, walituhoji uchi wa mnyama na kutupiga.

“Kiongozi Mkuu wa Uamsho, Sheikh Mselem Ally Mselem, mwenye heshima, mfasiri wa Kur’ani, alinihadithia alipohojiwa walimfanya nini, tumepigwa na hatukutibiwa, magereza wamejitahidi, lakini hawana nyenzo za matibabu.

“Watu wameumizwa vibaya, mengine hayasemeki, wanajisaidia haja ndogo damu wiki moja hadi mbili, tunaomba tufanyiwe uchunguzi wa afya zetu, ipo siku mahakamani italetwa maiti.

“Tumekamatwa sababu hatutaki Muungano, hiyo ndiyo kesi ya msingi, tunawaambia ukweli katika mihadhara na watu wanatuamini, tunaomba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iletwe mahakamani tuijadili,” alidai Sheikh Farid.

Mshtakiwa wa 12, Salum Alli Salum, aliomba mahakama imwite daktari ili aweze kufanyiwa uchunguzi wa afya yake kwani ameingiliwa kijinai kwa nguvu.

“Mheshimiwa tunalazimishwa kutoa maelezo wanayoyataka wao, wanatuingilia kinyume cha maumbile, wanaingiza majiti, chupa, wengine wanavuja nyuma, kama unaweza hakimu twende faragha nikakuonyeshe.

“Askari ameniingilia kisha akaniingiza jiti mpaka likakatika, kungekuwa na sehemu ningekuonyesha, Jeshi la Polisi la kwanza kuvunja sheria, waliofanya madhila haya wanawatukanisha Watanganyika na kufanya waonekane wabaya,” alidai mshtakiwa huyo.

Baada ya washtakiwa hao kutoa malalamiko yao, mahakama iliwaahidi washtakiwa hao waende wakahojiwe na muda wote watakuwa katika mazingira salama.

Sheikh Faridi na wenzake 19 wanashtakiwa kwamba kati ya Januari 2013 na Juni 2014 maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikula njama ya kutenda kosa la kuingiza watu nchini kufanya ugaidi.

Shtaka la pili linawakabili washtakiwa wote, wakidaiwa kuwa katika kipindi hicho walikubaliana kumuingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.

Katika shtaka la tatu linalomkabili Sheikh Farid, anadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014 maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akijua ni kosa, alimuingiza nchini Sadick na Farah kufanya ugaidi.

Sheikh Farid pia anadaiwa kuwahifadhi Sadick na Farah, huku akijua watu hao walitenda vitendo vya kigaidi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Jamal Swalehe, Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassani, Hussein Ally na Juma Juma.

Wengine ni Saidi Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Nassoro na Said Sharifu.

Wakati huohuo, kesi nyingine ya ugaidi inayomkabili Kiongozi Mkuu wa JUMIKI, Sheikh Mselem Ali Mselem na mwenzake, Abdallah Said Ali, imeahirishwa hadi Septemba 3, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa kwa sababu Sheikh Mselem hakuwapo anaumwa.

CHANZO: MTANZANIA.

Mjumbe wa CCM ‘ajiunga’ Ukawa

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Ali Mohamed Kessy ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM) akiwatangazia waandishi wa habari kuunga mkono muundo wa serikali tatu uwepo katika Katiba Mpya, mjini Dodoma jana. Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati namba moja ya bunge hilo, Ummy Mwalimu na Makamu wake, Prof Makame Mbarawa ambao walimwita Kessy kumtaka kukanusha kuhusu taarifa yake ya kuwapo tatizo la akidi kwenye vikao vya kamati.
Dodoma. Jana ilikuwa kama sinema pale viongozi wa Kamati Namba Moja ya Bunge Maalumu walipojikuta wakibishana na mjumbe wao mbele ya waandishi wa habari, huku siri za mambo ya ndani ya vikao zikianikwa hadharani.

Kamati hiyo inaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu na makamu wake ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, huku ikiwa imesheheni vigogo wengine wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Viongozi wengine katika kamati hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uhusiano na Uratibu), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.

Wamo pia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.

Jana asubuhi, Mwalimu na Profesa Mbarawa walifika mbele ya waandishi wa habari katika Hoteli ya St Gasper wakiwa wameambatana na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy.

Lengo la mwenyekiti na makamu wake lilikuwa ni kumbana Keissy ili akanushe taarifa aliyoitoa juzi kwenye moja ya televisheni kwamba kamati hiyo inaongoza kwa kuvunja kanuni hasa katika suala la akidi ya vikao kutotimia.

Sinema ilivyoanza
Walipofika mbele ya waandishi wa habari, Keissy alipewa fursa ili akanushe taarifa yake, lakini alibadili mada na kuanza kuzungumzia masuala ya muundo wa Serikali na Bunge, huku akisema yeye ni muumini wa serikali tatu na siyo mambo ya serikali mbili zinazopendekezwa na wengi kutoka katika chama chake.

Kauli hiyo iliwashtua Mwalimu na Profesa Mbarawa ambao walianza kumkatisha ili asiendelee.
“Keissy sikukuitia mambo hayo, huu ni mkutano wangu, naomba ukanushe nilichokuitia, hayo utazungumza baadaye tafadhali sana,” alisema Mwalimu.

Wakati huo Profesa Mbarawa na waandishi wa habari waliokuwapo walivunjika mbavu kwa vicheko, huku yeye akiendelea kusisitiza kwamba ni muumini wa Tanganyika.

Wakati akisema hayo, Profesa Mbarawa naye aliingilia kati na kumtaka Keissy kueleza kilichompeleka hapo huku akimtaka aache kelele za kupotosha wananchi kwa kuwa anachosema siyo kweli.


Alipopewa nafasi ya kuzungumzia jambo hilo, Keissy alisema: “Jana (juzi), mimi nilihesabu mara mbili nikaona Zanzibar hawajatimia lakini kumbe mmoja nilimfanya akawa mtu wa Tanganyika, kwa hilo nilighafilika, lakini mle ndani mambo siyo mazuri,” alisema Keissy.

Kabla hajaendelea Mwalimu alidakia na kumtaka anyamaze kimya kwa kuwa huo haukuwa mkutano wake, ili yeye (Mwalimu) aendelee kueleza mambo yaliyojiri ndani ya kamati.

“Jamani waandishi si mnaona amekanusha, huu ni mkutano wangu na yeye sitaki azungumze mambo ya mle ndani kwa kuwa msemaji ni mimi au makamu wangu au mtu yeyote atakayeteuliwa na mwenyekiti, sasa tunaendelea,” alisema Mwalimu.

Mara baada ya Mwalimu kutoa taarifa ya kamati yake kwa waandishi wa habari na kumaliza kujibu maswali, alinong’ona na Profesa Mbarawa na hapo wakampa nafasi Keissy ili azungumze kwa ufupi mambo yake lakini palepale mbele yao.

Kauli za Keissy
Akitumia fursa hiyo, Keissy alisema: “Kuna mambo yanafanywa mle ndani ambayo mimi na wenzangu wengine tunalazimishwa, hatukubaliani nayo likiwamo suala la kuizika Serikali ya Tanganyika wakati wa upande wa pili (Zanzibar) wanapewa nafasi na kunufaika na rasilimali za nchi hii, ndugu zangu huu ni uonevu.”

Alisema uonevu huo umekuwa mkubwa kwa wabunge wa Tanzania Bara ukilinganisha na wenzao wa Zanzibar ambao alisema wanakula fedha nyingi za bure ilihali hawafanyi kazi za Tanganyika.

“Ndugu zangu, hapa tusidanganyane, we fikiria watu zaidi ya 50 wanatoka kule Zanzibar na kuja kutuamulia mambo yetu, hii si halali hata kidogo. Haiwezekani mtu wa Zanzibar akaja kuzungumzia masuala ya Nkasi wakati hayajui,” alisema.

Alisema kuwa msimamo wake siku zote ni serikali tatu na kwamba hatayumbishwa na vitisho au jambo la aina yoyote hata kukiwa na kulazimishwa.

Mbunge huyo alisema kuwa kutakuwa na urahisi wa kuongoza Serikali kama Tanganyika itapewa hadhi yake kuliko ilivyo sasa kwa serikali mbili zinazopigiwa upatu.

Kwa mapendekezo yake alisema ni vyema likawepo Bunge la Tanganyika, Bunge la Zanzibar na kisha miongoni mwa wabunge hao, wachaguliwe wachache kuunda Bunge la Muungano.

Aliendelea kusisitiza kuwa wabunge kutoka Zanzibar wanawanyonya wenzao wa Tanzania Bara kwa kila kitu kauli ambayo ilionekana kumkera Profesa Mbarawa na kuamua kumkatisha asiendelee kuzungumza.

Wakati akiendelea kuzungumza, viongozi hao walimkatisha tena na kumwambia akubali waondoke pamoja kuendelea na vikao vya kamati. Baada ya hapo, Mwalimu na Profesa Mbarawa walinyanyuka na kuanza kuondoka, lakini Keissy alisimama na kuendelea kuzungumza na waandishi wa habari.

Baada ya kuona anaendelea, Profesa Mbarawa alirudi na kumshika mkono Kessy huku akisema; “Mheshimiwa Keissy twende bwana, maana ukimwacha huku huyu atazungumza mambo mengi.”

Wakati akiondoka eneo hilo, Keissy alipaza sauti akiwaambia waandishi wa habari: “Angalieni tunavyodhibitiwa, lakini msimamo ni huo wala sitayumba ngoja tukaendelee lakini mimi ndiyo mtoa habari namba moja.”

Msimamo wa serikali tatu ni wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) waliosusia Bunge.

CHANZO: MWANANCHI.