 |
| Viongozi wa Chama cha Wananchi CUF wakizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi ya chama hicho Vuga mjini Zanzibar |
Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi CUF limeazimia kutokuitambua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dkt, Ali Mohammed Shein kwa kile walicho dai kuwa serikali hiyo haikupata ridhaa wa wananchi baada ya kufanyika Uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar.
Maazimio hayo yametangazwa leo na Mwenyekiti wa kamati ya Uongozi ya Chama hicho Bw, Twaha Taslima wakati akizungumza na waandishi wa Habari ofisi ya CUF iliyopo Vuga mjini Unguja.
MAAZIMIO YA CUF HAYA HAPA
MAAZIMIO YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA CHAMA KATIKA KIKAO
CHAKE CHA TAREHE 2 – 3 APRILI, 2016 KILICHOFANYIKA MAZSONS HOTEL, MJINI
ZANZIBAR
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama Cha Wananchi)
limefanya kikao chake cha kawaida kwa siku
mbili, tarehe 2 hadi 3 Aprili, 2016 mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi ya Chama, Mheshimiwa Twaha Taslima.
Ajenda
kuu ya kikao hicho ilikuwa ni Hali ya Kisiasa Zanzibar na mwelekeo wa
CUF baada ya kufanyika kile kilichoitwa uchaguzi wa marudio wa tarehe 20
Machi, 2016.
Baada ya kupokea na kujadili kwa kina ajenda hiyo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:
1. Linawapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa ujasiri, uzalendo na ari
kubwa walioionesha kwa kuitikia kwa kiasi kikubwa wito wa chama chao
cha CUF wa kuwataka wasishiriki katika uhuni na ubakaji wa demokrasia
uliopewa jina la uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016. Baraza
Kuu la Uongozi limefurahishwa kuona zaidi ya asilimia 80 ya wapiga kura
wa Zanzibar hawakujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo haramu na
batili, na hivyo kuudhihirishia ulimwengu kwamba Chama Cha Mapinduzi
(CCM) hakina ridhaa ya wapiga kura hao.
2. Linawapongeza
waliokuwa wagombea wa CUF kwa nafasi zote za Urais, Uwakilishi na
Udiwani kwa kuheshimu maamuzi ya Chama na kutoshiriki uchaguzi haramu na
batili wa marudio licha ya njama nyingi zilizokuwa zikifanywa na Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, za
kulazimisha ushiriki wao. Msimamo wa wagombea hao umewadhihirishia na
kuwathibitishia CCM kwamba tofauti na wao, viongozi wa CUF hawajali
nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka ni kuleta mabadiliko ya kweli
kwa maslahi ya watu wote wa Zanzibar.
3. Linawapongeza kwa namna
ya pekee wagombea Urais, Uwakilishi na Udiwani wa vyama vyengine vya
upinzani ambavyo ni UMD, JAHAZI ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP, na
ACT-WAZALENDO, na vile vinavyoshirikiana kupitia UKAWA ambavyo ni
CHADEMA, NCCR na NLD vilivyoungana na wananchi wa Zanzibar kususia
uchaguzi haramu na batili wa marudio na kusimamia maamuzi halali ya
wapiga kura waliyoyafanya kupitia uchaguzi mkuu halali wa tarehe 25
Oktoba, 2015.
4. Linazishukuru na kuzipongeza jumuiya na taasisi
zote za kitaifa na kimataifa pamoja na nchi rafiki za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambazo zilikataa kuleta waangalizi wa uchaguzi
katika uchaguzi huo haramu na batili na hivyo kuungana na Wazanzibari
katika kutetea maamuzi yao halali waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu
halali uliokuwa huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
5.
Linavishukuru na kuvipongeza vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi
pamoja na waandishi wa habari na wapiga picha kwa jinsi vilivyosaidia
kuonesha ulimwengu uchaguzi mkuu uliokuwa halali, huru na wa haki wa
tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia kwa jinsi vilivyoanika uchafuzi wa tarehe
20 Machi, 2016 hasa kule kuonesha vituo vya kupigia kura vikiwa havina
watu na hivyo kuwasaidia Watanzania na ulimwengu kuujua ukweli ambao
CCM na Tume yao ya Uchaguzi walikuwa wakijaribu kuuficha.
6.
Linalaani tabia na mwenendo wa uongo, uzushi, na uvunjwaji wa Katiba,
Sheria na Maadili wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha
Salim Jecha, dhidi ya matakwa na maamuzi halali ya Wazanzibari
waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba,
2015 na kitendo chake cha kuiingiza Zanzibar katika dimbwi la chuki,
uhasama, uvunjifu wa haki za binadamu na udhalilishaji wa raia kwa
sababu tu ya kukiridhisha chama chake cha CCM ambacho kimekataliwa na
Wazanzibari. Vitendo vya Jecha Salim Jecha vimeishushia hadhi Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar na kuichafulia jina Zanzibar na Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania mbele ya jumuiya ya kimataifa na kuonekana haiko tofauti na
nchi nyengine za Afrika zisizoheshimu matakwa na maamuzi ya wananchi
katika uchaguzi.
7. Linalaani hatua ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli kuleta nguvu kubwa ya
vikosi vya ulinzi na usalama kuja kubaka demokrasia Zanzibar. Baraza
Kuu linalaani vikali nguvu kubwa iliyotumiwa na vyombo vya dola dhidi ya
raia wasio na hatia kwa lengo na madhumuni ya kuwatisha na kuwazuia
wasitumie haki zao za msingi kama ibada kwa kuwalazimisha kutotoka nje
ya nyumba zao kuanzia saa 2 usiku wakati muda huo ni muda wa ibada ya
sala kwa Waislamu ambao ni asilimia 99 ya wananchi wote wa Zanzibar.
Baraza Kuu pia linalaani mwenendo wa viongozi wa juu wa vyombo vya
ulinzi na usalama wa kutumika waziwazi kisiasa kwa kuegemea upande wa
CCM na kuwakandimiza viongozi na wanachama wa CUF kinyume na maadili ya
kazi zao.
8. Linalaani vitendo vya Serikali kuunda makundi ya
kiharamia ambayo yamekuwa yakiwahujumu raia wasio na hatia yakitumia
silaha za moto na silaha za kienyeji huku yakitumia gari za Idara Maalum
za SMZ. Baraza Kuu linalaani Jeshi la Polisi ambalo limekuwa
likiyalinda makundi haya na kutochukua hatua zozote dhidi yao licha ya
wananchi wanaohujumiwa kutoa taarifa kwa jeshi hilo. Badala yake, katika
matukio mengi Polisi imewageuzia kibao wananchi waliohujumiwa kwa
kuwakamata na kuwaweka ndani. Baraza Kuu linawataka Wakuu wa Jeshi la
Polisi kujirudi, kutekeleza majukumu yao ya kulinda usalama wa raia na
mali zao na na kufuata maadili yao na kuwacha kujifanya ni Idara ya
Polisi ya CCM.
9. Haliyatambui matokeo ya uchaguzi huo haramu na
batili, na kwa msingi huo halimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa
Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa kuwa Wawakilishi na wala
haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani. Baraza Kuu linaungana na
wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu hao na kwa hivyo
halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zitakazoundwa
na watu hao. CUF haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni
kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na
haikutokana na ridhaa ya watu. Kwa vyovyote vile, Serikali itakayoundwa
haitakidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki
kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo inaeleza kwa uwazi kabisa namna ya
kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
10. Linawataka
wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na
kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa
watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa
kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali
itakayoundwa na watawala hao.
11. Linaendelea kuutambua uchaguzi
mkuu uliokuwa halali, huru, wa haki na uliofanyika katika hali ya amani
na utulivu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia linayatambua matokeo yake
ambayo yalionesha wazi kwamba chaguo la Wazanzibari ni CUF na Maalim
Seif Sharif Hamad kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Kitendo cha zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari kususia uchaguzi haramu
na batili wa tarehe 20 Machi, 2016 kimezidi kuyapa nguvu maamuzi yao ya
tarehe 25 Oktoba, 2015 mbele ya macho ya Watanzania na dunia.
12.
Linaendelea kuwataka Wazanzibari kuwa watulivu na kulinda amani iliyopo
na linawahakikishia kwamba CUF inaendelea na juhudi zake za kutafuta
haki yao na kusimamia maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015
kwa njia za amani na za kidemokrasia. Njia hizo za amani zimefanikiwa na
kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa ambayo imeanza kuchukua hatua
dhidi ya ubakwaji wa demokrasia uliofanyika.
13. Linazishukuru na
kuzipongeza nchi washirika wa maendeleo kwa kuchukua maamuzi ya
kuzifutia misaada Serikali za kidikteta za CCM ambazo zimebaka
demokrasia na kukanyaga haki za wananchi wa Zanzibar. Baraza Kuu linatoa
wito kwa nchi hizo washirika wa maendeleo na jumuiya za kimataifa
kuchukua hatua zaidi dhidi ya Serikali za CCM na madikteta wake
walioshiriki katika ubakaji wa demokrasia Zanzibar zikiwemo hatua
makhsusi dhidi ya watu makhsusi waliohusika na ubakaji huo wa demokrasia
na uvunjaji wa haki za binadamu katika kipindi hiki.
MWISHO,
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawahakikishia wanachama wake wote na
Watanzania kwa ujumla kwamba chama chao kiko imara na hakitoyumba wala
kuyumbishwa katika kutetea na kupigania haki zao hadi tutakapofanikisha
ujenzi wa taifa imara linalosimamia na kuheshimu utawala wa sheria, haki
za binadamu, demokrasia na utu wa watu wote.
Baraza Kuu
linawataka viongozi wa Chama wa ngazi zote watekeleze majukumu yao ya
kichama katika nafasi zao na pia Wabunge na Wawakilishi waliopewa ridhaa
na Wazanzibari tarehe 25 Oktoba, 2015 kuwatumikia wananchi wote katika
kutatua matatizo yao kadiri hali na uwezo wao unavyoruhusu. Mbali na
maazimio haya, Maalim Seif Sharif Hamad atazungumza na wananchi katika
siku chache zijazo ili kuwaeleza kwa kina mwelekeo wa hali ya kisiasa ya
Zanzibar na hatua zinazochukuliwa na CUF kuhakikisha maamuzi halali ya
kidemokrasia ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015
yanaheshimiwa.
HAKI SAWA KWA WOTE
Limetolewa na:
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITEDN FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)
ZANZIBAR
3 APRILI, 2016