Sunday, 1 May 2016

Miaka 52 ya Muungano mimi kama shahidi

Mwalimu Julius K Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume
Na Othman Miraji
Watanzania wanaadhimisha miaka 52 ya Muungano wao wa Tanganyika na Zanzibar. Hongera. Siku 104 nyuma kutoka sasa Watanzania pia waliadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba nimeshuhudia kwa macho yangu matukio hayo mawili makubwa ya kihistoria na maendeleo yake hadi leo. Kwangu mimi matukeo hayo mawili yamefungamana. Bila ya kutokea Mapinduzi ya Zanzibar (12.01.1964) sifikiri kwamba tungekuwa na Muungano huu wa Tanzania tunaouadhimisha. Japokuwa Hayati Mwalimu Nyerere (Muasisi wa Muungano pamoja na Hayati Mzee Karume) aliwahi kunukuliwa akisema kwamba hata kama Chama cha Afro-Shirazi, ASP, cha Zanzibar kingeingia madarakani kwa njia za kikatiba na si kwa njia ya mapinduzi, Muungano bado ungefanyika. Mimi sina hakika.

Kwa sisi wanafunzi wachache wa Kizanzibari (ungeweza kuihesabu idadi yetu kwa vidole vya mikono miwili) tuliokuwa tukisoma wakati huo katika Shule ya Sekondari ya Aga Khan (sasa Tambaza ) mjini Dar es Salaam, habari ya Mapinduzi ya serikali yaliotokea Zanzibar Januari 12, 1964 yalitufikia kwa mshangao mkubwa. Akili zetu za ujana wakati huo zilivurugika kutokana na habari hiyo, japokuwa kila wakati tulitakiwa na wazee wetu tujielekeze zaidi katika masomo na si katika siasa za mivutano zilizotawala nyumbani wakati huo. Ilipopita miaka ndipo wengi wetu tulipotambua kwamba Mapinduzi hayo yalifungamana pia na siasa kubwa zaidi kuliko vimo vyetu vichanga vya utoto. Mwishowe tuligundua kwamba kumbe wadau katika Mapinduzi hayo walikuwa si Wazanzibari peke yao.

Na pale Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulipoundwa, Aprili 26, 1964 baadae ndipo kila mmoja wetu alipogundua kwa ghafla kwamba mnamo siku moja tu amegeuka kutoka kuwa raia wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Pia kwamba Zanzibar haitokuwa tena na kiti chake katika Umoja wa Mataifa, lakini kutoka wakati huo itawakilishwa na kiti kimoja cha taifa jipya lenye jina la Tanzania. Tuligundua baadae pia kwamba wadau wa Muungano walikuwa ni wengi, yakiwemo madola mkuu yaliokuwa yakisuguana katika Vita Baridi baina ya kambi ya kibepari ya Magharibi na ya kikoministi ya Mashariki. Madola hayo yalisaka kila njia ili kuwa na ushawishi katika uchoraji wa ramani ya njia itakayopitia Tanzania katika siku za mbele.Yalikuweko maslahi kadhaa yaliopingana ndani ya Muungano huo. Kujiuliza masuali mengi wakati huo kulikuwa hakuna faida. Kwa vyovyote Muungano ulishaundwa, hamna litakaloweza kuubadilisha ukweli huo. Baadhi yetu tulijiuliza mbona mambo yalikwenda fasta fasta, kasi ilikuwa kubwa mno? Tulijijibu wenyewe kwamba kulikuwa hakuna wakati wa kudurusu nini kilichoamuliwa jana, hakuna wakati wa kuulizana na kushauriana. Kwanini? Sijui.

Licha ya kwamba kila mmoja wetu baada ya kumaliza shule alielekea njia yake- baadhi walienda vyuo vikuu na wengine kutafuta ajira- nilishangaa kwamba katika shule za madaraja yote na pia katika vyuo vya juu katika pande zote mbili za Muungano hakujatolewa elimu juu ya Muungano. Si tu wanafunzi katika masomo yao ya historia na elimu ya uraia, lakini pia Watanzania, kwa ujumla, hawakupewa maarifa na kuelemishwa kwa undani juu ya Muungano wao, faida zake na sabababu zilizopelekea uundwe. Nilishangaa pia kuona vipi Muungano huo ulivyofanywa kuwa zaidi mali ya viogozi badala ya kuwa mali halali ya wananchi wote wa pande mbili. Lakini nilijitosheleza kwamba Muungano wa watu wa pande mbili hizo ulikuweko kwa miaka na dahari, na hautavunjika, ila tu huu wa sasa umesadifu kuandikwa karatasini na wanasiasa.

Katika miaka ya sitini tulikuwa tunaishi wakati wa Vuguvugu la Mwamko wa Afrika, tukivutiwa na tunu za Afrika ilioyoungana. Viongozi wetu waliotuongoza kuelekea ukombozi, akina Nkurumah wa Ghana, Jamal Abdel Nasser wa Misri, Julius Nyerere wa Tanganyika na Jomo Kenyatta wa Kenya walituambia kwamba Afrika ili iweze kusikika vilivyo na kuwa na nguvu katika jukwaa la kimataifa lazima nchi za Afrika ziungane. Nkurumah alienda mbali kutaka Afrika ilio na serikali, bunge, jeshi na rais mmoja. Mwalimu Nyerere alimtahadharisha mkuu huyo wa Ghana na kumwambia aste aste, polepole. Kwanza tuanze na Muungano wa nchi zilioko katika mkoa mmoja mmoja. Baadhi ya vijana wa wakati huo walivutiwa na Muungano wa Tanzania, kama kianzio cha ndoto ya kuwa na Muungano wa Afrika nzima. Hawajajali kwamba matayarisho yake hayajawa ya kutosha na kwamba wananchi wa pande hizo mbili hawakushauriwa kabla. Hata baadhi ya mawaziri wa huko Zanzibar walikuwa hawana taarifa hadi siku za mwisho kabla ya kutiwa saini Mkataba wa Muungano. Kwa vijana hao, lakini, lengo ndilo lilikuwa muhimu zaidi kuliko njia za kupita kulifikia lengo lenyewe.

Hadi miaka ya karibuni (baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa) ilikuwa mwiko kuzungumzia juu ya suala la Muungano na manung’uniko ( yaliyoitwa “Kero”) juu ya Muungano huo yalifichwa chini ya mkeka. Mara nyingi kero hizo zilisikika zaidi kutoka upande wa Zanzibar kuliko wa Tanganyika. Ni kawaida yule anayehisi anapoteza zaidi ndiye anayelalamika zaidi. Huenda kwa mujibu wa tarakimu za kifedha ikaonekana upande mmoja unabeba mzigo mkubwa zaidi kuliko vile inavostahiki au inapunjwa zaidi kuliko inavostahiki. Lakini kwa vile kunakosekana uwazi na kwamba Muungano umekuwa ukiendeshwa kwa kuoneana muhali na kienyeji kuliko kuwa wa kisayansi na wa kitarakimu, ni rahisi kwa kila upande kudai kwamba unaonewa na si kwamba unaonea.

Muungano wa Tanzania haujajengeka kwa nguvu za tarakimu na za kifedha, lakini, kama walivyosema waasisi wake, kutokana na udugu wa kihistoria wa watu wake. Ni Muungano wa Damu ambao si rahisi kuvunjika kwa sababu za kifedha. Muhimu zaidi ikumbukwe kwamba ni Zanzibar iliyowachia mamlaka yake ya juu kabisa ya kiutawala na utambulisho wake wa kimatifa, mambo ambayo kabisa mtu hawezi kuyatathmini kwa vipimo vya fedha na tarakimu.

Japokuwa hapo awali Mkataba wa Muungano ulitaka taasisi mbili za kutunga sheria- Bunge kwa upande wa Tanganyika na Baraza la Mapinduzi kwa upande wa Zanzibar- mwishowe ziidhinishe ibara ziliomo ndani ya Mkataba huo, kuna watu wanaodai kwamba kwa upande wa Zanzibar jambo hilo halijafanyika. Hivyo kuna wanasheria wa masuala ya katiba wanaouwekea alama ya kuuliza uhalali wa Mkataba huo. Lakini hayo, baada ya kupita miaka 52 ya Muungano na kama Wajerumani wanavyosema, hiyo ni theluji ilionyesha jana. Imeshayayuka. Au kwa msemo wa Kiswahili: Yaliopita si ndwele, tugange yajayo. Mkataba wa Muungano ulitaja mambo 11 tu yawe masuala ya Muungano, lakini sasa yameengezwa na kufikia 23. Hiyo ni kusema mamlaka ya Zanzibar ndani ya Muungano yamezidi kufifia.

Tume ya Marehemu Jaji Francis Nyalali iliyochunguza mwaka 1991 juu ya utayarifu wa Watanzania kama wanautaka mfufo wa vyama vingi vya siasa ilitaka utaratibu wa sasa wa kuwa na serikali mbili- ya Muungano na ya Zanzibar- ubadilishwe na uwe wa Shirikisho. Tume hiyo ilikubali kwamba kuna matataizo ndani ya Muungano na ikasema ingekuwa busara kero kuhusu Muungano huo zisikilizwe na zitafutiwa ufumbuzi. Lakini walitokea watu waliosema kwamba mfumo wa Shirikisho utafungua njia kwa Muungano wenyewe kuvunjika. Kuna watu walioamini na bado wanaamini kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yasingedumu hadi leo bila ya kuweko Muungano.

Udhaifu ninaouona mimi ni kwamba Watanzania wa pande zote mbili za Muungano hawajaelezewa kinagaubaga sababu za kuunganishwa hapo April 1964. Inasemekana Hayati Mzee Karume wa Zanzibar alilikubali wazo la Muungano kutoka kwa Hayati Mwalimu Nyerere wa Tanganyika kama njia kwa serikali mpya ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na ulinzi dhidi ya jaribio lolote la wapinga mapinduzi wa ndani na nje ya Zanzibar kutaka kuipindua serikali yake.

Ndani ya Baraza la Mapinduzi la Zanzibar kulikuweko pia watu waliokuwa wanafuata siasa za mrengo wa kikoministi na wa shoto ambao Mzee Karume inadaiwa alihisi wangeweza kutishia uongozi wake.

Lakini watafiti wengine wanahoji kwamba kulikuweko mbinyo mkubwa kutoka nchi za Magharibi, hasa kutoka Marekani, ili Mapinduzi ya Zanzibar yadhibitiwe kwa vile yalionekana kuwa ni ya hatari na huenda yangeeneza ushawishi wa Wakominsiti na wa nchi za Kambi ya Mashariki katika eneo zima la Mashariki ya Afrika. Wamarekani hawajataka kucheza bahati nasibu na halafu washindwe na kuiona Zanzibar inageuka kuwa „ Cuba ya Afrika Mashariki“. Wao waliiona Jamhuri ya kimapinduzi ya Watu wa Zanzibar kuwa ati ni kibaraka wa madola ya Mashariki, hivyo kwa wao Wamarekani Muungano wa Tanganyika ( iliokuwa wakati huo inasaidiwa sana na nchi za Magharibi) na Zanzibar ni njia bora ya kuzuwia kusambaa hatari ya ukoministi.

Haijapita miaka, Mapinduzi ya Zanzibar yaligeuka na yalianza „kuwatafuna watoto wake“ yenyewe, licha ya wapinzani wake wa asili. Hofu ilienea Visiwani na kuna watu waliopotea bila ya kujulikana hatima zao hadi leo. Wazanzibari wengi walikimbilia Tanzania Bara kunusuru maisha yao au wakihofia kwamba wangewekwa vizuizini. Baadhi ya wale waliofukuzwa makazini Zanzibar waliweza kujipatia ajira Bara na wengine kwenda ng’ambo. Serikali ya Muungano mjini Dar es Salaam ilijua fika nini kilichokuwa kinatendeka Zanzibar, lakini wachambuzi wanasema wakuu wa Bara hawajataka kujiingiza katika mambo ya ndani ya Visiwani. Walihofia wasije kuwakasirisha wakuu wa huko Zanzibar. Yote huenda ni kuulinda Muungano usipate mtikisiko na labda kuvunjika. Na hasa inavyosemekana kwamba katika miezi ya mwisho kabla ya kuuawa Hayati Mzee Karume uhusiano baina yake na Hayati Mwalimu Nyerere ulikuwa si wa uchangamfu mkubwa kama ulivyokuwa hapo mwanzo.

Malengo makubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo Chama cha Afro Shirazi yalijivunia nayo – kuondosha ubaguzi wa makabila na wa rangi, kuhakikisha kuna huduma za kijamii kwa watu wote, kutokomeza umaskini, kutoa bure huduma muhimu za kijami za elimu, afya pamoja na maji – yalianza kusahauliwa polepole. Badala yake viongozi walijikusanyia mali na kuwa kama masultani wepya, huku uhuru wa raia wa kutoa maoni ukibanwa.

Wahakiki wanasema kwamba Mzee Hayati Karume aliposaini Mkataba wa Muungano alifikiri Tanganyika na Zanzibar zinaingia katika Mfumo wa Shirikisho la nchi mbili zitakazokuwa na mamlaka mengi, tena sawa, kila moja katika mambo yake ya ndani, na mambo machache yawe ya Muungano. Kabla ya nchi zote za Afrika Mashariki kuwa huru, wazo la kuundwa Shirikisho la Afrika Mashariki baada ya uhuru lilikuweko na kupigiwa upatu sana. Inafikiriwa na baadhi ya watu kwamba kiongozi huyo wa Zanzibar wakati huo hajafikiria kwamba Muungano huo utakuwa kama huu wa sasa ambao unaweka mamlaka mengi sana kwa serikali ya Muungano. Utaratibu wa serikali ya Tanganyika kuwa ni ileile ya Muungano ulikusudiwa uwe kwa muda mfupi sana, labda mwaka mmoja, hadi pale katiba mpya ya kudumu ya Muungano itakapotungwa. Lakini hadi leo mfumo huu ungaliko, bado unaendelea, ikiwa ni miaka 52 tangu kuanzishwa Muungano. Hoja iliotolewa kwa miaka mingi kutoka upande wa Zanzibar ni kwamba hakuna msingi wowote wa kusema kwamba Tanganyika imepoteza utambulisho wake ndani ya Muungano huu. Kwa hakika Tanganyika imevaa joho la Muungano na imejipanua kimamlaka. Ni mamlaka ya Zanzibar, kama inavotajwa katika Mkataba wa Muungano, ndio ya kulindwa na kuendelezwa ili kwamba, kama alivosema Hayati Mwalimu Nyerere mara kadhaa, kusiweko dhana kwamba Tanganyika ilio kubwa na yenye rasilimali nyingi zaidi “imeimeza” Zanzibar ilio ndogo kieneo na kwa idadi ya wakaazi.

Ukweli ni kwamba kila miaka ilivyoenda utambulisho wa Zanzibar ndani ya Muungano, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, unapungua. Hilo ni jambao ambalo Wazanzibari wengi linawasumbua hata kufikia hadi wengi wao sasa wanataka mfumo wa serikali tatu kama Tume ya Katiba Mpya ya Jaji Warioba ilivyopendekeza miaka miwili ilopita. Katika uchunguzi wake, tume hiyo imegundu kwamba zaidi ya asilimia 60 ya Wazanzibar wanataka Muungano wa Mkataba baina ya Tanganyika na Zanzibar.

Wazanzibari wanalikumbuka baraza la mawaziri la mwanzo la serikali ya Muungano hapo mwaka 1964, chini ya Hayati Mwalimu Nyerere kama rais. Lilikuwa na mawaziri 20 ( akiwemo mwanasheria mkuu wa kutoka upande wa Bara asiyekuwa na kura). Kati yao 13 walikuwa wanatokea Bara (Nyerere, Kawawa, Kambona, Munanka, Maswanya, Mgonja, Shaba, Eliofoo, Jamal, Bryceson, Tewa, Sijaona na Lusinde) na 7 walitokea Zanzibar (Karume, Jumbe, Hanga, Idriss Abdulwakili, Babu, Hasnu Makame na Hassan N. Moyo). Linganisha na baraza la Mawaziri la sasa chini ya Rais Magufuli ambalo lina mawaziri 23 (pamoja na mwanasheria mkuu wa serikali kutoka Bara asiyekuwa na kura) . Lina Wazanzibari wanne tu (Makamo wa rais Bi Samia Suluhu, Dk. Shein – kutokana na mamlaka aliyokuwa nayo kama rais wa Zanzibar – Dk. Hussein Mwinyi na Profesa Makame Mbarawa.

Tangu kuweko Muungano hakuna Mzanzibari aliyewahi kushika nafasi za juu katika taasisi za Muungano kama Benki Kuu, jeshi au polisi. Kuna idadi ndogo sana ya Wazanzibari wanaofanya kazi katika balozi za Tanzania nchi za nje na pia sehemu ya Zanzibar katika michango inayopata Tanzania kama misaada, mikopo au ruzuku kutoka nchi na taasisi za nje ni haba mno. Ilipokataliwa Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu Duniani, OIC, kwa kuambiwa kwamba masuala ya mambo ya kigeni na ushirikiano wa kimataifa yako chini ya serikali ya Muungano, Wazanzibari wengi walihuzunishwa. Mfumo wa serikali ya Muungano wa utozaji na ukusanyaji kodi umelaumiwa mara kadhaa na wafanya biashara wa Zanzibar kwamba unawaonea, hautilii maanani kwamba uchumi wa Zanzibar ni wa kivisiwa, tafauti na ule wa Bara.

Hadi mwaka 1992 ulipoingia mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, maoni yeyote yaliyohoji au kuonesha kutoridhika na mfumo wa Muungano uliokuweko yalinyamazishwa. Lakini watu waliendelea kuelezea maoni yao na kutaka kuchangia katika kutunga mustakbali mwema wa Muungano wao. Marais wa Zanzibar waliopita, Mzee Jumbe, Dr. Salmin Amour na pia Dr. Amani Karume hawajawa na wakati rahisi pale walipokuwa wanasimama kidete kabisa kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano. Mara kadhaa maalalamiko aliyokuwa akiyatoa aliyekuwa makamo rais wa kwanza wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff, juu ya kupunjwa Zanzibar katika faida za Muungano yamekuwa yakibezwa kutokana tu na maslahi ya kichama badala ya kushughulikiwa.

Zanzibar inahitaji iuangalie uhusiano wake namna ulivyo na Tanzania Bara kwani unatoa sura kwamba Tanganyika ndio mlinzi wa serikali ya Zanzibar kwa vyovyote vile, bila ya kujali nini kinatokea ndani kwenyewe Visiwani. Maadam chama tawala cha CCM kinabakia madarakani katika pande zote mbili za Muungano. Maono ya CCM tangu kuundwa kwake kuelekea Zanzibar yamekuwa kuwekea uzito zaidi suala la usalama katika visiwa hivyo kuliko lile la maendeleo.

Zanzibar imeshindwa kutamba na kuingia kwa njia huru katika mikataba ya kiuchumi na kifedha bila ya ridhaa ya serikali ya Muungano. Haiwezi kufurukuta na kuwa na siasa zake huru juu ya mambo ya fedha na sarafu zinaoambatana na mikakati yake ya maendeleo, kwa vile masuala hayo ni ya Muungano. Siasa zozote mbovu za Benki Kuu ya Tanzania zinaumiza moja kwa moja uchumi wa Zanzibar. Kugharimia urari wa malipo huko Bara kunaiumiza pia Zanzibar- ughali wa maisha kupanda na kuweko mriupuko wa bei za bidhaa.

Ukitizama uzoefu wa Miungano katika sehemu nyingine za dunia ni kwamba pale Muungano unapokuwa baina ya nchi kubwa na nchi ndogo kunakuweko kila wakati hofu ya nchi ndogo „kumezwa“ na nchi kubwa. Miungano kama hiyo iliojengeka kwa hofu kutoka upande mmoja haijadumu, imevunjika. Mifano mizuri ni ile iliokuweko baina ya Misri na Syria na kuundwa Muungano wa Jamhuri ya Kiarabu baina ya mwaka 1958-1961. Wasyria walihiyari kujitoa kutoka Muungano huo kwa vile waliona hatamu na nyadhifa nyingi za juu katika serikali ya Muungano zilikamatwa na Wamisri.

Shirikisho la Senegambia ambalo lilikuwa baina ya Senegal na Gambia, nchi mbili huko Afrika Magharibi, lilikufa mwaka wa 1989 baada ya kudumu miaka saba tu. Gambia ilikataa kuwa na mfumo wa serikali ya Muungano ikihofia kumezwa na Senegal ilio kubwa kieneo na kwa idadi ya wakaazi. Pia tusiusahau Muungano wa Kisoviet (Urusi) baina Russia na Jamhuri nyingine za Kisoviet na ambao ulisambaratika mwaka 1999 baada ya kuweko kwa karibu miaka 80. Waeritrea wilikataa kubakia ndani ya Ethiopia na walikamata bunduki kupigana dhidi ya majeshi ya Ethiopia ili kuikomboa nchi yao baada ya kukaliwa kwa zaidi ya miaka 20. Watu wa nchi ndogo ya Timor Mashariki huko Kusini Mashariki ya Asia baada ya Mreno kuondoka nchini mwao mwaka 1975 hawajakubali ukoloni huo nafasi yake ichukuliwe na ukoloni wa nchi kubwa jirani ya Indonesia. Walipigana hadi walipopata uhuru mwaka 2002. Wasahara Magharibi huko Afrika Kusini wanapigana, hawataki kulikubali takwa la Morocco kwamba nchi yao iwe sehemu ya miliki ya Ufalme wa Morocco.

Baadhi ya wakati huzushwa suala kama Tanganyika au Zanzibar zitamudu kuishi kila moja peke yake bila ya Muungano. Suala hilo hasa linaelekezwa zaidi kwa Zanzibar kama inaweza kuishi bila ya Tanganyika. Tanganyika inaweza sana, ukiangalia uchumi wake mkubwa. Lakini haitopenda kuwa na jirani ambaye hatabiriki, hajulikani atakuwa vipi baada ya kuvunjika Muungano. Hiyo ndio maana Rais aliyepita wa Muungano, Jakaya Kikwete, alimwambia wazi hivi karibuni katibu mkuu wa Chama cha Upinzani cha CUF, Maalim Seif Shariff, kwamba CCM inahofia kwamba pindi Maalim Seif Shariff atakuwa rais wa Zanzibar basi atauvunja

Muugano. Hilo Maalim Seif Shariff amelikataa moja kwa moja, na kusisitiza kwamba yeye ni muumini wa Muungano, lakini Muungano anaoutaka ni ule wa haki. Anasema Muungano wa sasa unaibana Zanzibar na anakumbusha msemo wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee Karume, kwamba Muungano ni kama koti. Usishange mtu anapotaka kulivua pale linapombana sana na kushindwa kupumua. Maalim Seif Shariff anashikilia kwamba yeye ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa urais wa Zanzibar wa Oktoba mwaka jana na ambao ulivunjwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Wazanzibari wengi sana hawana wazo la kuuvunja Muungano. Vivyohivyo walivyo Watanganyika wengi. Wengi wao hawajawahi kuishi katika nchi nyingine isipokuwa hii ya sasa yenye jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawaijui ile Zanzibar kabla ya 1964. Vivyohivyo kwa Watanganyika. Ni wachache walio hai wanaijuwa Tanganyika. Suali linazushwa kila wakati ikiwa Muungano huu ni mzuri na wenye manufaa mbona nchi nyingine za jirani hazijavutiwa nao? Tukumbuke kwamba Muungano huo ulisadifu kufanyika katika wakati ambao viongozi waliouasisi walihitajiana. Na ingekuwa si wakati huo na matukeo yaliozunguka wakati huo, kama vile kutokea Mapinduzi ya Zanzibar na uhasama wa madola makuu uliokuweko wakati huo wa Vita Baridi, sidhani kwamba ingewezekana kuwa na Muungano wa Tanzania wa aina hii. Suala la Muungano wa damu, japokuwa ni muhimu, lakini ni la pembeni.

Licha ya yote hayo, inafaa pia tuachane na ile ambayo imekuwa dhana potofu hadi miaka ya karibuni kwamba kuhoji mambo fulani yanayofanyika ndani ya Muungano- ambayo hayatimizi lile lengo mama la awali la usawa baina ya pande mbili- ni uhaini, kukosa uzalendo au sawa na kuupinga Muungano wenyewe. Suala la kuhoji mambo ya yanayofanyika kuhusu Muungano, kuudadisi na kuudurusu baada ya kila muda ni jambo linaloupa afya Muungano pamoja na hewa mpya ya kupumua nayo kila wakati. Muungano ni zoezi endelevu na kila inapohitajika kuufanyia marekebisho au mabadiliko ni sahihi kabisa kufanya hivyo. Siasa za mkwamo hazisaidii. Watu wasigope kuja na ubunifu mpya kuhusu Muungano wao. Wakati mwingine woga ni mbaya zaidi kuliko yale magonjwa ya hatari sana kwa mwanadamu. Katika mchezo wa mpira inabidi wakati mwingine ubadilishe mbinu (tactics ) za mchezo ili ushinde. Vilevile kwa Watanzania juu ya Muungano wao.

Muungano mzuri na ulio wa amani ni ule unaowapa watu wote wa pande zote za Muungano haki ya kuchangia na kujiamilia mustakbali wao tangu kutoka ngazi za chini kabisa hadi juu kabisa. Chachu nyingine inayojenga Muungano imara ni kuheshimiwa haki za binadamu kwa raia wote ndani ya Muungano, raia wawe huru kuchagua mfumo wa kisiasa wanaoutaka na viongozi gani wanataka wawaongoze kwa ajili ya maendeleo yao ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Kwa vyovyote, kwamba Muungano wao umefikia miaka 52, licha ya matatizo yote, ni jambo la fahari kwa Watanzania. Wana kila haki ya kujivunia. Wamezipiku nchi nyingi zilizojaribu kufanya hivyo na zikashindwa njiani. Watanganyika na Wazanzibari kwa pamoja wamethibitisha kwamba mara nyingine “kupepesuka si kuanguka”. Happy Birthday Muungano.

Bila Muungano Watanganyika wasingeoa Zanzibar?


Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika Mwalimu Julius K Nyerere na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Abeid Aman Karume wakisaini hati za makubaliano ya Muungano wa Tanzania.

Na Ally Mohammed.
APRILI 26, mwaka huu 2016, Tanzania imetimiza miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ni hatua kubwa na ni jambo la kupendeza kuona tunasherehekea kitu kilichotufanya tukawa wamoja.

Pamoja na umoja wetu huu tunaojivunia sasa, ni jambo la kawaida kuona minyukano, vituko na mabishano kila inapokaribia uchaguzi na hata baada ya uchaguzi hapa Zanzibar.

Ule msemo wa kuna maisha baada ya uchaguzi kwa Zanzibar nimeushuhudia siku za mwisho wakati wa uongozi wa Rais Amani Abeid Karume na mwanzoni tu mwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoshirikisha vyama vya CCM na CUF.

Huu mnyukano wa CCM na CUF na tangu zama za ZNP, ZPPP na ASP nini hasa kilichopo ni Zanzibar kujiogopa au kuogopwa?

Mandhari nzuri na fukwe, pia upepo wa marashi ya karafuu sicho haswa kinapelekea kutokuwa na muelekeo wa kustawi kwa demokrasia katika visiwa hivi kwani kila mmoja kwa uwezo wake anayo fursa ya kutembelea fukwe kuanzia Kizimkazi mpaka Nungwi bila ya bughudha yeyote ile. Na hii inanasibishwa na msemo adhimu wa “Zanzibar ni njema atakae na aje”.

Kwenye siku za kuelekea Mapinduzi ya Januari 12, 1964, kulikuwa na tetesi kuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na Kassim Hanga, kuwa na mpango wa kuangusha Serikali ya Zanzibar.

Lakini, Rais wa Tanganyika wakati huo, Julius Nyerere pamoja na Nchi za Magharibi walikuwa na hofu kwamba Zanzibar ingefanikisha mapinduzi hayo ingeweza kuwa “Cuba ya Afrika” na kwa vile ipo karibu na Tanganyika, ilizidi kumtia hofu Nyerere.

Nyerere alianza kuona kitisho hicho na kuamua kuwashawishi Milton Obote na Jomo Kenyatta kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki ili kujiweka salama na kitisho cha Zanzibar.

Wakati Nyerere akiiona Zanzibar kama balaa lijalo, Marekani nao kwa upande wao waliiona Zanzibar kama kizingiti kikubwa maana ilishaanza kuelekea kwa China, Urusi na Cuba kwenye siasa za Ukomunisti na hivyo Marekani kuona jinsi itavyokuwa na upungufu wa uwezo katika ukanda huu.

Tishio hilo la Zanzibar kwa Marekani lilizidi kuhanikiza na kumshawishi Nyerere afanye Muungano na Zanzibar ili kuimeza na kupunguza kitisho hicho.

Pia tusisahau kuwa kwa wakati huo, Zanzibar ilikuwa ni nchi yenye uchumi mkubwa kuliko Tanganyika na hivyo kuweka tishio hilo kuwa la kweli katika pande zote.

Sababu nyingi zilizosababisha Muungano wakati huo hazipo tena na sasa kuna sababu mpya na zenye misingi ya wananchi wenyewe wa Zanzibar na Tanganyika pia.

Tumeanza kusikia wananchi wakidai Muungano wa Serikali Tatu, Muungano wa Mkataba, Mamlaka Kamili, Kero za Muungano, Kura ya Maoni kuhusu uhalali wa Muungano wenyewe na jambo kubwa la Mabadiliko ya Katiba.

Pia tumeshuhudia viongozi mbalimbali wa SMZ kutoka CCM wakieleza kwa namna tofauti kuwa hawawezi kuishi bila ya Muungano na kuwa Zanzibar haiwezi kusimama yenyewe bila ya Muungano.

Hoja zao nyingi zimejawa na woga na pia hazina ushahidi wowote wa hayo wayasemayo.
Kwa mfano, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliandika makala ndefu katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015 na kueleza wasiwasi kama huo na kunasibisha matukio ya kumwagiwa tindikali kwa wasichana wawili raia wa Uingereza, uwepo wa kikundi cha Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu (Uamsho) kuwa ni miongoni mwa dalili hizo za kuelekea kwenye ugaidi ikiwa CUF watashinda Zanzibar.

Hayo yote na mengineyo ni sehemu ya woga kwa vile hakuna kesi hata moja ya ugaidi ambayo imehukumiwa na kuthibitishwa tuhuma zake.

Watuhumiwa 14 wa kesi ya ugaidi kutoka Zanzibar bado wapo rumande kwa zaidi ya miaka miwili huku upande wa mashtaka ukiwa haujakamilisha upelelezi wa mashtaka yao.

Zanzibar haijawahi kuwa na tatizo la udini, tangu enzi na dahari kwani Zanzibar kuna makanisa makubwa makubwa na yenye historia ndefu sana, mfano wa makanisa ya Mbweni, Kizimbani, Chachani na Mkunazini.

Hakuna kumbukumbu zozote au mahala popote pale kwenye taarifa za kupigwa au kuuawa mtu kwa kubaguliwa katika misingi ya dini yake.

Moja ya mnasaba wa kauli za woga kwa kisingizo cha udini inaweza kuwa hoja ya Padri Evarist Mushi kuuliwa kwa kupigwa risasi hapa Zanzibar na kisha kukamatwa watu ingawa mpaka leo hii mtuhumiwa hajatiwa hatiani na sheria kufuata mkondo wake na yupo nje akiendelea na shughuli zake, wengi walihusisha kukamatwa kwake na sababu za kisiasa.

Mtiririko wa matukio ya kila namna ya kutegwa mabomu na miripuko isiyoua, uchomwaji moto wa baadhi ya nyumba za wananchi, nyumba za ibada na maskani za vyama vya siasa ni baadhi ya matukio ambayo mpaka leo hii hakuna hata moja lililothibitishwa kimahakama na watuhumiwa wake kuhukumiwa.

Hii inaleta tafsiri mbili kubwa kuwa Jeshi la Polisi lina uwezo mdogo ama linatumika kisiasa na huenda lipo nyuma ya matukio haya ama inawajua hakika waliofanya na haiwachukulii hatua.

Tangu mwaka 1995 wakati uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliporejeshwa, wafuasi ambao wamekikamatwa mara zote ni wale wa vyama vya upinzani hususani CUF.

Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla katika hili la Muungano kumekuwa na maneno mengi yanayolenga kuleta hofu ambayo yanatolewa na baadhi ya viongozi wakubwa tu kusema maneno ambayo hata hayana mantiki.

Je, bila ya Muungano Wazanzibari wasingeoa Tanganyika au kuolewa Tanganyika?
Hoja hii ya kuoa na kuolewa ni hoja dhaifu sana kwa sababu Wazanzibari wamechanganya damu na mataifa ambayo hata mnasaba nayo hatuna na wala sio kwa dhana ya Muungano.

Jengine wanachochea hofu kuwa Muungano ukivunjika basi Wazanzibari watahama Tanganyika na kurudi kwao ili tu mtu mwenye mali au familia aone ni jambo haliwezakani.

Pia tumesikia wabunge kadhaa wakisema ukivunjwa Muungano basi mchele wa Mbeya itakuwa ndiyo mwisho kufika visiwani. Kwamba moja ya faida ya Muungano ni kwa Wazanzibari kula mchele wa Mbeya!

Huu Muungano una faida nyingi sana na kutoa fursa kubwa sana kwa pande zote, kwa muda wake na sababu zilizowekwa na kuuasisi mwaka Aprili 26, 1964 hazipo tena leo inapaswa kuangaliwa upya mfumo na matakwa yake kwa kizazi cha leo na kijacho.

Ukisema tumeunganika kwa sababu za kihistoria basi Zanzibar ilipaswa kuungana na Uingereza, Oman, Yemen, India pia kwa vile hao wamefika mwanzo Zanzibar na wana historia ndefu zaidi na Zanzibar kuliko Tanganyika.

Pili ukisema kwa sababu ya muingiliano wa kidamu, Zanzibar ilipaswa pia iungane na Kenya kwa ndugu zao walioko Lamu, Malindi na Mombasa.

Pengine pia Zanzibar ilitakiwa iwe na Muungano na Commoro. Kuna vitabu vimewahi kumnukuu Nyerere akisema kwamba angetamani visiwa vya Zanzibar viwe mbali sana na Tanganyika. Kwamba kama angeweza, angeweza kuvisukuma mbali baharini. Inawezekana vipi mtu atamani kumsukuma ndugu yake mbali kiasi hicho?

Kauli nyingine yenye utata ni ile iliyowahi kutolewa na Balozi Ali Karume kuwa “Sultan Jamshid alikuwa mtawala wa Kigeni Zanzibar”. Hii inaleta taabu kidogo kuilewa kwani kati ya Ali Karume na Jamshid nani ni mgeni hapa Zanzibar?

Sultan Jamshid kaburi la babu yake Sayyid Said bin Sultan lipo Zanzibar wakati kaburi la babu yake Ali Karume, Amani Karume, halipo Zanzibar. Ukitaka kujua kuhusu hili, pitia kitabu cha Ibrahim Noor Sharif Tanzania na Propaganda za Udini.

Yaliyowakuta akina Kassim Hanga, Abdulrahman Babu, Saleh Sadalla, Amani Thani, Khamis Ubwa na wengine yanafanana na yanayowakuta Uamsho leo pamoja na viongozi wa CUF na wengineo nje ya CCM.

Tumeona wengi wa hao waliopo CCM wanatetea muungano huu wakiwa wapo kwenye vyeo tu na kulinda tonge zao.

Wengi wakitolewa kwenye mfumo au kustaafu nao akili zao hurudi na kuona mapungufu makubwa ya Muungano huu.

Zanzibar tuliona Baraza la Wawakilishi kuogopa maazimio yao wenyewe waliyoyapitisha kama mapendekezo katika mchakato wa katiba mpya na kwenda kushikana uchawi Dodoma kwa akina Pandu Ameir Kificho na Marehemu Awadh Salmin.

Hapa ndipo unapoona kujiogopa kwa Zanzibar yenyewe kwa upande mmoja na pia kushikana kwake kunavyoleta woga kwa watu nje ya Zanzibar.

Hapo utaona kuwa mpaka leo Muungano unaishi kwa dhana kubwa ya woga. Marekani waliiogopa Zanzibar ila si kweli kuwa wanaiogopa leo tena.

Tanganyika bado wanaiogopa Zanzibar ukisikiliza kauli za viongozi mbalimbali hasa wa upande wa CCM.

Na pia woga umewajaa Wazanzibari wenyewe ndani ya CCM kuona hawawezi bila ya Muungano huu hivi ulivyo.

Ukiyapima manufaa ya Muungano huu ya miaka 50 hayamithiliki zaidi ya dhana zilizojengwa na ambazo hukosa majibu muhimu ya kisheria ama kijamii.

Kwa mfano je, Tanganyika imeenda wapi baada ya Muungano?
Aboud Jumbe alipopeleka hoja yake hakujibiwa ila alifanyiwa jambo binafsi na kuvuliwa nyadhifa zote pale Dodoma.

Seif Shariff na AMAHURU hawakujibiwa hoja zao na mwisho walifukuzwa na kufungwa.
Mfululizo wa matukio haya unalenga kuwa hapa kinachofichwa ni nini?

Muungano kwa sasa unasimama kwenye misingi mibovu ambayo kila mmoja anajiuliza maswali mengi yasiyo majibu.

Tunaposherehekea kutimiza miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wakati pia wa kuangalia namna bora tunaweza kuwa na Muungano ambao utakuwa na mizania sawa kwa washirika wote wa Muungano huu.

Majipu yataondoka na CCM

John Magufuli, Rais wa Tanzania (kulia) akiwa na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete
WIKI iliyopita, Rais John Magufuli aliitisha mkutano wa ghafla kukutana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya mikoa na wilaya zote nchini.

Mwaliko huo ulikuwa wa ghafla na uliambatana na sharti moja kuu la viongozi hao kutofika Dar es Salaam wakiwa wamevaa sare za chama.

Gharama za safari zililipwa na Ikulu na makada hao waliondoka wakifurahia jinsi Ikulu ilivyowakarimu kwa chakula safi, kingi na cha kusaza!

Mkutano huo ulifanyika Ikulu na ilionekana wazi kuwa, waandaaji walikuwa ni maofisa wa Ikulu. Abdulrahmani Kinana, Katibu Mkuu na vijana wake wa makao makuu, hawakuwa na raha.

Walionekana wazi kuchoka na kusubiri mkutano huo uishe ili waendelee na shughuli zake nyingine.
Baada ya kufika katika ukumbi wa mkutano huo, hata itifaki za kawaida za mikutano ya ndani ya CCM zilikuwa hazieleweki, jambo lililomfanya Kinana kusimama mara kadhaa kurekebisha hapa na pale ili mambo yaende.

Kinana alikuwa na ujumbe mmoja kwa washiriki – kwamba mwezi Juni mwaka huu, Rais Magufuli atakabidhiwa chama kama mwenyekiti.

Kabla ya mkutano huo, nje ya ukumbi wa mikutano Ikulu na kwenye hoteli walikofikia makada, gumzo kuu lilikuwa ni kama CCM itakuwa salama chini ya Magufuli.

Wapo waliojidanganya kuwa Jakaya Kikwete, mwenyekiti wa sasa, hawezi kukabidhi chama mpaka 2017. Mashabiki hao wa Jakaya walisema Rais Magufuli aachwe aendelee na kazi ya kutumbua majipu serikalini, chama kibaki na Jakaya, ili kibaki salama.

Pale ukumbini, baada ya Kinana kutangaza kuwa Rais Magufuli atakabidhiwa chama mwezi Juni, kundi dogo la makada mashabiki wa Magufuli walishangilia, huku wakijishtukia wenyewe kwa wenyewe.

Walio wengi hawakuona sababau ya kushangilia kwa sababu kwanza ni utaratibu wa kawaida kufanya hivyo, na pili, kushangilia ni sawa na kusema wamechoka na uongozi wa Jakaya.

Baada ya mgongano ya kiitifaki, Rais Magufuli alipata nafasi ya kuwahutubia. Kwa kusudi la makala hii nitataja machache ya aliyozungumzia.

Kwanza, alisema amewaita viongozi hao kuwashukuru kwa kumpigania hadi akachaguliwa kuwa rais. Alikiri kuwa bila wao, asingekuwa hapo alipo. Pili, aliwaeleza kuwa amewaita kuwahakikishia kuwa nchi iko salama na chama kitakuwa salama.

Tatu, alisema amewaita kuwahakikishia wale wenye mashaka na kasi yake ya utumbuaji majipu, na walioanza kupinga hatua hizo waache kumkatisha tamaa. Akatumia muda mrefu kueleza baadhi ya hisia zinazoenezwa kuwa anakiuka haki za binadamu, kuwa mizigo bandarini imepungua, na kuwa atadhalilisha CCM.

Mpaka hapa kuna mambo mawili makuu ya kutazamwa kwa umakini. Kwanza, Rais Magufuli alifanya kampeini kwa kusisitiza, “Tanzania ya Magufuli” itafanya hili na lile. Alikuwa mwangalifu sana kutotanguliza CCM mbele ya umma uliokuwa umekata tamaa na CCM.

Hata baada ya kuapishwa, mara mbili ametofautiana na Kikwete katika vikao vya kamati kuu. Mara ya mwisho walitofautiana kuhusu suala la uchaguzi wa Meya wa Jiji la DSM.

Katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe wa kamati kuu walilalamika kuwa kuna mawaziri na watumishi wa serikali wanashabikia uchaguzi ufanyike na meya atoke Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).

Kikwete aliunga mkono na kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya wote walio serikalini na wanashibikia jiji liende Ukawa. Kabla ya kuhitimisha ajenda hiyo, Rais Magufuli akaomba kuzungumza.

Katika mchango wake, akakiri kuwa wapo wanaounga mkono na yeye ni mmoja wao. Akasema kama ni kosa lilifanyika pale CCM iliporuhusu uasi ndani yake na kusababisha mkoa wa Dar es Salaam uwe na madiwani wengi wa Ukawa.

Akakumbusha kuwa hata yeye wakati wa kampeni alifika mahali akaacha kwenda kwenye vikao vya usiku vya kufanya tathmini ya kampeini kwa sababu ya fitina na uasi.

Akasisitiza kuwa kama CCM haitaacha majungu, yeye hatakuwa tayari kuitetea. Akahitimisha kwa kusema, ni vizuri “tuwaache Ukawa watutawale Dar es Salaam ili tuonje uchungu wa kutawaliwa kwa sababu ya uasi wetu”.

Baada ya mchango wa Magufuli, Jakaya Kikwete aliahirisha kikao kwenda kunywa chai. Mgongano huu wa Kikwete na Magufuli hauwezi kuiacha CCM ikawa salama.

Hii ni kwa sababu huwezi kusifia hatua anazochukua Magufuli bila kulaani uongozi wa Jakaya. Mpaka sasa Magufuli hajaanzisha jambo jipya serikalini, bali anachofanya ni kukosoa utendaji wa Rais Kikwete.

Kwa hiyo, tangazo kwamba Magufuli atakabidhiwa CCM mwezi Juni si tangazo la heri kwa CCM ya Kikwete. Ni tangazo la kutumbua majipu ndani ya CCM yakiwamo yale yaliyomwezesha Magufuli kuingia madarakani.

Hata kama Magufuli anatamba hadharani kuwa hakuna mfanyabiashara yeyote aliyemchangia hata senti moja, lakini CCM na vyombo vyake vilifanya madudu makubwa kumwezesha Magufuli “kushinda” urais.
Matajiri walichangia CCM iliyokuwa inamnadi yeye. Je, yuko tayari kufumua hata jipu hilo?

Jambo la pili ni ukweli kuwa majipu anayoyatumbua Magufuli si ya wapinzani bali watendaji wa serikali ya CCM. Kwa hiyo, majipu yanayotumbuliwa ni matawi lakini. Mashina ya majipu ni CCM.

Je, uking’oa shina mti utapona? Huu ndiyo wasiwasi unaoikumba CCM ikiwa mikononi mwa Magufuli. Kwa hiyo, wana CCM wanaoijua CCM wanajua kuwa CCM haitakuwa salama, ingawa yeye aliwahakikishia kuwa itakuwa salama.
Kwanini alilazimika kuwahakikishia usalama? Magufuli anaishi kwenye nadharia kuwa mafisadi ndani ya serikali na ndani ya chama, hawakutumwa na chama kufanya uchafu.

Magufuli anaishi katika njozi kuwa anaweza kutumbua majipu yaliyo katika sehemu nyeti – tena bila ganzi – halafu mgonjwa akabaki kuchekelea na kushangilia.

Wenye hekima na wazee wa chama wanajua majipu mengine yameumbwa ndani ya CCM, na ndiyo yanashikilia uhai wa CCM. Ukiyatumbua, umeitumbua CCM. Hata kwa hekima ipi, hayatumbuliki. Na yakitumbulika, yanaondoka na CCM.

Ufisadi wa mabilioni na mikataba feki ndiyo imeifikisha CCM na serikali yake hapa ilipo. Hata kwa kitendo cha Magufuli kuita makada wa CCM kwa kutumia fedha ya serikali wakati akidai kubana matumizi, tayari ametengeneza kipere kitakachogeuka jipu.

Uzoefu pale Ikulu na Lumumba – makao makuu ya CCM – ni kuwa mikutano ya namna hiyo hutumia mara tatu ya gharama halisi.

Hiyo ndiyo CCM atakayokabidhiwa Magufuli mwezi Juni. Magufuli hajui CCM. Kama angeijua, asingeikaribisha Ikulu kwa ajili tu ya kuihakikishia kuwa itakuwa salama yake.
CHANZO: MWANAHALISI ONLINE

Kikwete kupandishwa kizimbani?


Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Na Ahmed Rajab
UONGOZI ni dhamana. Ni dhamana kubwa na nzito mtu kujitwika nayo au hata kutwikwa nayo. Mzigo wa uongozi unazidi kuwa mzito uongozi huo unapokuwa uongozi wa taifa. Hili ni wazi, na halina shaka, isipokuwa kwa wasiotaka kulijuwa.

Dhamana nayo ina majukumu yake. Na majukumu hayo yanazidi kuwa nyeti dhamana hiyo inapokuwa ni dhamana ya kuliongoza dola, watu wa hilo dola, yaani wananchi, na rasilmali zake ambazo kwa hakika huwa ni rasilmali za hao wananchi.

Kuna wenye kuhoji kwamba aliyesimamia utawala wa awamu ya nne anastahiki ashitakiwe kwa matumizi mabaya ya madaraka aliyokuwa nayo.

Wanayataja mambo mawili makuu: la kwanza, ufisadi uliokithiri na la pili, kuporwa kwa haki za Wazanzibari kutokana na kufutwa kwa uchaguzi uliokuwa huru na wa haki wa Oktoba 2015.
Madai yote hayo mawili ni mazito.

Wenye kuyatoa wanaendelea kuhoji kwamba kwa kutochukua hatua imara kupambana na ufisadi Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwezesha pawepo nafasi kubwa iliyowaruhusu wezi kuiba mali ya serikali.

Wakati huo huo nafasi hiyo au mazingira hayo yamewawezesha watumishi wa serikali waendeshe mambo ovyo ovyo.

Kuendesha mambo ovyo ovyo, kienyeji, kwa kujizingatia “sisi kwa sisi” tu bila ya kuwajali wananchi walio wengi kumekuwa na athari zake. Athari hizo ni ovu na nyingi.

Miongoni mwazo ni kuzusha hali zinazoupalilia ufisadi wa kisiasa na wa kiuchumi, kuzusha hali au mazingira yasiyoweza tena kuudhibiti ubadhirifu wa fedha za umma. Na ni hali hizo hizo zinazoiruhusu serikali iwe inatoa mikopo kiholela, mikopo inayowafaidisha zaidi wanasiasa na watumishi wakuu wa serikali.

Kwa jumla kuna ushahidi mkubwa wenye kuonyesha na kuthibitisha jinsi ufisadi ulivyojengeka nchini, hususan katika awamu ya nne, kwa ubia uliozidi kufanikishwa baina ya wanasiasa, mafisadi katika sekta ya binafsi na watumishi wakuu wa serikali.

Hili ni jengo la ufisadi lililojengeka juu ya misingi iliyochimbwa na kusimamishwa na wanasiasa wa chama kinachotawala.

Chama hicho kimekumbwa na ugonjwa uleule uliovikumba vyama vilivyopigania uhuru katika nchi nyingi za Kiafrika. Huu ni ugonjwa wa kuamini kwamba ni vyama hivyo tu vyenye haki ya kutawala na viongozi wa vyama hivyo tu ndio wenye haki ya kuitwa watawala.

Wakishaitwa watawala, wakavikalia viti vya utawala huanza kujiona kuwa wao ndio serikali na serikali ndio dola.

Kwa hivyo, kwa kuwa wao wanajiona kuwa ndio serikali basi mantiki yao inawafanya waamini kwamba wao pia ndio dola. Siyo tu kwamba dola ni lao wao peke yao lakini wao ndio hasa dola. Wao ndio dola na dola ndio wao. Ndiyo maana wanalisarifu dola watakavyo. Chambilecho Joseph Mihangwa wanaligeuza dola kuwa “shamba la bibi”.

Kwa hakika, makala ya Mihangwa katika matoleo mawili yaliyopita ya gazeti hili pamoja na makala ya ukurasa wa mbele wa toleo la wiki iliyopita chini ya kichwa cha maneno “Nchi ilivyotafunwa mbele ya Kikwete” ni makala ambayo kila Mtanzania anapaswa ayasome.

Makala yote hayo matatu yanatoa mwanga kuonyesha jinsi utawala wa awamu ya nne ulivyokithiri si katika ufisadi tu bali pia kwa uzembe katika uendeshaji wa serikali.

Ukishayasoma makala hayo hutokuwa na shaka yo yote kwamba Rais wa awamu ya nne ni mtu anayetakiwa afikishwe mahakamani ila Katiba tuliyo nayo huenda ikamkinga. Juu ya hayo, kuna wenye kusema kwamba kwa Magufuli chochote kinaweza kuzuka na kwamba hata ile haramu ya Zanzibar inaweza ikawarejea wenyewe.

Hata hivyo licha ya Magufuli na ayafanyayo, si wengi wenye matumaini hayo. Hoja yao kubwa ni kwamba hakuna wa kuaminiwa, na kuaminika, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Yeyote yule anayeibuka akawa na ujasiri wa kuwaambia kweli watawala kwamba wako uchi na wanahitaji wajistiri huambiwa kuwa ni msaliti na haini. Jaza yao huwa ni kudhalilishwa na kugandamizwa. Na wenye kuwagandamiza huwa ni wale wale waliokuwa wakipigania haki na usawa wakati wa kupambana na ukoloni. Mfumo wa kisiasa wa aina hiyo haukubali abadan kuruhusu pawepo na mfumo mbadala.

Hayo si mageni katika historia ya ulimwengu. Tangu Mapinduzi ya Ufaransa (1789 hadi 1799), mara nyingi wakombozi wa nchi mbali mbali wamekuwa wakigeuka na kuwa wagandamizi. Waliokuwa wakionewa wakawa ndio wenye kujitutumua kuwaonea wengine. Na wakionea na wakiwaumiza watu kwa kuzikanyaga haki zao za binadamu hawadhani kuwa wanawajibika kuwaomba radhi wananchi.

Hii ndiyo moja ya sababu zinazowafanya baadhi ya watu katika nchi za Kiafrika wawe wanahoji kimwehu kwamba bora kutawaliwa na wakoloni kushinda kutawaliwa na Waafrika wenzetu. Hoja yao kubwa ni kwamba kimsingi maisha yao ya kawaida hayakubadilika tangu enzi za ukoloni. Wanasema hawaoni tofauti kubwa kwa namna wanavyotawaliwa sasa na walipokuwa wakitawaliwa na wakoloni.

Sababu ya hayo ni kwamba hawa watawala wetu wa leo wamerithi mengi kutoka kwa wakoloni. Wamerithi sera na hata namna ya kufikiri, namna ya kuyatumia madaraka waliyo nayo na namna ya utendaji kazi wao. Wanayakumbatia na kuyapakata madaraka kama ni yao wao watawala peke yao bila ya kuwashirikisha wengi wa wananchi.

Mambo ya ufisadi hayako kwetu tu lakini wenzetu nao pia wanayo ila wao wameweza kuzitumia nguvu za umma kupambana nayo. Wameweza pia kuzitumia taasisi za kidemokrasia kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa. Tuchukulie mifano ya nchi kadhaa za Amerika ya Kati na Amerika ya Kusini.

Sheria katika baadhi ya nchi hizo zinaruhusu marais wastaafu na hata wa sasa wafikishwe mahakamani. Hivi karibuni marais wawili wastaafu wa Honduras na El Salvador walishtakiwa kwa ufisadi.

Serikali ya Rais mstaafu wa Honduras Rafael Leonardo Callejas ilifanya mengi katika ustawi wa jamii lakini mafanikio hayo hayakuweza kumkinga Callejas asishtakiwe. Alikabiliwa na mashtaka saba ya ufisadi alioufanya wakati wa muhula wake wa urais (Januari 1990 hadi Januari 1994). Nchini Honduras, Rais ana muhula mmoja tu wa kutawala wa miaka minne.

Mnamo 2005, Bunge la Honduras liliibatilisha sheria iliyokuwa ikiwakinga Marais wastaafu wasishtakiwe. Sheria hiyo ilipobatilishwa Callejas mwenyewe, kwa hiyari yake, alijipeleka mahakamani na akafunguliwa kesi kwa mashtaka yote yaliyomkabili. Alifanyiwa kesi na halafu Mahakama ikamwachia huru baada ya kuona kwamba hakuwa na hatia.

Halafu Desemba mwaka jana alishtakiwa na Mahakama ya Marekani kwa kuhusika na kashfa ya ufisadi ya Shirikisho la Soka la FIFA wakati alipokuwa mkuu wa Shirikisho la Soka la nchi yake.

Siku kadhaa baada ya kushtakiwa Callejas mwenyewe akenda Marekani ambako alitiwa mbaroni na siku chache baadaye aliachiwa na Mahakama kwa dhamana. Mwezi uliopita alikiri kwamba alikuwa na hatia ya kupokea hongo ya dola za Marekani 500, 000 mwaka 2012, fedha ambazo alikuwa azile yeye na afisa mwengine.

Nchini El Salvador hakimu mmoja alimuamuru Rais mstaafu Francisco Flores ashtakiwe kwa tuhuma za kuziingiza katika akaunti yake binafsi na akaunti ya chama chake dola za Marekani milioni 15 wakati alipokuwa Rais baina ya 1999 na 2004. Fedha hizo zilizokuwa zimechangwa zilikusudiwa waathirika kwa zilzala iliyotokea nchini humo.

Halafu kuna RaisOtto Pérez Molina wa Guatemala aliyechaguliwa Rais 2012 na aliyelazimika kujiuzulu urais Septemba mwaka jana baada ya kukabiliwa na mashtaka ya ufisadi. Molina hivi sasa yuko jela pamoja na aliyekuwa makamu wake. Wote wawili wanakabiliwa na mashtaka ya ulaji rushwa.

Yaliyomkuta Molina ni mara ya mwanzo kumkuta Rais aliye madarakani tangu mfumo wa demokrasia ushamiri katika nchi za Amerika ya Kusini.

Na kuna ya Brazil ambako Rais mstaafu Luiz Inácio Lula da Silva ameshtakiwa wakati uchunguzi ukifanywa kuhusu shutuma za kashfa ya ufisadi zinazoikabili kampuni ya Petrobras, ambayo ni kampuni ya mafuta yenye kumilikiwa na serikali ya Brazil.

Shutuma hizo zinazomkabili Lula ni kitisho kwa mrithi wake Rais Dilma Rousseff ambaye anayumbayumba kisiasa kwa vile Bunge limo katika mchakato wa kumshtaki kwa kutumia vibaya madaraka. Lula anasema shtuma zote hizo ni njama za kisiasa zinazopikwa na maadui wao wa kisiasa.

Kote huko katika eneo la nchi za Amerika ya Kusini Marais siku hizi wanahaha. Wananchi wa huko wakitiwa nguvu na jumuiya za kiraia, zisizo za kiserikali, wamekuwa wakipiga kelele na kuzishinikiza serikali zichukuwe hatua dhidi ya ufisadi na dhidi ya wakubwa wao wenye kushutumiwa kwa mashtaka ya ufisadi.

Rais mstaafu wa Panama Ricardo Martinelli naye anakabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu wa fedha za umma, njama za kuwafanyia ujasusi mahasimu wake wa kisiasa na mashtaka mingine ya ufisadi. Kwa amekimbilia Florida, Marekani, lakini Mahakama Kuu ya Panama imetoa amri akamatwe na arudishwe kwao kupandishwa kizimb

Huku kwetu Kikwete anaweza akaponea chupuchupu. Kwa hali ilivyo, Katiba ndiyo imekuwa kinga yake wakati alipokuwa Rais na sasa baada ya kuuacha urais. Si Katiba peke yake lakini ana kinga nyingine — ule moyo wa kulindana walio nao watawala wetu.

Kwa hivyo, hata kama patakuweko na kipengele cha sheria au mwanya wa kisheria utaoweza kumfanya ashtakiwe kutakuwako na huo moyo wa wakubwa kulindana ambao huenda ukakoroga mambo. Wakubwa wanaweza kufanya hivyo kwa sababu hawaitii maanani demokrasia na wamezoea kuubeza mfumo huo.

Kutokana na hayo ni kheri tuwe na demokrasia ya kibwanyenye kushinda kukosekana demokrasia ya yo yote. Angalau katika mfumo huu wa demokrasia ya kiini macho viongozi wanaweza wakawajibishwa kwa ufisadi wao.