|
Jaji Joseph Sinde Warioba akitolewa nje ya ukumbi wa Ubungo Plaza jijini
Dar es salam baada ya kuzuka kwa vurugu katika ukumbi huo jana. |
Fredy Azzah na Shabani Matutu, Dar es Salaam
MDAHALO wa
kujadili Katiba inayopendekezwa ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu
Nyerere, jana ulivunjika baada ya kutokea vurugu ambako Mwenyekiti wa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipigwa
vibao shingoni na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa CCM.
Hali hiyo
ilijitokeza kwenye Hoteli ya Blue Pearl iliyopo Ubungo Dar es Salaam,
baada ya kuvunjika mdahalo huo uliokuwa umehudhuriwa na mamia ya watu,
wengi wao wakiwa vijana.
Baada ya vurugu hizo, waandaji waliamua
kuwatoa nje ya ukumbi wasemaji wa mdahalo huo akiwamo Warioba,
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Profesa
Palamagamba Kabudi na Profesa Mwesiga Baregu.
Wengine waliokuwa
wazungumze kwenye mdahalo huo ni Humphrey Polepole na Rais wa Chama
cha Wanasheria Zanzibar, Awadhi Said, ambao wote walikuwa wajumbe wa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Warioba, aliyewahi kushika
wadhifa wa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, alipigwa vibao viwili
shingoni alipofika kwenye mlango kuu wa kutoka ukumbini ambako kulikuwa
na msongamano mkubwa wa watu. Wakati huo, Warioba na viongozi wenzake
walikuwa wakitolewa nje ya ukumbi huo.
Hatua hiyo ilifanya mlinzi
wake na baadhi ya watu waliokuwa wakimtoa kiongozi huyo waongeze mwendo
na kumkimbiza kiongozi huyo wa taifa kwenye chumba maalumu cha wageni wa
heshima (VIP lounge), kilichoko ndani ya hoteli hiyo.
Wakati Warioba akipigwa vibao, miongoni mwa watu waliokuwa karibu nyuna yake ni Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM, Paul Makonda.
Kwa
sababu hiyo, baadhi ya vijana walichangia kumpiga kada huyo wa UVCCM
aliyekuwa amevalia shati jeupe, huku wakimzuia kuingia kwenye chumba
cha VIP ambako Jaji Warioba alikuwa amepelekwa.
Kufanikiwa kwa
vijana hao kumzuia Makonda kuingia kwenye chumba hicho, kulitoa fursa ya
kuendelea kupigwa hadi alipoponyoka na kukimbilia katika ofisi moja
katika jengo hilo na kujifungia.
Baada ya kujificha katika chumba hicho, vijana hao waliitana na kuhamasishana ili wavunje mlango huo na kumtoa Makonda.
Hata
hivyo baada kufanikiwa kuvunja mlango huo, vijana hao hawakumuona
Makonda hadi walinzi wa hoteli hiyo na askari kanzu walipofika hapo na
kuwafukuza.
Vurugu zilivyoanza
Vurugu katika mdahalo huo zilianza muda mfupi kabla ya Jaji Warioba aliyekuwa msemaji wa kwanza, kumaliza hotuba yake.
Baada
ya kumaliza kuichambua Katiba inayopendekezwa, Jaji Warioba alisema
katika kuitetae katiba hiyo, baadhi ya watu wamekuwa wakimtumia Baba wa
Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere kuunga mkono hoja zao.
“Tunatumia jina la Mwalimu ili kuunga mkono hoja zetu wakati mwingine ninajiuliza hivi tunatumia Mwalimu yuleyule ama…
“Mwalimu
amekufa akisema hajaona hata sehemu ya kutia koma katika Azimio la
Arusha, kuna watu waliwahi kumletea Mwalimu barua wakimwambia afungue
akaunti nje ya nchi ndiyo fedha zake zitakuwa salama… Mwalimu siyo tu
alikataa lakini alitangaza kila kitu hadharani.
“Leo Mwalimu
angekuwapo angekubali watu wafungue akaunti nje ya nchi, angekubali
watu wapewe zawadi wakae nazo… nikasema huyo wao siyo Mwalimu, Mwalimu
alikuwa ni mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi mgumu hata unaomhusu
yeye,” alisema Warioba.
Vijana na mabango
Baada ya maneno
hayo, baadhi ya vijana takriban 20, walisimama na kunyanyua juu mabango
yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali wa kumtukana Jaji Warioba na mengine
yakisifu Katiba inayopendekezwa.
Kitendo hicho kilifanya baadhi ya watu kujaribu kuwakalisha chini huku wengine wakichana mabango hayo hali iliyozusha vurugu.
Wakati
wote huo Jaji Warioba alikuwa amesimama akijaribu kuwasihi watu hao
kukaa chini, lakini hali hiyo ilionekana kutozaa matunda.
Baada ya
muda vijana hao walijitenga pembeni karibu na jukwaa kuu huku wakiwa
na mabango yao, wakiimba nyimbo mbalimbali za CCM.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu watoke ukumbini huku wengine wakiwa wanarudi kuketi kwenye viti vyao.
Wakati
vurugu hizo zikiendelea, Profesa Kabudi na Butiku kwa nyakati tofauti,
walionekana wakimtaka Makonda kuwatuliza vijana hao wa CCM ambao
alidaiwa yeye yeye ndiye aliwaingiza katika ukumbi huo.
Wakati
viongozi wakimtaka Makonda kufanya hayo, vijana wengine walionekana
kumvuta Makonda wakitaka kumpiga hali iliyomlazima kumtumia kama kinga,
Amon Mpanju, ambaye alikuwa Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
akiwakilisha kundi la walemavu.
Hali iliendelea hivyo hadi baadhi
ya vijana waliokuwa wamekaa walipohamasishana na kuwapiga wale
waliokuwa na mabango, kwa kutumia viti hali iliyofanya wakimbie na
kutoka nje ya ukumbi huo.
Baada ya vijana hao kutoka nje, hali
iliwageukia Makonda na Mpanju ambao baada ya kuona hali imekuwa tete,
walikimbilia kwenye jukwaa kuu na kukaa karibu na Jaji Warioba.
Huku
hali ikiwa bado ya taharuki, viongozi hao (Warioba na wenzake) waliamua
kutoka nje ya ukumbi na ndipo zahama ya kupigwa vibao kwa Jaji Warioba
ilipojitokeza.
Butiku: Hii ni siku ya aibu
Baada ya vurugu
hizo kuisha Jaji Warioba hakurejea na badala yake Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisimama na kuiita siku ya
aibu kwa Watanzania.
Alisema tukio la vurugu ndani ya ukumbi wa mdahalo huo limeshuhudiwa na Watanzania nchi nzima.
“Baadhi
ya wahuni waliofanya tukio hilo tunawatambua hivyo katika mikutano yetu
ijayo hatutawaruhusu kushuhudia midahalo yetu,” alisema.
Butiku
alisema kuwa tukio hilo halitakuwa mwisho wa kuendelea kwa midahalo ya
taasisi iliyopangwa kufanyika Mwanza, Mbeya, Zanzibar na Tanga.
Jaji Warioba apata watetezi
Akizungumzia
kadhia iliyotokea katika mkutano huo, mmoja wa waliohudhuria mdahalo
huo, Halfan Said, alisema amesikitishwa na fujo zilizofanywa na vijana
wa CCM waliofikia hatua ya kumpiga Jaji Warioba.
“Warioba kama
raia mwingine wa kawaida anayo haki ya kutoa maoni yake na yanastahili
kuheshimiwa na pia hakustahili kufanyiwa vurugu aliyofanyiwa na vijana
hawa wa CCM ambao wameshindwa kuheshimu hata madaraka aliyowahi
kuitumikia nchi hii na chama chake,” alisema.
Rudovick Mosha
alisema kuonekana kwa kada wa CCM, Paul Makonda, kunaonyesha dhahiri
chama hicho kilikuwa nyuma ya mpango huo mchafu wa kumfanyia vurugu Jaji
Warioba katika mdahalo huo.
Katibu Mkuu wa Mtandao wa Wanafunzi
Tanzania (TSNP-Tanzania), Alphonce Lusako, alisema amesikitishwa kwa
tukio la vijana wa CCM kushindwa kusikiliza hoja na badala yake kufanya
vurugu.
“Inatubidi vijana nchini tufikie mahali tukatae kutumika
na kusema kuwa imetosha kutumika tuweze kusonga mbele kuepusha
yaliyotokea,” alisema Lusako.
Naye Pius Mchulu alisema kumpinga Jaji Warioba ni kuukomaza na kuboresha ujinga na umasikini kwa wanyonge.
Aliyekuwa
Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea
Nkya, alitoa onyo kwa kundi lililofanya tukio hilo lenye nia ya
kunyamazisha sauti za watu kuwa watakuwa wamejitafutia anguko.
“Suala
la kusema na kusikilizwa ndiyo demokrasia na unapozuia mwisho hautakuwa
mbali kwani Mungu anawaona na mwisho wa maovu yao unakaribia.
“Aliyeandaa tukio hilo la vurugu kwa Jaji Warioba atakutana na upanga wa Mungu na hata baki salama,” alisema Nkya.
Mbunge
wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema tukio hilo
limedhihirisha kwamba dola inazama kwa kuwa mbinu wanazotumia kwa sasa
ni dhaifu zilizowahi kutumiwa zamani na madikteta.
Katika vurugu hizo za kurushiana viti, mwandishi wa BBC, Arnold Kayanda alijikuta akipigwa kichwani na kiti.
Mabango, nyimbo zatawala
Baadhi
ya mabango ya karatasi waliyosimama nayo vijana wa CCM yalikuwa na
ujumbe uliosomeka: “Katiba inayopendekezwa tumepokea na tunaiunga
mkono”, “Katiba hii tumeiona, tumeielewa na tunaikubali”. Mabango
mengine yalikuwa na ujumbe wa matusi kwa Jaji Warioba.
Vijana hao
ambao hata hivyo hawakuwa wengi katika ukumbi huo walianza kusikika
wakiimba nyimbo za CCM kwa maneno ya ‘CCM nambari wani’.
Mmoja wa vijana hao alikataa kutaja jina lake lakini alisikika akisema kuwa, “tumechoka kudanganywa na Jaji Warioba.”
Wakati
zilipozuka vurugu hizo na watu wakaanza kutoka nje, polisi walikuwa
wakipiga risasi hewani nje ya ukumbi lakini hawakuingia ndani kuzuia
vurugu hizo.
CHANZO: MTANZANIA