Sunday, 13 April 2014

Mvua yaleta kizaazaa

Jeshi la Polisi Kikosi cha Uokoaji jana kililazimika kutumia nguvu kuwaokoa wakazi wawili wa Jangwani waliokuwa wamezingirwa na maji, lakini wakigoma kuokolewa.PICHA|MAKTABA 

Dar es Salaam. Vifo, uharibifu wa mali, miundombinu na mafuriko, msongamano wa magari, baadhi ya wakazi wa jiji hilo kukimbia makazi yao, wengine kulala kwenye magari na nyumba za wageni vimewakumba wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku ya nne mfululizo.

Timu ya waandishi wa gazeti hili walifanya uchunguzi maeneo mbalimbali na kushuhudia hali halisi ilivyo, huku wanawake na watoto wakionekana kupata shida zaidi kwa kukaa nje ya nyumba zao, wengine kuhamia kwenye majengo ya shule.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam alisema jana kuwa walikuwa wakiendelea kukusanya taarifa za maafa ikiwamo vifo alivyosema ni vingi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadik alisema kuwa yupo kwenye kikao na watatoa taarifa zaidi za maafa baadaye.

Tegeta, Boko na Bunju

Mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minne, amefariki dunia baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kujaa maji na kushindwa kujiokoa kutokana na ulemavu, wakati mama yake akiwa kwenye shughuli za biashara.

Majirani wa mtoto huyo walisema tofauti na kawaida yao kumtoa mtoto huyo mvua inaponyesha, jana walimsahau na mama yake aliporejea alikuta maiti ya mtoto wake ikielea chumbani.
Katika mvua hizo takribani kaya 180 zimekumbwa na mafuriko huku wakazi wake wakijikuta hawana pa kwenda.

“Mimi nimekuwa hapa tangu Tanu imezaliwa, nyumba yangu imejaa maji nimeshazeeka sina mtu wa kunisaidia, wala sijui wapi nitakwenda. Nomba Serikali inisaidie,”alisema Hussein Ngaoma ambaye ni mjumbe wa nyumba kumi katika eneo hilo.

Naye Husna Ally ambaye pia nyumba yake imekumbwa na mafuriko alisema: “Nasikitika, maana nimepata hasara kubwa. Mimi ni mfanyabiashara katika eneo hili la Boko, nina duka la kuuzia samani limejaa maji na sijaweza kuokoa chochote. Mzigo wa Sh30 milioni umeharibika wote.”

Jeti Lumo

Katika eneo hilo licha ya kujaa maji, mfanyabiashara ndogondogo amefariki dunia kwa kusombwa na maji alipokuwa akijaribu kuokoa jiko lake la kuchomea mishikaki lililotumbukia kwenye mtaro.


Wakizungumza na gazeti hili wakazi wakazi wa eneo hilo walisema kuwa wakati mvua zilipoanza kunyesha, marehemu huyo waliyemtaja kwa jina moja la Ismail alikuwa akiendelea na kazi yake ya kuchoma nyama kando ya barabara, lakini baadaye maji yakafurika na kulisomba jiko lake, ndipo mtu huyo alipoingia kwenye mtaro huo ili alitoe, ndipo akasombwa na maji yaliyokuwa yakienda kwa kasi.

“Tulikuwa hapa na Ismail tunachoma nyama mvua ilikuwa inanyesha ghafla maji yakafurika na kubeba jiko, alipoingia mtaroni kulitoa maji yakamsomba. Nasikitika kuwa hatukuweza kumwokoa akapoteza maisha,” alisema Mwajuma Said.

Msasani na Mikocheni

Waandishi wetu walishuhudia eneo maarufu la ‘My fair plaza’ likiwa limezingirwa na maji huku wafanyakazi wakijitahidi kuyatoa maji, huku wakazi wa Msasani Bonde la Mpunga wakionenekana kuhangaika kuokoa vitu ndani ya nyumba zao, zilizoingiliwa na maji.

“Mvua ilianza kunyesha jana asubuhi, maji yakazidi kujaa kama unavyoona tunajitahidi kuokoa vinavyookoleka na tunahofia kupata magonjwa ya milipuko,” alisema mkazi wa eneo hilo Judith Peter.

Mkwajuni, Jangwani na Kigogo

Katika eneo la Jangwani watu walionekana wakiwa wamekimbia makazi yao huku wengine wakiokoa baadhi ya vyombo vyao huku magari ya Kampuni Barabara ya Strabag inayojenga barabara ya magari yaendayo kasi yakiwa yamefunikwa na maji na umati wa watu ulikiendelea kushangaa mafuriko.

Baadhi ya wakazi wa Bonde la Mto Msimbazi eneo la Vingunguti wamelazimika kugeuza shule kama makazi yao ya muda kwa hofu ya kukumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Gazeti hili lilifika kwenye Shule ya Msingi Mtakuja na kushuhudia wanawake, watoto na wanaume wachache wakiwa wamejikunyata kwenye baadhi ya vyumba vya madarasa ya shule hiyo waliyoyafanya makazi ya muda.

Mmoja wa wanawake hao, Amina Said alisema baada ya mvua kuanza kunyesha juzi jioni maji yalianza kutiririka na kujaa bondeni karibu na nyumba anayoishi hivyo akalazimika kumchukua mwanawe na kukimbilia shuleni hapo.

“Nilikuwa sina sehemu nyingine ya kukimbilia na mtoto hivyo shule na ndiyo ikawa mkombozi. Mafuriko yangetukuta tusingepona…tulilala kwenye haya madawati na mvua ikiendelea kunyesha tutaendelea kukaa hapa,” alisema Said.

Mama huyo alisema juzi usiku vyumba vyote saba vya madarasa ya shule hiyo vilikuwa vimejaa watu waliolazimika kuziacha nyumba zao na kwenda kulala shuleni hapo.


Huku wengine walilimbilia shuleni walioshindwa kufika nyumbani kutokana na barabara kufurika maji na kusababisha magari na hata bajaji kushindwa kutembea hao walilazimika kulala kwenye nyumba za wageni.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wahudumu katika nyumba ya kulala wageni ya New Kampala iliyopo eneo la Gongo mboto, Khalid Fikiri alisema walianza kupokea wageni kwa wingi majira ya saa nne na nusu usiku tofauti na ilivyo siku za kawaida.

“Kwa kawaida tunapokea wageni sita lakini juzi tulipokea wageni kumi na sita kutokana na kukwama njiani kwa sababu ya mvua”alibainisha Fikiri.

Alisema kutokana na kutambua uhitaji wa baadhi ya wageni waliokuwa wanaenda kuomba vyumba vya kulala kwa walikokuwa na fedha nusu pia waliwapa malazi.

“Tunatozaga 10,000 kwa chumba ila kwa waliokuwa na fedha pungufu hatukusita kuwasaidia,” alikiri Fikiri.

Naye Meneja wa nyumba kulala wageni ya Gladys Maxmillian Machango alisema alipokea wageni waliokuwa wamekwama na kushindwa kufika nyumbani kutokana na mvua.

Wawili wagoma kuokolewa

Jeshi la Polisi Kikosi cha Uokoaji jana kililazimika kutumia nguvu kuwaokoa wakazi wawili wa Jangwani waliokuwa wamezingirwa na maji, lakini wakigoma kuokolewa.

Katika tukio hilo lililovutia watu wengi, waokoaji walichukua takriban saa mbili kushawishi wazee hao mwanamke na mwanaume ili waokolewe, huku wakiendelea na shughuli zao wakati vikosi hivyo vikijaribu kuwatoa kwa kutumia mtumbwi.

Maofisa wa polisi waliokuwa katika eneo hilo walionyesha kukerwa na hali hiyo, huku wakiwa wamechanganyikiwa kwa kile kilechoelezwa kwamba wakitumia nguvu wazee hao wangeweza kujirusha katika maji yaliyokuwa yamejaa, yakienda kwa kasi hivyo kuhatarisha maisha.

=Imeandaliwa na Hilda Sigala, Suzan Mwilo, Herieth Makwetta, Ibrahim Yamola na Mpoki Bukuku
Kizaazaa

CHANZO: MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment