Rais wa pili wa Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi. |
ABOUD Jumbe Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, kuanzia mwaka 1972 – 1984 hatunaye tena; amefariki dunia Agosti 14, mwaka huu katika hali ya upweke wa kuhuzunisha licha ya mchango wake mkubwa kwa Zanzibar na Tanzania, kisiasa na kijamii.
Kisa?. Ni kwa sababu alimaliza vibaya katika uwanja wa siasa, kwa kuhoji muundo wa Tanzania aliosaidia kuuimarisha kwa miaka 12 kama Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; kufanya avuliwe nafasi zote za kichama na kiserikali.
Bila Aboud Jumbe Mwinyi, vyama vya TANU na Afro-Shirazi (ASP) visingeungana mwaka 1977 kuunda CCM, maana ni Jumbe aliyeridhia upande wa Zanzibar, jambo ambalo lisingewezekana kwa mtangulizi wake, hayati Abeid Amani Karume ambaye kwa kipindi chote cha utawala wake (1964 – 1972) alidai Muungano ulimbana kama koti na akatamani uvunjike.
Bila Aboud Jumbe Mwinyi, wazo juu ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi lisingepita mwaka 1973, maana ni yeye aliyeridhia kwa upande wa Zanzibar bila maoni ya Wazanzibari na akaruhusu Mzanzibari, Hasnu Makame kuteuliwa Waziri wa kwanza wa Wizara ya Kuendeleza Makao Makuu (CMD), jambo ambalo lisingewezekana enzi za Karume.
Changamoto iliyomkabili Jumbe wakati wa utawala wake ni mlipuko wa mawazo kinzani juu ya Muungano visiwani miongoni mwa raia na viongozi wa serikali, kwamba kitendo cha Rais Karume kuiingiza Zanzibar katika Muungano kilikuwa cha kisaliti kwa Wazanzibari; na pale alipojaribu kutafuta suluhu kwa njia ya Mahakama Maalumu ya Katiba kuhusu aina ya muundo sahihi uliokusudiwa na kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ilimvua nafasi zote za uongozi wa chama na serikali ikimtuhumu kwa usaliti, kisha akawekwa kizuizini nyumbani kwake Mji Mwema, Kigamboni ambako mauti yamemkuta.
Kufuatia kifo cha Karume kwa kupigwa risasi Aprili 7, 1972, Wazanzibari walitaka nafasi yake ichukuliwe na mfuasi wake shupavu na kiongozi wa Kikosi cha Usalama Zanzibar, Kanali Seif Bakari. Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliingilia kati kwa maelezo kwamba, kwa kuwa Karume aliuawa na mwanajeshi, Luteni Humud Humud, kuteuliwa kwa Bakari ambaye ni mwanajeshi kungetoa tafsiri mbaya kwamba kuuawa kwake lilikuwa jaribio la Mapinduzi ya kijeshi.
Nyerere akampendekeza kwa mafanikio, Aboud Jumbe, mhitimu mwenzake wa Chuo Kikuu, Makerere na mwalimu kwa taaluma, kurithi nafasi ya Karume kwa miguno ya wahafidhina wa siasa za chuki na visasi Zanzibar.
Chini ya Jumbe, milango ya demokrasia ilifunguka Visiwani: Desemba 1972, ASP kilifanya Mkutano Mkuu wake wa kwanza tangu mwaka 1964; mwaka 1974, Zanzibar ikaruhusu wanafunzi wa Kizanzibari kwenda kusoma Chuo Kikuu, Dar es Salaam; na mwaka 1979 Zanzibar huru ikapata Katiba yake ambapo kwa miaka 15 mfululizo ilitawaliwa kwa njia ya “Amri ya Rais” Karume.
Kuungana kwa TANU na ASP, Februari 5, 1977 kuunda CCM chenye kushika hatamu za utawala wa nchi (Party Supremacy), kulikuwa na lengo la kuimarisha Muungano na pia njia ya kudhibiti mawazo hasi kutoka ASP yenye nguvu Visiwani na Baraza lake la Mapinduzi kwani mara nyingi hakikuongea lugha moja na TANU juu ya muundo wa Muungano.
Wazanzibari, chini ya ASP walionesha kutoridhika na marekebisho manane ya Katiba ya Muungano yaliyoonekana kama hatua ya kutaka kuimeza Zanzibar.
Kwa imani sasa kwamba CCM kilikuwa kimeshika hatamu Bara na Visiwani kufuatia kifo cha TANU na ASP, mwaka huohuo 1977, NEC ya CCM ilichapisha pendekezo kwenye vyombo vya habari kukaribisha maoni kutoka kwa wananchi juu ya namna ya kuboresha Muungano kwa kufanyia marekebisho kwa mara ya tisa, Katiba ili yawasilishwe kwenye Bunge la Muungano kujadiliwa na kuridhiwa.
Kwa hatua hiyo, CCM ikawa imefungulia jini nje ya chupa. Wakati sehemu kubwa kutoka Tanzania Bara walitaka Muungano uendelee kwa muundo wa sasa, sehemu kubwa ya Wazanzibari walililia mabadiliko makubwa wakitaka Zanzibar irejeshewe uhuru na sehemu ya madaraka yake.
Tafsiri nyingi hasi kwa Muungano zilitolewa; ikiwamo kwamba, kwa kuwa Tanganyika ilikabidhi eneo lake, madaraka na kila kitu pamoja na jina kwa Serikali ya Muungano ambapo Zanzibar haikufanya hivyo, basi Tanganyika ndiyo Muungano na Muungano ndio Tanganyika; na hatua yoyote ya kutaka kuongeza orodha ya mambo ya Muungano kutoka 11 ya mwanzo, ni kutaka kumeza Zanzibar ndani ya Tanganyika.
Hayo yakisemwa Zanzibar, upande wa Bara ulidai kwamba, kwa kuwa TANU na ASP viliweza kuungana bila matata kuunda CCM chenye kushika hatamu za nchi na serikali, hapakuwa na sababu ya kuendelea na muundo wa Muungano wa serikali mbili bali serikali moja. Kwa Wazanzibari, hatua hii ilionekana kama jaribio la samaki mkubwa kutaka kummeza mdogo huku wakidai kuwa, Muungano wa serikali mbili ulifikiwa kwa makubaliano ya Nyerere na Karume pekee bila maoni wala ridhaa ya Wazanzibari.
Kundi lenye nguvu zaidi Visiwani, lililojumuisha viongozi waandamizi wa serikali na ambalo maoni yake yalitangazwa mfululizo na Redio ya mafichoni, maarufu kama “Kiroboto Tapes” na kurushwa kwa masafa yaliyoingilia Redio Zanzibar, lilitaka muundo wa Shirikisho lenye serikali tatu.
Joto la ukinzani lilipozidi Visiwani huku Jumbe akituhumiwa kukubali “kuolewa” Bara, aliona aweke makazi Bara, Mji Mwema Kigamboni; na kuruka kwa ndege kila asubuhi kwenda Zanzibar kufanya kazi na kurejea jioni.
Akihojiwa na gazeti la serikali, The Sunday News”, Januari 1984 kabla ya kung’atuliwa, kuhusu hatima ya Muungano kufuatia mawazo kinzani Visiwani alisema, “Maoni juu ya ukweli kuhusu Muungano hayajabadilika tangu uanzishwe…..suala hapa si kwamba Muungano utadumu au hapana, bali ni muundo upi unaotakiwa ili uimarike”.
Jumbe alitetea uhuru wa mawazo kama huo na akaonya usitafsiriwe kama usaliti wala kuzua uhasama wa kivikundi. Na kwa kuona kwamba kulikuwa na mtanziko wa kimawazo na maoni Visiwani, alimwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali Visiwani,Bashir Swanzy, kuandaa Hati ya Mashitaka kwa ajili ya kuwasilisha kwenye Mahakama Maalumu ya Katiba (ibara 125 ya Katiba yetu) kuiomba itoe tafsiri ni muundo upi wa Muungano uliokusudiwa chini ya Mkataba (Hati) wa Muungano tofauti na wa sasa.
Kikaitishwa kikao cha NEC cha dharura, Januari 1964, kujadili mawazo kinzani na hasi Visiwani kwa hisia kwamba yalichochewa au kuruhusiwa na uongozi ili kupotosha dhana ya Muungano; hali ya kuchafuka kwa hewa kisiasa ikatangazwa.
Ni kwa sababu hii Jumbe alivuliwa na NEC nyadhifa zote za chama na serikali, kuanzia Urais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Umakamu wa Rais wa Muungano na Ujumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama na NEC, na kuwa mtu baki hadi kifo kimemkuta.
Kalale Pema, Mwanamapinduzi, Aboud Jumbe Mwinyi.
No comments:
Post a Comment