Rais wa pili wa Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi. |
KIFO cha Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea adhuhuri yaJumapili iliyopita kiliufunga, bila ya kishindo, mlango mmoja muhimu wa historia ya karibuni ya Zanzibar. Mauti yalipomkuta, Jumbe alikuwa na umri wa miaka 96.
Tanzania, na hususani Zanzibar, imeondokewa na mtu aliyekuwa mwingi na aliyekuwa na mengi. Aboud Jumbe Mwinyi alizaliwa mtaa wa Mkamasini, Ng’ambo, Unguja Juni 14, 1920.
Kama ilivyo kawaida ya watoto wa Kizanzibari, elimu yake ya kwanza ilikuwa ni ya mafunzo ya dini alipotiwa chuoni (madrasa) kusoma Qur’an. Tangu ujana wake akisifika kwa namna alivyokuwa akiisoma suratil Fatiha (mlango wa kwanza wa Qur’an).
Wenye kuyajua mambo haya wanasema kwamba Jumbe akiisoma Al Fatiha kama Mtume Muhammad (SAW) alivyokuwa akiisoma kwa kuipa kila herufi haki yake.
Jumbe alisomea masomo ya msingi na ya sekondari huko huko Unguja. Pamoja na Sheikh Ali Muhsin Barwani, Jumbe alikuwa mmoja wa wanafunzi wa yule mwalimu mashuhuri Lawrence William Hollingsworth.
Huyu alikuwa Mwingereza aliyefundisha Zanzibar kwa miaka mingi sana. Baada ya kumaliza masomo ya sekondari katika Skuli ya Serikali Mnazimmoja (siku hizi Skuli ya Ben Bella), Jumbe alichaguliwa kwenda kusomea stashahada ya elimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, akibobea katika somo la biolojia.
Ali Muhsin alikuwa amekwishamtangulia Makerere lakini wote wawili walikutana huko na Julius Nyerere, mwanafunzi mwenzao kutoka Tanganyika. Kutoka 1943 hadi 1945 Jumbe na Nyerere walikuwa wanachama wa Jumuiya ya Mijadala (Debating Society).
Mwaka wao wa mwisho Makerere, Jumbe na Nyerere walikuwa wenyeviti wa mabweni ya wanafunzi; Jumbe alikuwa mwenyekiti wa Ssejongo na Nyerere wa Bamuja. Baadaye katika uhai wao, mmoja kati ya hao wawili atakuja kumzidi akili na kumpiku mwenzake.
Aboud Jumbe atakumbukwa kwa mambo mawili, ualimu na siasa. Hizo siasa ndizo zilizomfikisha hatimaye katika kilele cha uongozi akiwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar (1972-1984). Katika kipindi hichohicho alikuwa pia Makamu wa Rais wa Tanzania chini ya Nyerere.
Nyadhifa hizo zilimfanya awe maarufu nje ya mipaka ya Tanzania lakini kwao Zanzibar alipata umaarufu hata kabla hajazivaa siasa. Alirudi kutoka Makerere mwaka 1945 na tangu 1946 alikuwa akisomesha skuli ya serikali ya sekondari ambayo nilipoingia mimi kuanza masomo ya sekondari ilikuwa ikiitwa King George VI Grammar Secondary School (siku hizi inaitwa Lumumba School).
Miongoni mwa wanafunzi mashuhuri wa skuli hiyo waliosomeshwa na Jumbe ni mwanahistoria, Profesa Abdul Sherrif, waziri mkuu wa zamani Salim Ahmed Salim, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Seif Sharif Hamad, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Comoro, Salim Himidi na mawaziri wa zamani wa Zanzibar, Ali Salim Ahmed na Ali Juma Shamhuna.
Hawa wawili wa mwisho tulikuwa darasa moja na Maalim Aboud Jumbe ndiye aliyekuwa mwalimu wetu wa klasi tulipokuwa Form 1.
Ninamkumbuka mwalimu aliyekuwa mpole, mtaratibu asiye na ghasia wala vishindo. Hajawa mkali, mtu wa kuwakaripia watoto au wa vitisho.
Ninamkumbuka kwamba alikuwa mwalimu razini aliyekuwa akiwapenda wanafunzi wake wa kabila na tabaka zote. Jumbe pia alikuwa mkubwa wa maskauti na aliwavutia wanafunzi wengi wawe maskauti.
Zaidi ya yote ninamkumbuka maalim wetu kwamba alikuwa mtu wa bashasha, ingawa ukihisi kama ndani ya nafsi yake akionyesha kama mtu aliyekuwa na huzuni ya aina fulani. Labda akiyaona mengi katika jamii yaliyokuwa yakimkirihisha au kumuudhi.
Ama mimi binafsi, Maalim Aboud Jumbe alikuwa na mambo yake mawili yaliyokuwa yakinikera. Kwanza, alikuwa na tabia ya mara kwa mara kupotea asije skuli, hasa siku za Jumatatu.
Pili, na hili likiniudhi sana, alikuwa na tabia akiwa darasani ya kwenda kwenye ubao na kuandika, kwa hati zake nzuri, maelezo ya somo alilokuwa akisomesha.
Akimaliza akipenda kwenda nyuma ya darasa na kuyasoma aliyoyaandika halafu akijilaumu kuwa hakuandika vizuri na akirejea kwenye ubao na akiyafuta yote aliyokuwa ameyaandika. Akituudhi kwa sababu wengi wetu tulikuwa tumeshayaandika maelezo yake vitabuni mwetu. Ilibidi tuanze tena upya.
Jumbe hakuwa mwalimu wa somo moja. Alimudu kusomesha masomo mbalimbali. Akifundisha sayansi, biolojia (elimu viumbe), historia na Kiswahili, ambacho akikisarifu vizuri sana. Kwa hakika, alikuwa mwingi wa nahau (au sarufi) ya hii lugha yetu. Siku hizo sarufi ya Kiswahili ikifundishwa kwa kufuata mifumo au mitindo iliyoachwa na wazungu waliokuwa wataalamu wa lugha hiyo, akiwemo Bibi Ethel O. Ashton aliyetunga kitabu muhimu na kilicho maarufu kuhusu sarufi ya Kiswahili.
Zama zetu tulipokuwa tukiingia skuli za serikali za sekondari ilikuwa lazima tusome moja ya lugha tatu pamoja na Kiingereza tulichokuwa tukisomeshewa. Ilibidi tuchague ama Kiswahili, Kiarabu au Kigujerati (mojawapo ya lugha za Kihindi).
Kwa hiyo, kwa vile niliamua kusoma lugha ya Kiarabu sikubahatika kusomeshwa Kiswahili na Maalim Aboud Jumbe. Hata hivyo nilipata bahati kubwa ya kusomeshwa naye historia. Darasa zake, kwa mfano kuhusu “kudhoofika na kuanguka kwa Milki ya Kirumi”, siku zote zilikuwa zikisisimua na zikinifanya nihisi kama nilikuwa nikiishi katika enzi za Warumi.
Kadhalika nikipenda kumsikiliza alipokuwa akisimulia misafara ya wagunduzi wa Kireno kama kina Afonso de Albuquerque, Pedros Alvares Cabral na Vasco da Gama. Wagunduzi hao wa Kireno wana umuhimu mkubwa katika historia ya Afrika, ya Eshia na ya nchi za Amerika ya Kusini kwa sababu ndio waliowatangulia, au tuseme waliowafungulia njia wakoloni wa Kizungu waliokuja kuzipora nchi zetu na kutudhalilisha.
Tulikuwa na waalimu waliokuwa wakituamsha kisiasa walipokuwa wakitusomesha lakini sikumbuki kama Jumbe alikuwa mmojawao. Hayo si ajabu kwa sababu alikuwa mtu wa hadhari hasa kwa vile kwa mujibu wa sheria na kanuni za serikali ya kikoloni ya wakati huo waalimu hawakuruhusiwa kujiingiza katika mambo ya siasa.
Si kwamba hakutaka au hakujaribu. Inawezekana kwamba alipokuwa mwanafunzi Unguja katika skuli za msingi na sekondari akizizungumza siasa. Na inamkinika sana kwamba alianza kupata mwamko wa siasa za kijitu uzima alipokuwa Makerere akijadiliana na kina Nyerere.
Jumbe katika miaka ya mwanzo ya 1950 alikuwa mmoja wa waasisi wa Jumuiya moja ya Kitaifa huko Zanzibar (Zanzibar National Union), iliyokuwa kiini cha kunyanyua mwamko wa hisia za kizalendo, hasa uzalendo wa Kizanzibari.
Jumuiya hiyo, iliyoasisiwa na wasomi, iliwaunganisha Wazanzibari wa kila kabila. Mmojawao alikuwa Ahmed Lamki, aliyewahi kukamatwa nchini Misri alikokuwa akisoma wakati wa utawala wa Mfalme Farouk, baada ya kutuhumiwa kwamba alikuwa Mkomunisti.
Kwa bahati mbaya jumuiya hiyo ya kizalendo haikudumu. Waingereza walihakikisha kwamba itakufa. Wazanzibari walituwa fitna za kikabila na wale waliokuwa serikalini, kama Jumbe, wakalazimishwa kujiuzulu kwenye jumuiya hiyo. Baada ya kuundwa Zanzibar Nationalist Party (ZNP au Hizbu), Lamki akawa mmoja wa wakereketwa wa Hizbu na yalipotokea Mapinduzi 1964, aliihama nchi akaishia Oman alikoteuliwa Balozi.
Jumbe aliendelea kusomesha King George hadi ulipokaribia uchaguzi wa 1961. Hapo ndipo alipojiuzulu serikalini akajiunga rasmi na ASP, akiwa mmoja wa wasomi wachache waliokiunga mkono chama hicho.
Wenzake wengine waliojiuzulu serikalini na wakajitokeza waziwazi kuwa wana-Afro walikuwa pamoja na akina Othman Sharif, Hasnu Makame na Idris Abdulwakil.
Kwa hakika, Jumbe alikuwa mwanachama wa siri wa ASP tangu 1957. Jumbe ndiye aliyetunga mswada wa Ilani ya ASP ya mwaka 1961.
Katika chaguzi zilizofanywa Januari na Juni 1961 za kuwania viti katika Majlis Tashrii (Baraza la Kutunga Sheria), Jumbe aligombea kitu cha jimbo la Fuoni. Mara zote mbili alishinda uchaguzi na akateuliwa Mnadhimu wa Upinzani katika Baraza na ndani ya chama cha ASP akateuliwa Katibu wa Mipango.
Hicho kilikuwa kipindi ambapo siasa zilianza kukolea na kuwa zi moto Zanzibar. Harakati za kupigania Uhuru zilikuwa zimekwishapamba moto na ufa wa mpasuko mkubwa wa kisiasa ulikwishaanza kuonekana katika jamii. Nchi iligawika takriban nusu kwa nusu; upande mmoja ukikiunga mkono chama cha ASP na mwengine cha Hizbu.
Serikali ya kikoloni ya Uingereza iliandaa mikutano mawili ya kikatiba Lancaster House, jijini London mnamo 1962 na 1963 na mara zote alikuwa mjumbe wa upande wa ASP katika mazungumzo hayo ambayo hatimaye yalipelekea Zanzibar ipewe Uhuru Desemba 10, 1963.
Uhuru ulikabidhiwa serikali ya pamoja iliyoundwa na vyama vya ZNP na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), kilichojiengua kutoka ASP. Hata kabla ya mwezi kamili kutimia serikali hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Sheikh Muhammed Shamte Hamadi, kiongozi wa ZPPP, ilipinduliwa na wafuasi wa ASP, walioungwa mkono na“makomred”, yaani wafuasi wa chama cha Umma Party, kilichokuwa kikiongozwa na mwanamapinduzi Abdulrahman Mohamed Babu.Umma Party nacho kiliundwa na wanachama waliojiengua kutoka Hizbu baada ya kuzuka tofauti kali za kiitikadi baina yao na wahafidhina wa Hizbu.
Siku ya Mapinduzi, Januari 12, 1964, Aboud Jumbe ghafla aligeuka sura na akawa “mwanamapinduzi”. Kinadharia siasa za kimapinduzi hazikuwa zake. Wala katika harakati zake za kisiasa hakuonyesha kuwa alikuwa mtu wa kuweza kulisimamia tukio kama la “Mapinduzi”.
Lakini palipopambazuka Jumapili ya Januari 12, 1964 Aboud Jumbe alionekana Raha Leo, kulikokuwako steshini ya redio ya serikali, “Sauti ya Unguja”, na ambako kwa siku chache tangu siku hiyo
ndiko kulikokuwa makao makuu ya Mapinduzi. Jumbe alikuwa kama “mratibu” wa Mapinduzi.
Hashil Seif Hashil, mmoja wa makomred waliopata mafunzo ya kijeshi mjini Havana, Cuba, kuhusu mbinu za kupindua serikali na vita vya mwituni (guerrilla warfare) alikuwako Raha Leo akiwapa vijana mafunzo ya haraka haraka ya namna ya kutumia bunduki. Katika kitabu kinachotarajiwa kutoka karibuni (kiitwacho “Mimi, Umma Party na Mapinduzi ya 1964”) Hashil anaeleza jukumu alilokuwa nalo Jumbe siku hiyo.
Hashil ameeleza kwamba hapo Raha Leo ilikuwa Maalim Aboud aliyemuamrisha yeye pamoja na komred mwenzake aliyetoka naye Cuba, Amour Dugheish, wende kukiteka kituo cha polisi cha Malindi, kilichokuwa ngome ya mwisho ya serikali iliyopinduliwa. Kadhalika, alikuwa yeye Aboud Jumbe aliyemtaka komred mwengine, Hamed Hilal, ende kuliteka gereza kuu la Kiinua Miguu.
Jumbe pia alimpa Hashil jukumu la kukiongoza kikundi kilichokwenda kukiteka kituo cha mawasiliano ya simu cha Cable & Wireless kilichokuwapo ilipo sasa Hoteli ya Serena, hapo Kelele Square, Mji Mkongwe.
Sitomtendea haki Hashil nikiendelea kudokoa zaidi kutoka kwenye kitabu chake ambacho nimebahatika kuwa ndiye mwenye kukihariri. Labda niongeze moja tu linalomhusu Jumbe siku hiyo ya Mapinduzi.
Hashil anakumbuka kwamba alipotokea “Field Marshal” John Okello kwa mara ya kwanza Raha Leo, Jumbe alishangaa na aliuliza: “Nani huyu? Katokea wapi?”
Yote hayo yanathibitisha kuwa Jumbe hakuwa miongoni mwa waasisi wa Mapinduzi. Aliyapandia kama walivyoyapandia wengine baada ya kambi ya polisi ya Mtoni ilipokuwa imekwishatekwa na serikali ya Shamte ikiwa hoi, shingo kitanzini. Walioyapanga Mapinduzi wanaojulikana sasa kwa lakabu ya “Kamati ya watu 14” ni watu ambao hawakuwa wakimuamini Jumbe.
Baada ya Mapinduzi Jumbe aliteuliwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi, wadhifa alioushika kwa muda mfupi na alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi la kwanza. Kuanzia 1964 hadi 1972 alikuwa waziri wa afya akiwa pia waziri wa nchi katika ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania.
Miaka yote hiyo alikuwa akifanya kazi chini ya kivuli cha Sheikh Abeid Amani Karume na akiwaogopa wale jamaa wa Kamati ya Watu 14, waliokuwa wakiongozwa na Kanali Seif Bakari. Watu wengi wakishangaa na wakijiuliza aliwezaje kunusurika yasimfike yaliyowafika wasomi wenzake?
Juu ya sifa zote alizokuwa nazo Jumbe, hakuwa mtu wa kuweza kumuelezea kwa urahisi. Alikuwa mgumu kufahamika. Hivi ninavyomtafakari napata taabu kutafuta maneno muwafaka ya kumuelezea. Wala sina hakika ni Jumbe yupi nimuelezee. Aboud Jumbe alikuwa mtu mmoja lakini alikuwa na khulka, tabia za zaidi ya mtu mmoja.
Labda Jumbe atayeselelea katika kumbukumbu za Watanzania ni Jumbe aliyemrithi Karume, aliyedhani kuwa angeweza pia kumrithi na Nyerere na akaja akapinduliwa na Nyerere.
Jumbe huyu vilevile mwishowe alipendwa na Mola wake kwani aliyajutia mengi aliyoyatenda katika medani ya kisiasa na katika maisha yake. Kufika huko alipata mtihani mkubwa.
Mtihani ulianza mara baada ya mauaji ya Sheikh Karume Aprili 7, 1972. Gengi la Kamati ya Watu 14 likidhani mmoja wao atamrithi Karume. Nyerere alizicheza karata zake vyema na akalazimisha, kwa njia zake Jumbe, aibuke Rais wa pili wa Zanzibar. Hapo tukaiona sura nyingine ya Jumbe.
Baada ya kuwa Rais kila mara alikuwa akikunja uso na akijifanya si mtu wa kuchezewa. Kwa upande mwengine, aliichezea akiba ya sarafu za kigeni aliyoiacha Karume.
Alianza kujinunulia ndege ya aina ya jet, alitoa fedha za kuisaidia Pakistan. Kwa ufupi, alizifuja dola za Kimarekani za baina ya milioni 400 au 500. Wengine wanasema zilifika hata milioni 600. Nyingi alizitumilia Bara.
Tatizo kubwa alilokuwa nalo ni kwamba hakuwa na washauri wazuri. Mwaka 1977 alijiachia yeye na Zanzibar waingie katika mtego wa tembo alipokubali vyama vya Zanzibar na Tanganyika (ASP na TANU) viungane na kukizaa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alipokuja kutanabahi kwamba Zanzibar imepoteza mamlaka yake hakuwa na hatua madhubuti ya kuweza kuchukua kuiokoa jahazi. Nyerere alimuweza na wenzake wa Zanzibar, kina Maalim Seif Sharif Hamadi, walimcheza.
Kuna watu waliojaribu kumshauri akiwemo Salim Rashid, aliyekuwa Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi lakini kwa jumla akipendelea kujifanyia mambo yake kwa siri kubwa. Tabia hiyo ukiichanganya na kibri cha madaraka ndiyo iliyomponza.
Hata hivyo, japokuwa mwishowe Nyerere alimpindua tusiusahau ushujaa wake Jumbe wa kuthubutu kumkabili Nyerere na kumwambia asilotaka kulisikia kwamba Muungano ukiimeza Zanzibar. Na aliandika kitabu “The Partner-ship: Tanganyika Zanzibar Union 30 Turbulent Years” kuhusu masaibu yaliyoikuta Zanzibar ndani ya Muungano.
Aliyamaliza maisha yake akiwa mtu wa taqwa (mcha Mungu).Hata mazishi yake aliusia yafuate Sunna ya Mtume yasiwe na mbwembwe za kiserikali.
Inasikitisha kuwa wakubwa wa Zanzibar wamemwendea kinyume kwa kutangaza maombelezi ya siku saba. Mwenyewe aliusia taa’zia iwe kwa muda wa siku mbili. Sasa haya ya siku saba yametokea wapi?
Mara ya mwisho mimi kumuona Aboud Jumbe ilikuwa katika hoteli moja aliyoshukia London miaka kadhaa iliyopita. Alikuja kwa matibabu na nilikwenda kumuona nikifuatana na Sheikh Issa Othman Issa, Imam Mkuu wa Masjid Maamur, Upanga, Dar es Salaam.
Mwalimu wangu alikuwa amejitupa kitandani, alikuwa amenywea na akili yake yote ilikuwa katika mas’ala ya dini. Kazi ilikuwa kwa Sheikh Issa kwani siku hiyo Alhaj Sheikh Aboud Jumbe hakuwa akitaka kujua lolote isipokuwa kuijua zaidi dini yake kutoka kwa Sheikh Issa.
No comments:
Post a Comment