Thursday, 25 August 2016

Jinsi Jumbe na Nyerere walivyopigana mwereka

Sheikh Aboud Jumbe, Rais wa zamani wa Zanzibar
Na Ahmed Rajab
AGOSTI 15 mwaka huu, siku alozikwa Sheikh Aboud Jumbe kuna rafiki yangu mmoja alinikumbusha makala niliyowahi kuyaandika katika jarida lichapishwalo London la New African wakati Jumbe alipokuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania.

Miongoni mwa mengi makala hayo yalizungumzia upinzani aliokuwa akiukabili Jumbe.

Wakati huo, kuta za Mji Mkongwe, Unguja, hasa zile za marikiti ya Darajani, ziligeuka na kuwa kama kuta za Beijing, China, wakati wa Mapinduzi ya Utamaduni, ambayo wenyewe Wachina wakiyaita “Wenhua Dageming” (1966-1976) yaliyoanzishwa na Mwenyekiti Mao aliyekuwa akiliongoza taifa hilo la Kikomunisti.

Wafuasi wa Mapinduzi ya Utamaduni walikuwa wakizitumia kuta kuandikia au kubandika mabango yenye maneno yao ya propaganda ama ya kumuunga mkono Mao au ya kuwashambulia mahasimu wake au nadharia zao.  Kwenye kuta, na pia kwenye mabango, ndipo zilipopatikana habari za kuaminika kuhusu yaliyokuwa yakijiri China.

Wachina walikuwa wakizitegemea sana kuta na mabango, kushinda magazeti rasmi,  kwa habari muhimu. Waliokuwa wakiandika kwenye kuta na mabango hayo wakiandika kwa rangi nyekundu, nyeupe na nyeusi. Ilikuwa ni kampeni kubwa iliyowahamasisha wananchi na ikijulikana nje ya China kama “wall poster campaign” (kampeni ya mabango ya ukutani).

Mtindo huo wa kupeleka ujumbe katika jamii kwa kutumia kuta uliigwa na wanaharakati wa Zanzibar nchi hiyo ilipokuwa chini ya utawala wa Jumbe.Tofauti iliyokuwako kati ya kampeni hizo mbili ni kwamba ile ya China ikiongozwa na kuhamasishwa na kiongozi mkuu kabisa nchini humo; ile ya Zanzibar ikimlenga kiongozi aliyekuwa na madaraka kama hayo katika visiwa hivyo.

Tofauti ya pili ni kwamba ile ya China, kwa vile ilipata idhini ya Mao, ikifanywa kwa uwazi, dhahir shahir, lakini ya Zanzibar kwa vile ilikuwa ni yenye kuasi ikifanywa kwa kificho na kwa siri kubwa.

Watu walikuwa wakiamka asubuhi na wakishtukia kuta zimechorwa vibonzo au zimeandikwa maneno yenye kumpinga Jumbe. Kampeni nzima dhidi ya Jumbe ilikuwa na ujumbe mmoja tu: kutetea mfumo wa kidemokrasia.

Tofauti ya tatu ni kwamba kampeni ya China iliendeshwa na umati wa watu lakini ile ya Zanzibar ikifanywa na watu wachache sana. Walikuwa katika vuguvugu dogo lisilokuwa na jina lakini lililokuwa na athari ya aina yake ya kuleta mwamko wa kisiasa, angalau katika eneo la Mji Mkongwe.

Safari moja nikiwa na hamsini zangu karibu na ilipo ofisi ya waziri kiongozi nilishtukia kijana mmoja akinigusa bega na kuniambia kwamba ni yeye niliyearifiwa kuwa atanitafuta kunielezea harakati zao za upinzani wa kwenye kuta. Ilikuwa mara yangu ya mwanzo kukutana naye. Alinitaka nimfuate nikaonane na mwenzake.

Nilishangaa nilipomuona mwenzake aliyekuwa mkubwa wake kwa umri na kumtambua kwamba ni mtu tuliyesoma pamoja katika skuli ya msingi. Wawili hao walianza usuhuba wao wa kisiasa walipokuwa wamefungwa jela kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Sheikh Abeid Amani Karume Aprili 7, 1972.
Yule kijana hivi sasa ni marehemu na mwenzake, mkubwa wake siku hizi ameguria Bara wala hapiti Unguja.

Upinzani wao dhidi ya utawala wa Jumbe ukiihangaisha sana serikali na hasa idara ya Usalama. Baada ya kuta kuandikwa matamshi ya kuipinga serikali na kuchorwa wajihi wa Jumbe kwenye vibanzo kazi ilikuwa ni ya polisi kuingia mitaani asubuhi na kufuta yaliyokuwa kwenye kuta.

Siku hizi harakati kama hizo kwingi duniani huendeshwa katika “kuta” za Facebook na kwenye mitandao mingine ya kijamii.

Upinzani mkali zaidi aliukabili Jumbe kutoka kwa bosi wake serikalini- Rais Julius Nyerere, ambaye baadaye alikuwa pia bosi wake chamani baada ya kuunganishwa vyama vyao, Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) cha Zanzibar na kuundwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Uhasama wa Nyerere dhidi ya Jumbe ulianza siku nyingi chini kwa chini. Kama nilivyogusia katika makala yangu ya wiki iliyopita Jumbe hakuwa mgeni kwa Nyerere wala Nyerere hakuwa mgeni kwa Jumbe. Viongozi hao wakijuana tangu walipokuwa wanafunzi katika Chuo cha Makerere, Uganda (1943-1945).

Alipouawa Karume, Nyerere alikuwa na jambo moja lililokuwa likimla roho na ambalo akitaka kulitafutia dawa kwa haraka. Lilikuwa nani atayemrithi Karume katika kiti cha urais wa Zanzibar na kuwa msaidizi wake mkuu katika serikali ya Muungano?
Kwa muda wa kama saa 48 baada ya kuuawa Karume, mtu aliyeonekana akiidhibiti nchi alikuwa Kanali Ali Mahfoudh. Yeye ndiye aliyeandika tangazo alilolisoma Jumbe katika redio ya serikali akiamrisha kufungwa kwa anga ya Zanzibar na kuchukuliwa hatua nyingine za ulinzi.

Wakati mmoja aliwakusanya wajumbe wote wa Baraza la Mapinduzi katika chumba kimoja kwa mkutano. “Ningelitaka ningeweza kuwapiga risasi wote,” Ali Mahfoudh aliwahi kuniambia zaidi ya mara moja miaka kadhaa baadaye.

Nikipenda kumchokoza kwa kumwambia kwamba alikuwa na madaraka kwa muda wa saa 48 na akaacha yakamponyoka. Mara zote akinijibu, tena kwa ukali, kwamba yeye hakuwa na nia ya kunyakua madaraka. Suala hilo halijamjia akilini hata chembe ya sekunde.

Mahfoudh alikuwa mtiifu wa Mapinduzi ya Zanzibar na akimuona Karume kama baba yake. Na yeye ndiye aliyeandaa mkakati wa nani akamatwe kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Karume, wengi wao wakiwa makomred wenzake, wafuasi wa zamani wa chama cha Umma Party.

Ingawa Mahfoudh alikuwa na uwezo wa kijeshi hakuwa na nguvu za kisiasa na asingeliweza asilan kuhodhi madaraka ya kisiasa. Nguvu hizo zilikuwa katika Baraza la Mapinduzi, na zaidi miongoni mwa wale waliokuwemo katika ile iliyojulikana kama “Kamati ya watu 14”, ambao ndio walioyaandaa Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Hapakuwepo hata mmoja miongoni mwa hao watu 14 ambaye Nyerere angeweza kuamini afanye naye kazi kwa ukaribu. Akiwadharau na wakati huo huo akiwaogopa wote 14. Bahati yake alikuwemo Jumbe katika Baraza la Mapinduzi na pia serikalini akiwa waziri aliyekuwa akishughulikia mambo ya Muungano pamoja na kuwa waziri wa afya.

Tathmini ya mwanzo ya Nyerere kuhusu Jumbe ni kwamba angalau alikuwa msomi kama yeye na wangeweza kuelewana. Bahati nyingine aliyokuwa nayo Nyerere ni kwamba alikuwepo pia Sheikh Thabit Kombo, Katibu Mkuu wa ASP, chama kilichokuwa kikitawala Zanzibar. Nyerere akionyesha kumuheshimu Kombo. Kwa upande wake Kombo, kinyume cha Karume, alikuwa siku zote akimsikiliza Nyerere.

Kutokana na yote hayo, Nyerere hakupata taabu alipomtaka Kombo amuunge mkono baada ya kupiga hesabu zake nakuona kuwa la kufanywa ni Jumbe kumrithi Karume. Nyerere, akisaidiwa na Kombo, alifanya aliyoyafanya na akaweza kuwaziba midomo wale ambao wangeweza kumkalia Jumbe vibaya.

Kwa upande waJumbe, urais ulikuwa zawadi asiyoifikiria seuze kuitarajia. Bahati yake kwamba alikuwako Nyerere kama ilivyokuwa bahati ya Nyerere kwamba alikuwako Jumbe. Wawili hao wakisikilizana zaidi ya Nyerere alivyokuwa akisikilizana na Karume katika miaka ya mwisho ya uhai wa Karume.

Pamoja na yote hayo, Jumbe alipiga mbali. Aliamini kuwa urais wa Zanzibar utamfikisha kwenye urais wa Tanzania. Niligusia wiki iliyopita jinsi Jumbe alivyoanza kubadilika alipokuwa Rais. Akionekana kama hayupo, kama mtu aliyejaa mawazo, aliyekuwa mbali na kila mara akikunja uso.

Alibadili hata namna ya alivyokuwa akizungumza; aliacha kuzungumza kwa lafudhi ya Kiunguja, akaanza kuzungumza kwa lafudhi ya Kibara. Kuna walioitafsiri tabia hiyo kuwa ni jaribio lake la kutaka kujipendekeza Bara akijiandaa kwa uongozi wa taifa zima. Mara nyingine akionekana kama mtu aliyekuwa akiigiza, kama mwigizaji katika tamthilia ya kisiasa.

Kwa hakika, na hili nilikwishaligusia wiki iliyopita, Jumbe ananipa taabu kumchora kwa maandishi. Kuyasimulia maisha ya mtu kunahitaji fani ya aina yake.
Na mtu aliyekuwa na maisha yaliyojaa mengi kama ya Jumbe humkang’anya mwandishi. Alikuwa mwanasiasa ambaye si rahisi kumpachika katika shubaka moja maalum kwa sababu anaweza kuingia kwingi.

Moja ya mambo yanayomfanya mtu ajulikane kuwa huyu ni fulani bin fulani au binti fulani ni mkusanyiko wa tabia zake. Za Jumbe zilikuwa nyingi mno na nyingi zikikinzana. Kwa mfano alikuwa karimu kama tulivyoshuhudia alipoamua kuipelekea Pakistan msaada wa fedha nchi hiyo ilipopata maafa ya zilzala, nikikumbuka vizuri. Lakini pia mtu huyo huyo alikuwa na uchoyo fulani.

Kadhalika, ingawa alikuwa msomi lakini hakuwa na tabia ya kusoma magazeti jambo ambalo likimkera Nyerere. Rafiki yangu mmoja aliwahi kunieleza jinsi Nyerere alivyomlalamikia kwa kusema: “Makamu wangu hata gazeti hasomi.”

Ijapokuwa alitamani awe Rais wa Tanzania, hata hivyo mwishoni mwa maisha yake ya kisiasa akisema kwamba Zanzibar ilighilibiwa kuukubali Muungano wa serikali mbili. Hapo ndipo alipouvaa uzalendo wa Kizanzibari na akajaribu kuirejeshea nchi yake mamlaka yake kamili.

Jumbe, lakini, alishindwa kutekeleza azma yake kwa sababu ya watu wawili: mmoja mwenyewe na wa pili Nyerere.
ITAENDELEA

Tuesday, 23 August 2016

Aboud Jumbe (1920- 2016): Mtoto wa Mkamasini aliyekuwa mwingi wa mengi


Rais wa pili wa Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi.
Na Ahmed Rajab,
KIFO cha Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea adhuhuri yaJumapili iliyopita kiliufunga, bila ya kishindo, mlango mmoja muhimu wa historia ya karibuni ya Zanzibar. Mauti yalipomkuta, Jumbe alikuwa na umri wa miaka 96.

Tanzania, na hususani Zanzibar, imeondokewa na mtu aliyekuwa mwingi na aliyekuwa na mengi. Aboud Jumbe Mwinyi alizaliwa mtaa wa Mkamasini, Ng’ambo, Unguja Juni 14, 1920.

Kama ilivyo kawaida ya watoto wa Kizanzibari, elimu yake ya kwanza ilikuwa ni ya  mafunzo ya dini alipotiwa chuoni (madrasa) kusoma Qur’an. Tangu ujana wake akisifika kwa namna alivyokuwa akiisoma suratil Fatiha (mlango wa kwanza wa Qur’an).

Wenye kuyajua mambo haya wanasema kwamba Jumbe akiisoma Al Fatiha kama Mtume Muhammad (SAW) alivyokuwa akiisoma kwa kuipa kila herufi haki yake.
Jumbe alisomea masomo ya msingi na ya sekondari huko huko Unguja. Pamoja na Sheikh Ali Muhsin Barwani, Jumbe alikuwa mmoja wa wanafunzi wa yule mwalimu mashuhuri Lawrence William Hollingsworth.

Huyu alikuwa Mwingereza aliyefundisha Zanzibar kwa miaka mingi sana.  Baada ya kumaliza masomo ya sekondari katika Skuli ya Serikali Mnazimmoja (siku hizi Skuli ya Ben Bella), Jumbe alichaguliwa kwenda kusomea stashahada ya elimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, akibobea katika somo la biolojia.

Ali Muhsin alikuwa amekwishamtangulia Makerere lakini wote wawili walikutana huko na Julius Nyerere, mwanafunzi mwenzao kutoka Tanganyika. Kutoka 1943 hadi 1945 Jumbe na Nyerere walikuwa wanachama wa  Jumuiya ya Mijadala (Debating Society).

Mwaka wao wa mwisho Makerere, Jumbe na Nyerere walikuwa wenyeviti wa mabweni ya wanafunzi; Jumbe alikuwa mwenyekiti wa Ssejongo na Nyerere wa Bamuja. Baadaye katika uhai wao, mmoja kati ya hao wawili atakuja kumzidi akili na kumpiku mwenzake.

Aboud Jumbe atakumbukwa kwa mambo mawili, ualimu na siasa. Hizo siasa ndizo zilizomfikisha hatimaye katika kilele  cha uongozi akiwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar (1972-1984). Katika kipindi hichohicho alikuwa pia Makamu wa Rais wa Tanzania chini ya Nyerere.

Nyadhifa hizo zilimfanya awe maarufu nje ya mipaka ya Tanzania lakini kwao Zanzibar alipata umaarufu hata kabla hajazivaa siasa. Alirudi kutoka Makerere mwaka 1945 na tangu 1946 alikuwa akisomesha skuli ya serikali ya sekondari ambayo nilipoingia mimi kuanza masomo ya sekondari ilikuwa ikiitwa King George VI Grammar Secondary School (siku hizi inaitwa Lumumba School).

Miongoni mwa wanafunzi mashuhuri wa skuli hiyo waliosomeshwa na Jumbe ni mwanahistoria, Profesa Abdul Sherrif, waziri mkuu wa zamani Salim Ahmed Salim, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Seif Sharif Hamad, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Comoro, Salim Himidi na mawaziri wa zamani wa Zanzibar, Ali Salim Ahmed na Ali Juma Shamhuna.

Hawa wawili wa mwisho tulikuwa darasa moja na Maalim Aboud Jumbe ndiye aliyekuwa mwalimu wetu wa klasi tulipokuwa Form 1.

Ninamkumbuka mwalimu aliyekuwa mpole, mtaratibu asiye na ghasia wala vishindo. Hajawa mkali, mtu wa kuwakaripia watoto au wa vitisho.

Ninamkumbuka kwamba alikuwa mwalimu razini aliyekuwa akiwapenda wanafunzi wake wa kabila na tabaka zote. Jumbe pia alikuwa mkubwa wa maskauti na aliwavutia wanafunzi wengi wawe maskauti.

Zaidi ya yote ninamkumbuka maalim wetu kwamba alikuwa mtu wa bashasha, ingawa ukihisi kama ndani ya nafsi yake akionyesha kama mtu aliyekuwa na huzuni ya aina fulani. Labda akiyaona mengi katika jamii yaliyokuwa yakimkirihisha au kumuudhi.

Ama mimi binafsi, Maalim Aboud Jumbe alikuwa na mambo yake mawili yaliyokuwa yakinikera. Kwanza, alikuwa na tabia ya mara kwa mara kupotea asije skuli, hasa siku za Jumatatu.

Pili, na hili likiniudhi sana, alikuwa na tabia akiwa darasani ya kwenda kwenye ubao na kuandika, kwa hati zake nzuri, maelezo ya somo alilokuwa akisomesha.
Akimaliza akipenda kwenda nyuma ya darasa na kuyasoma aliyoyaandika halafu akijilaumu kuwa hakuandika vizuri na akirejea kwenye ubao na akiyafuta yote aliyokuwa ameyaandika. Akituudhi kwa sababu wengi wetu tulikuwa tumeshayaandika maelezo yake vitabuni mwetu. Ilibidi tuanze tena upya.

Jumbe hakuwa mwalimu wa somo moja. Alimudu kusomesha masomo mbalimbali. Akifundisha sayansi, biolojia (elimu viumbe), historia na Kiswahili, ambacho akikisarifu vizuri sana. Kwa hakika, alikuwa mwingi wa nahau (au sarufi) ya hii lugha yetu. Siku hizo sarufi ya Kiswahili ikifundishwa kwa kufuata mifumo au mitindo iliyoachwa na wazungu waliokuwa wataalamu wa lugha hiyo, akiwemo Bibi Ethel O. Ashton aliyetunga kitabu muhimu na kilicho maarufu kuhusu sarufi ya Kiswahili.

Zama zetu tulipokuwa tukiingia skuli za serikali za sekondari ilikuwa lazima tusome moja ya lugha tatu pamoja na Kiingereza tulichokuwa tukisomeshewa. Ilibidi tuchague ama Kiswahili, Kiarabu au Kigujerati (mojawapo ya lugha za Kihindi).

Kwa hiyo, kwa vile niliamua kusoma lugha ya Kiarabu sikubahatika kusomeshwa Kiswahili na Maalim Aboud Jumbe. Hata hivyo nilipata bahati kubwa ya kusomeshwa naye historia. Darasa zake, kwa mfano kuhusu “kudhoofika na kuanguka kwa Milki ya Kirumi”, siku zote zilikuwa zikisisimua na zikinifanya nihisi kama nilikuwa nikiishi katika enzi za Warumi.

Kadhalika nikipenda kumsikiliza alipokuwa akisimulia misafara ya wagunduzi wa Kireno kama kina Afonso de Albuquerque, Pedros Alvares Cabral na Vasco da Gama. Wagunduzi hao wa Kireno wana umuhimu mkubwa katika historia ya Afrika, ya Eshia na ya nchi za Amerika ya Kusini kwa sababu ndio waliowatangulia, au tuseme waliowafungulia njia wakoloni wa Kizungu waliokuja kuzipora nchi zetu na kutudhalilisha.

Tulikuwa na waalimu waliokuwa wakituamsha kisiasa walipokuwa wakitusomesha lakini sikumbuki kama Jumbe alikuwa mmojawao. Hayo si ajabu kwa sababu alikuwa mtu wa hadhari hasa kwa vile kwa mujibu wa sheria na kanuni za serikali ya kikoloni ya wakati huo waalimu hawakuruhusiwa kujiingiza katika mambo ya siasa.

Si kwamba hakutaka au hakujaribu. Inawezekana kwamba alipokuwa mwanafunzi Unguja katika skuli za msingi na sekondari akizizungumza siasa. Na inamkinika sana kwamba alianza kupata mwamko wa siasa za kijitu uzima alipokuwa Makerere akijadiliana na kina Nyerere.

Jumbe katika miaka ya mwanzo ya 1950 alikuwa mmoja wa waasisi wa Jumuiya moja ya Kitaifa huko Zanzibar (Zanzibar National Union), iliyokuwa kiini cha kunyanyua mwamko wa hisia za kizalendo, hasa uzalendo wa Kizanzibari.

Jumuiya hiyo, iliyoasisiwa na wasomi,  iliwaunganisha Wazanzibari wa kila kabila. Mmojawao alikuwa Ahmed Lamki, aliyewahi kukamatwa nchini Misri alikokuwa akisoma wakati wa utawala wa Mfalme Farouk, baada ya kutuhumiwa kwamba alikuwa Mkomunisti.

Kwa bahati mbaya jumuiya  hiyo ya kizalendo haikudumu. Waingereza walihakikisha kwamba itakufa. Wazanzibari walituwa fitna za kikabila na wale waliokuwa serikalini, kama Jumbe, wakalazimishwa kujiuzulu kwenye jumuiya hiyo.  Baada ya kuundwa Zanzibar Nationalist Party (ZNP au Hizbu), Lamki akawa mmoja wa wakereketwa wa Hizbu na yalipotokea Mapinduzi 1964, aliihama nchi akaishia Oman alikoteuliwa Balozi.

Jumbe aliendelea kusomesha King George hadi ulipokaribia uchaguzi wa 1961. Hapo ndipo alipojiuzulu serikalini akajiunga rasmi na ASP, akiwa mmoja wa  wasomi wachache waliokiunga mkono chama hicho.

Wenzake wengine waliojiuzulu serikalini na wakajitokeza waziwazi kuwa wana-Afro walikuwa pamoja na akina Othman Sharif, Hasnu Makame na Idris Abdulwakil.
Kwa hakika, Jumbe alikuwa mwanachama wa siri wa ASP tangu 1957. Jumbe ndiye aliyetunga mswada wa Ilani ya ASP ya mwaka 1961.

Katika chaguzi zilizofanywa Januari na Juni 1961 za kuwania viti katika Majlis Tashrii (Baraza la Kutunga Sheria), Jumbe aligombea kitu cha jimbo la Fuoni. Mara zote mbili alishinda uchaguzi na akateuliwa Mnadhimu wa Upinzani katika Baraza na ndani ya chama cha ASP akateuliwa Katibu wa Mipango.

Hicho kilikuwa kipindi ambapo siasa zilianza kukolea na kuwa zi moto Zanzibar. Harakati za kupigania Uhuru zilikuwa zimekwishapamba moto na ufa wa mpasuko mkubwa wa kisiasa ulikwishaanza kuonekana katika jamii. Nchi iligawika takriban nusu kwa nusu; upande mmoja ukikiunga mkono chama cha ASP na mwengine cha Hizbu.

Serikali ya kikoloni ya Uingereza iliandaa mikutano mawili ya kikatiba Lancaster House, jijini London mnamo 1962 na 1963 na mara zote alikuwa mjumbe wa upande wa ASP katika mazungumzo hayo ambayo hatimaye yalipelekea Zanzibar ipewe Uhuru Desemba 10, 1963.

Uhuru ulikabidhiwa serikali ya pamoja iliyoundwa na vyama vya ZNP na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), kilichojiengua kutoka ASP. Hata kabla ya mwezi kamili kutimia serikali hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Sheikh Muhammed Shamte Hamadi, kiongozi wa ZPPP, ilipinduliwa na wafuasi wa ASP, walioungwa mkono na“makomred”, yaani wafuasi wa chama cha Umma Party, kilichokuwa kikiongozwa na mwanamapinduzi Abdulrahman Mohamed Babu.Umma Party nacho kiliundwa na wanachama waliojiengua kutoka Hizbu baada ya kuzuka tofauti kali za kiitikadi baina yao na wahafidhina wa Hizbu.

Siku ya Mapinduzi, Januari 12, 1964, Aboud Jumbe ghafla aligeuka sura na akawa “mwanamapinduzi”. Kinadharia siasa za kimapinduzi hazikuwa zake. Wala katika harakati zake za kisiasa hakuonyesha kuwa alikuwa mtu wa kuweza kulisimamia tukio kama la “Mapinduzi”.

Lakini palipopambazuka Jumapili ya Januari 12, 1964 Aboud Jumbe alionekana Raha Leo, kulikokuwako steshini ya redio ya serikali, “Sauti ya Unguja”, na ambako kwa siku chache tangu siku hiyo
ndiko kulikokuwa makao makuu ya Mapinduzi. Jumbe alikuwa kama “mratibu” wa Mapinduzi.

Hashil Seif Hashil, mmoja wa makomred waliopata mafunzo ya kijeshi mjini Havana, Cuba, kuhusu mbinu za kupindua serikali na vita vya mwituni (guerrilla warfare) alikuwako Raha Leo akiwapa vijana mafunzo ya haraka haraka ya namna ya kutumia bunduki. Katika kitabu kinachotarajiwa kutoka karibuni (kiitwacho “Mimi, Umma Party na Mapinduzi ya 1964”) Hashil anaeleza jukumu alilokuwa nalo Jumbe siku hiyo.

Hashil ameeleza kwamba hapo Raha Leo ilikuwa Maalim Aboud aliyemuamrisha yeye pamoja na komred mwenzake aliyetoka naye Cuba, Amour Dugheish, wende kukiteka kituo cha polisi cha Malindi, kilichokuwa ngome ya mwisho ya serikali iliyopinduliwa. Kadhalika, alikuwa yeye Aboud Jumbe aliyemtaka komred mwengine, Hamed Hilal, ende kuliteka gereza kuu la Kiinua Miguu.

Jumbe pia alimpa Hashil jukumu la kukiongoza kikundi kilichokwenda kukiteka kituo cha mawasiliano ya simu cha Cable & Wireless kilichokuwapo ilipo sasa Hoteli ya Serena, hapo Kelele Square, Mji Mkongwe.

Sitomtendea haki Hashil nikiendelea kudokoa zaidi kutoka kwenye kitabu chake ambacho nimebahatika kuwa ndiye mwenye kukihariri. Labda niongeze moja tu linalomhusu Jumbe siku hiyo ya Mapinduzi.

Hashil anakumbuka kwamba alipotokea “Field Marshal” John Okello kwa mara ya kwanza Raha Leo, Jumbe alishangaa na aliuliza: “Nani huyu? Katokea wapi?”
Yote hayo yanathibitisha kuwa Jumbe hakuwa miongoni mwa waasisi wa Mapinduzi. Aliyapandia kama walivyoyapandia wengine baada ya kambi ya polisi ya Mtoni ilipokuwa imekwishatekwa na serikali ya Shamte ikiwa hoi, shingo kitanzini. Walioyapanga Mapinduzi wanaojulikana sasa kwa lakabu ya “Kamati ya watu 14” ni watu ambao hawakuwa wakimuamini Jumbe.

Baada ya Mapinduzi Jumbe aliteuliwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi, wadhifa alioushika kwa muda mfupi na alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi la kwanza. Kuanzia 1964 hadi 1972 alikuwa waziri wa afya akiwa pia waziri wa nchi katika ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania.

Miaka yote hiyo alikuwa akifanya kazi chini ya kivuli cha Sheikh Abeid Amani Karume na akiwaogopa wale jamaa wa Kamati ya Watu 14, waliokuwa wakiongozwa na Kanali Seif Bakari. Watu wengi wakishangaa na wakijiuliza aliwezaje kunusurika yasimfike yaliyowafika wasomi wenzake?

Juu ya sifa zote alizokuwa nazo Jumbe, hakuwa mtu wa kuweza kumuelezea kwa urahisi. Alikuwa mgumu kufahamika. Hivi ninavyomtafakari napata taabu kutafuta maneno muwafaka ya kumuelezea. Wala sina hakika ni Jumbe yupi nimuelezee. Aboud Jumbe alikuwa mtu mmoja lakini alikuwa na khulka, tabia za zaidi ya mtu mmoja.

Labda Jumbe atayeselelea katika kumbukumbu za Watanzania ni Jumbe aliyemrithi Karume, aliyedhani kuwa angeweza pia kumrithi na Nyerere na akaja akapinduliwa na Nyerere.

Jumbe huyu vilevile mwishowe alipendwa na Mola wake kwani aliyajutia mengi aliyoyatenda katika medani ya kisiasa na katika maisha yake. Kufika huko alipata mtihani mkubwa.

Mtihani ulianza mara baada ya mauaji ya Sheikh Karume Aprili 7, 1972. Gengi la Kamati ya Watu 14 likidhani mmoja wao atamrithi Karume. Nyerere alizicheza karata zake vyema na akalazimisha, kwa njia zake Jumbe, aibuke Rais wa pili wa Zanzibar.  Hapo tukaiona sura nyingine ya Jumbe.

Baada ya kuwa Rais kila mara alikuwa akikunja uso na akijifanya si mtu wa kuchezewa. Kwa upande mwengine, aliichezea akiba ya sarafu za kigeni aliyoiacha Karume.

Alianza kujinunulia ndege ya aina ya jet, alitoa fedha za kuisaidia Pakistan. Kwa ufupi, alizifuja dola za Kimarekani za baina ya milioni 400 au 500. Wengine wanasema zilifika hata milioni 600. Nyingi alizitumilia Bara.

Tatizo kubwa alilokuwa nalo ni kwamba hakuwa na washauri wazuri. Mwaka 1977 alijiachia yeye na Zanzibar waingie katika mtego wa tembo alipokubali vyama vya Zanzibar na Tanganyika (ASP na TANU) viungane na kukizaa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alipokuja kutanabahi kwamba Zanzibar imepoteza mamlaka yake hakuwa na hatua madhubuti ya kuweza kuchukua kuiokoa jahazi. Nyerere alimuweza na wenzake wa Zanzibar, kina Maalim Seif Sharif Hamadi, walimcheza.

Kuna watu waliojaribu kumshauri akiwemo Salim Rashid, aliyekuwa Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi lakini kwa jumla akipendelea kujifanyia mambo yake kwa siri kubwa. Tabia hiyo ukiichanganya na kibri cha madaraka ndiyo iliyomponza.

Hata hivyo, japokuwa mwishowe Nyerere alimpindua tusiusahau ushujaa wake Jumbe wa kuthubutu kumkabili Nyerere na kumwambia asilotaka kulisikia kwamba Muungano ukiimeza Zanzibar. Na aliandika kitabu “The Partner-ship: Tanganyika Zanzibar Union 30 Turbulent Years” kuhusu masaibu yaliyoikuta Zanzibar ndani ya Muungano.

Aliyamaliza maisha yake akiwa mtu wa taqwa (mcha Mungu).Hata mazishi yake aliusia yafuate Sunna ya Mtume yasiwe na mbwembwe za kiserikali.

Inasikitisha kuwa wakubwa wa Zanzibar wamemwendea kinyume kwa kutangaza maombelezi ya siku saba. Mwenyewe aliusia taa’zia iwe kwa muda wa siku mbili. Sasa haya ya siku saba yametokea wapi?

Mara ya mwisho mimi kumuona Aboud Jumbe ilikuwa katika hoteli moja aliyoshukia London miaka kadhaa iliyopita. Alikuja kwa matibabu na nilikwenda kumuona nikifuatana na Sheikh Issa Othman Issa, Imam Mkuu wa Masjid Maamur, Upanga, Dar es Salaam.

Mwalimu wangu alikuwa amejitupa kitandani, alikuwa amenywea na akili yake yote ilikuwa katika mas’ala ya dini. Kazi ilikuwa kwa Sheikh Issa kwani siku hiyo Alhaj Sheikh Aboud Jumbe hakuwa akitaka kujua lolote isipokuwa kuijua zaidi dini yake kutoka kwa Sheikh Issa.

Aboud Jumbe: Shujaa aliyeinua taifa, amekufa na upweke


Rais wa pili wa Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi.
Na Joseph Mihangwa,
ABOUD Jumbe Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, kuanzia mwaka 1972 – 1984 hatunaye tena; amefariki dunia Agosti 14, mwaka huu katika hali ya upweke wa kuhuzunisha licha ya mchango wake mkubwa kwa Zanzibar na Tanzania, kisiasa na kijamii.

Kisa?.  Ni kwa sababu alimaliza vibaya katika uwanja wa siasa, kwa kuhoji muundo wa Tanzania aliosaidia kuuimarisha kwa miaka 12 kama Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; kufanya avuliwe nafasi zote za kichama na kiserikali.

Bila Aboud Jumbe Mwinyi, vyama vya TANU na Afro-Shirazi (ASP) visingeungana mwaka 1977 kuunda CCM, maana ni Jumbe aliyeridhia upande wa Zanzibar, jambo ambalo lisingewezekana kwa mtangulizi wake, hayati Abeid Amani Karume ambaye kwa kipindi chote cha utawala wake (1964 – 1972) alidai Muungano ulimbana kama koti na akatamani uvunjike.

Bila Aboud Jumbe Mwinyi, wazo juu ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi lisingepita mwaka 1973, maana ni yeye aliyeridhia kwa upande wa Zanzibar bila maoni ya Wazanzibari na akaruhusu Mzanzibari, Hasnu Makame kuteuliwa Waziri wa kwanza wa Wizara ya Kuendeleza Makao Makuu (CMD), jambo ambalo lisingewezekana enzi za Karume.

Changamoto iliyomkabili Jumbe wakati wa utawala wake ni mlipuko wa mawazo kinzani juu ya Muungano visiwani miongoni mwa raia na viongozi wa serikali, kwamba kitendo cha Rais Karume kuiingiza Zanzibar katika Muungano kilikuwa cha kisaliti kwa Wazanzibari; na pale alipojaribu kutafuta suluhu kwa njia ya Mahakama Maalumu ya Katiba kuhusu aina ya muundo sahihi uliokusudiwa na kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ilimvua nafasi zote za uongozi wa chama na serikali ikimtuhumu kwa usaliti, kisha akawekwa kizuizini nyumbani kwake Mji Mwema, Kigamboni ambako mauti yamemkuta.

Kufuatia kifo cha Karume kwa kupigwa risasi Aprili 7, 1972, Wazanzibari walitaka nafasi yake ichukuliwe na mfuasi wake shupavu na kiongozi wa Kikosi cha Usalama Zanzibar, Kanali Seif Bakari.  Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliingilia kati kwa maelezo kwamba, kwa kuwa Karume aliuawa na mwanajeshi, Luteni Humud Humud, kuteuliwa kwa Bakari ambaye ni mwanajeshi kungetoa tafsiri mbaya kwamba kuuawa kwake lilikuwa jaribio la Mapinduzi ya kijeshi.

Nyerere akampendekeza kwa mafanikio, Aboud Jumbe, mhitimu mwenzake wa Chuo Kikuu, Makerere na mwalimu kwa taaluma, kurithi nafasi ya Karume kwa miguno ya wahafidhina wa siasa za chuki na visasi Zanzibar. 

Chini ya Jumbe, milango ya demokrasia ilifunguka Visiwani:  Desemba 1972, ASP kilifanya Mkutano Mkuu wake wa kwanza tangu mwaka 1964; mwaka 1974, Zanzibar ikaruhusu wanafunzi wa Kizanzibari kwenda kusoma Chuo Kikuu, Dar es Salaam; na mwaka 1979 Zanzibar huru ikapata Katiba yake ambapo kwa miaka 15 mfululizo ilitawaliwa kwa njia ya “Amri ya Rais” Karume.

Kuungana kwa TANU na ASP, Februari 5, 1977 kuunda CCM chenye kushika hatamu za utawala wa nchi (Party Supremacy), kulikuwa na lengo la kuimarisha Muungano na pia njia ya kudhibiti mawazo hasi kutoka ASP yenye nguvu Visiwani na Baraza lake la Mapinduzi kwani mara nyingi hakikuongea lugha moja na TANU juu ya muundo wa Muungano.

Wazanzibari, chini ya ASP walionesha kutoridhika na marekebisho manane ya Katiba ya Muungano yaliyoonekana kama hatua ya kutaka kuimeza Zanzibar.

Kwa imani sasa kwamba CCM kilikuwa kimeshika hatamu Bara na Visiwani kufuatia kifo cha TANU na ASP, mwaka huohuo 1977, NEC ya CCM ilichapisha pendekezo kwenye vyombo vya habari kukaribisha maoni kutoka kwa wananchi juu ya namna ya kuboresha Muungano kwa kufanyia marekebisho kwa mara ya tisa, Katiba ili yawasilishwe kwenye Bunge la Muungano kujadiliwa na kuridhiwa. 

Kwa hatua hiyo, CCM ikawa imefungulia jini nje ya chupa. Wakati sehemu kubwa kutoka Tanzania Bara walitaka Muungano uendelee kwa muundo wa sasa, sehemu kubwa ya Wazanzibari walililia mabadiliko makubwa wakitaka Zanzibar irejeshewe uhuru na sehemu ya madaraka yake.

Tafsiri nyingi hasi kwa Muungano zilitolewa; ikiwamo kwamba, kwa kuwa Tanganyika ilikabidhi eneo lake, madaraka na kila kitu pamoja na jina kwa Serikali ya Muungano ambapo Zanzibar haikufanya hivyo, basi Tanganyika ndiyo Muungano na Muungano ndio Tanganyika; na hatua yoyote ya kutaka kuongeza orodha ya mambo ya Muungano kutoka 11 ya mwanzo, ni kutaka kumeza Zanzibar ndani ya Tanganyika.

Hayo yakisemwa Zanzibar, upande wa Bara ulidai kwamba, kwa kuwa TANU na ASP viliweza kuungana bila matata kuunda CCM chenye kushika hatamu za nchi na serikali, hapakuwa na sababu ya kuendelea na muundo wa Muungano wa serikali mbili bali serikali moja. Kwa Wazanzibari, hatua hii ilionekana kama jaribio la samaki mkubwa kutaka kummeza mdogo huku wakidai kuwa, Muungano wa serikali mbili ulifikiwa kwa makubaliano ya Nyerere na Karume pekee bila maoni wala ridhaa ya Wazanzibari.

Kundi lenye nguvu zaidi Visiwani, lililojumuisha viongozi waandamizi wa serikali na ambalo maoni yake yalitangazwa mfululizo na Redio ya mafichoni, maarufu kama “Kiroboto Tapes” na kurushwa kwa masafa yaliyoingilia Redio Zanzibar, lilitaka muundo wa Shirikisho lenye serikali tatu.

Joto la ukinzani lilipozidi Visiwani huku Jumbe akituhumiwa kukubali “kuolewa” Bara, aliona aweke makazi Bara, Mji Mwema Kigamboni; na kuruka kwa ndege kila asubuhi kwenda Zanzibar kufanya kazi na kurejea jioni. 

Akihojiwa na gazeti la serikali, The Sunday News”, Januari 1984 kabla ya kung’atuliwa, kuhusu hatima ya Muungano kufuatia mawazo kinzani Visiwani alisema, “Maoni juu ya ukweli kuhusu Muungano hayajabadilika tangu uanzishwe…..suala hapa si kwamba Muungano utadumu au hapana, bali ni muundo upi unaotakiwa ili uimarike”.

Jumbe alitetea uhuru wa mawazo kama huo na akaonya usitafsiriwe kama usaliti wala kuzua uhasama wa kivikundi. Na kwa kuona kwamba kulikuwa na mtanziko wa kimawazo na maoni Visiwani, alimwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali Visiwani,Bashir Swanzy, kuandaa Hati ya Mashitaka kwa ajili ya kuwasilisha kwenye Mahakama Maalumu ya Katiba (ibara 125 ya Katiba yetu) kuiomba itoe tafsiri ni muundo upi wa Muungano uliokusudiwa chini ya Mkataba (Hati) wa Muungano tofauti na wa sasa.

Kikaitishwa kikao cha NEC cha dharura, Januari 1964, kujadili mawazo kinzani na hasi Visiwani kwa hisia kwamba yalichochewa au kuruhusiwa na uongozi ili kupotosha dhana ya Muungano; hali ya kuchafuka kwa hewa kisiasa ikatangazwa.

Ni kwa sababu hii Jumbe alivuliwa na NEC nyadhifa zote za chama na serikali, kuanzia Urais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Umakamu wa Rais wa Muungano na Ujumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama na NEC, na kuwa mtu baki hadi kifo kimemkuta.

Kalale Pema, Mwanamapinduzi, Aboud Jumbe Mwinyi.

Monday, 22 August 2016

MAZOEZI YA POLISI YAZUA TAHARUKI KISIWANI PEMBA


Askari wa Jehi la Polisi wakifanya mazoezi ya kukabiliana na uhalifu kisiwani Pemba. (Picha kwa hisani ya Pemba News Media)

Shughuli za masomo katika skuli za Madungu Sekondari na Shamiani leo zilisimama kwa muda baada na baadhi ya wanafunzi kupata mshtuko na kupoteza fahamu kutokana na milio ya baruti iliyokuwa ikisika katika mji wa Chake Chake majira ya asubuhi.

Milio hiyo iliyofanana na miripuko ya mabomu ilianza kusikika majira ya saa 2:30 za asubuhi pale jeshi la polisi mkoa wa kusini Pemba walipokuwa wakifanya mazoezi ya kujitayarisha na matukio mbali mbali kwenye maeneo tofauti ya mji wa Chake Chake.

Polisi walionekana wakiwa wamevalia kamili katika mazoezi hayo ambayo baadhi ya wananchi wameyahusisha na maandalizi ya kukabiliana na maandamano ya UKUTA yaliyotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanyika tarehe 1 Septemba, walianza kupiga baruti hizo na kuzua hofu kubwa kwa wananchi wa mji wa Chake Chake.

Kutokana na tokeo hilo wanafunzi tisa wa Skuli ya Madungu Sekondari walipoteza fahamu kutokana na mshtuko na kukimbizwa katika hospitali ya Chake Chake.

Wakizungumza na Pemba News Media huko katika Hospitali ya Chake Chake baadhi ya wanafunzi walisema wakiwa darasani wakiendelea na mitihani ya majaribio walisikia milio hiyo na kutaharuki huku wengine wakipoteza fahamu.

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika skuli hiyo Hanima Daud Khamis amesema akiwa darasani na wenzake alisikia mlio wa kitu kama bomu lilimtia wasiwasi mkubwa na ndipo baadhi ya wenzake walipoanguka na kupoteza fahamu na ndipo walipopatiwa msaada wa kupelekwa hospitali.

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao wamesema ipo haja kwa jeshi la polisi kutoa taarifa wakati wanapofanya shughuli za mazoezi hasa za upigaji baruti kwa vile wananchi wa kisiwa cha Pemba si mara nyingi kusikia miripuko na milio ya risasi hivyo kunaweza kusababisha badhara kwao.

Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Madungu Serkondari Moh`d Shamte amesema kitendo kilichofanywa na jeshi la polisi kufanya mazoezi yao na kupiga baruti karibu na eneo la skuli halikuwa na kiungwana kwa vile limesababisha taharuki kubwa.

“Ni vyema kama jeshi la polisi walikuwa na mazoezi wangetoa taarifa kwa skuli ili tusije au tutoe taarifa ya tahadhari kwa wanafunzi, pia shughuli kama hizo hazikupaswa kufabywa katika eneo la mjini”

Naye mwalim Omar Salim wa Skuli ya Madungu ameelezea kusikitishwa kwake na kitendo hicho ambacho kimewathiri baadhi ya wanafunzi huku wakilazimika kusitisha mitihani ya majaribio iliyokuwa ikiendelea katika skuli hiyo.

“Si kitendo kizuri hasa ukizingatia hili ni eneo la skuli lenye wanafunzi wengi ni bora wengetupa taarifa na mapema tukaaghirisha mitihani, lakini hata tulipowafuata hawakutupa majibu ya kuridhisha”

Daktari Mkuu wa Wodi za wanawake na wanaume kwenye hospitali ya Chake Chake Dk. Rahila Salim Omar amethibitisha kupokea wanafunzi tisa waliopoteza fahamu kutoka skuli ya Magungu Sekondari hata hivyo amesema hali zao sio mbaya na hadi saa 9 za alasiri watatu walikwisha ruhusiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Moh`d Sheghan Moh`d amesema ni mazoezi ya kawaida ya kukabiliana na matukio mbali mbali yaliyokuwa yakifanywa na jeshi hilo leo asubuhi na kudai kuwa taarifa zilisambazwa katika maeneo mbali mbali.
Aliwataka wananchi kutokuwa na hofu kwa vile huo ni utaratibu wa kawaida unaofanywa mara kwa mara na jeshi hilo kila baada ya muda.

Mbali na eneo hilo la Madungu lakini pia zoezi hilo lilifanyika katika maeneo ya Gombani, Mkanyuni, Machomanne, Tibirinzi, Changaani na Chake Chake Mjini.

CHANZO: PEMBA NEWS MEDIA.

Wednesday, 10 August 2016

HATUA ZISIPOCHUKULIWA, TUNAELEKEA KUWA NA VIPAZA SAUTI BADALA YA VYOMBO VYA HABARI

Studio ya ITV
NA BIN MAZROUY
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekipiga faini yab TZS milioni 10 kituo cha Televisheni cha ITV

ITV wamepigwa faini hiyo kutokana na kipindi kutoka bungeni kilichokuwa kinaendesha mahojiano ya moja kwa moja, ambapo Mbunge wa Iringa Mjini Mchngaji Petter Msigwa alisikika akisema "Naibu Spika amekuwa kama anavaa pampas, hataki kubanduka kwenye kiti kuongoza bunge".

Kauli hii ya Mchungaji Msigwa imetafsiriwa kama ni kauli ya kuudhi na imeisababishia ITV kuangukiwa na rungu zito la faini badala ya Mtoaji wa kauli hiyo.

TCRA wanadai katika mahijiano hayo muongozaji wa kipindi alishindwa kusimamia mjadala uliokuwa ukiendelea na kuruhusu mgeni wake kutoa kauli yenye kuudhi.

TCRA hawakuitendea haki ITV katika maamuzi haya ukizingatia kuwa kipindi kilikuwa kinarushwa moja kwa moja (LIVE) na mtangazaji hajui Source wake anakwenda kuzungumza kitu gani juu ya kile alichomuuliza hivyo kukosa nafasi ya kuhariri kile kinachoonekana kuudhi.

Kinachoonekana katika maamuzi haya ni muendelezo wa vitisho kwa vyombo vya habari dhidi ya kile kinachoonekana kuwa ni kuwakosoa viongozi wenye mamlaka ya uendeshaji wa vyombo vya maamuzi ya Wananchi.

Kwa hali hii sasa vyombo vya habari vitaacha kuandaa vipindi na mijadala yenye kuikosoa serikali pamoja na kutokuwaalika wale wenye kuonekana kuikosoa serikali na viongozi wake kwa maslahi mapana ya taifa kwa kuhofia rungu la adhabu za faini ama hata kunyimwa kabisa leseni ya kuendeshea vyombo hivyo kutoka kwa wenye mamlaka ya kufanya hivyo.

Ikiwa hali hii itaachwa iendelee tutarajie vyombo vyetu vya habari kuwa vipaza sauti tu vya watawala kufikisha ujumbe wao kwa watu wa chini badala ya kuwa majukwaa yenye kuibua hoja za kujenga taifa letu.

Ili kuepusha vyombo vya habari kuwa vipaza sauti vya watawala ipo haja kwa wadau wa habari kuoingana na viashiria hivi vya vitisho dhidi ya vyombo vya habari kwa maslahi ya taifa.