Mjumbe wa Baraza kuu la Uongozi la CUF na Mwakilishi wa Jimbo la Mjimkongwe Mh. Ismail Jussa Ladhu. |
Migongano hiyo ya kimtazamo inazidi kuliweka taifa
katika umbile la mshazari, huku matumaini ya kupatikana kwa Katiba mpya
ya Jamhuri ya Muungano yakionekana kupotea kutokana na kundi la wabunge
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukataa kuendelea kushiriki
Bunge la Katiba kwa madai kuwa CCM imekuja na rasimu yake.
Hata hivyo misimamo hiyo si kwamba inaonekana
kuwachanganya wananchi tu bali pia inazidisha taharuki ya wananchi
kutoelewa hatima ya upatikanaji wa Katiba na mfumo upi ambao ni sahihi
katika kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikisha umri wa
miaka 50.
Kundi la Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar, wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd
limeeleza neema, fanaka na matunda ya Muungano wa Serikali mbili
kiuchumi, kisiasa, kiulinzi na kiusalama.
Wakati huohuo kundi la viongozi wa CUF chini ya
Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, linasisitiza kuwa
lazima Zanzibar ipate mamlaka kamili ya dola.
Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF Ismail Jussa Ladhu,
akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Vuga,
amesema CUF iliunga mkono pendekezo la Serikali tatu kama ngazi ambayo
ingekisaidia chama hicho kufikia malengo ya kupatikana mamlaka kamili ya
Zanzibar.
Jussa anasema bila Zanzibar kupata uraia wake,
hati ya kusafiria, mambo ya nje, kiti Umoja wa Mataifa, Sarafu na benki
kuu, Serikali tatu hazina tija wala faida yeyote kwa Wazanzibar.
Anasema madai ya msingi ya Wazanzibari ni kupatikana kwa mamlaka huru za Tanganyika na Zanzibar.
Anasema yatakapopatika masuala hayo na kubaki
katika mikono ya Zanzibar kama dola kamili, Zanzibar itakapoweza
kujikwamua na kupiga hatua nyingi za kiuchumi, kinyume na hali ilivyo
sasa ya kuwa kama mgeni mualikwa katika Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
Amesisitiza kuwa lengo kuu la kukutana kwa Rais
mstaafu wa Zanzibar Dk Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif
Novemba 5 mwaka 2009, licha ya kusaka maridhiano ya kisiasa na kuzika
uhasama, ilikuwa ni mpango wa kuweka nguvu ya pamoja ili kuipatia
Zanzibar mamlaka kamili.
Bila ya kupepesa maneno Jussa amesema kwamba kwa
bahati mbaya warithi wa Dk Karume wamekuwa wakiyumba, huku wakishndwa
kuungana na kudai masuala ya msingi bila ya Wazanzibari kuungana na kusimama pamoja, madai yao hayataweza kufikiwa.
Wassira amjibu Jussa
Akijibu mapigo ya Jussa katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Jimbo la Mtoni , Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Stephen Wasira
anasema kimsingi wanachokitaka CUF na viongozi wake si Muungano bali
wana nia na dhamaira ya kuligawa taifa na kuvunja Muungano.
Wassira anasema Muundo wa Muungano wa Serikali
mbili si kioja au kituko kwani hata mataifa ya Uingereza na Marekani
yana mfumo wa aina hiyo, huku wakiwa na kiti kimoja Umoja wa Mataifa .
Anasema kudai kiti Umoja wa Mataifa, sarafu, uraia
au Benk Kuu ni mwelekeo wa kuvunja Muungano. Akamtuhumu Jussa na
wenzake kuwa ni mawakala wa mabeberu na wakoloni wanaopigania Zanzibar
irejee katika mikono ya watawala waliopinduliwa mwaka 1964.
Wassira anasema mwanasiasa huyo amekuwa akikerwa
na kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi kwani hata wakiwa kwenye Kamati za
Bunge maalumu la Katiba ametaka siku ya Januari 12,1964 iondolewe katika
orodha ya sikuu za kitaifa.
Balozi Seif anasema ikiwa wajumbe wa Ukawa
wataendelea kushikilia msimamo wao wa kukataa kurudi bungeni ili kujenga
nguvu ya hoja na kupatikana katiba bora, watakaopoteza turufu na kupata
hasara ni Wazanzibari
Anasema kwa kiasi kikubwa madai ya Zanzibar ili
iweze kujikwamua kiuchumi na kushamirisha maendeleo yake, yamezingatiwa
katika Rasimu ya Katiba Mpya, hivyo ni jukumu la Wazanzibari kutambua
jambo hilo na kupigania kupatikana Katiba Mpya.
Seif naye anena
Maalim Seif anasema hakuna mbunge atakayerejea
bungeni kupitisha rasimu ya katiba ambayo haikuzingatia matakwa na madai
ya msingi ya wananchi.
Kwa kuwa CCM wanataka kubaki na serikali mbili,
basi moja iwe ya Tanganyika na ya pili ya Zanzibar; zote zikiwa na
mamlaka kamili kama ilivyokuwa kabla ya kuungana mwaka April 26, 1964
Ni wazi kinachoonekana sasa kadri unavyofuatilia
madai ya CCM na CUF ni kama mchezo wa paka na panya ambao unafanyika
huku taifa likihitaji ipatikane katiba mpya ambayo itazingatia mahitaji
mapya kulingana na wakati, usalama wa nchi, utulivu na mapatano ya
kijamii.
CHANZO: MWANANCHI.
Matamshi ya Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Umoja wa
Mataifa (UNDP) Hellen Clark yanayowataka wabunge wa kundi la Ukawa
kurudi bungeni, yanadhirisha madai kuwa nje ya bunge ni vigumu
kupatikana Katiba mpya na wanachokifanya Ukawa ni kupoteza wakati.
Msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano uko
wazi kufuatia kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba endapo rasimu mpya ya
katiba haitapitishwa kwa kukosekana theluthi mbili ya maamuzi ya Wajumbe
wa Bunge maalum la Katiba, taifa litaongozwa na Katiba ya mwaka 1977.
CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment