Na Othman Khamis Ame - OMPR
Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya
Mwaka 2012 inatarajia kuzindua Chapisho
la Tatu la Taarifa za msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi Tarehe 23
April mwak huu wa 2014 katika kusherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tannganyika
na Zanzibar.
Uzinduzi huo
unaotarajiwa kufanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya
Mrisho Kikwete utafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Mjini
Dar es salaam.
Taarifa ya
uzinduzi huo imefahamika ndani ya Kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2012 kilichofanyika chini ya Mwenyekiti Mwenza wa
Kamati hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye
ukumbi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa iliyopo Mjini Dodoma.
Akitoa
Taarifa ya Wizara ya Fedha ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Muigulu Nchemba alisema maandalizi ya
machapisho mengine 10 yanaendelea kufuatia kukamilika kwa zoezi la Sensa ya
Watu lililofanyika mwezi Oktoba mwaka 2012 Nchini kote Tanzania.
Mh. Nchemba
aliyataja baadhi ya machapisho hayo yatazingatia zaidi takwimu zilizokusanywa
na wataalamu wa Sensa zinazohusu Vizazi na ndoa, Elimu, Uhamiaji na Makazi
pamoja na hali ya ulemavu.
Alizipongeza
Taasisi na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa kupitia Walaamu wao kwa
kushirikiana na Wizara hiyo katika kufanikisha kazi ya Sensa licha ya
changamoto kubwa za upatikanaji wa fedha.
“
Tunawashukuru wadau wetu wa maendeleo ambao kwa kweli wametusaidia kutuunga
mkono katika zoezi hilo na zaidi ya Shilindi Bilioni Tatu {3,000,000,000 }
walizitenga kwa ajili ya kazi hiyo “. Alisema Mh. Muigulu Nchemba.
Akitoa
Taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi ya uhakiki wa Baadhi ya mipaka ya Wilaya
Tanzania Bara na Zanzibar kwenye Kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa yaTakwimu Tanzania Dr.
Albina Chua alisema zoezi la uhakiki huo tayari limeshafanyika kwa Wilaya za
Gairo na Chemba kwa Tanzania Bara na Wete na Micheweni kwa upande wa Zanzibar.
Dr. Albina
alisema uhakiki huo wa mipaka ya Wilaya na Halmashauri umekuja kufuatia
mapungufu yaliyojitokeza katika baadhi ya Wilaya hizo na kusababisha kuwemo kwa
matumizi ya mipaka zaidi ya mmoja.
Alisema
Utekelezaji wa kazi hiyo ulitokana na matokeo ya kazi ya awali iliyofanywa
katika Wilaya ya Gairo ambapo Kamati ya Taifa ya ushauri ya Sensa iliagiza kufanyika kama sampuli ya kujua tatizo la
utoaji wa mipaka ya kiutawala.
Naye
Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mohd Hafidh akitoa Taarifa
ya Utekelezaji wa Kazi hiyo ya uhakiki wa mipaka kwa upande wa Zanzibar alisema
kazi hiyo imeanza kwa kuundwa kwa Timu ya Maofisa watakaoshughulikia kazi hiyo.
Alisema kazi
hiyo iliyoanza Tarehe 8 Aprili mwaka huu inatyarajiwa kuchukuwa wiki mbili
katika Wilaya ya Wete na kuendelea katika Wilaya ya Micheweni lengo ni
kuziwezesha Taasisi husika kujua changamoto mbali mbali za mipaka ya Wilaya na
namna ya kuzitafutia ufumbuzi ili kuwa na Mipaka inayofanana.
Akitoa
shukrani zake kwa Wajumbe wa Kamati hiyo Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya
Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Sekreteri ya Kamati Kuu ya Taifa ya
Sensa kwa Kazi kubwa inayoendelea kuifanya tokea kumalizika kwa zoezi la Sensa
ya watu na Makazi Nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment