Friday, 26 September 2014

Mahakama yajivua mipaka ya Bunge

Mahakama haina mamlaka ya kuamua ni kwa kiwango gani cha maboresho au marekebisho ambayo Bunge la Katiba linaweza kuyafanya katika Rasimu ya Katiba.” Mahakama
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imejivua katika mgogoro wa mamlaka ya Bunge la Katiba kuhusu ni kwa kiwango gani bunge hilo lina  mamlaka ya kufanya  marekebisho au kuboresho Rasimu ya Katiba Mpya iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Badala yake, mahakama hiyo imesema hayo ni masuala ya kisiasa zaidi kuliko kisheria. Mahakama hiyo ilitoa msimamo huo jana wakati ikitoa amri kuhusiana na kesi ya kuhoji mamlaka ya Bunge la Katiba, chini ya kifungu cha 25(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.

Hata hivyo, haikutoa sababu za amri hiyo na badala yake ilisema kuwa itatoa sababu hizo Oktoba 7. Kesi hiyo ilifunguliwa na mwanahabari, Saed Kubenea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa niaba ya Serikali.

Katika kesi namba 28 ya mwaka 2014, Kubenea alikuwa anaiomba Mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya kifungu hicho kuhusu mamlaka ya Bunge na pia, itamke kama lina mamlaka ya kuacha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Wakili wa Kubenea, Peter Kibatala akisaidiana na Mabere Marando walisema kwa mujibu wa kifungu hicho, bunge hilo lina mipaka na halina mamlaka ya kuacha maudhui ya Rasimu hiyo.

Akijibu hoja hizo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alidai kuwa bunge hilo lina mamlaka ya kufanya mabadiliko yoyote na kwamba, halifungwi na Rasimu hiyo kwa kuwa ni nyaraka ya kazi tu kwa bunge hilo.

Katika amri yake jana, Mahamaka ilisema imebaini kuna utata na mkinzano wa maana katika kifungu hicho katika lugha ya Kiswahili na lugha ya Kiingereza.

Hivyo, mahakama kupiti jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo, Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Dk Fauz Twaib na Aloysius Mujulizi, ilitoa tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hilo baada ya kusoma Sheria yote ya Mabadiliko ya Katiba

Ilisema licha ya utata huo, mamlaka ya kutengeneza masharti ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamaanisha mamlaka ya kuandika na kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupigiwa kura na wananchi wa Tanzania.

Pia, ilisema mamlaka hayo yatatekelezwa kwa msingi wa Rasimu ya Katiba baada ya kuwa imewasilishwa mbele ya Bunge la Katiba na mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Kwa kufanya hivyo, Bunge la Katiba linaweza kuboresha au kuirekebisha Rasimu ya Katiba,” alisema Jaji Mwarija alipokuwa akisoma amri hiyo.

Aliongeza: “Mamlaka hayo yana mpaka tu kama ilivyokuwa kwa shughuli za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, katika misingi ya kitaifa na maadili yaliyotolewa katika kifungu cha 9 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.”

Ilisisitiza kuwa hayo ni masuala zaidi ya kisiasa kuliko ya kisheria, isipokuwa tu bila kukiuka kifungu cha 9 (2).

Kifungu hicho kinasema: “Tume ya Mabadiliko ya Katiba itaongozwa na misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya Jamii  na kinataja mambo ambayo ni sharti yahifadhiwe na kudumishwa, ikiwamo Jamhuri ya Muungano.”

Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Kibatala alisema wameridhishwa na jinsi Mahakama ilivyoweza kutekeleza jukumu lake kwa wakati na wamefurahi kuwa imeitambua Rasimu ya Katiba tofauti na mdaiwa alivyodai kuwa hiyo ni nyaraka ya kazi tu kwa bunge hilo.

Alisema bado Mahakama haikuweza kukata kiu yake na ya mteja wake.

CHANZO: MWANANCHI.

Vitisho vyaanza Kamati ya Uandishi

Makamo wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ally Iddi akisoma moja miongoni mwa ujumbe wa vitisho kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokea Zanzibar unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii alipokuwa akizungumza na Wandishi wa hababri jana Dodoma.
MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ameitaka jamii kuacha kutumia mitandao ya kijamii kutishia maisha ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

Balozi Iddi aliyasema hayo Mjini Dodoma jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya vitisho vilivyotolewa kwa wajumbe wa Bunge hilo wa Kamati ya Uandishi katika mitandao ya kijamii.

Alisema si vizuri kuwatishia wajumbe hao kwani waliteuliwa kwenye kamati hiyo kwa mujibu wa sheria.
“Wajumbe wa kamati hii, wanaitwa wasaliti, sijui kwanini wanaitwa hivyo na sijui msaliti ni nani kati ya waliobaki kuandika katiba au waliotoka nje,” alisema.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewahakikishia usalama wa kutosha wajumbe hao ili wasidhurike.

“Vyombo vya dola vipo na vitafanya kazi yake, niwahakikishie kwamba, wajumbe hawataendelea kuwa salama hata watakaporudi Zanzibar,” alisema.

Alisema Serikali ya Zanzibar, imeridhishwa na Rasimu inayopendekezwa na Bunge hilo iliyosomwa juzi bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Bw. Andrew Chenge.

“Baadhi ya mambo machache yaliyokuwa na ukakasi upande wa Zanzibar, yamefanyiwa marekebisho katika Katiba inayopendekezwa.

“Katika hoja 17 zilizowasilishwa kwenye Kamati ya Uandishi na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, zote zimeingizwa kwenye Katiba isipokuwa tatu ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi wa kujiuzulu kwa Bw. Othman kwenye Kamati hiyo akisema alitakiwa kushiriki kama Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar hivyo kutokuwepo kwake si kikwazo cha kupatikana Katiba

“Waliokuwepo katika kamati hii upande wa Zanzibar, walikuwa wanatosha,” alisema.
CHANZO: MAJIRA

Thursday, 25 September 2014

Waraka wa Warioba kwa Wasira

Jaji Joseph Sinde Warioba.
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ameandika waraka kumjibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira kwa kauli yake kuwa ndiye aliyemkimbiza CCM kwenda upinzani mwaka 1995.

Katika waraka wa maandishi alioutuma kwa gazeti hili, Jaji Warioba alisema maelezo ya Wasira dhidi yake katika mahojiano maalumu na gazeti hili hayakuwa sahihi na hivyo akamtaka ajifunze kusema ukweli kwa kuwa mambo anayosema yanaweza kumrudia baadaye.

Waraka wenyewe
Tarehe 22 Septemba 2014, Gazeti la Mwananchi lilitoa taarifa ya mahojiano kati yake na Mheshimiwa Steven Wasira. Katika mahojiano hayo, Mheshimiwa Wasira alisema mimi ndiye niliyemkimbiza CCM.

Tangu mchakato wa Katiba Mpya kuanza nilikuwa napata taarifa kwamba Mheshimiwa Wasira alikuwa amenifanya mtaji wake katika kutetea msimamo wake. Wakati mmoja kuna kiongozi mwenzake aliniuliza kama nina ugomvi binafsi na Mheshimiwa Wasira kwa sababu kila akipata nafasi kwenye vikao vyao ananishambulia. Wakati wa mabaraza ya Katiba nilipata taarifa za aina hiyo. Nilichofanya ni kuwaarifu viongozi wake wa CCM.

Mengi aliyosema Mheshimiwa Wasira siyo ya kweli. Napenda nitoe ufafanuzi kwa machache yafuatayo:-
Niligombea mara mbili na Mheshimiwa Wasira. Baada ya Uchaguzi wa 1990 ambao nilishinda kwa kura nyingi sana, uchaguzi huo ilitenguliwa kwa sababu nilifanya kampeni kwa kutumia gari la Waziri Mkuu.

Uchaguzi ulirudiwa mwaka 1992. Niliunda timu ya kampeni, Mheshimiwa Wasira akiwa kiongozi. Aliniomba atangulie jimboni kuandaa mazingira. Alipofika huko akaanza kampeni dhidi yangu na kutangaza kwamba anagombea. Wakati huo kura za maoni zilikuwa zinapigwa na wajumbe wa halmashauri kuu ya wilaya.

Wajumbe walikuwa kama 600. Nilipata kura 400 na Mheshimiwa Wasira alipata kura chache akiwa mtu wa tatu au nne. Baada ya matokeo akatangaza anajitoa kwenye mchakato na jina lake lisipelekwe NEC. Alikataliwa kwa sababu kufuatana na kanuni, muda wa mtu kujitoa ulikuwa umepita.

Mwaka 1995, kura za maoni zilikuwa zinapigwa kwenye kata. Tulianza na Kata ya Sarama ambayo iko upande wa mashariki, siku ya tatu tulifika Nyamuswa ambacho ndicho kijiji ninachotoka. Nyamuswa ilikuwa kituo cha tano kati ya vituo 12.

Baada ya hapo tulielekea magharibi ya jimbo anakotoka Mheshimiwa Wasira. Baada ya kura kupigwa katika Kata ya Guta, Mheshimiwa Wasira alijitoa kwa sababu aliona hawezi kunishinda hata kama angepata kura zote za kata mbili zilizobaki. Siyo kweli kwamba Nyamuswa ilikuwa ya mwisho kupiga kura na siyo kweli wananchi wa kata nzima walipiga kura. Kumbukumbu zote zinaweza kupatikana wilayani na makao makuu ya CCM.

Mheshimiwa Wasira anasema kwamba nilikuwa Jaji na kesi iliyopelekwa mahakamani ni kama kesi ya tumbili kupelekwa kwa nyani, kwa maana kwamba majaji walinipendelea. Kumbukumbu za kesi hiyo zipo. Wakati huo sikuwa jaji. Isitoshe huko nyuma uchaguzi nilioshinda 1992 ulitenguliwa. Kwa nini wakati huo sikupendelewa? Kumbukumbu za kesi zinaeleza kwa nini Mheshimiwa Wasira alifungiwa kugombea kwa kipindi.

Mheshimiwa Wasira ni kiongozi wa Taifa kwa kipindi kirefu. Ni mbunge wangu na namtambua hivyo. Tunaweza kuwa na mtazamo tofauti katika baadhi ya mambo lakini hiyo si sababu ya kusema mambo yasiyo ya kweli kwa nia ya kujijenga kisiasa.

Yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM. Yeye ni Waziri mwandamizi. Yeye anafikiria kugombea urais. Ni vizuri basi akajifunza kusema kweli (ambayo ni ahadi mojawapo ya WanaCCM). Akumbuke anayosema yanaweza kumrudia mbele ya safari.

J.S. Warioba
24-09-2014

CHANZO: MWANANCHI.

Katiba Mpya: Ni mchezo wa namba

Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum la Katiba Andrew Chenge.
Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba jana ilikabidhi bungeni Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ikiwa na ibara 289 kulinganisha na 271 za Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba.

Rasimu hiyo pia ina sura mpya mbili ambazo ni Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Akiwasilisha rasimu hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge aliliambia Bunge kuwa Ibara 233 za rasimu hiyo zinatokana na Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Chenge, ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alisema ibara 47 za Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba zimebaki kama zilivyokuwa, 186 zimefanyiwa marekebisho, 28 zimefutwa na 41 ni mpya.

Rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa imefuta kabisa muundo wa Muungano wa shirikisho ambao ungezaa muundo wa serikali tatu na badala yake imerudisha muundo wa sasa wa serikali mbili.

Chenge alisema kamati za Bunge hilo pamoja na wajumbe walio wengi, waliona kuingiza muundo wa shirikisho ilikuwa ni kukiuka makubaliano ya Muungano yaliyofikiwa mwaka 1964.

Kwa kurejesha muundo wa serikali mbili uliokuwa ukipigiwa chapuo na CCM, Rasimu hiyo imependekeza kuwapo kwa makamu watatu wa rais.

Chenge alisema uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgombea mwenza atakayekuwa makamu wa kwanza wa rais.

Chini ya muundo huo, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), atakuwa makamu wa pili wa rais ilhali Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa makamu wa tatu wa rais.

Chenge alisema mapendekezo hayo yamezingatia ukweli kuwa kuwapo kwa mgombea mwenza anayekuwa makamu wa kwanza wa rais, kutafanya rais na makamu wake kutoka chama kimoja.

Rasimu hiyo inayopendekezwa, imepunguza Tunu za Taifa kutoka saba zilizokuwamo kwenye Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba hadi nne huku mambo ya muungano yakiongezwa kutoka saba hadi 14.

Katika Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Tunu za Taifa zilikuwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa; sasa zimebaki Lugha ya Kiswahili, Muungano, utu na undugu na amani na utulivu. Tunu tatu ambazo ni uzalendo, uadilifu na umoja zimeondolewa.

Mambo ya Muungano
Katika Rasimu ya Tume, mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ulinzi na usalama.

Mambo mengine yalikuwa ni uraia na uhamiaji, sarafu na benki kuu, mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.

Rasimu inayopendekezwa imetaja mambo ya muungano kuwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama, usafiri wa anga, uraia, uhamiaji, polisi, sarafu na benki kuu na kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na bidhaa zinazotengenezwa Tanzania na kusimamiwa na idara ya forodha.

Mengine ni mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani, elimu ya juu, Baraza la Taifa la Mitihani, Utabiri wa Hali ya Hewa na utumishi Serikali ya Jamhuri.

Mambo mengine ambayo yalikuwa katika Rasimu ya Warioba yaliyowekwa kando ni pendekezo la wabunge kutokuwa mawaziri ikipendekezwa utaratibu wa sasa wa wabunge kuwa mawaziri uendelee kutumika.

Chenge alisema Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, imeweka ukomo wa mawaziri kuwa wasizidi 30 wakati naibu mawaziri watateuliwa kulingana na mahitaji mahsusi. Tume ya Warioba ilipendekeza mawaziri wasiozidi 15.

Rasimu hiyo inayopendekezwa imefumua muundo wa Bunge uliopendekezwa na Rasimu ya Warioba kuwa wawe 75 wa kuchaguliwa majimboni na watano kutoka kundi la watu wenye ulemavu, badala yake imesema muundo wa sasa uendelee ukiwa na wabunge 360 kwa sharti la kuwapo uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume.

Rasimu hiyo imetupilia mbali pendekezo la mtu anayetaka kugombea ubunge awe na elimu isiyopungua kidato cha nne na kurudisha kuwa ajue tu kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.

“Haki ya wananchi kumwajibisha mbunge kabla ya miaka mitano imeondolewa kutokana na mapendekezo ya kamati na wajumbe na watafanya hivyo baada ya miaka mitano,” alisema.

Rasimu hiyo imembana mgombea binafsi wa ubunge kwamba atakoma kuwa mbunge pale tu itakapotokea amejiunga na chama chochote cha siasa nchini.

Pendekezo la Warioba la kutaka Spika wa Bunge na Naibu wake wasitokane na wabunge wa Bunge la Jamhuri au kuwa viongozi wa juu wa vyama, nalo limewekwa kando na badala yake spika kupendekezwa achaguliwe miongoni mwa wabunge au kutoka kwa Watanzania wenye sifa ambao watajitokeza kuomba nafasi hiyo kama ilivyo sasa.

Hata hivyo, Chenge alisema wamependekeza Naibu Spika ni lazima atoke miongoni mwa wabunge.

Mgombea binafsi
Chenge alisema pamoja na kwamba mgombea huru wa nafasi ya urais ni haki ya kikatiba, lakini kamati yake imelazimika kuchukua tahadhari na kuweka masharti juu ya mgombea huyo.

Masharti hayo ni pamoja na kuweka kipengele katika Katiba kinacholitaka Bunge kutunga sheria itakayoweka masharti ya mgombea huru ikiwamo idadi ya watu watakaohitajika kumdhamini.

Pia sheria hiyo itaweka sharti la lazima linalomzuia kujiunga na chama chochote cha siasa, kuainisha vyanzo vya mapato vya kugharimia kampeni zake na kuweka wazi ilani yake ya uchaguzi.

Masuala ya kuingizwa kwa Mahakama ya Kadhi na kuruhusiwa kwa uraia wa nchi mbili ambayo yaliwagawa wajumbe wa Bunge hilo katika makundi mawili nayo hayakuingizwa katika rasimu hiyo.

Kuhusu Mahakama ya Kadhi, Chenge alisema kamati yake imezingatia mijadala ya wajumbe, taarifa za kamati za Bunge hilo na Katiba za nchi mbalimbali katika kufikia uamuzi huo.

Alisema katiba inayotungwa inahusu Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na Mahakama ya Juu hivyo masuala ya Mahakama ya Kadhi yanaweza kusimamiwa na sheria inayohusu mahakimu.

Kuhusu suala la uraia pacha, Chenge alisema waliozaliwa Tanzania lakini wakapoteza uraia na kuamua baadaye kurudi nchini, watarejeshewa uraia wao baada ya kuukana uraia wa nje. Alisema Watanzania wanaoishi nje ya nchi wakiwa na uraia wa nchi hizo, watakapokuja nchini hawatakuwa na uraia wa nchi mbili, badala yake watapewa hadhi maalumu.

Baada ya kukamilika kwa uwasilishaji huo, Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alitoa fursa kwa wajumbe wa Bunge hilo kuipitia Rasimu jioni na leo watakutana kwenye kamati zao 12 kwa lengo la kuhakiki ni kwa kiasi gani waliyoyapendekeza wakiwa ndani ya kamati na kwenye mijadala yamezingatiwa.

Kesho wajumbe wote watakutana katika Bunge zima kwa lengo la kuhakiki kwa pamoja kuhusu yale yatakayoletwa na sekretarieti kutoka kwenye kamati za Bunge hilo. Septemba 28, wajumbe hao watakutana tena kwenye kamati kwa lengo la kupewa maelekezo ya namna ya kukaa ndani ya ukumbi na pia namna watakavyopiga kura siku inayofuata.

Sitta alisema upigaji wa kura utaanza Septemba 29 hadi Oktoba 2 na baada ya hapo itajulikana kama rasimu hiyo imepitishwa kwa wingi wa kura wa theluthi mbili kwa pande zote za Muungano au la.

CHANZO: MWANANCHI.

Wednesday, 24 September 2014

Dk.. Shein:Tutaendelea Kuhakikisha Malengo ya Elimu katika Mipango Yote ya Maendeleo Yanatekelezeka

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Walimu na Wanafunzi katika Sherehe za Miaka 50 ya Elimu bila malipo zilizofanyika kitaifa katika Uwanja wa Amaan Studium Mjini Unguja jana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa malengo yote katika mipango ya maendeleo ya nchi yanayohusu uimarishaji wa elimu yanafikiwa na kutoa matokeo yanayotarajiwa.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Elimu bila Malipo yaliyofanyika kwenye uwanja wa Amaan mjini Unguja leo, Dk. Shein amesema Serikali inatambua kuwa mafanikio ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi yanategemea kuimarika kwa kiwango cha elimu hivyo ndio maana suala la uimarishaji wa elimu limepewa kipaumbele katika mipango mbalimbali ya maendeleo.

Aliitaja mipango hiyo kuwa ni pamoja na Dira ya Maendeleo 2020, Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II),Mpango wa Maendeleo ya Elimu, Malengo ya Milenia ya Elimu na Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2010.

Katika kufanya hivyo, aliwaambia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuongeza nafasi za masomo katika viwango vyote kuanzia skuli za maandalizi hadi chuo kikuu ili kutoa fursa kwa kila mtoto kupata elimu katika ngazi zote.

Sambamba na kuongeza fursa za masomo, kwa upande mwingine alisema Serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi zote unazidi kuongezeka kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mazingira ya utoaji elimu nchini.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuzipatia skuli vifaa na nyezo za kisasa za kufundishia ikiwemo vitabu, vifaa vya maabara, kompyuta na walimu bora ili kuwawezesha wanafunzi kufaulu masomo yao vyema.

Dk. Shein alitoa mfano wa hatua mzuri iliyofikiwa katika kuwapatia wanafunzi vitabu katika skuli za sekondari ambapo alieleza kuwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Serikali ya Marekani hivi sasa kila mwanafunzi katika ngazi hiyo ana vitabu vya masomo anavyovidhibiti mwenyewe na kwenda navyo nyumbani.

Katika hotuba yake hiyo, Dk. shein alitoa wito kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuendeleza juhudi za ufundishaji wa taaluma ya tekinolojia ya habari na mawasiliano katika skuli za Unguja na Pemba ili Zanzibar iweze kwenda sambamba na maendeleo na mabadiliko ya karne 21 ambayo yanazingatia matumizi ya tekinolojia hiyo.

Hata hivyo ameitaka wizara hiyo kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti matumizi kwa kutunga kanuni zinazokataza matumizi mabaya ya mitandao na simu za mikononi kwa wanafunzi maskulini.

Kuhusu maslahi ya walimu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwahakikishia walimu kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kwa kuwapatia mafunzo zaidi pamoja na kuwaongezea mishahara kadri uchumi unavyokua na hali inavyoruhusu.

Dk. Shein alizungumzia pia suala la ukosefu wa ajira kwa wahitimu wengi wanaomaliza vyuo mbali mbali huku akitambua changamoto inayowakabili wengi wa wahitimu hao ya kukosa maarifa ya kutosha kujiajiri hivyo kutegemea ajira.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Awali Bibi Zahra Ali Hamad alieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta ya elimu na kuongeza kuwa ongezeko kubwa la bajeti ya elimu mwaka hadi mwaka ni hatua inayodhihirisha umakini wa Serikali katika kuimarisha elimu nchini.

Tarehe kama leo 1964, miezi tisa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Sheikh Abeid Amani Karume alitangaza elimu bila malipo kwa kila mwananchi na kuondosha kabisa ubaguzi katika mfumo wa elimu Zanzibar.

Mapema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiri wa Baraza laMapinduzi alipokea maandamano ya wanafunzi kutoka skuli mbalimbali za Unguja na Pemba na baadae kufuatiwa na burudani za vikundi vya sanaa na michezo.

IMETOLEWA NA IKULU ZANZIBAR.

Siri ya AG Z’bar kujiuzulu Bunge la Katiba yabainika

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman
SIRI ya Mwanasheria Mkuu (AG) wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kujiuzulu ujumbe wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, imebainika.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo, kililiambia MTANZANIA kuwa wakati vikao vya kamati hiyo vikiendelea, Othman alipendekeza mambo 17 yenye maslahi kwa Zanzibar yaingizwe ndani ya Katiba inayopendekezwa na Bunge, lakini yakakatiliwa.

Kujiuzulu kwa kigogo huyo wa SMZ kulizua taharuki ya ndani ya Bunge la Katiba na hata baadhi ya wajumbe kutaka kujua sababu ya kufikia hatua hiyo.

Kikiendelea kufafanua suala hilo, chanzo hicho kilisema baada ya kukataliwa kwa maswala hayo, Othman aliamua kumwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, na kumweleza uamuzi wake wa kujiuzulu.

Kutokana na sintofahamu hiyo, iliwalazimu viongozi wa juu wa CCM kukutana kwa dharura na kuazimia kufukuzwa kazi kwa mwanasheria huyo kwa kile walichodai amekisaliti chama.

Chanzo hicho kilisema baada ya Othman kupata taarifa hiyo, aliwasiliana na Ikulu ya Zanzibar na kuomba nafasi ya kukutana na Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

“Baada ya kukutana na Dk. Shein, Othman alieleza namna Kamati ya Uandishi ilivyopinga kuingizwa kwa mambo 17 ambayo yana maslahi kwa Zanzibar. Kutokana na uzito wa hoja hizo, kiliitishwa kikao cha Baraza la Mapinduzi.

“Kikao hicho kiliwashirikisha mawaziri wote wa SMZ wakiongozwa na Mwenyekiti Dk. Shein, walipewa taarifa hiyo na kuijadili kwa kina na kisha kukubaliana na hoja za Mwanasheria Mkuu juu ya masuala hayo 17.

“Kikao kile chini ya Dk. Shein kiliazimia hoja hizo 17 ziwasilishwe kwenye Baraza la Mawaziri la Muungano,” kilisema chanzo chetu.

Hatua hiyo ya Baraza la Mapinduzi kuungana na Othman, ilifanya juzi Baraza la Mawaziri la Muungano chini ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukaa, na pamoja na mambo mengine lilijadili hoja 17 za SMZ na kukataa baadhi yake.

Taarifa zilizopatikana mjini Dodoma tangu kujiuzulu kwa mwanasheria huyo, zinasema baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wamekuwa na vikao vya siri lengo likiwa ni kushinikiza mambo hayo 17 kuingizwa kwenye Katiba mpya.

Katiba hiyo inayopendekezwa inatarajiwa kuwasilishwa leo kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Kabla ya kujiuzulu, Othman mara kadhaa alinukuliwa na vyombo vya habari akitetea muundo wa Muungano wa Serikali tatu.

KAULI YA IKULU Z’BAR
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Hassan Hassan, alikana kuwapo kwa taarifa hizo huku akitaka atafutwe Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

“Hakuna kikao chochote kilichoketi na kujadili suala la Mwanasheria Mkuu ila ninachoweza kusema mtafute Makamu wa Pili yeye ndio msemaji wa Serikali,” alisema Hassan.

CHANZO: MTANZANIA

Hatima ya Bunge la katiba kujulikana kesho

Wakili wa Said Kubenea, Peter Kibatara (kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Hatima ya Bunge la Katiba huenda ikajulikana kesho wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar  es Salaam itakapotoa hukumu ya kesi ya kulipinga Bunge hilo iliyofunguliwa  na mwanahabari Saed Kubenea.

Uamuzi huo ulifikiwa jana baada ya kumaliza kusikiliza hoja za pande zote, upande wa mdai (Kubenea) na upande wa mdaiwa (Serikali).

Katika kesi hiyo namba 28 ya mwaka 2014, Kubenea  anaiomba  mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya kifungu hicho kuhusu mamlaka ya Bunge hilo na pia itamke iwapo lina mamlaka ya kuacha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni.

Kabla ya mahakama kufikia hatua hiyo ya kupanga tarehe ya kutoa hukumu yake kwanza, kuliibuka mvutano wa kisheria kuhusu utata wa tafsiri ya kifungu cha 25(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 katika lugha mbili zilizotumika kuandika sheria hiyo.

Utata huo unatokana na tofauti ya tafsiri ya kifungu kinachohojiwa katika toleo la lugha ya Kiingereza na la Kiswahili. Utata huo uliibuliwa na Jaji Aloysius Mujulizi. Majaji wengine katika jopo hilo ni Augustine Mwarija na Dk Fauz Twaib.

Baada ya mabishano makali mahakama iliwataka mawakili wa pande zote kufika mahakamani kesho kwa ajili ya kusikiliza hukumu endapo itakuwa imekamilika na iwapo itakuwa bado, basi mahakama itatoa maelekezo mengine.