Saturday, 19 April 2014

UKAWA kuzunguka nchi nzima


Viongozi wa UKAWA wakizungumza na waandishi wa Habari miongoni mwa mikutano yao. (Picha sio halisi)

Na Nassor Khamis, Zanzibar.

MUUNGANO wa Vyama vinavyounda Umoja wa katiba ya Wananchi(UKAWA) ndani ya Bunge maalum la katiba  wamesema kumekuwa na juhudi zinazo fanywa ili kuleta maridhiano ila hawapo tayari kwa maridhiano hayo badala yake wanakusudia kuzunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi kile kinacho endelea kutokana na mchakato wa katiba mpya.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ambae pia ni Mwenyekiti wa umoja huo, Bw, Freeman Aikaeli Mbowe wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa hoteli Mansoun iliyopo Shangani Mjini Unguja.

Alisema kuwa ziara hiyo ya kuzungukza nchi nzima itaanza siku ya Jumatano kwa kufanya maandamano pamoja na mkutano wa hadhara katika viwanja vya Demokrasia Kibanda maiti mjini Unguja ukifuatiwa na mkutano mwengine Kisiwani Pemba siku ya Alkhamis.

Alisema kuwa wamefikia hatua hiyo kufuatia kuachwa kujadiliwa kwa rasimu ya pili ya katiba yenye muundo wa serikali tatu iliyobeba maoni ya Wananchi na badala yake kujadili rasimu inayopendekezwa na chama cha Mapinduzi inayotetea mfumo wa muundo wa serikali mbili jambo ambalo hawakubaliani nalo.

“UKAWA hatuwezi kuvumilia vitendo vya ukiukwaji wa sheria vinavyofanywa na CCM kwani katiba hii inayotafutwa ni ya wananchi sio ya chama cha Mapinduzi.”alieleza Mbowe.

Aidha amesema kuwa lengo la mikutano hiyo ni kuwaamsha wananchi wa Tanzania kudai haki yao ya msingi juu yakupatikana kwa katiba inayotokana na maoni yao waliyoyawasilisha kwa tume mabadiliko ya katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Warioba.

Aidha amelitaka jeshi la Polisi nchini kutoa haki ya kufanya mikutano hiyo kama wananvyo fanya kwa Katibu mkuu wa CCM Bw, Abdurrahman Kinana anvyozunguka nchi nzima kufa nya mikutano ya hadhara.

“Katibu mkuu wa CCM Abdurrahman Kinana akishirikiana na Nape Nauye pamoja na viongozi wengine wa CCM wamekuwa wakizunguka Nchi nzima kuhamasisha watu kukubaliana na mapendekezo ya CCM katika mchakato huu hivyo na sisi tupewe fursa hiyo.” Alisema Mh, Mbowe.

Akizungumza katika mkutano huo Mwenywkiti wa Chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Haruna Lipumba alieleza kuwa wajumbe wanaounda  umoja huo wameamua kutoka bungeni kutokana na kuchoshwa na kauli za ubaguzi miongoni mwa Watanzania wa matabaka mbalimbali jambo linaloharibu mustakbali mzuri wa upatikanaji wa katiba hiyo.

Alifahamisha  kuwa kumekuwa kukitolewa kauli za kibaguzi dhidi ya Watanzania watokao kisiwa cha Pemba pamoja na wananchi wenye asili ya kihindi na kiarabu pamoja na vitisho kwa wananchi pamoja na uchochezi wa kidini huku viongozi wa serikali wakishindwa kukemea vitendo hivyo jambo ambalo ni hatari kwa taifa.

Akizungumzia kitendo cha Kuzuiwa kwa mkutano wa hadhara wa UKAWA uliokuwa ufanyike April 19 mwaka huu Profesa Lipumba amesema hayo ni maagizo yliyotelewa na viongozi wakuu wa serikali kutoka Dar es salam akiwamo Waziri mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nae Mwenyekiti wa NCCR- MAGEUZI Bwana James Mbatia amewataka Wazanzibari wasikubali kutenganishwa kwa misingi ya udini na maeneo wanayotoka kama inavyoelezwa na baadhi ya viongozi wenye lengo la kuwagombanisha kwa maslahi yao.

Alisema kuwa kitendo cha Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri mkuu Sera na uratibu bwa Bunge kutoa kauli za kuanzishwa kwa dola ya kiislamu Zanzibar pamoja nav Jeshi kuchukua Nchi endapo utapitishwa mfumo wa srikali tatu ni kuchochea vurugu pamoja na kujenga khofu kwa Wananchi.

No comments:

Post a Comment