Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka Zanzibar
zinasema Sitta alikutana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein,
Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Rais Mstaafu, Aman
Karume na mwanasiasa wa siku nyingi wa CCM, Mzee Hassan Nassor Moyo.
Zanzibar kwa sasa ndiyo moyo wa upatikanaji wa
Katiba Mpya kutokana na wajumbe wake katika Bunge kutegemewa ama
kuipitisha au kuikwamisha kwa kuwa kila upande kati ya mbili
zinazovutana, hauna uhakika wa kupata theluthi mbili za kura.
Baada ya kuondoka bungeni na kutangaza kususia
vikao vya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu, siku mbili baadaye viongozi
wa Ukawa waliingia Zanzibar wakitaka kufanya mikutano ya hadhara
kuwaeleza wananchi sababu za kufanya hivyo, lakini wakazuiwa na polisi
na hadi jana walikuwa wanasubiri kibali.
Safari ya Sitta
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad pamoja
na kuthibitisha ziara ya Sitta Zanzibar kuwa alikuwa akutane na Dk
Shein, alisema hafahamu lolote kuhusu mkutano wake na Maalim Seif ambaye
pia ni Katibu Mkuu wa CUF.
“Sifahamu malengo ya safari wala walichokwenda
kuzungumza, ila ni kweli kwamba alifika Zanzibar leo (jana) na
alitarajiwa kuondoka jioni kurejea Dodoma,” alisema Hamad na kuongeza:
“Hilo la kuonana na Maalim Seif silifahamu ila
ninachojua aliniambia nimfanyie miadi ya kuonana na Dk Shein na
nikaifanya kama alivyoelekeza.”
Mapema habari zilizolifikia gazeti hili kutoka
Zanzibar zilisema, Sitta baada ya kukutana na Karume, Shein na Mzee Moyo
alitarajiwa kukutana na Maalim Seif saa 9:00 alasiri.
Katibu wa Maalim Seif, Issa Kheri Hussein
alithibitisha kwamba Sitta alikutana na kiongozi huyo nyumbani kwake,
Mbweni saa 9:30 alasiri jana, lakini alidai kutokuwa na taarifa za
mazungumzo hayo.
“Hilo naweza kulithibitisha kwamba mkutano huo
umefanyika lakini mazungumzo yenyewe yalikuwa ya faragha na mimi baada
ya Sitta kufika niliondoka, hivyo sikuweza kufahamu kilichozungumzwa kwa
undani, pengine mpaka nizungumze na Maalim mwenyewe,” alisema Hussein.
Ziara ya Sitta kwenda Zanzibar imekuja wakati
ambao kumekuwa na wasiwasi mkubwa wa kukwama kwa vikao vya Bunge hilo
kutokana na msimamo wa Ukawa.
Leo vikao vya Bunge hilo vinatarajiwa kuendelea mjini Dodoma
bila wajumbe wa Ukawa ambao viongozi wake wamesisitiza kwamba hawatarudi
hadi pale watakaporidhika kwamba kuna utashi wa kweli wa kuwezesha
kupatikana kwa Katiba Mpya.
Ukawa unaundwa na wajumbe wapatao 200 kutoka vyama
vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, NLD, DP na baadhi ya wajumbe kutoka
kundi la 201.
Viongozi wa Ukawa
Viongozi wa Ukawa kwa nyakati tofauti walisema
wamesikia kuhusu safari ya Sitta kwenda Zanzibar lakini hawakuwa na
taarifa za ndani kuhusu mazungumzo yake na Maalim Seif.
Hata hivyo, walisema hata kama amekwenda kwa lengo la kupata suluhu, hawezi kufanikiwa pasipo kuwashirikisha.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema: “Inawezekana kweli Sitta ataonana na Maalim Seif, lakini lazima
afahamu kwamba kurejea kwetu katika Bunge lazima uwe uamuzi wa chama
ambacho mimi ni mwenyekiti wake na Maalim ni Katibu Mkuu.”
“Kwa hiyo uamuzi wetu wa kuondoka pale bungeni
ulikuwa ni uamuzi wa kichama, maana mimi kama mwenyekiti wa CUF niko
katika Bunge hilo na tulishauriana na wabunge pamoja na wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi lakini zaidi ya hapo tuna makubaliano na wenzetu
katika Ukawa,” alisema.
Alisema Ukawa wataweza kurejea katika Bunge kwa
sharti moja kubwa kwamba lazima rasimu itakayojadiliwa iwe ni ile
inayotokana na kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji
Joseph Warioba.
“Kinachoonekana pale bungeni ni kwamba wapo watu
wanataka kutushirikisha sisi tujadili rasimu yao wanayotaka kuileta kwa
njia wanazozijua wao, hilo hatutalikubali, kwa hiyo mazungumzo yoyote
lazima yawe na lengo,” alisema.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye pia ni
mjumbe katika Bunge hilo alisema: “Sisi msimamo wetu uko wazi, kwa
sababu CCM wameonyesha msimamo mkali kuhusu kile wanachokitaka, wanataka
kutumia wingi wao basi tumewaachia waendelee kwani tatizo liko wapi?
Mimi sioni kwa nini wanahangaika wakati uwezo wa kupitisha Katiba
wanayoitaka wanao.”
Aliungana na Profesa Lipumba kwamba hakuna
maridhiano yatakayofanywa nje ya Ukawa na kwamba hata kama Sitta
amekutana na Maalim Seif, tayari walishakubaliana kuwa na msimamo wa
pamoja katika suala hilo la Katiba.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia mbali na
kusema amesikia kuhusu ziara ya Sitta Zanzibar, alisisitiza kwamba
utashi wa kisiasa ndiyo utakaoiokoa Katiba Mpya.
Imeandikwa na Neville Meena, Edwin Mujwahuzi, Sharon Sauwa na Ibrahim Bakari, Dodoma.
CHANZO: MWANANCHI.
Imeandikwa na Neville Meena, Edwin Mujwahuzi, Sharon Sauwa na Ibrahim Bakari, Dodoma.
CHANZO: MWANANCHI.