Thursday, 26 June 2014

Msekwa atoboa siri ya CCM kung’ang’ania serikali mbili

Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Pius Msekwa
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa ametoboa siri ya chama hicho kung’ang’ania Muungano serikali mbili akisema hiyo ndiyo sera yake pekee iliyopitishwa na wanachama wake wote kwa kura ya maoni.
 
Msekwa alieleza hayo katika mahojiano maalumu na wahariri wa gazeti hili yaliyofanyika nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam.

Msekwa ambaye katika habari iliyochapishwa na gazeti hili jana alieleza kuwa binafsi, hana tatizo na suala la idadi ya Serikali katika Muungano, alisema kamwe hawezi kukishauri chama chake kukubaliana na mapendekezo ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya muundo wa serikali tatu.

“Siwezi kuishauri CCM kukubali serikali tatu. Hili la Serikali mbili ni sera ya CCM, siyo tu sera ya kawaida, bali hii ni sera pekee iliyopitishwa na wanachama wote kwa kura ya maoni,” alisema Msekwa ambaye pia ni Spika mstaafu wa Bunge.

Alisema tofauti na sera hiyo ya serikali mbili, sera nyingine za chama hicho huanzia katika ngazi ya Kamati Kuu, kujadiliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na kupitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa.

Msimamo ulikoanzia
Kiini cha sera hiyo kutengenezewa utaratibu maalumu, kilitokana na sakata la Kundi la Wabunge 55 (G55), kuanzisha agenda ya kutaka Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano na hatimaye Bunge kupitisha Azimio la kuanzisha serikali hiyo.

Msekwa ambaye wakati huo alikuwa Naibu Spika lakini akiongoza Bunge kutokana na aliyekuwa Spika, Chifu Adam Sapi Mkwawa kuwa mgonjwa, alisema ushauri wa kurudi kwa wanachama wa CCM kuwauliza wanataka serikali ngapi ulitolewa na Mwalimu Julius Nyerere.

Itakumbukwa kuwa hatua ya Bunge kupitisha azimio hilo la kuanzisha Serikali ya Tanganyika ilimkera Mwalimu hadi akatunga kitabu, Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania akiwashutumu aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela na aliyekuwa Katibu Mkuu wa (CCM), Horace Kolimba.

“Mwalimu alitueleza kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa, kuwa Bunge limekwishapitisha azimio na likipitishwa ni lazima litekelezwe na Serikali. Alisema mkikataa azimio la Bunge hivihivi mtaleta mgongano wa kikatiba, msiamue peke yenu, nendeni kwa wanachama wote muwaulize ili uamuzi uwe wa wote,” alisema.

Alisema kutokana na ushauri huo, mwaka 1993 CCM iliandaa na kusimamia upigaji kura za siri za maoni katika kila tawi, wanachama wakitakiwa kujadili na kuchagua kati ya serikali moja, mbili au tatu.

“Matokeo yalipofika katika Halmashauri Kuu, ilionekana wanachama walio wengi katika matawi mengi walitaka serikali mbili, na hapo ndipo ikapitishwa sera ya serikali mbili,” alisema na kusisitiza:

“Siwezi kwenda kinyume na wanachama wengi wa CCM, ila mimi binafsi kama mtaalamu wa katiba na baada ya kusoma mambo mengi, hili la idadi ya serikali halinipi shida, bali ninachoona cha muhimu ni uimara wa Muungano.”

Mvutano wa muundo wa serikali uliibuka baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba kupendekeza Tanzania kuwa na serikali tatu; ya shirikisho, Tanganyika na Zanzibar.

Huku baadhi ya wananchi hususan vyama vya upinzani vikiunga mkono mapendekezo hayo, CCM kimeweka wazi msimamo wake wa kupinga msuguano ambao ulichangia kwa kiwango kikubwa mpasuko ndani ya Bunge Maalumu la Katiba na kuwafanya wajumbe ambao waliunda Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao huku wakiweka sharti la kujadiliwa kwa mapendekezo ya Tume ya Warioba kurejea bungeni.

CHANZO: MWANANCHI

Monday, 23 June 2014

Balozi Seif azuwia ujenzi katika eneo la Masoko Makongwe Wete

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Na Othman Khamis Ame - OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Seif Ali Iddi ameonya kuzuiwa kufanywa kwa ujenzi wa aina wowote katika eneo la Masoko makongwe liliopo Mtaa wa Selemu ndani ya Mji wa Wete hadi Serikali Kuu itakapotoa maamuzi yake.

Balozi Seif alitoa onyo hilo mara baada ya kuliangalia eneo hilo lililoleta mgogoro baina ya Uongozi wa Baraza la Mji Wete pamoja na Wafanyabiashara wa soko hilo dhidi ya mfanyabiashara Ahmed Abdulla Mapete aliyeuziwa sehemu hiyo na baadhi ya watendaji wa Baraza la Mji Wete kinyume na taratibu za Serikali.

Alisema Serikali ilitenga eneo hilo maalum kwa ajili ya huduma za soko ili litoe huduma kwa wakaazi wa Mji huo tokea mwaka 1942. Hivyo amewaagiza wafanyabiashara wanaoendesha biashara zao katika sehemu hiyo waendelee kama kawaida hadi Serikali Kuu itakapotoa maamuzi kutokana na mgogoro huo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimekea vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma wanaoamua kujichukulia maamuzi mikononi mwao kinyume na taratibu zilizowekwa na Serikali na hatua za kuwawajibisha hazitochelea kuwachukulia dhidi ya watumishi hao.

“ Hili ni soko lililotengwa na Serikali kwa ajili ya kuwajengea mazingira wananachi kupata huduma za msingi za mahitaji yao ya kila siku. Sasa hii tabia ya baadhi ya watendaji kujichukulia maamuzi kwa kuzitelekeza mali za Serikali wamepewa amri na nani ? “ Alikemea Balozi Seif.

Balozi Seif alisema kwamba mtu ye yote atakayeamua kuuza eneo la Serikali bila ya idhini ya Taasisi inayohusika na masuala ya ardhi aelewe kwamba anafanya makosa na Serikali haitakuwa tayari kulipa fidia endapo mali au jengo aliloiweka katika ardhi hiyo itaondoshwa.

Alifahamisha kwamba mgogoro wa soko kongwe la Selemu Wete tayari unaeleweka Serikalini na muda si mrefu maamuzi rasmi ya suala hilo la muda mrefu yatatolewa kwa mujibu wa sheria na taratibu za Serikali.

Vikundi 13 vya wajasiri amali Pemba vyapatiwa mikopo.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiambatana na Mkewe Mama Pili Juma Iddi Kushoto yake, Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Nd. Mwanajuma Majid pamoja na Waziri wa Uwezeshaji, ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar wakiwasili uwanja wa Michezo Micheweni kwa ajili ya uzinduzi wa uitoaji Mikopo ya mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.


Na Othman Khamis Ame - OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefungua milango kwa kuruhusu kila mwananchi na hasa Vijana kujituma kwa kutumia kipaji alichonacho katika kufanya kazi itakayomsaidia kuendesha maisha yake ya kila siku.

Alisema vipaji walivyonavyo baadhi ya watu  kama kazi za  amali pamoja na kilimo na ufugaji vinaweza kuondosha vikwazo vya wananchi hao katika kuelekea kwenye matumaini mema.

Balozi Seif alisema hayo wakati akizindua utoaji wa mikopo ya mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Kisiwani Pemba huko Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo shughuli kama hiyo tayari ameshaifanya kwa vikundi cha wajasiri amali  wa kisiwa cha Unguja.

Vikundi 13 vya wajasiri amali hao kutoka Wilaya zote Nne za Pemba wamekabidhiwa hundi za mikopo ya fedha zenye thamani ya shilingi milioni 30,000,000/- kati ya Milioni 70,000,000/- zilizoidhinishwa na mfuko huo wa uwezeshaji wananchi Kiuchumi.

Balozi Seif alisema Serikali iliamua kuimarisha mfuko huo ukilenga Vijana, akina mama na makundi maalum ya jamii kwa kuwapatia mitaji itakayowawezesha kujiajiri ili kupunguza utegemezi.

Alifahamisha kwamba mkopo wa fedha zilizotolewa ni maalum kwa kusaidia wananchi wa kipato cha chini ambao hawana njia madhubuti za kuendesha maisha yao.
 
“Kila Kijana ana haki ya kuipata huduma hii. Hivyo vijana wetu tunawafungulia milango na cha msingi ni kufuata taratibu zilizowekwa na Wizara husika katika kukopa na kurejesha “. Alieleza Balozi Seif. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba wale waliosaidia kuchangia mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi waendelee na juhudi hizo ambazo ni jambo jema kwa vile huduma za mikopo hiyo itakuwa imekurubishwa kwa walengwa.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto Bibi Asha Abdulla alisema uanzishwaji wa mfuko huo utawaongezea mtaji wajasiri amali ambao hushindwa kuchukuwa mikopo katika taasisi za kibenki kutokana na ukubwa wa riba.

Alisema juhudi zitaendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Wizara inayosimamia Uwezeshaji  katika kuujengea nguvu zaidi mfuko huo ili uzidi kuwahudumia wajasiri amali kwa kipindi kirefu kijacho.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo ya uzinduzi wa utoaji mikopo ya mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto Mh. Zaiban Omar Mohamed alisema maombi 433 kutoka vikundi 40 tayari yameshapokelewa na mia 109 kati ya hayo yameshapitishwa.

Waziri Zainab alisema vikundi vinavyohitaji kukopeshwa  lazima viwe na shughuli za uzalishaji unaoweza kuhimili ulipaji mkopo sambamba na kujiongezea mapato ili viweze kujiendesha kwa muda mrefu.

Vikundi 13 vya Wilaya Nne zilizomo ndani ya Kisiwa cha Pemba vimepatiwa hundi za fedha za mikopo hiyo inayohitaji kurejeshwa kwa muda utakaokubalika kati ya pande hizo mbili.

Vikundi hivyo ni Heri ya moyo mmoja, kulegea si kung’oka, tudumishe amani na juhudi zetu vilivyomo Wilaya ya Micheweni wakati vile vya Wilaya ya Wete ni pamoja na Usilolijua, tupendane na haviliki.

Vyengine ni Maendeleo, Nia safi iwepo, Pemba Sea Cliff vya Wilaya ya Chake chake wakati vile vya Wilaya ya Mkoani ni Muelekeo, Tuishi kwa usalama pamoja na walemavu.
 
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi vifaa vya ukulima wa mwani vilivyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Shein kwa ajili ya kikundi cha ukulima wa mwani cha Maneno hayasaidii kitu cha Wilaya ya Micheweni.

Dr. Shein alitoa msaada huo wa Kamba na Tai Tai wenye thamani ya shilingi Milioni 3,000,000/- kufuatia ahadi aliyopitowa kwa Kikundi hicho wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Mkoa wa Kaskazini Pemba miezi ya hivi karibuni.

Agenda ya CUF mchakato wa Katiba Mpya

Mjumbe wa Baraza kuu la Uongozi la CUF na Mwakilishi wa Jimbo la Mjimkongwe Mh. Ismail Jussa Ladhu.
Wakati viongozi wa CCM wakizunguka jimbo kwa jimbo kutetea Mfumo wa Muungano wa Serikali mbili, Chama Cha Wananchi (CUF), kimesema hakiungi mkono hata pendekezo lililotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba la kutaka Muungano wa Serikali tatu.

Migongano hiyo ya kimtazamo inazidi kuliweka taifa katika umbile la mshazari, huku matumaini ya kupatikana kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano yakionekana kupotea kutokana na kundi la wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukataa kuendelea kushiriki Bunge la Katiba kwa madai kuwa CCM imekuja na rasimu yake.

Hata hivyo misimamo hiyo si kwamba inaonekana kuwachanganya wananchi tu bali pia inazidisha taharuki ya wananchi kutoelewa hatima ya upatikanaji wa Katiba na mfumo upi ambao ni sahihi katika kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikisha umri wa miaka 50.

Kundi la Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd limeeleza neema, fanaka na matunda ya Muungano wa Serikali mbili kiuchumi, kisiasa, kiulinzi na kiusalama.

Wakati huohuo kundi la viongozi wa CUF chini ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, linasisitiza kuwa lazima Zanzibar ipate mamlaka kamili ya dola.

Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF Ismail Jussa Ladhu, akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Vuga, amesema CUF iliunga mkono pendekezo la Serikali tatu kama ngazi ambayo ingekisaidia chama hicho kufikia malengo ya kupatikana mamlaka kamili ya Zanzibar.

Jussa anasema bila Zanzibar kupata uraia wake, hati ya kusafiria, mambo ya nje, kiti Umoja wa Mataifa, Sarafu na benki kuu, Serikali tatu hazina tija wala faida yeyote kwa Wazanzibar.

Anasema madai ya msingi ya Wazanzibari ni kupatikana kwa mamlaka huru za Tanganyika na Zanzibar.
Anasema yatakapopatika masuala hayo na kubaki katika mikono ya Zanzibar kama dola kamili, Zanzibar itakapoweza kujikwamua na kupiga hatua nyingi za kiuchumi, kinyume na hali ilivyo sasa ya kuwa kama mgeni mualikwa katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesisitiza kuwa lengo kuu la kukutana kwa Rais mstaafu wa Zanzibar Dk Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Novemba 5 mwaka 2009, licha ya kusaka maridhiano ya kisiasa na kuzika uhasama, ilikuwa ni mpango wa kuweka nguvu ya pamoja ili kuipatia Zanzibar mamlaka kamili.

Bila ya kupepesa maneno Jussa amesema kwamba kwa bahati mbaya warithi wa Dk Karume wamekuwa wakiyumba, huku wakishndwa kuungana na kudai masuala ya msingi bila ya Wazanzibari kuungana na kusimama pamoja, madai yao hayataweza kufikiwa.


Wassira amjibu Jussa
Akijibu mapigo ya Jussa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jimbo la Mtoni , Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Stephen Wasira anasema kimsingi wanachokitaka CUF na viongozi wake si Muungano bali wana nia na dhamaira ya kuligawa taifa na kuvunja Muungano.

Wassira anasema Muundo wa Muungano wa Serikali mbili si kioja au kituko kwani hata mataifa ya Uingereza na Marekani yana mfumo wa aina hiyo, huku wakiwa na kiti kimoja Umoja wa Mataifa .

Anasema kudai kiti Umoja wa Mataifa, sarafu, uraia au Benk Kuu ni mwelekeo wa kuvunja Muungano. Akamtuhumu Jussa na wenzake kuwa ni mawakala wa mabeberu na wakoloni wanaopigania Zanzibar irejee katika mikono ya watawala waliopinduliwa mwaka 1964.

Wassira anasema mwanasiasa huyo amekuwa akikerwa na kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi kwani hata wakiwa kwenye Kamati za Bunge maalumu la Katiba ametaka siku ya Januari 12,1964 iondolewe katika orodha ya sikuu za kitaifa.

Balozi Seif anasema ikiwa wajumbe wa Ukawa wataendelea kushikilia msimamo wao wa kukataa kurudi bungeni ili kujenga nguvu ya hoja na kupatikana katiba bora, watakaopoteza turufu na kupata hasara ni Wazanzibari

Anasema kwa kiasi kikubwa madai ya Zanzibar ili iweze kujikwamua kiuchumi na kushamirisha maendeleo yake, yamezingatiwa katika Rasimu ya Katiba Mpya, hivyo ni jukumu la Wazanzibari kutambua jambo hilo na kupigania kupatikana Katiba Mpya.

Seif naye anena
Maalim Seif anasema hakuna mbunge atakayerejea bungeni kupitisha rasimu ya katiba ambayo haikuzingatia matakwa na madai ya msingi ya wananchi.

Kwa kuwa CCM wanataka kubaki na serikali mbili, basi moja iwe ya Tanganyika na ya pili ya Zanzibar; zote zikiwa na mamlaka kamili kama ilivyokuwa kabla ya kuungana mwaka April 26, 1964

Ni wazi kinachoonekana sasa kadri unavyofuatilia madai ya CCM na CUF ni kama mchezo wa paka na panya ambao unafanyika huku taifa likihitaji ipatikane katiba mpya ambayo itazingatia mahitaji mapya kulingana na wakati, usalama wa nchi, utulivu na mapatano ya kijamii.


Matamshi ya Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) Hellen Clark yanayowataka wabunge wa kundi la Ukawa kurudi bungeni, yanadhirisha madai kuwa nje ya bunge ni vigumu kupatikana Katiba mpya na wanachokifanya Ukawa ni kupoteza wakati.

Msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano uko wazi kufuatia kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba endapo rasimu mpya ya katiba haitapitishwa kwa kukosekana theluthi mbili ya maamuzi ya Wajumbe wa Bunge maalum la Katiba, taifa litaongozwa na Katiba ya mwaka 1977.

CHANZO: MWANANCHI.

Maalim Seif mgombea pekee ukatibu mkuu CUF

Katibu mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim, Seif Sharif Hamad.
Dar es Salaam. Wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad (Maalim Seif) akiwa mgombea pekee wa nafasi ya katibu mkuu wa chama hicho, makada wawili wamejitokeza kumvaa Profesa Lipumba katika nafasi ya uenyekiti.

Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ameshikilia nafasi hiyo ya ukatibu mkuu wa CUF kwa miaka 15 tangu mwaka 1999 alipoachana na cheo cha umakamu mwenyekiti, na iwapo atapitishwa na mkutano huo atakuwa amekalia cheo hicho kwa miaka 20 mfululizo.

Akitoa taarifa kuhusiana na mkutano mkuu wa sita wa chama hicho unaotarajia kuanza leo Dar es Salaam, Mkurugenzi Haki za Binadamu, Habari na Uenezi, Salum Biman alisema hakuna mwanachama aliyejitokeza kupambana na Maalim Seif.

 “Hiyo nafasi ilitangazwa mwezi mzima, lakini hakuna mwanachama aliyejitokeza,” alisema na kuongeza;“Hata wewe ungekuwa mwanachama wa CUF, ungekuwa na haki ya kugombea nafasi hiyo, hakuna mwanachama aliyekatazwa.”

Kuhusu nafasi ya mwenyekiti, Biman alisema kuna wanachama wawili wamejitokeza kupambana na Profesa Lipumba. Aliwataja wagombea waliojitokeza kuwa ni Chief Lutayosa Yemba kutoka Shinyanga na mwingine aliyemtaja kwa jina la Ibrahim kutoka Mkoa wa Pwani.  Hata hivyo, taarifa nyingine zimemtaja pia Mbezi Adam Bakar kutoka Temeke, Dar es Salaam.

“Wagombea hao ndiyo watakaopambana na Profesa Lipumba katika nafasi ya uenyekiti,” alisema.
Kuhusu nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Bimani alisema aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Machano Khamis ameachia ngazi na kumpisha Waziri wa Afya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Juma Haji Duni.

Alisema mkutano huo utawashirikisha wajumbe 800 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na utafanyika kwa siku tano, unatarajia kumalizika Juni 27, mwaka huu.

“Taarifa mbalimbali za chama zitasomwa baada ya miaka mitano ya utendaji. Katika mkutano huo, mwenyekiti Profesa Lipumba na katibu mkuu wake wataachia ngazi ili kupisha uchaguzi mkuu uweze kufanyika.”

Aliongeza kuwa mkutano huo utateua pia wajumbe 45 wa Baraza Kuu kutoka kila kanda na wajumbe wanawake ambao ni asilimia 30 ya wajumbe wote wa mkutano mkuu.

“Hadi sasa Wilaya 10 za Zanzibar na 90 za Bara zimeshakamilisha uongozi wa wilaya, hivyo zitatuwezesha kufanikisha uchaguzi katika mkutano mkuu,” alisema.

Mbali na uchaguzi huo alisema mkutano huo utarekebisha baadhi ya vipengele vya katiba na kanuni za chama hicho.
 
 Alisema baada ya uchaguzi wa kamati kuu, mwenyekiti kwa kushirikiana na makamu watateua wakurugenzi wa idara ambao watathibitishwa na Baraza Kuu kabla ya kupendekeza majina ya manaibu katibu ambao watathibitishwa na uongozi.