Thursday, 25 August 2016

Jinsi Jumbe na Nyerere walivyopigana mwereka

Sheikh Aboud Jumbe, Rais wa zamani wa Zanzibar
Na Ahmed Rajab
AGOSTI 15 mwaka huu, siku alozikwa Sheikh Aboud Jumbe kuna rafiki yangu mmoja alinikumbusha makala niliyowahi kuyaandika katika jarida lichapishwalo London la New African wakati Jumbe alipokuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania.

Miongoni mwa mengi makala hayo yalizungumzia upinzani aliokuwa akiukabili Jumbe.

Wakati huo, kuta za Mji Mkongwe, Unguja, hasa zile za marikiti ya Darajani, ziligeuka na kuwa kama kuta za Beijing, China, wakati wa Mapinduzi ya Utamaduni, ambayo wenyewe Wachina wakiyaita “Wenhua Dageming” (1966-1976) yaliyoanzishwa na Mwenyekiti Mao aliyekuwa akiliongoza taifa hilo la Kikomunisti.

Wafuasi wa Mapinduzi ya Utamaduni walikuwa wakizitumia kuta kuandikia au kubandika mabango yenye maneno yao ya propaganda ama ya kumuunga mkono Mao au ya kuwashambulia mahasimu wake au nadharia zao.  Kwenye kuta, na pia kwenye mabango, ndipo zilipopatikana habari za kuaminika kuhusu yaliyokuwa yakijiri China.

Wachina walikuwa wakizitegemea sana kuta na mabango, kushinda magazeti rasmi,  kwa habari muhimu. Waliokuwa wakiandika kwenye kuta na mabango hayo wakiandika kwa rangi nyekundu, nyeupe na nyeusi. Ilikuwa ni kampeni kubwa iliyowahamasisha wananchi na ikijulikana nje ya China kama “wall poster campaign” (kampeni ya mabango ya ukutani).

Mtindo huo wa kupeleka ujumbe katika jamii kwa kutumia kuta uliigwa na wanaharakati wa Zanzibar nchi hiyo ilipokuwa chini ya utawala wa Jumbe.Tofauti iliyokuwako kati ya kampeni hizo mbili ni kwamba ile ya China ikiongozwa na kuhamasishwa na kiongozi mkuu kabisa nchini humo; ile ya Zanzibar ikimlenga kiongozi aliyekuwa na madaraka kama hayo katika visiwa hivyo.

Tofauti ya pili ni kwamba ile ya China, kwa vile ilipata idhini ya Mao, ikifanywa kwa uwazi, dhahir shahir, lakini ya Zanzibar kwa vile ilikuwa ni yenye kuasi ikifanywa kwa kificho na kwa siri kubwa.

Watu walikuwa wakiamka asubuhi na wakishtukia kuta zimechorwa vibonzo au zimeandikwa maneno yenye kumpinga Jumbe. Kampeni nzima dhidi ya Jumbe ilikuwa na ujumbe mmoja tu: kutetea mfumo wa kidemokrasia.

Tofauti ya tatu ni kwamba kampeni ya China iliendeshwa na umati wa watu lakini ile ya Zanzibar ikifanywa na watu wachache sana. Walikuwa katika vuguvugu dogo lisilokuwa na jina lakini lililokuwa na athari ya aina yake ya kuleta mwamko wa kisiasa, angalau katika eneo la Mji Mkongwe.

Safari moja nikiwa na hamsini zangu karibu na ilipo ofisi ya waziri kiongozi nilishtukia kijana mmoja akinigusa bega na kuniambia kwamba ni yeye niliyearifiwa kuwa atanitafuta kunielezea harakati zao za upinzani wa kwenye kuta. Ilikuwa mara yangu ya mwanzo kukutana naye. Alinitaka nimfuate nikaonane na mwenzake.

Nilishangaa nilipomuona mwenzake aliyekuwa mkubwa wake kwa umri na kumtambua kwamba ni mtu tuliyesoma pamoja katika skuli ya msingi. Wawili hao walianza usuhuba wao wa kisiasa walipokuwa wamefungwa jela kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Sheikh Abeid Amani Karume Aprili 7, 1972.
Yule kijana hivi sasa ni marehemu na mwenzake, mkubwa wake siku hizi ameguria Bara wala hapiti Unguja.

Upinzani wao dhidi ya utawala wa Jumbe ukiihangaisha sana serikali na hasa idara ya Usalama. Baada ya kuta kuandikwa matamshi ya kuipinga serikali na kuchorwa wajihi wa Jumbe kwenye vibanzo kazi ilikuwa ni ya polisi kuingia mitaani asubuhi na kufuta yaliyokuwa kwenye kuta.

Siku hizi harakati kama hizo kwingi duniani huendeshwa katika “kuta” za Facebook na kwenye mitandao mingine ya kijamii.

Upinzani mkali zaidi aliukabili Jumbe kutoka kwa bosi wake serikalini- Rais Julius Nyerere, ambaye baadaye alikuwa pia bosi wake chamani baada ya kuunganishwa vyama vyao, Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) cha Zanzibar na kuundwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Uhasama wa Nyerere dhidi ya Jumbe ulianza siku nyingi chini kwa chini. Kama nilivyogusia katika makala yangu ya wiki iliyopita Jumbe hakuwa mgeni kwa Nyerere wala Nyerere hakuwa mgeni kwa Jumbe. Viongozi hao wakijuana tangu walipokuwa wanafunzi katika Chuo cha Makerere, Uganda (1943-1945).

Alipouawa Karume, Nyerere alikuwa na jambo moja lililokuwa likimla roho na ambalo akitaka kulitafutia dawa kwa haraka. Lilikuwa nani atayemrithi Karume katika kiti cha urais wa Zanzibar na kuwa msaidizi wake mkuu katika serikali ya Muungano?
Kwa muda wa kama saa 48 baada ya kuuawa Karume, mtu aliyeonekana akiidhibiti nchi alikuwa Kanali Ali Mahfoudh. Yeye ndiye aliyeandika tangazo alilolisoma Jumbe katika redio ya serikali akiamrisha kufungwa kwa anga ya Zanzibar na kuchukuliwa hatua nyingine za ulinzi.

Wakati mmoja aliwakusanya wajumbe wote wa Baraza la Mapinduzi katika chumba kimoja kwa mkutano. “Ningelitaka ningeweza kuwapiga risasi wote,” Ali Mahfoudh aliwahi kuniambia zaidi ya mara moja miaka kadhaa baadaye.

Nikipenda kumchokoza kwa kumwambia kwamba alikuwa na madaraka kwa muda wa saa 48 na akaacha yakamponyoka. Mara zote akinijibu, tena kwa ukali, kwamba yeye hakuwa na nia ya kunyakua madaraka. Suala hilo halijamjia akilini hata chembe ya sekunde.

Mahfoudh alikuwa mtiifu wa Mapinduzi ya Zanzibar na akimuona Karume kama baba yake. Na yeye ndiye aliyeandaa mkakati wa nani akamatwe kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Karume, wengi wao wakiwa makomred wenzake, wafuasi wa zamani wa chama cha Umma Party.

Ingawa Mahfoudh alikuwa na uwezo wa kijeshi hakuwa na nguvu za kisiasa na asingeliweza asilan kuhodhi madaraka ya kisiasa. Nguvu hizo zilikuwa katika Baraza la Mapinduzi, na zaidi miongoni mwa wale waliokuwemo katika ile iliyojulikana kama “Kamati ya watu 14”, ambao ndio walioyaandaa Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Hapakuwepo hata mmoja miongoni mwa hao watu 14 ambaye Nyerere angeweza kuamini afanye naye kazi kwa ukaribu. Akiwadharau na wakati huo huo akiwaogopa wote 14. Bahati yake alikuwemo Jumbe katika Baraza la Mapinduzi na pia serikalini akiwa waziri aliyekuwa akishughulikia mambo ya Muungano pamoja na kuwa waziri wa afya.

Tathmini ya mwanzo ya Nyerere kuhusu Jumbe ni kwamba angalau alikuwa msomi kama yeye na wangeweza kuelewana. Bahati nyingine aliyokuwa nayo Nyerere ni kwamba alikuwepo pia Sheikh Thabit Kombo, Katibu Mkuu wa ASP, chama kilichokuwa kikitawala Zanzibar. Nyerere akionyesha kumuheshimu Kombo. Kwa upande wake Kombo, kinyume cha Karume, alikuwa siku zote akimsikiliza Nyerere.

Kutokana na yote hayo, Nyerere hakupata taabu alipomtaka Kombo amuunge mkono baada ya kupiga hesabu zake nakuona kuwa la kufanywa ni Jumbe kumrithi Karume. Nyerere, akisaidiwa na Kombo, alifanya aliyoyafanya na akaweza kuwaziba midomo wale ambao wangeweza kumkalia Jumbe vibaya.

Kwa upande waJumbe, urais ulikuwa zawadi asiyoifikiria seuze kuitarajia. Bahati yake kwamba alikuwako Nyerere kama ilivyokuwa bahati ya Nyerere kwamba alikuwako Jumbe. Wawili hao wakisikilizana zaidi ya Nyerere alivyokuwa akisikilizana na Karume katika miaka ya mwisho ya uhai wa Karume.

Pamoja na yote hayo, Jumbe alipiga mbali. Aliamini kuwa urais wa Zanzibar utamfikisha kwenye urais wa Tanzania. Niligusia wiki iliyopita jinsi Jumbe alivyoanza kubadilika alipokuwa Rais. Akionekana kama hayupo, kama mtu aliyejaa mawazo, aliyekuwa mbali na kila mara akikunja uso.

Alibadili hata namna ya alivyokuwa akizungumza; aliacha kuzungumza kwa lafudhi ya Kiunguja, akaanza kuzungumza kwa lafudhi ya Kibara. Kuna walioitafsiri tabia hiyo kuwa ni jaribio lake la kutaka kujipendekeza Bara akijiandaa kwa uongozi wa taifa zima. Mara nyingine akionekana kama mtu aliyekuwa akiigiza, kama mwigizaji katika tamthilia ya kisiasa.

Kwa hakika, na hili nilikwishaligusia wiki iliyopita, Jumbe ananipa taabu kumchora kwa maandishi. Kuyasimulia maisha ya mtu kunahitaji fani ya aina yake.
Na mtu aliyekuwa na maisha yaliyojaa mengi kama ya Jumbe humkang’anya mwandishi. Alikuwa mwanasiasa ambaye si rahisi kumpachika katika shubaka moja maalum kwa sababu anaweza kuingia kwingi.

Moja ya mambo yanayomfanya mtu ajulikane kuwa huyu ni fulani bin fulani au binti fulani ni mkusanyiko wa tabia zake. Za Jumbe zilikuwa nyingi mno na nyingi zikikinzana. Kwa mfano alikuwa karimu kama tulivyoshuhudia alipoamua kuipelekea Pakistan msaada wa fedha nchi hiyo ilipopata maafa ya zilzala, nikikumbuka vizuri. Lakini pia mtu huyo huyo alikuwa na uchoyo fulani.

Kadhalika, ingawa alikuwa msomi lakini hakuwa na tabia ya kusoma magazeti jambo ambalo likimkera Nyerere. Rafiki yangu mmoja aliwahi kunieleza jinsi Nyerere alivyomlalamikia kwa kusema: “Makamu wangu hata gazeti hasomi.”

Ijapokuwa alitamani awe Rais wa Tanzania, hata hivyo mwishoni mwa maisha yake ya kisiasa akisema kwamba Zanzibar ilighilibiwa kuukubali Muungano wa serikali mbili. Hapo ndipo alipouvaa uzalendo wa Kizanzibari na akajaribu kuirejeshea nchi yake mamlaka yake kamili.

Jumbe, lakini, alishindwa kutekeleza azma yake kwa sababu ya watu wawili: mmoja mwenyewe na wa pili Nyerere.
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment