Wengi wamekuwa wakieleza kuwa kero zipo lukuki katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umetimiza miaka 50 sasa.
Kero hizo zimetumika kama kete ya kutetea muundo
unaofaa wa Muungano ingawa mjadala sasa umehamia kwenye serikali mbili
au tatu.
Hata hivyo, katika kero hizo, zipo ambazo zimeanza kupatiwa ufumbuzi na zipo ambazo zimeibuka upya tena kwa kasi.
Miongoni mwa kero ambazo ni ngeni kwa wengi, ni
kutokujulikana zilipopelekwa fedha za Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya
Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB) iliyonjika mwaka 1965.
Kero hiyo, ilikuwa ikizungumzwa chini chini na
baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na hata
wanasiasa wa pande zote mbili za Muungano.
Kutokana na watu wengi kuhoji, fedha hizo, wakati
wa uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Rais Jakaya
Kikwete naye alizungumzia kero hiyo na kuahidi kuwa itafanyiwa kazi.
Hata hivyo, ili kupata maelezo ya kina juu ya kero
hii, gazeti hili linazungumza na Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), Edwin Mtei, ambaye pia aliyekuwa Waziri wa Fedha kati ya
mwaka 1978 hadi 1981.
Mtei, ambaye pia aliwahi kuwa katibu mkuu wa
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) na ameshika nafasi mbalimbali
katika jumuiya hiyo kabla ya kuvunjika, anaeleza historia ya akiba hiyo
ya Zanzibar na wapi ilipo.
Anasema ni kweli kuwa baada ya kuvunjika kwa EACB mwaka 1965, Zanzibar ilikuwa na akiba ya fedha zake katika bodi hiyo.
Anasema Zanzibar ilikuwa na kiasi cha fedha kama
asilimia 4, huku Kenya, Uganda na Tanzania (Bara) zikiwa na kiasi
kikubwa cha fedha.
Je, zipo wapi fedha za Zanzibar?
Mwanasiasa huyo anasema fedha hizo baada ya kuvunjika kwa bodi
hiyo, fedha hazipo tena na anashangazwa na watu wanaoibuka leo na kudai
sasa kana kwamba bado zipo BoT.
Anasema anakumbuka wakati huo, mara baada ya
kuvunjika kwa bodi hiyo, ulifanyika mgawanyo wa fedha katika hazina za
nchi hizo kuanzisha benki kuu.
Anasema fedha za Tanzania Bara zilifanya kazi
mbalimbali na zile za Zanzibar ziliingizwa katika kazi ya kuanzishwa
kwa tawi la BoT Zanzibar kwani wakati huo kulikuwa na tawi moja
lililokuwa Dar es Salaam.
“Nakumbuka fedha za Zanzibar tulitumia katika
ujenzi wa BoT, tawi la Zanzibar, ujenzi ambao ulikuwa na gharama kubwa
ukihusisha kujengwa kwa eneo maalumu la kuhifadhi fedha hizo,” anasema
Mtei.
Anaongeza kuwa kabla ya hapo, Zanzibar ilikuwa
haina tawi la Benki Kuu hivyo, fedha hizo ndizo zilitumika kuanzishwa
tawi la kwanza.
“Ni kweli kulikuwa na malalamiko ya Zanzibar baada
ya bodi kuvunjika, lakini hatukuzitumia fedha hizi kwa mambo mengine,
ila tulifungua tawi la Benki Kuu Zanzibar,” anasema.
Anaeleza kuwa anachokumbuka ni kuwa fedha za
Zanzibar zilikuwa asilimia nne katika jumuiya hiyo na kwa jumla Tanzania
ilikuwa na asilimia 35 katika bodi hiyo.
“Kuanzisha BoT Zanzibar haikuwa kazi ndogo kwani
ilibidi tutafute majumba strong (imara). Tujenge mahali pa kuhifadhi
fedha na ujenzi ni gharama hasa strong room (chumba maalumu cha
kuhifadhi fedha), ” anasema Mtei.
Anaongeza kuwa kwa kumbukumbu zangu, wakati huo,
kwenye vikao vya uamuzi huo, Zanzibar ilikuwa inaongozwa na Katibu wa
Wizara ya Fedha aliyemtaja kwa jina moja la Sheha.
“Sheha ndiye aliyekuwa anahudhuria vikao, alikuwa akija na kukutana nami tunajadili,” anasema.
Serikali moja EAC
Akizungumzia mvutano wa kisiasa kwa sasa, kutokana
na mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya, anasema ni vyema maoni ya
wengi yafuatwe na kuheshimiwa.
Hata hivyo, anasema baada ya Muungano kudumu kwa miaka 50,
angetaka ndoto iwe ni kuwa na nchi moja katika ukanda wa Afrika ya
Mashariki.
“Mimi kama mchumi nataka nchi kubwa moja. Tuache
kuzungumzia mambo ya kutugawanya, inawezekana kuna nchi ndogondogo
lakini lazima ziunganishwe na kuwa moja kubwa kupitia Shirikisho la
Afrika ya Mashariki,” anasema.
“Nchi hii ni moja ambayo nadhani tuanze kuifikiria
sasa iwe na Tanganyika, Zanzibar, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na
hata Zambia na Malawi
“Mimi nimejifunza katika political science
(sayansi ya siasa) kuwa nchi inapokuwa moja kubwa, basi uchumi wake
unastawi na watu wanapata maendeleo ya kiuchumi kuliko kuwa nchi ndogo,”
anasema.
Anaongeza, hata hivyo, kuwa ni vyema kujiuliza ni kwa nini miaka 50 ya Muungano sasa, bado Watanzania wengi ni maskini?
“Lazima, tufikirie mbele zaidi, kwenye vikao vya
umoja wa mataifa, zinapozungumza nchi kubwa, utaona kabisa kila mjumbe
anakuwa makini na hata kama yupo nje anarudi kusikiliza, lakini kama ni
nchi ndogo wajumbe wanatoka kuvuta sigara nje ya ukumbi.”
Anaongeza kuwa Watanzania na wakazi wa ukanda wa
Afrika ya Mashariki wanapaswa kufikiria kuwa na nchi moja kubwa kama
Marekani, Ujerumani au Brazil kama kweli wanataka kukuza uchumi wao.
Muungano ni maridhiano.
Akizungumza muundo wa Muungano, Mtei anasema ni muhimu kuwapo kwa Muungano ambao unaridhiwa na nchi zote wanachama.
Anasema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni
lazima uendelezwe na kulindwa, lakini, kwa kuzingatia masilahi na
maridhiano ya kila upande.
“Tuwapinge wote ambao wanataka kuvunja Muungano,
pia tuondoe kero zote zilizopo kwani Muungano ni makubaliano ya watu
wote kwa masilahi yao,” anasema.
Mtei ambaye ni muumini wa Kilutheri ana historia
ndefu ya maisha ambayo yanafurahisha. Ni mtu ambaye alilelewa na mama
yake mzazi na kukulia katika maisha ya umaskini, akichunga mbuzi baada
ya kutoka shule ya Ngaruma iliyokuwa ikimilikiwa na Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania. Baadaye alikwenda Old Moshi, Tabora, kisha Chuo
Kikuu Makerere, Uganda.
CHANZO: MWANANCHI.
CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment