 |
| Maalim Seif Sahrif Hamad (wa nne kulia) akiwa katika moja ya vikao pamoja na Mwalimu Nyerere mwaka 1984. |
Na Ahmed Rajab.
KAMA ilivyo kwa Julius Kambarage
Nyerere ndivyo ilivyo kwa Seif Sharif Hamad. Wote ni maarufu kimataifa kwa jina
moja tu. Mmoja Mwalimu, mwengine Maalim.Majina mawili yenye maana moja. Majina
hayo hutamkwa tofauti kutegemea mtu yuko wapi na amekulia katika mazingira
gani.
Wote wawili, Mwalimu na Maalim,walikuwa na kazi ya ualimu kabla hawajawa
wanasiasa waliobobea.
Nilianza kumjuwa Maalim kabla hajawa mwalimu tulipokuwa wanafunzi katika skuli
ya King George VI Memorial Grammar Secondary School, (siku hizi Skuli ya
Sekondari ya Lumumba) iliyoko Saateni, Unguja.Alikuwa mbele yangu kwa miaka
miwili.
Hakuwa mzungumzaji sana. Kwa hakika, hakuwa akichanganyika sana na wanafunzi
wengine. Miaka hiyo nikimuona tu skuli, akiwa mmoja wa wanafunzi kutoka Pemba
waliokuwa wakiishi katika bweni ya Beit el Ras, nje kidogo ya mji.Wakiletwa
skuli kila asubuhi na kurejeshwa mchana kwa magari ya bweni.
Seif wa siku hizo alikuwa mrefu, mwembamba, aliyepinda kidogo na aliyekuwa
akivaa sare ya skuli, shati jeupe na suruali ya khaki.
Mara nyingine akija skuli akiwa amepiga kanzu na kofia. Mwalimu Mkuu wa
skuli,G.G.Davies, akiruhusu kanzu na kofia kuwa ni sare mbadala.
Nadhani sikio moja la Seif likimpa taabu kwani alikuwa heshi kutia pamba
sikioni. Jengine ninalolikumbuka ni kwamba alikuwa akitafakari sana.
Daima uso wake ulikuwa chini akiwa mwenye mawazo. Akifikiri nini? Sijui. Na
alikuwa na macho, ambayo Waingereza wangeliyaita “meditative eyes”, yaani macho
ya tafakuri au ya mazingatio.
Waliosoma naye darasa moja wanasema Seif hakuwa mtu wa maneno mengi, wa mizaha
isiyo na maana. Alikuwa mtulivu, mpole na mkimya. Wanasema ilikuwa taabu
kuzijuwa fikira zake kwa vile alikuwa si mbobokaji.
Akipendelea kuchunguza mambo tu na kuwasikiliza wengine kwa makini. Hata katika
mijadala ya skuli alikuwa si mtetezi ingawa alikuwa hakosi kuhudhuria mijadala
hiyo.
Seif alionyesha mapema dalili za uongozi. Alipokuwa darasa la kumi alikuwa
kepteni wa bweni lao akiwasimamia hata wakubwa zake kwa umri.
Kwenye bweni lao akijulikana kwa kupenda kusoma. Baada ya saa nne za usiku
jenereta lilipokuwa linazimwa, Seif alikuwa akiwasha taa ya kandili au karabai
na akiendelea kusoma. Nadhani hiyo ndiyo sababu iliyomfanya baadhi ya wakati
aonekane kama mtu aliyekosa usingizi.
Alipoingia Kidato cha Tano alikuwa ama kiranja au naibu wa kiranja wa skuli.
Tangu enzi hizo vijana wa Kipemba walikuwa wakinung’unika kwa namna kisiwa chao
kilivyokuwa kikionewa na watawala licha ya kwamba Zanzibari kipata sehemu kubwa
ya mapato yake kutoka mauzo ya karafuu za Pemba na, kwa hivyo, kisiwa cha
Unguja kikinufaika zaidi.
Kulikuwa na jengine lililokuwa likiwaudhi: sisi wa Unguja tukipenda kuwafanyia
stihizai.
Tukiwatumbukiza katika kapu moja na tukiwafanyia tashititi na kuwacheka, kwa
mfano, kwa lafudhi zao au kwamba eti wakipenda sana vitu vitamu kiasi cha
kuwafanya wawe wanakula haluwa kwa chai ya maziwa.
Nadhani idhilali hizo ndizo zilizozidi kuwafanya wawe kitu kimoja na
zilizowafanya waamue kuwa na chama chao cha wanafunzi wazawa wa Pemba.
Badala ya kujiunga na All Zanzibar Students’ Union (AZSU), chama cha wanafunzi
wa Zanzibar nzima, wao waliunda chama walichokiita rasmi Pemba Students’
Union(PSU, Chama cha Wanafunzi wa Pemba). Wengine wakikiita Pemba-Born
Students’ Union, yaani Chama cha Wanafunzi Waliozaliwa Pemba.
Chama cha PSU kilikuwa na kamati ya watu watano na Seif ndiye aliyekuwa
kiongozi wao.
Wanafunzi hao wa Kipemba wakishikamana bila ya kujali vyama vyao vya siasa.Seif
alikuwa mfuasi waAfro-Shirazi Party (ASP).Mwanafunzi mwengine wa Kipemba, Enosh
Timothy Bilal, niliyekuwa nikikaa naye deski moja skuli na aliyekuwa akiishi
Beit el Ras,naye pia alikuwa mfuasi mkubwa wa ASP.
Nakumbuka kuna wakati vijana hawa kutoka Pemba walianzisha vuguvugu lao lisilo
rasmi waliloliita “Pemba Yekka”. Waliliigiza jina la chama cha Kabaka Yekka cha
Uganda, chama ambacho kilikuwa kikimuunga mkono Kabaka Mutesa, mfalme wa
Wabaganda.
Kwa lugha ya Kiganda “yekka” maana yake ni “tu”, kwa hivyo “Kabaka Yekka”
ilikuwa na maana ya “Kabaka Tu”.
Wabaganda wakiyatumia matamshi hayo kusalimiana. Mmoja akisema “Kabaka”,
mwengine akiitika “Yekka” na halafu kila mmojawao akionyesha juu kidole chake
cha shahada.
Wafuasi waPemba Yekka hawakuwa wakisalimiana kwa kaulimbiu hiyo iliyokuwa na
maana ya “Pemba Tu”.
Nilipoondoka Zanzibar 1964 kwenda Uingereza kwa masomo, Seif alikuwa
ameshahitimu Kidato cha Sita na alilazimishwa kusomesha skuli za sekondari.
Kwanza aliajiriwa Lumumba alikosomesha Kiingereza, Fasihi na Historia.
Nasikia Maalim Seif alikuwa mwalimu mzuri. Aliendelea kusomesha hadi 1972, pale
serikali ya Rais Aboud Jumbe ilipompatia nafasi ya kuingia Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam alikohitimu na kutunukiwa shahada ya B.A.(Hons) miaka mitatu baadaye.
Tangu 1964 sikumshuhudia tena Seif hadi mwezi wa mfungo wa Ramadhani katika
miaka ya kati ya 1970 nilipokutana naye Mombasa. Ilisadifu kwamba akija
kufuturu Mji wa Kale katika nyumba niliyoshukia ya Maalim Saleh Abdallah
Jahadhmy “mwandani”, mwalimu wetu wa zamani aliyekuwa na asili ya Lamu.
Tulikuwa tukifuturu watu wanne; mwengine akiwa kijana wa Kikenya. Wakati wa
futari, Maalim Jahadhmy alikuwa akiulizauliza habari za siasa. Wakati wote,kama
kawaida yake, Seif alikuwa akisikiliza tu. Hakujifanya mjuaji ingawa nina
hakika akiyajuwa mengi.Mimi ndiye niliyejidai kujuwa na nikimjibu Jahadhmy.
Maalim aliweza kuchupa na kutua kwenye medani ya siasa za kitaifa alipoteuliwa
na Jumbe awe waziri wa elimu wa Zanzibar 1977.
Jumbe, mwalimu wetu wa zamani katika skuli ya King George, akimpenda Maalim na
alimsaidia kwa kumpa fursa ya kusoma masomo ya juu na kwa kumuingiza katika
siasa za kitaifa. Unaweza kusema kwamba ndiye aliyemjenga.
Mwalimu Nyerere, ambaye mwanzoni akimpenda Maalim, akijigamba kwamba ni yeye
aliyemjenga.
Niliwahi kuandika katika ukurasa huu nilipomkuta Mwalimu akibugia njugu na bia
chumbani kwake katika hoteli ya Intercontinental jijini Nairobi kabla ya Chama
cha Mapinduzi (CCM) kumpata mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa 1995.
Mwalimu aliniuliza watu wakisemaje kuhusu mchuano huo.
Nikamjibu: “Wanasema una mtu wako.”
“Nani?”
“Salim (Salim Ahmed Salim)”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu mtoto wako.”
Kumwambia hivyo aliruka na akanambia kwa mkazo: “Lakini wote watoto wangu.
Kwani hata Seif, nani unadhani kamjenga?”
Nikamwambia: “Wewe” kwa sababu nikijuwa kwamba ndivyo alivyotaka nimwambie.
“Tena!” Mwalimu alisema kwa hamasa na kana kwamba akijipongeza akiwa anapiga
soga barazani na vijana wa mjini.
Ilikuwa wazi alipoyasema hayo kwamba aliona fahari kubwa kujihusisha na Maalim
kwani aliutambua uwezo wake, kipaji chake na utendajikazi wake.
Ndio maana alimkabidhi nyadhifa kubwa kubwa ndani ya CCM. Hata wakati wa
sokomoko la kisiasa Zanzibar katika enzi ya Rais mstaafu Salmin Amour, Nyerere
aliwahi kutamka kwamba ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar lazima umhusishe Maalim.
Na kuna ule mkutano wa siri Butiama ambao mpaka leo hatujui kilipita nini baina
ya Maalim na Mwalimu.
Tunachokijuwa ni kwamba Maalim hakuzuzuka kwa kupendwa na Mwalimu. Alithubutu
kusimama imara akitetea msimamo wake kuhusu Zanzibar, hatua ambayo ilisababisha
akamatwe na kuwekwa ndani gerezani.
Katika ushirikiano wa Maalim na Mwalimu kuna kadhia moja iliyomtia doa Maalim,
doa litalomganda maisha. Hii ni kadhia ya jinsi Mwalimu na CCM walivyompindua
Jumbe.
Kuna wanaomtuhumu Maalim kwamba alimwendea kinyume Jumbe na kumfanyia hiyana.
Juu ya hayo, tusisahau tu kwamba historia ina mifano mingi ya watu waliowahini
wenzao kwa malengo adhimu.
Maalim amejaribu sana kujitetea lakini utetezi wake bado haukuwaridhisha
wanaomtuhumu.
Kwa upande mwingine, msimamo wa Maalim kuhusu suala la usawa wa Tanganyika na
Zanzibar ulimfanya awe mwiba uliokuwa ukimchoma Mwalimu. Aliushikilia msimamo
huo hata alipokuwa waziri kiongozi wa Zanzibar (1984-1988). Mwishowe Mwalimu
alibidi ampikie jungu la kumfukuzisha kutoka CCM.
Moja ya sababu zilizomfukuzisha Maalim kutoka CCM ni idadi ndogo sana ya kura
alizopata Rais Idrissa Abdul Wakil huko Pemba katika uchaguzi wa chama kimoja
uliofanywa 1985.
Lawama ilimwangukia Maalim kuwa eti alimtilia fitna Abdul Wakil Pemba na ndio
maana huko aliondokea patupu.
Baada ya kufukuzwa CCM na kabla ya vyama vya siasa kuhalalishwa nchini 1992,
Maalim Seif alikuwa akiliongoza vuguvugu la KAMAHURU pamoja na akina Shaaban
Mloo, Maulidi Makame, Ali Haji Pandu na Hamad Rashid.
Kilikuwa kipindi kigumu kwake. Wakati huo katika miaka ya 1980 tayari
kulikuwako na vuguvugu la Wazanzibari nje ya nchi lililoasisiwakwenye mkutano
uliofanywa mjini Malmo, Sweden, chini ya uenyekiti wa Abdulrahman Babu,
aliyekuwa kiongozi wa chama cha zamani cha Umma Party.
Vuguvugu hilo likiitwa Harakati za Kuleta Mabadiliko ya Kidemokrasia (kwa ufupi
HAMAKI na kwa Kiingereza likiitwa Zanzibar Democratic Alternative).
Waliokuwa kwenye vuguvugu hilo walikuwa Wazanzibari wa itikadi tofauti za
kisiasa.Miongoni mwao alikuwa Dk. Yusuf Saleh Salim aliyekuwa na mahusiano
mazuri na viongozi wa KAMAHURU.
Alipokuwa akiongoza KAMAHURU ndipo ukomavu wa kisiasa wa Maalim ulipoanza
kudhihirika na dunia ilipoanza kutambua kwamba Zanzibar ina kiongozi wa kipaji
cha juu.
Naweza kusema kwamba miongoni mwa
magwiji wa kisiasa waliovutiwa naye alikuwa Babu.
Watu wawili hao walikuwa na itikadi tofauti lakini kwa maslahi ya Zanzibar
fikira zao zilioana.
Ninayajuwa hayo kwa sababu mimi
ndiye niliyewakutanisha ana kwa ana kwa mara ya kwanza.
Ilikuwa 1988 nilipowaalika kwa chakula cha usiku nyumbani kwangu, siku hizo
nikiwa katika mtaa wa Stoke Newington, London.
Babu baadaye alijiunga na NCCR-Mageuzi lakini akitambua kwamba kiongozi
atayeweza kuleta mageuzi ya kimaendeleo Zanzibar ni Maalim. Alikuwa na sababu
zilizomfanya ajiunge na NCCR-Mageuzi lakini hazikuwa za kutokuwa na imani na
Maalim.
Maalim Seif hajakamilika na wala hawezi kukamilika kwani ni mwanadamu.Hata
hivyo,ninaamini ukiwachukuwa wanasiasa wote wa Zanzibar ya leo ukawaweka kwenye
mezani uwapime kwa vigezo vyote vya umahiri wa kisiasa, Maalimatawapiku
wenzake.
Yeye pamoja na Rais Mstaafu Dk. Amani Karume ni viongozi wenye sifa tofauti,
kwa mfano, na zile walizokuwa nazoakina Sheikh Ali Muhsin Barwani (aliyekuwa
kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party au Hizbu) na Sheikh Abeid Amani Karume
(aliyekuwa kiongozi wa ASP). Hao walikuwa viongozi wa kihistoria.
Watu wengi husahau kwamba kwa upande wa Sheikh Ali jambo la mwanzo alilolifanya
baada ya kuingia siasa ni kujiuzulu kutoka Jumuiya ya Waarabu akiuweka mbele
Uzanzibari wake.
Sheikh Karume, kwa upande wake, akionekana na wengi wa Wazanzibari waliokuwa
wakijifaharisha na “Uafrika” kuwa ni mkombozi wao.
Babu, niliyekuwa mimi nikimfuata, kidogo ananipa taabu. Ninaweza nikamuweka
katika shubaka la viongozi wa kihistoria lakini nadhani nitakuwa sahihi zaidi
nikimpachikakwenye shubaka la peke yakeakiwa mkunga wa historia.
Hawa viongozi wa leo, Maalim Seif na Dk. Karume, wamethibitisha kwamba wao ni
viongozi wenye ujasiri na bisara (vision) kubwa. Tunaweza kuyamithilisha
Maridhiano yao ya 2010 kuwa, kwa kiwango fulani, kama yale ya Afrika ya Kusini.
Amani Karume alikuwa kamaFW de Klerk kwa kuwa na ujasiri wa kuwashawishi
wenzake wafuate mkondo wa kihistoria baada ya kutanabahi kwamba Zanzibar
imekuwa ikielekea pabaya na watu wake wamechoka na uhasama.
Maalim, kiongozi aliyekuwa upande wa haki na aliyedhulumiwa, amekuwa kama
Nelson Mandela.Kwa bahati mbaya, Maalim hadi leobado anadhulumiwa. Ni dalili ya
ujasiri wake kuwa ameweza kuwafanya wafuasi wake wawe watulivu na wayakubali
Maridhiano.
Wa mwanzo kumbandika Maalim sifa ya “Umandela” walikuwa wafungwa aliowakuta
gerezani Unguja alipokuwa katiwa ndani kuanzia Mei 11, 1989.Julai na Septemba 6
ya mwaka huo aliniandikia barua mbili akiwa jela akinieleza maisha yake
yalivyokuwa huko kifungoni.
Miezi sita baadaye aliniletea waraka alioandika wenye kurasa 32 akizichambua
siasa za kimataifa, za barani Afrika na za Tanzania.
CHANZO: RAIA MWEMA.