Na Othman Khamis
Ame - OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefungua milango kwa
kuruhusu kila mwananchi na hasa Vijana kujituma kwa kutumia kipaji alichonacho
katika kufanya kazi itakayomsaidia kuendesha maisha yake ya kila siku.
Alisema vipaji walivyonavyo baadhi ya
watu kama kazi za amali pamoja na kilimo na ufugaji vinaweza
kuondosha vikwazo vya wananchi hao katika kuelekea kwenye matumaini mema.
Balozi Seif alisema hayo wakati akizindua
utoaji wa mikopo ya mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Kisiwani Pemba huko
Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo shughuli kama hiyo tayari ameshaifanya
kwa vikundi cha wajasiri amali wa kisiwa cha Unguja.
Vikundi 13 vya wajasiri amali hao kutoka Wilaya
zote Nne za Pemba wamekabidhiwa hundi za mikopo ya fedha zenye thamani ya
shilingi milioni 30,000,000/- kati ya Milioni 70,000,000/- zilizoidhinishwa na
mfuko huo wa uwezeshaji wananchi Kiuchumi.
Balozi Seif alisema Serikali iliamua
kuimarisha mfuko huo ukilenga Vijana, akina mama na makundi maalum ya jamii kwa
kuwapatia mitaji itakayowawezesha kujiajiri ili kupunguza utegemezi.
Alifahamisha kwamba mkopo wa fedha
zilizotolewa ni maalum kwa kusaidia wananchi wa kipato cha chini ambao hawana
njia madhubuti za kuendesha maisha yao.
“Kila Kijana ana haki ya kuipata huduma
hii. Hivyo vijana wetu tunawafungulia milango na cha msingi ni kufuata taratibu
zilizowekwa na Wizara husika katika kukopa na kurejesha “. Alieleza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba
wale waliosaidia kuchangia mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi waendelee na
juhudi hizo ambazo ni jambo jema kwa vile huduma za mikopo hiyo itakuwa
imekurubishwa kwa walengwa.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi
wa Jamii, Wanawake na Watoto Bibi Asha Abdulla alisema uanzishwaji wa mfuko huo
utawaongezea mtaji wajasiri amali ambao hushindwa kuchukuwa mikopo katika
taasisi za kibenki kutokana na ukubwa wa riba.
Alisema juhudi zitaendelea kuchukuliwa na
Serikali kupitia Wizara inayosimamia Uwezeshaji katika kuujengea nguvu
zaidi mfuko huo ili uzidi kuwahudumia wajasiri amali kwa kipindi kirefu kijacho.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla
hiyo ya uzinduzi wa utoaji mikopo ya mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi,
Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto Mh. Zaiban Omar
Mohamed alisema maombi 433 kutoka vikundi 40 tayari yameshapokelewa na mia 109
kati ya hayo yameshapitishwa.
Waziri Zainab alisema vikundi vinavyohitaji
kukopeshwa lazima viwe na shughuli za uzalishaji unaoweza kuhimili
ulipaji mkopo sambamba na kujiongezea mapato ili viweze kujiendesha kwa muda
mrefu.
Vikundi 13 vya Wilaya Nne zilizomo ndani
ya Kisiwa cha Pemba vimepatiwa hundi za fedha za mikopo hiyo inayohitaji kurejeshwa
kwa muda utakaokubalika kati ya pande hizo mbili.
Vikundi hivyo ni Heri ya moyo mmoja,
kulegea si kung’oka, tudumishe amani na juhudi zetu vilivyomo Wilaya ya
Micheweni wakati vile vya Wilaya ya Wete ni pamoja na Usilolijua, tupendane na
haviliki.
Vyengine ni Maendeleo, Nia safi iwepo, Pemba
Sea Cliff vya Wilaya ya Chake chake wakati vile vya Wilaya ya Mkoani ni
Muelekeo, Tuishi kwa usalama pamoja na walemavu.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi vifaa vya ukulima wa mwani
vilivyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali
Mohd Shein kwa ajili ya kikundi cha ukulima wa mwani cha Maneno hayasaidii kitu
cha Wilaya ya Micheweni.
Dr. Shein alitoa msaada huo wa Kamba na
Tai Tai wenye thamani ya shilingi Milioni 3,000,000/- kufuatia ahadi
aliyopitowa kwa Kikundi hicho wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Mkoa wa
Kaskazini Pemba miezi ya hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment