Tuesday, 2 September 2014

Mgomo wa wafanyabiashara watikisa Kariakoo

Baadhi ya maduka Kariakoo yakiwa yamefungwa baada ya maofisa wa TRA kuanza uhakiki wa watumiaji wa mashine za risiti za kielektroniki (EFD) jijini Dar es Salaam.
WAFANYABIASHARA wa maduka ya soko la Kariakoo wameanza mgomo kwa muda usiojulikana kuanzia jana, sambamba na kuishinikiza Serikali kupunguza kodi ya asilimia 18 wanayotozwa kupitia mashine za kielektroniki (EFDs).

Wamefikia hatua hiyo ikiwa ni siku moja baada ya TRA kutangaza kufanya ukaguzi endelevu na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wale watakaokaidi kutumia mashine hizo.

Wakizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao walisema kuwa walifikia hatua ya kufunga maduka ili kupinga makato ya kodi kubwa inayowakosesha maslahi.

Mmoja wa wamiliki wa duka la nguo, Kibatala Kimweli, alisema ameamua kufunga duka ili asifanyiwe uhakiki na TRA, kwani tangu ameanza kutumia mashine hizo amebaini kupata hasara inayotokana na kukatwa kodi ya asilimia 18.

“Kilio chetu tunataka punguzo la kodi kwani ikiwa kubwa faida inakuwa ndogo, ndiyo maana mnaona hali hii ya mgomo inaendelea, kama walivyosema ni zoezi endelevu na sisi tutafunga maduka bila kuacha halafu tuone watatoa wapi kodi na nani atatumia mashine zao,” alisema.

Kimweli alitaja sababu nyingine za kufunga maduka hayo kuwa ni kutopatiwa elimu ya kutosha wafanyabiashara wengi, kama ilivyokuwa imeamuliwa na Rais Jakaya Kikwete Aprili 22, mwaka huu.

Naye Halima Bakary, alidai kuwa mfumo unaotumiwa na Serikali unawatoza kodi kubwa, hali inayowafanya wafanyabiashara wengi kukwepa na kutumia njia nyingine zisizokubalika.

Akizungumzia kuhusu mgomo huo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alisema kwamba wao wataendelea kusimamia sheria kuhakikisha kila mfanyabiashara anatumia mashine hizo kwa ajili ya kulipa kodi.

“Sheria tunazozitumia zimetungwa na wabunge ambao ndio wanawawakilisha wafanyabiashara hao, hivyo suala la kusimamia sheria lipo mikononi mwa TRA na hawatakuwa tayari kusimamisha uhakiki wa mashine hizo kwa wafanyabiashara wadanganyifu na wale wasiozitumia kabisa, lazima watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.

Kayombo aliongeza kuwa wafanyabiashara hao wameanza mgomo baada ya hivi karibuni kufanyika kwa ukaguzi wa kila duka na kubaini kuwapo kwa baadhi yao wanaotumia mashine ambazo hazijasajiliwa TRA, ikiwamo na wengine wasiozitumia.

Alisema kuwa wamebaini uwapo wa baadhi ya wafanyabiashara wasiotoa risiti halali kulingana na thamani ya bei ya bidhaa wanazouza.

Kayombo alisema TRA itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wanaoshawishi wenzao kufunga maduka na kuacha kutumia mashine za EFD’s, kwani hadi sasa tayari baadhi yao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.

Aliongeza kuwa katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam maduka 70 yalibainika kutotumia stakabadhi, na kati yao 11 yamefungiwa.

MTANZANIA.

Ndege ya Kenya yaanguka Tanzania



Masalia ya ndege ya Kampuni ya Safari Express Limited iliyoanguka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuua watu watatu jana
Ndege ya Kampuni ya Safari Express Limited imeanguka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuwateketeza watu watatu waliokuwamo ndani.

Ndege hiyo yenye namba za usajili 5Y-SXP iliruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza Jumapili saa 1:26 usiku ikielekea Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Kenya ambako ilitakiwa kutua saa 2:36 usiku.

Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete alikiri ndege hiyo kuanguka kwenye hifadhi hiyo na walikuwa katika harakati za kuitafuta.

Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege nchini, kutoka Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, David Nyamwihura alisema ajali hiyo ilitokea takriban maili 20 kutoka Serengeti, katika eneo la Kogatembe na watu wote watatu waliokuwamo wamefariki dunia.

Meneja wa Udhibiti wa JKIA, Clever Davor aliliambia gazeti la Daily Nation la Kenya kuwa ndege hiyo ilipoteza mawasiliano na rada ya uwanja huo ikiwa imeruka angani urefu wa futi 14,000.

Awali, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KCAA) ilitoa taarifa juu ya kuchelewa kwa ndege hiyo iliyokuwa ikitarajiwa kutua katika uwanja wa JKIA saa 2 usiku.

Jana asubuhi, Kamanda wa Viwanja vya Ndege wa Kenya (KAPU), Joseph Ole Tito alithibitisha kupotea kwa ndege hiyo kabla ya kuonekana baadaye katika Hifadhi ya Serengeti.

Polisi wa Kenya hawakueleza ndege hiyo ya mizigo aina ya Fokker F-27-500 ilikuja nchini kwa shughuli gani.

Ndege zote zinazotoka Kenya kwenda nchi za jirani, huanzia safari zake katika viwanja vya JKIA, Wilson au Wajir ili kuwa na usimamizi wa karibu.

MWANANCHI.

Monday, 1 September 2014

Sheikh Ponda aiangukia mahakama

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda.
KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameiangukia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa kuiomba itumie busara kusimamisha kesi ya uchochezi inayomkabili mkoani Morogoro.

Maombi hayo yaliyokwama mara kadhaa kutokana na sababu za kisheria, yaliwasilishwa jana kupitia wakili wake, Juma Nassoro, wakati rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtia hatiani kwa kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chang’ombe Markaz na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja nje, ikisikilizwa.

Wakili Nassoro akiwasilisha maombi hayo mbele ya Jaji Augustine Shangwa, aliiomba mahakama hiyo isimamishe kesi ya uchochezi inayomkabili Ponda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, hadi itakapotoa uamuzi wa rufaa hiyo.

“Mheshimiwa jaji endapo Mahakama ya Morogoro ikimtia hatiani Ponda na kumhukumu wakati Mahakama Kuu ikikubali hoja zake za rufaa na kutengua hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itaishushia hadhi mahakama.

“Mahakama ikisimamisha kesi ya Morogoro, upande wa Jamhuri hautaathirika kwa kuwa ndio waliofungua kesi, naomba mahakama yako tukufu itumie busara kusimamisha kesi hiyo,” alidai Nassoro.

Katika rufaa hiyo, Ponda anadai hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

Ponda na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh milioni 59.6 na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali eneo la ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd na uchochezi.

Katika hukumu iliyotolewa Mei 9, 2013, Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa wa Mahakama ya Kisutu alimtia hatiani Ponda peke yake kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo la Agritanza Ltd, na ikawaachia huru washtakiwa wengine wote.

Jaji Shangwa aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10, mwaka huu kwa ajili ya upande wa Jamhuri kujibu hoja za Sheikh Ponda.

MTANZANIA.

Ujerumani yajitosa Katiba mpya

Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke
UBALOZI wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani nchini umejitosa katika mjadala wa Bunge la Katiba mpya linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma.

Pamoja na hali hiyo, Ujerumani imekanusha kuhusika kusaidia kikundi chochote nchini kinachojihusisha na masuala ya siasa, ikiwamo suala la Katiba.

Tamko kwa vyombo vya habari lililotolewa jana na Ofisa Mawasiliano wa Ubalozi wa Ujerumani, John Merikion, limesema Serikali ya Ujerumani kimaadili haiingilii mambo ya siasa za ndani za nchi nyingine.

Tamko hilo limekuja baada ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Agustino Matefu, mwishoni mwa mwezi uliopita kuzituhumu baadhi ya nchi za Ulaya na Asia, ikiwamo Ujerumani kuwa zinafadhili Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukwamisha mchakato wa Katiba mpya.

Matefu, ambaye ni Mwenyekiti wa Kundi la Tanzania Kwanza, nje ya Bunge, alidai kuwa nchi za Uholanzi, Oman na Ujerumani zinahusika na mpango huo kwa kuzitumia taasisi zake za ndani ya nchi.

Kutokana na kauli hiyo, Merikion alisisitiza kuwa Serikali ya Ujerumani na maofisa wake hawafanyi ushawishi wowote kuhusu mwelekeo wa mjadala wa Katiba unaoendelea hivi sasa nchini.

“Kutokana na habari za mara kwa mara katika vyombo vya habari nchini Tanzania, Ubalozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani unatamka kwamba Serikali ya Ujerumani kimaadili haiingilii mambo ya siasa za ndani za nchi nyingine.

“Kwa hali hii, Serikali ya Ujerumani na maofisa wake hawafanyi ushawishi wowote kuhusu mwelekeo wa mjadala wa Katiba unaoendelea hivi sasa nchini Tanzania,” ilisema taarifa hiyo ya Ubalozi wa Ujerumani.

Tamko hilo lilizidi kusisitiza kuwa mashirika mengi ya Kijerumani yanafanya kazi na mawakala wa asasi za kiraia duniani kote ili kuimarisha shughuli za mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, aina hiyo ya shughuli za ushirikiano hufanyika pia nchini Tanzania, zikilenga katika mipango ya elimu na mafunzo ambapo utaratibu huo hutolewa kwa wawakilishi wa vyama vyote vikubwa vya siasa nchini.

“Shughuli za kisiasa huwa hazisaidiwi au kufadhiliwa na mashirika haya ambayo hutenda kazi zake kwa kutumia pesa zinazotolewa na Serikali ya Ujerumani,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa ubalozi huo kuzungumzia masuala yanayohusu mchakato wa Katiba mpya unaoendelea nchini.

Tangu Aprili 16, mwaka huu, baada ya Ukawa kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, kumekuwa na madai kadhaa, yakiwamo ya kuwahusisha viongozi wa umoja huo kukwamisha mchakato wa Katiba kutokana na fedha wanazopewa kutoka nchi za Ulaya.

Awali Matefu alidai kuwa taasisi hizo zimekuwa zikifadhili shughuli mbalimbali za Ukawa, ikiwamo kutoa fedha ambazo zimekuwa zikiingizwa katika akaunti binafsi za viongozi wa umoja huo.

Matefu alidai katika kukamilisha mpango huo, Freeman Mbowe na Dk. Willibrod Slaa wamepewa fedha hizo kupitia akaunti zao binafsi kiasi cha Sh 1,700,000 katika awamu ya kwanza, huku awamu ya pili na tatu jumla ikiwa ni dola 850,000.

Mbali na hao, alidai CUF kupitia Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, kupitia akaunti yake binafsi amepokea kiasi cha dola za Marekani 400,000 kutoka Oman.

MTANZANIA.

Waraka wa makanisa kusambazwa hadi jumuiya

Msalaba
Iringa. Waraka uliotolewa juzi na Jukwaa la Wakristo Tanzania wakitaka mchakato wa Katiba Mpya usitishwe, jana ulisomwa katika baadhi ya makanisa na sasa utasambazwa katika jumuiya ndogo za Kanisa Katoliki.

Akizungumzia waraka huo katika Ibada ya Jumapili, Paroko wa Parokia ya Mkwawa ya Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa, Padri Oscar Rutechura alisema amechukua uamuzi huo ili kuwawezesha waumini kuelewa vizuri tamko la viongozi wao wa dini kuhusu mchakato wa katiba unaoendelea.

“Katika ibada hii ya leo nitatoa mahubiri kwa muda mfupi, nitafanya hivyo ili niweze kufanya mambo mengi yaliyoko mbele yangu,” alisema Padri Rutechura kabla ya kusoma waraka huo.

Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).

Padri Rutechura alitaja mapendekezo sita yaliyomo kwenye waraka huo ambayo ni: Kuitaka Serikali irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kulitaka Bunge kuboresha maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba na kuacha kuyadharau na kuyapuuza.

Mengine ni kutaka mchakato wa Katiba usitishwe, Bunge la Katiba liendeshwe kwa mujibu wa kanuni, wananchi waendelee kusoma na kufuatilia mchakato na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihusishwe na kupewa mamlaka ya kujibu maswali yanayojitokeza.

Padri Rutechura alisisitiza kuwa ametumiwa waraka huo na Askofu wa Jimbo la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye kwa sasa ndiye Rais TEC kwa ajili ya kuusoma kwa waumini wote.

Alisema baada ya kuusoma angetoa nakala na kuzigawa kwa viongozi wa jumuiya ndogondogo ili waumini wote wa parokia hiyo wapate fursa ya kuusoma na kuuelewa na watoe uamuzi sahihi.

Padri Rutechura aliwataka waumini kuhakikisha wanajiandikisha kwa wingi kwenye daftari la kudumu la wapigakura pindi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itakapotangaza kuanza kuandikisha upya wapigakura.

Alisema hatua hiyo itawasaidia waumini hao kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupiga kura ya maoni kupata Katiba Mpya au kuipinga, kuchagua viongozi wanaofaa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Wakati huohuo, polisi wilaya mpya ya kipolisi, Mbalizi mkoani Mbeya wamewakamata waumini 16 wa Kanisa la Katoliki, Parokia ya Songwe kwa madai ya kutaka kufanya vurugu kwenye kanisa lao.
Paroko wa Parokia hiyo, Ernest Mwashiuya alisema waumini hao walikamatwa jana na kwamba taarifa zaidi zitatolewa na polisi.

Baadhi ya waliokamatwa walisema tukio hilo lilitokea Jumamosi saa 12 jioni wakati wanajadili sehemu ya kusalia ibada ya Jumapili baada ya kutokuwa na imani na paroko wao. Walisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Paroko Mwashiuya, Jumapili ya Agosti 24 kutamka kwamba waumini wasio na imani naye wasifike kanisani hapo tena.

“Polisi walifika nyumbani kwa Emmanuel Kalomba tulikokuwa tukisali na kutukamata,” alisema mmoja wa waumini waliokamatwa na kuachiwa kwa dhamana.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi alisema hakuwa na taarifa.

Waraka wenyewe huu hapa.


JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA

TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA 

Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es salaam , tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:

Tunaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya Maoni ya WANANCHI kuhusu mabadiliko hayo na kutuletea Rasimu yenye maoni mengi ya Watanzania bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsi na kabila. Pia tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama Randama, Nyaraka zenye maoni ya wananchi, picha, tafiti mbalimbali na hata orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni katika Tume.

Tume pia iliweza kuandaa Tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za Tume na Maoni yote yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume iliandaa Rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya WANANCHI. Tume imedhihirisha kuwa, ilitenda KIZALENDO na, kwa mantiki hiyo, wajumbe wote bila kujali vyama vyao, dini zao na upande wa Muungano walikotoka, waliweza kujadili kwa uwazi na kweli na mwisho wakaridhiana katika kila Ibara iliyopendekezwa. Hili linatufundisha kuwa Katiba ni MARIDHIANO na si jambo la maslahi ya kisiasa, bali ni suala la maslahi ya WANANCHI.

Tunaamini kuwa kila Mjumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya WANANCHI aliheshimu kiapo chake na hivyo kufanya kazi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hili. Baada ya Tume kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao kweli kwa uovu” (Warumi 1:18).

Katika mijadala ya Bunge Maalum la Katiba (BMK) yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya maslahi kwa WANANCHI, na ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa yanadhihirisha hili: Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa bila sababu za msingi kutolewa wakati mchakato unaendelea.

Hali hii imefanya zile nyaraka na kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa. Kwa sababu hiyo, tumeona Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha takwimu na taarifa mbalimbali ambazo WANANCHI hawawezi kuzipata kwa ajili ya kuoanisha baina ya kinachojadiliwa Bungeni na kilichomo katika Rasimu na viambatanisho vyake vyote.

Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na kwa maslahi ya nani? Bunge la Katiba limeshindwa kusimamia Kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na kuridhiwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Kushindwa huku kusimamia kanuni kumesababisha vurugu ndani ya Bunge Maalumu na kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata Katiba bora ya nchi yetu.

Matumizi ya ubabe na wingi wa Wabunge wa Chama Tawala (CCM), badala ya Kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na Chama Tawala dhidi ya maslahi ya WANANCHI. Mijadala katika Bunge Maalumu la Katiba imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume.

Hali hii imelifanya Bunge Maalumu la Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza heshima na hadhi yake. Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa KATIBA NI MATOKEO YA TENDO LA MARIDHIANO NA SI SUALA LA MASLAHI YA KIKUNDI CHA WATU WACHACHE.

Hatua iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa BMK unaoendelea umeondoa kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge, ukomo wa ubunge, n.k., na kuwezesha maoni na maslahi ya Chama Tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia ya kulinda maslahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora. Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo;

1. Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya Katiba kwa uwazi.

2. Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa na Chama Tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na sio kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.

3. Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano muafaka, uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977 yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda Rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba.

 4. Kwamba baada ya Bunge Maalum la Katiba kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi katika Bunge la Katiba.

5. Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko katika Rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.

 6. Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba Mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.

Jukwaa la Wakristo Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba AMANI ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya. Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya mshikamano, umoja na amani ya Taifa letu.

Ifahamike kuwa WANANCHI wa Tanzania wako juu ya Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe WANANCHI wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa tu Chama hicho kimeyapuuza na kimekataa Maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi. “Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao.

Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutabakari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenyekuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”.

(Rejea Warumi 1: 28-32) IKUMBUKWE KUWA RASIMU YA PILI YA KATIBA NI WARAKA HALALI NA RASMI NA NDIYO MAWAZO YA WATANZANIA NA TUNAHIMIZA KUWA KATIBA NI YA WANANCHI NA INAHITAJI MARIDHIANO NA SIO UBABE. Imetolewa leo Agosti 28, 2014 Na MKUTANO WA JUKWAA LA WAKRISTO Tanzania Episcopal Conference (TEC) The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT) Christian Council of Tanzania (CCT) The Seventh Day Adventists (SDA)

CUF kuandamana siku tatu kupinga Bunge la Katiba

Makamu mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji akoinyesha waraka wa siri wa CCM unaodaiwa kuandaliwa kwa ajili ya Rasimu ya Katiba inayojadiliwa Dodoma, alipokuwa akifungua kongamano la wanachama wa chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kitafanya maandamano ya siku tatu za kazi kupinga kuendelea kufanyika kwa vikao vya Bunge la Katiba ambayo yatafanyika katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.

Maandamano hayo ni mwendelezo wa hatua ambazo zimekwishachukuliwa na chama hicho pamoja na vyama vingine vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Aprili 16, mwaka huu, wajumbe kutoka vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi vinavyounda Ukawa walitoka nje ya Bunge wakidai kuchakachuliwa kwa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko la Katiba.

Jana, uongozi wa CUF uliitisha kongamano la wanachama wake ili kuwauliza nini kifanyike baada ya wajumbe wa chama hicho kutoka nje ya Bunge lakini chombo hicho kikapuuza madai yao.

Kongamano hilo lilifunguliwa na makamu mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji ambaye aliongoza kongamano hilo hadi maazimio hayo yalipotolewa.

Akisoma maazimio ya wanachama baada ya kutoa maoni yao, ofisa uchaguzi wa CUF, Abdulrahman Lugone alisema wanachama wengi wameazimia maandamano yafanyike kwa siku tatu katika Mkoa wa Dodoma na yaishie katika majengo ya Bunge.

“Tunataka maandamano haya yafanyike katika siku za kazi ili kupeleka ujumbe mzito kwa jamii kwamba maoni yao ndiyo msingi mkuu wa Katiba,” alisema katika kongamano hilo lililofanyika katika makao makuu ya chama hicho Buguruni wilayani Ilala.

Alisema pia maandamano hayo yatafanyika siku hiyo hiyo mkoani Dar es Salaam na kuishia kwenye ofisi ndogo za Bunge ambako kuna ofisi nyingi za Serikali.

“Tunaomba wafanyakazi na wananchi wanaopinga kuendelea kufanyika kwa vikao vya Bunge hilo watuunge mkono kwa kushiriki katika maandamano haya,” alisema.

Lugone alisema vyama vingine vinavyounda Ukawa vinaombwa siku za maandamano zitakapotangazwa kusitisha shughuli zao ili wafuasi wake waweze kushiriki kwenye maandamano hayo.

Alisema makao makuu ya chama hicho yanaratibu maandamano hayo na kwamba wafuasi wa chama hicho watatangaziwa tarehe ya kufanyika. Wakati kongamano hilo linaendelea makao makuu ya CYF, nje ya uzio kulikuwa na polisi zaidi ya 25 waliokuwa kwenye magari matatu ambao walifika kuanzia saa 5.00 asubuhi na kuondoka saa 7.30 mchana baada ya kumalizika kwa kongamano hilo.

Akifungua kongamano hilo, Duni ambaye pia ni Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, alisema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ameonyesha udhaifu mkubwa katika kukiongoza chombo hicho.

Alisema udhaifu aliouonyesha katika kusimamia kanuni katika Bunge hilo ni kielelezo kwamba hana uwezo wa kuwa rais, licha ya kuonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo.

Sitta amekuwa akitajwa kuwania nafasi ya urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015.

Alisema udhaifu huo ni pamoja na kumpa nafasi Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuzungumza kabla ya Rais Jakaya Kikwete katika ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba.

“Alitakiwa kuzungumza kwanza Rais Kikwete ndipo Jaji Warioba angekuwa wa mwisho kutoa hutuba yake lakini Sitta alichakachua, tunasikitika tulimpa kura nyingi katika uchaguzi wa kuliongoza Bunge hilo kwa kufuata rekodi za nyuma, lakini ameshindwa kusimamia kanuni,” alisema Duni.

Akizungumzia mfumo wa serikali tatu, alisema mfumo huo hauwezi kupingwa kwa sababu hayo ni maoni ya wananchi.

“Ikumbukwe kwamba Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza Serikali tatu, Tume ya Jaji Kisanga pia ilipendekeza serikali tatu na Tume ya Warioba imetoa maoni ya wananchi waliopendekeza serikali tatu, hao CCM ni akina nani wanaokataa maoni ya wananchi,” alihoji Duni.

MWANANCHI

Ukawa wamgomea Kikwete

Rais Jakaya Kikwete akiagana na Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa (wa tatu kushoto) baada ya mkutano wa vyama vya siasa vyenye wabunge mjini Dodoma jana, Wengine kutoka kushoto ni Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, John Cheyo wa UDP na Phillip Mangula wa CCM. Picha  na Ikulu.
Dodoma. Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana waligoma mbele ya Rais Jakaya Kikwete kuruhusu wajumbe wao kurejea katika Bunge Maalumu la Katiba, walipokutana katika kikao cha kusaka suluhu ya mkwamo wa mchakato wa Katiba.

Mkutano wa jana ulikuwa na sehemu mbili kuu, wa kwanza ulifanyika katika Ikulu ya Kilimani, Dodoma ambako viongozi hao walikutana na Rais Kikwete na mwingine katika Hoteli ya St. Gasper ambao uliwashirikisha viongozi na maofisa wa vyama vilivyoshiriki bila Rais Kikwete.

Mkutano huo ni matunda ya jitihada zinazofanywa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambacho kiliratibu mazungumzo hayo yaliyochukua zaidi ya saa mbili na nusu, katika Ikulu ya Kilimani, wakati yale ya St. Gaspar yalichukua takriban saa moja na nusu.

Viongozi walioshiriki kikao hicho cha Ikulu ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Magdalena Sakaya.

Wengine ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Katibu Mkuu wake, Mosena Nyambabe, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, Mwenyekiti wa UDP ambaye pia ndiye mwenye zamu ya uenyekiti wa TCD, John Cheyo na Mwenyekiti wa UPDP pamoja na mwakilishi wa vyama visivyokuwa na wabunge ndani ya TCD, Fahmi Dovutwa.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Rais Kikwete baada ya kuanza kwa kikao hicho alitoa fursa kwa kila aliyekuwapo kuzungumza na hapo zilijitokeza hoja mbalimbali, nyingi mwelekeo wake ukiwa ni kutaka kusitishwa kwa Bunge Maalumu ili kutoa fursa kwa nchi kuendelea na masuala mengine makubwa.

Chanzo chetu kilisema: “Rais amekuwa msikivu kweli, amewasikiliza wote lakini ugumu ulianza kuonekana pale ilipotolewa kauli ya kuwauliza wale watu wa Ukawa kama wanaonaje wakirejea halafu hoja zao zikazungumzwa ndani ya Bunge Maalumu, yaani hawataki kabisa kusikia hilo.”

Kuhusu hoja ya kusitishwa kwa Bunge, habari zinasema ilijadiliwa kwa kirefu na wataalamu wa sheria wakijaribu kutoa uzoefu wao, lakini kikwazo kilichoonekana ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo haimpi Rais mamlaka ya kusitisha Bunge.

“Rais alisema hoja zao ni nzuri na zina mashiko, lakini suala kubwa likawa ni kwamba tunafikaje huko wanakopendekeza? Maana sheria iko kimya kuhusu mamlaka ya Rais kusitisha Bunge Maalumu, ndiyo maana sasa tulitoka Ikulu tukaenda St. Gaspar ili kujadili, ngoja tusubiri hiyo tarehe 8 maana siyo mbali,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.

Kauli ya TCD 
Baada ya kikao cha St. Gasper, Mwenyekiti wa TCD, Cheyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba mazungumzo na Rais Kikwete yalikuwa mazuri na kwamba wamekubaliana kukutana naye tena Septemba 8, mwaka huu baada ya kuwa wamezifanyia kazi hoja ambazo zilijitokeza kwenye vikao hivyo.

“Kama nilivyowaambia siku ile tulipokutana, tulikuwa na ajenda mbili tu kubwa, kwanza ni mchakato wa Katiba Mpya unavyokwenda na ajenda ya pili ni jinsi tunavyoweza kusonga mbele na kuwa na maandalizi ya uchaguzi mzuri mwakani,” alisema Cheyo lakini akikataa kujibu maswali mengine ya waandishi wa habari.

Cheyo alisema baada ya kukutana na Rais Kikwete, waliendelea na kikao cha viongozi wa vyama kwa ajili ya kuona jinsi ya kuyafanyia kazi mambo yaliyojitokeza, hivyo wameamua kuunda kamati ndogo ya watu wanne itakayoongozwa na Mbatia kwa ajili ya kutekeleza wajibu huo.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Kinana, Profesa Lipumba na Dk Slaa ambao wamepewa wajibu wa kuwasilisha ripoti yao kwenye kikao cha wenyeviti wa vyama vinavyounda TCD ili ijadiliwe kabla ya kikao cha Septemba 8, ambacho hata hivyo, hakijafahamika kitafanyika wapi.

Habari zinasema miongoni mwa mambo yatakayofanyiwa kazi ni pamoja na kuona kama Bunge linaweza kusitishwa bila kuleta athari zozote za kisheria na kisiasa, lakini wakizingatia uwapo wa makundi mengine ndani ya Bunge hilo hasa wabunge wa kuteuliwa kupitia kundi la 201.

“Lakini hapa kuna suala moja kwamba Ukawa wako nje ya Bunge, ni vigumu kuwaamrisha wale walioko ndani ya Bunge ili watekeleze matakwa yao, kwa hiyo kuna kazi kubwa sana ya kufanya,” kilisema chanzo chetu.

Mgomo wa Ukawa 
Dalili za Ukawa kukataa kurejea bungeni zilianza kuonekana mapema baada ya mazungumzo yasiyo rasmi ambayo yalifanyika katika moja ya kumbi za Hoteli ya Dodoma ambako walikwenda kupata chai baada ya kuwasili.

Wakati wakitoka kwenye ukumbi huo kuelekea Ikulu Kilimani, baadhi yao walisikika wakipeana tahadhari kwamba wasikubali wazo la kurejea bungeni, ambalo ni dhahiri walikuwa wamepewa wakati wakinywa chai.

Baadaye ndani ya basi dogo wakati wakielekea Ikulu, Lissu alisikika akisema: “Eti wanataka turejee, yaani tumekaa nje muda wote huo halafu leo hii tuje hapa kujadili kurudi, eti kurudi haiwezekani kabisa.”

Pia habari kutoka katika Ukumbi wa St. Gaspar zinasema hata katika kikao hicho, viongozi hao walishauriwa kurejea bungeni ili hoja za kuahirishwa kwa Bunge Maalumu zitolewe huko, lakini waligoma.

Taarifa zinasema Ukawa walijenga hoja kwamba Bunge Maalumu halipaswi kuendelea kwa sababu kuna kila dalili kuwa muda uliopo hautoshi kukamilisha mchakato na ikizingatiwa kwamba nchi inakabiliwa na mambo mengi ukiwamo Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Pia kulikuwa na hoja kuhusu mambo ya Daftari la Wapigakura na mabadiliko ya sheria ambazo zinagusa taasisi kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi, sheria mbalimbali zinazihusu vyama vya siasa na mambo ya matokeo ya rais kuhojiwa nadhani,” kilieleza chanzo kingine.

Kushindwa kupatikana kwa suluhu ya mchakato wa Katiba, kunaendelea kuuweka mchakato huo njiapanda hasa ikizingatiwa kwamba Bunge Maalumu linaendelea kesho kupokea ripoti za kamati kuhusu uchambuzi wa sura 15 za Rasimu ya Katiba.

Nukuu
“Eti wanataka turejee, yaani tumekaa nje muda wote huo halafu leo hii tuje hapa kujadili kurudi, eti kurudi haiwezekani kabisa.” Lissu