Wednesday, 14 May 2014

Milioni 500/- zatengwa kukabili dengue

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Stephen Kebwe
Serikali  imetenga Sh. milioni 500 kwa ajili ya kunyunyiza dawa za kuua mazalia ya mbu kwenye maeneo chepechepe jijini Dar es Salaam, katika jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa dengue.

Vile vile, imewaagiza watendaji wa vitongoji kusimamia usafi kwenye maeneo yao.

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, aliyasema hayo wakati alitoa kauli ya serikali bungeni jana kuhusu ugonjwa wa homa ya dengue, baada ya Mbunge wa Kigamboni ( CCM), Dk. Ndugulile Faustine, kutaka taarifa ya serikali kuhusu hatua ilizochukua kudhibiti ugonjwa huo.

Dk. Kebwe alisema Wizara imeandaa mpango wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huo na kwamba umeshirikisha sekta mbalimbali na kwamba hadi sasa zaidi ya Sh. milioni 132 zimetumika kwa ajili ya ugonjwa huo na kwamba fedha zaidi zitaendelea kutolewa.

“Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu kwani hauambukizwi kwa kumhudumia mgonjwa au kwa kugusa maji maji yanayotoka kwa mgonjwa...tunawashauri wananchi kwenda vituo vya afya haraka pindi waonapo dalili za ugonjwa huo,” alisema.

Alisema sehemu kubwa ya ugonjwa huo inachochewa na mazingira machafu na kwamba mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zinachangia kuongezeka kwa mazalia ya mbu na kwamba utupaji, uzoaji na uhifadhi wa taka katika miji nchini hauridhishi hali inayotoa fursa kwa mazalia ya mbu kuongezeka.

Dk. Kebwe alisema hadi sasa hakuna chanjo wala dawa maalum kwa ajili ya kudhibiti au kutibu ugonjwa huo na kwamba njia kubwa ni kumzuia binadamu asiumwe na mbu.

USHAURI
Alisema mbinu shirikishi za kutokomeza mbu lazima zitiliwe mkazo na kwamba njia bora na rahisi ni kutokomeza mazalia yote ya mbu.

Pia, alisema watu wavae nguo zinazofunika mikono na miguu na kutumia dawa zinazofukuza mbu, watoto walale kwenye vyandarua vyenye viatilifu wakati wa mchana.

JINSI YA KUJIKINGA
Alisema njia ya kujikinga ni kufukia madibwi ya maji yaliyotuama au kunyunyuzia viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madibwi, kuondoa vitu vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari na kufyeka vichaka karibu na makazi.

Nyingine ni kuhakikisha maua yanayopadwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama, kufunika mashimo ya majitaka kwa mfuniko imara na kusafisha grata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Alisema timu ya taifa ya masafa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo halmashauri za Jiji la Dar es Salaam na wadau wa maendeleo wanakutana kila mara baada ya wiki mbili kutathmini mikakati ya kamati ya dharura iliyowekwa.

Nyingine alisema serikali ilitoa tamko kuanzia Machi, mwaka huu, kuendelea kutoa taarifa ya taadhari ya ugonjwa huo kupitia kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya, ikiwa ni pamoja na namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa, mwongozo kwa watumsihi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli, vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Pia, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia redio na runinga na kwamba wizara kwa kushirikiana na halmashauri za jiji wameendelea kutumia maafisa afya wakiwamo wa kata na uongozi wa mitaa kuwaelimisha wananchi namna ya kudhibiti ugonjwa kwa kutumia vipaza sauti.

Dk. Kebwe, alisema hatua nyingine ni kutoa elimu ya afya kwa watumishi wa afya pamoja na madaktari na mafundi sanifu wa maabara namna ya kutambua ugonjwa huo katika hospitali za Muhimbili, Amana, Mwananyamala na Temeke.

HALI ILIVYOKUWA JANA

Hospitali kadhaa jijini Dar es Salaam zimeendelea kupokea wagonjwa kwa mujibu wa taarifa za jana.

MWANANYAMALA
Juzi mgonjwa mmoja aligunduliwa na kutibiwa kisha kuruhusiwa na kufanya idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuugua ugonjwa huo katika hospitali hiyo kuwa 140.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Faustinias Ngonyani, alisema jana kuwa wagonjwa wote walitibiwa na kuruhusiwa.

Alisema ugonjwa huo ulipolipuka walipokea wagonjwa 139 na mmoja aliongezeka juzi na idadi ya wagonjwa 140 ambamo alisema kati yao wagonjwa sita ni watumishi wa hospitali hiyo, ambao hali zao zinaendelea vizuri.

AGA KHAN

Hospitali ya Aga Khan  imesema kwa wiki moja wamepokea wagonjwa 26, kati yao 17 walitibiwa na kuruhusiwa huku tisa wakiwa wamelazwa.

Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo, Loveluck Mwasha, alisema waliolazwa ni Wachina saba na Watanzania wawili na kuwa hali zao zikiendelea vizuri.

MUHIMBILI
Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana alikuwapo mgonjwa mmoja.

Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano Mwandamizi wa MNH, Aminieli Eligaesha, mgonjwa huyo alikuwa amelazwa kwenye kitengo cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) cha hospitali hiyo na alikuwa anafanyiwa vipimo ili kujua ugonjwa unaomsumbua ingawa dalili za awali zilionyesha kuwa anasumbuliwa na dengue.

TEMEKE
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk. Amani Malima, alisema idadi ya wagonjwa katika hospitali yake imeongezeka na kufikia 20 na kuwa kati yao wapo watumishi 10 wa wilaya hiyo.

DK. BUBERWA AAGWA KWA MAJONZI

Vilio na simanzi vilitawala jana wakati wakuagwa kwa mwili wa Dk. Gilbert Buberwa (36) katika Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam ambaye alifariki Jumapili iliyopita kwa ugonjwa wa dengue.

Dk. Buberwa ambaye alikuwa daktari bingwa wa magonjwa ya akili, alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Wafanyakazi wa Hospitali ya Temeke pamoja na madaktari wengine  walijikuta wakitokwa na machozi wakati wakiuaga mwili huo, huku wengine wakionekana kuwa na majonzi.

Mwakilishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambaye ni mtaalamu wa magojwa ya akili, Dk. Ayubu Magimba, alisema serikali imepata pigo kubwa kwa kifo cha  Dk. Buberwa kwa kuwa alikuwa akitegemewa kwa kiasi kikubwa.

Alisema wanasikitika kumpoteza mtu ambaye alikuwa ni makini na kwa mkoa wa Dar es Salaam alikuwa akitegemewa sana.

Hata hivyo, Dk. Magimba, alishindwa kuendelea kuzungumza kutokana na kutokwa na machozi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kuagwa kwa mwili huo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk. Amani Malima, alisema hospitali yake imepata pigo kubwa kwani walikuwa wakimtegemea kila idara.

“Dk. Buberwa alikuwa kichwa, pia alikuwa ni msaidizi wangu licha ya kwamba ni daktari bingwa wa masuala ya akili alikuwa na uwezo wa kuangalia idara zote na hata wodi za wanawake alikuwa akitibu hakuna kilichokuwa kinamshinda, hivyo hata nikiondoka ninakuwa sina wasiwasi kwa kuwa nimeacha jembe langu,” alisema Dk. Malima.

Dk. Malima alisema mwili wa marehemu umepelekwa nyumbani kwake Kinyerezi, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika leo.

 
CHANZO: NIPASHE

CCM lawamani mchakato Katiba mpya

Imeelezwa kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), haina nia yoyote njema ya kusimamia mchakato na kuhakikisha Watanzania wanapata  Katiba mpya itakayotokana na mawazo yao kwa kuwa inaogopa lawama za kuvunja Muungano.

Kadhalika, imeelezwa kwamba mtu pekee ambaye ataweza kunusuru mchakato wa kupata Katiba mpya ni Rais Jakaya Kikwete.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), James Jesse, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Kituo Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

"Ninaamini Rais Kikwete alikuwa na nia njema ya kuacha historia ya kuandika  Katiba mpya, lakini kwa bahati mbaya amezidiwa nguvu kutoka ndani ya chama chake CCM," alisema Jesse.

Alisema kama mchakato wa kujadili rasimu iliyotolewa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba, ungeachwa ukaenda kama ulivyokuwa umepangwa bila kuingiliwa, kusingekuwa na migogoro ndani ya Bunge la Katiba.

Alifafanua kuwa endapo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wataendelea kukaidi kuingia katika Bunge la Katiba, hakuna kitu chochote kitakachoamuliwa kwa kuwa upande wa Zanzibar kura zikipigwa hawatafikia theluthi mbili ya kura zote.

"Hata ingekuwaje, Bunge la Katiba haliwezi kupitisha maamuzi yoyote ya sura za rasimu ikiwa Ukawa watakuwa nje hususani wajumbe wa kule Zanzibar," alisisitiza.

Jesse alisema ili wajumbe wa CCM wapitishe maamuzi, wanatakiwa kushinikiza sheria ibadilishwe ili watumie mfumo wa nusu ya kura zitakazopigwa badala ya theluthi mbili, jambo ambalo alisema litazua maswali mengi.

Aliongeza kuwa Watanzania wasilaumu Ukawa kukaidi kuendelea na mjadala wa Bunge la Katiba, badala yake wajiulize sababu za msingi zilizowafanya watoke nje.

"Profesa Lipumba ni msomi na mtu mwenye akili timamu, asingeweza kutoka nje bila sababu za msingi, kuna mambo ya misngi wanayotaka yatekelezwe lakini wanashindwa kutokana na uchache wao,'' alisema.

Aliongeza: "CCM hawashindi kutokana na hoja zao kuwa na maana ama nzuri bali wanatumia nguvu ya hoja kutokana na wingi wao na hawa Ukawa wanashindwa hata kama wana hoja nzuri kiasi gani kutokana na uchache wao," alifafanua.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Katiba ambayo ipo chini ya LHRC, Dk. Koti Kamanga, alisema Bunge la Katiba limevurugwa na wanasiasa ambao wanaendekeza itikadi za vyama vyao.

Alisema serikali haina nia njema ya kupatikana Katiba mpya kwa kuwa imevunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba hatua hiyo inadhoofisha mchakato mzima kwa kuwa kukitokea mkanganyiko wa hoja znazojadiliwa hakuna mtu atakayezijibu.

CHANZO: NIPASHE

Zaidi ya wachimba migodi 200 wafa Uturuki

Wachimba migodi wakisaidia kwenye juhudi za uokozi wa wenzao waliokwama kwenye mgodi wa makaa ya mawe wa Soma, kusini mwa Instanbul.
Uturuki imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa huku idadi ya waliokufa kwenye mripuko uliotokea katika moja ya ajali mbaya kabisa kuwahi kutokea kwenye sekta ya madini nchini humo ikipindukia watu 200.

Bendera ya Uturuki ndani na nje ya nchi hiyo inapepea nusu mlingoti kuomboleza msiba huo mkubwa, huku zaidi ya watu 300 wakiendelea kukwama chini ya ardhi katika mji wa Sama ulio kwenye jimbo la Manisa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani, dpa, wakati moto uliporipuka usiku wa kuamkia leo, kwenye mgodi huo kulikuwa na watu 787.

Vikosi kadhaa vya uokoaji vinashiriki kwenye uokozi na Waziri wa Nishati wa Uturuki, Taner Yiildiz, amesema hadi sasa watu waliokolewa ni 365:


"Operesheni za uokoaji zinaendelea. Hadi sasa tumeshapoteza wachimba madini wetu 201. Tunahofia kwamba idadi inaweza kuongezeka. Nilisema pia kwamba kuna kiasi cha watu 80 waliojeruhiwa, 60 kati yao wakiwa ni wachimba madini." Alisema Waziri Yiildiz akiwa nje ya mgodi huo.


Vifo hivyo vimesababishwa na hewa ya sumu inayotokana na moto. Hadi asubuhi ya leo, bado moto huo unaosemekana kusababishwa na hitilafu za umeme, ulikuwa ukiendelea kuwaka, masaa 18 baada ya mripuko kutokea.

Waziri Yiildiz pia amesema kuwa baadhi ya wafanyakazi wako umbali wa kilomita mbili chini ya ardhi na usawa wa kilomita nne kutoka lango kuu la kutokea, jambo linalokwamisha jitihada za uokozi. Waandishi wa habari wanasema wachimba madini hao hawakuweza kutumia lifti kujiokoa kwani mripuko huo ulikuwa umekata kabisa umeme mgodini humo.

Waziri Yiildiz pia amesema kuwa baadhi ya wafanyakazi wako umbali wa kilomita mbili chini ya ardhi na usawa wa kilomita nne kutoka lango kuu la kutokea, jambo linalokwamisha jitihada za uokozi. Waandishi wa habari wanasema wachimba madini hao hawakuweza kutumia lifti kujiokoa kwani mripuko huo ulikuwa umekata kabisa umeme mgodini humo.

Waziri Mkuu Tayyip Erdogan ameahirisha ziara yake ya kikazi nje ya nchi na anatazamiwa kulitembelea eneo hilo la ajali, lililo umbali wa kilomita 250 kusini mwa mji mkuu Istanbul.

Kampuni ya Soma Holding inayomiliki mgodi huo imesema mgodi wao ulifanyiwa majaribio ya usalama miezi miwili iliyopita, lakini vyombo vya habari nchini Uturuki vimeripoti kwamba chama tawala cha AKP kilikataa wito wa upinzani bungeni, kutaka mgodi wa Soma kuhakikiwa mwezi uliopita.

Uturuki ina historia ya ajali mbaya za migodini, inayochangiwa na kanuni mbaya za usalama. Mwaka 1992, ajali kama hiyo iliua zaidi ya watu 260 katika mgodi ulio karibu na Bahari Nyeusi

CHANZO: DW.

Dk Shein akataa kuongeza posho BLW

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Ali Mohammed Shein.
Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amekataa maombi ya kuwaongezea posho wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) kutoka Sh150,000 hadi Sh200,000.

Uamuzi huo wa Dk Shein umetokana na hali ya uchumi Zanzibar kutoruhusu nyongeza hiyo kwa sasa.

Katibu wa BLW, Yahya Khamisi Hamad alithibitisha jana kuwa baraza hilo lilipeleka kwa Rais Shein maombi la kutaka posho ya vikao hivyo iangaliwe upya kutokana na sababu mbalimbali, lakini kulingana na mazingira ya hali ya uchumi ilivyo kwa wakati huu imeshindikana kufanya hivyo.

Hamad alisema Dk Shein amewataka wajumbe kuwa na subira kwa kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi na suala hilo linaweza kufikiriwa.

Alisema Dk Shein alitoa msimamo huo alipokutana na Spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kwa nia ya kumweleza uamuzi kuhusu suala hilo. “Rais amekataa maombi ya nyongeza ya posho za vikao vya wajumbe wa BLW kutokana na hali ya mazingira ya kiuchumi kutokuwa mazuri kwa wakati huu, amewataka wawe na subira hadi hali ya mambo itakapotengamaa,” alisema Hamad.

Alisema kamati ya uongozi ya baraza hilo tayari imekwishataarifiwa kuhusu maombi ya posho kukataliwa na wajumbe wote kutoka CCM na CUF walitarajiwa kutaarifiwa jana kuhusu uamuzi huo.

Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho ya Sh 150,000 kwa siku mbali na mshahara na posho nyingine zinazokaribia Sh4,500,000 kwa mwezi.

Akizungumzia kikao cha bajeti kinachoanza leo mjini Zanzibar, Hamad alisema kikao hicho kitalazimika kupunguzwa kwa siku ili kuwahi Bunge Maalumu la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalofanyika Dodoma ambalo lipo likizo na linatarajiwa kukutana Agosti 5.

Alisema kwa mujibu wa ratiba, kikao cha bajeti kinatarajia kutumia siku 56, tofauti na miaka mingine ili kukimbizana na muda na kuwataka wajumbe kujadili bajeti ili kuokoa muda na kuwahi Bunge la Katiba.

Aidha, katibu huyo wa BLW alisema kikao hicho kitakuwa na maswali 90, miswada miwili ya sheria ukiwamo wa Sheria ya Fedha na ule wa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali mwaka 2014/2015.

Tayari, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee amesema SMZ katika mwaka huu wa fedha inatarajia kutumia Sh 705.1 bilioni, kati ya hizo, makusanyo ya Serikali yatakuwa ni Sh 399 bilioni na kiasi kingine cha Sh 305.3 bilioni ni misaada ya wahisani na mikopo mbalimbali.

CHANZO: MWANANCHI.

Waziri akwepa hoja, amshambulia Lissu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Hassan Suluhu akiwasilisha bunge makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa mwaka fedha 2014/15, mjini Dodoma jana.
Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan alikataa kueleza walipo waasisi sita wa Muungano ambao kambi ya upinzani ilidai kuwa waliuawa na kuzikwa handaki moja, badala yake akatumia nafasi hiyo kumshambulia mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akidai hizo ni propaganda na upotoshaji.

Juzi wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Lissu aliitaka Serikali kutoa maelezo bungeni kuhusu sababu za kuuawa kwa waasisi sita wa Muungano wa Tangayika na Zanzibar na kuzikwa katika handaki moja visiwani Zanzibar.

Lissu aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdalah Kassim Hanga, aliyekuwa waziri mkuu, Abdul Aziz Twalam aliyekuwa Waziri wa Fedha na Abdulaziz na Saleh Akida aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar.

Pia aliwataja Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa ambao alisema nao waliuawa na kuzikwa katika handaki moja eneo la Kama nje kidogo ya Zanzibar.

“Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa, walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo... tunataka kuambiwa ukweli kwanini mchango wao kuhusu Muungano umefichwa,” alisema Lissu juzi.

Lakini alipoulizwa kuhusu madai hayo, Waziri Hassan alionekana kuzigeuza hoja hizo kuwa ni za Lissu pekee badala ya kambi ya upinzani na kumshambulia mbunge huyo akidai kuwa ni mpotoshaji, anayepiga propaganda na mchochezi.

Waziri huyo, ambaye ni Mzanzibari, alisema alipuuza maswali yote kuhusu waasisi hao akisema mbunge huyo wa Chadema alipotoka katika hotuba yake na ndio maana hakutaka kuzungumzia katika majumuisho ya bajeti ya ofisi yake bungeni.

“Yule Lissu sio mkweli na ndio maana sisi tulimpuuza,” alisema waziri huyo.

“Hakuna kitu kama hicho na endapo kingekuwepo sisi Serikali tungeshatoa ufafanuzi ili watu wapate kujua ukweli wake,” aliongeza Waziri Samia bila kutoa ufafanuzi wa nini kiliwatokea watu hao walioshika nafasi za juu serikalini mara baada ya Mapinduzi na Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.

Pamoja na kudai kuwa aliona hoja hizo ni upotoshaji, Waziri huyo, ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Bunge la Katiba, aliwasihi wabunge wa upinzani kupeleka hoja zao katika Bunge Maalumu la Katiba linalojadili uundwaji wa Katiba Mpya, ambalo pia limetawaliwa na suala la muundo wa Muungano na kero zake.

Waziri Samia alisema hoja hizo zinalenga kuwaaminisha Watanzania mambo ambayo hayapo ili kuwajaza chuki dhidi ya Serikali yao na pia alidai zina uchochezi ndani yake.

Waziri Samia aliwashauri wabunge pamoja na Watanzania kupuuza kauli hizo akidai mbunge huyo hautakii mema Muungano na ndio maana anaibua mambo aliyodai kuwa ni ya uongo na ya uchochezi.

Madai ya Lissu

Lissu alitoa madai hayo akinukuu kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru kilichoandikwa na Harith Ghassany ambacho kinaonyesha jinsi ambavyo viongozi hao wa SMZ waliuawa na kuzikwa katika kaburi moja.

“Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja,” alisema Lissu.

Jitihada za kumpata Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, Balozi Seif Ali Idd na Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Mohamed Abood kuzungumzia msimamo wa SMZ kuhusu kauli hiyo hazikuzaa matunda kwa kuwa simu zao ziliita bila majibu.

Akizungumzia suala hilo, mbunge wa viti maalumu, Anna Abdallah alisema naye alidai hoja hizo za Lissu ni za uchochezi ambao usipopuuzwa, unaweza kusababisha chuki kwa jamii.

“Ule ulikuwa ni uchochezi, na upinzani wa aina hiyo ni wa ajabu sana… kwa mtazamo wake yeye anafikiri anawafurahisha Wazanzibari, lakini wamemuona ni mtu wa ajabu,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.

Pamoja na uzito wa tuhuma hizo, baadhi ya wabunge waliohojiwa na gazeti hili jana walionekana kuzungumza kimkakati kwamba hawakusikiliza hotuba hiyo.

Utata mkubwa bado umezunguka kutoweka kwa Hanga na wenzake machapisho mbalimbali yanawatambua kama watu waliokuwa mstari wa mbele katika Mapinduzi ya Zanzibar na ambao waliunga mkono Muungano mara baada ya mapinduzi hayo.

CHANZO: MWANANCHI

Tuesday, 13 May 2014

Pacha wazaliwa wakishikana mikono Marekani

Mama wa mapcha hawa amesema mapacha wake ni zawadi kubwa kwake
Mama mmoja nchini Marekani, amejifungua watoto pacha wakiwa wameshikana mikono.
Watoto hao pia walikuwa wanapumua bila usaidizi wowote walipotolewa kutoka katika mashine yenye hewa ya Oxygen.

"Tayari wanaonekana kuwa marafiki ,’’ alisema mama yao Sarah Thistlethwaite.Mama wa watoto hao, alisema kuwa watoto hao waliopewa majina ya Jillian na Jenna Thistlewaite walikuwa wameshikana katika kitovu na kutumia Kondo moja la nyuma , hali ambayo madaktari walisema ni nadra.
Walizaliwa Ijumaa katika jimbo la Ohio, wakiwa wameshikana mikono.
Inaarifiwa ni mama mmoja tu kati ya akina mama elfu kumi mwenye uwezo wa kujifungua watoto pacha wa aina hiyo.
Bi Thistlewaite, mwenye umri wa miaka 32,alilazimika kupumzika kwa wiki kadhaa kabla ya kujifungua kwani pacha wanaozaliwa wakiwa wameshikana mikoni ni hali nadra ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya watoto na mama kabla ya kuzaliwa.
Mama huyo alisema kupokea watoto wake ilikuwa zawadi tosha kwake wakati huu wa kusherehekea siku ya akina mama duniani.

Marekani kutafuta mateka Nigeria

Marekani imesema inapeleka vifaa vya uchunguzi nchini Nigeria kusaidia katika juhudi za kuwatafuta wasichana wanaozuiliwa na kundi la Boko Haram.
Wasichana hao walitekwa nyara kutoka shule moja Kusini mwa eneo la Borno mwezi mmoja uliopita.

Amesema msaada huo wa Marekani kutoka wizara za mambo ya nje na ulinzi na pia kutoka idara ya uchunguzi ya FBI.Msemaji wa Rais Obama Jay Carney amesema kikosi cha maafisa 30 kiko nchini Nigeria tayari kushiriki juhudi hizo.
Hatua hiyo imechukuliwa wakati baadhi ya Jamaa za wasichana waliotekwa nyara wakielezea majonzi baada ya kutazama kanda ya video iliyotolewa na kundi hilo.
Baadhi wameiambia BBC kuwa kanda hiyo imewapa matumaini lakini wameshangaa kuona wasichana hao ambao wengi ni Wakristu wamevalia mavazi ya Kiislam.
Akizungumza kwa uchungu nduguye mmoja wa wasicha waliotekwa ameiambia BBC ni heri kanda hiyo ingeonyesha maiti za wasichana hao kwa kuwa hiyo ingeondoa wasiwasi unaoendelea kukithiri na kuumiza mioyo ya wengi.
Kwenye kanda hiyo ya video kiongozi wa Boko Haram , Abubakar Shekau anasikika akiambia serikali ya Nigeria yuko tayari kubadilishana baadhi ya wasichana hao na wafuasi wake waliofungwa jela.
Hatahivyo wizara ya mambo ya ndani ya Nigeria imetupilia mbali pendekezo hilo.

Seneta Ali Ndume kutoka eneo ambapo wasichana hao walitekwa nyara anaisihi serikali kulegeza msimamo.

CAG aibua madudu Benki ya Posta

Dodoma. Wakati Watanzania waliohitimu vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi wakihaha kutafuta kazi, Benki ya Posta Tanzania (TPB) imeajiri wafanyakazi 40 katika nafasi mbalimbali, huku matangazo ya nafasi hizo za kazi yakitolewa kupitia barua pepe na anuani za ndani za benki hiyo.
TPB iliajiri wafanyakazi hao kuanzia Julai 2012 hadi Aprili 2013 na waliokuwa na uwezo wa kuona tangazo hilo ni wale tu waliokuwa na neno la siri (password) ya barua pepe na anuani za ndani za benki hiyo. Jambo hilo lilitoa mwanya kwa wafanyakazi kuwapeleka marafiki, jamaa au ndugu ili kupata fursa hiyo.
Pia, benki hiyo iliajiri wafanyakazi watatu katika nafasi za juu na kuwalipa viwango vya mishahara tofauti na vilivyoainishwa katika muongozo wa utumishi wa benki hiyo. Ufisadi wote huo umesababisha Sh185milioni kutowekea kusikojulikana.
Hayo yamebainishwa katika ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2012/13, ambapo pia imefafanua jinsi benki hiyo ilivyotumia mamilioni ya fedha kukarabati jengo la benki hiyo na nyumba ya mkurugenzi wake mkuu.
“Ajira hizo zilikuwa zikitangazwa kwa njia ya matangazo ya ndani kupitia barua pepe ambazo zinaonekana kwa wafanyakazi wa ndani tu au mtu husika aliyetumiwa barua pepe ya tangazo,” inaeleza ripoti hiyo.
“Mtu yeyote asiye na ‘password’ hawezi kuona tangazo hilo. Jambo hilo lilitoa mwanya kwa wafanyakazi kuwaleta marafiki, jamaa au ndugu ili kupata fursa hiyo.”
Kuhusu ajira za watumishi watatu ripoti hiyo inaeleza kuwa “mmoja alipewa mshahara wa Sh3.6 milioni kwa mwezi badala ya kulipwa Sh2.4milioni. Mwingine analipwa Sh5 milioni badala ya Sh2.4 milioni na mwingine analipwa Sh5,5 milioni badala ya Sh3.3milioni.”
Kuhusu ukarabati wa jengo la benki hiyo tawi la Mkwepu, ripoti hiyo inaeleza kuwa kampuni ya Kiaren Investment ndiyo ilipewa kazi hiyo na kutakiwa kulipwa Sh86 milioni lakini ikalipswa Sh144milioni.
Baadhi ya wananchi wameitaka Serikali kuifanyia kazi ripoti hiyo ya CAG na kuwachukulia hatua wote waliofanya ufisadi.
huo.

Wachina tisa walazwa, JK aagiza hatua za dharura

Rais Jakaya Kikwete.
Dar/Arusha. Wakati raia tisa wa China wakibainika kuugua ugonjwa wa dengue na kulazwa hapa nchini, Rais Jakaya Kikwete amevunja ukimya na kuagiza wizara zake mbili kukabiliana na ugonjwa huo kwa dharura.
Ugonjwa huo uliingia nchini tangu mwaka 2010 lakini mlipuko wake mkubwa ulibainika Machi mwaka huu na hadi jana wagonjwa zaidi ya 400 walikuwa wameambukizwa, huku watatu wakiripotiwa kufariki dunia, akiwamo Daktari Bingwa wa magonjwa ya akili, Dk Gilbert Buberwa anayezikwa leo, Dar es Salaam.
Rais jana aliziagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na ile ya Fedha kushirikiana Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuchukua hatua za dharura kupambana nao kwa kuhakikisha vinapatikana vipimo vya kutosha na dawa.
Wachina walazwa
Taarifa kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam zilieleza kuwa wagonjwa waliobainika kuugua homa hiyo hadi jana ni raia hao wa China na Watanzania wachache wenye historia ya kusafiri nje ya nchi hasa China, Ufilipino na Kusini mwa India.
Muuguzi katika kitengo cha magonjwa ya kuambukiza cha Aga Khan, Nyangee Lugoe alisema hospitali hiyo ilianza kupokea wagonjwa tangu Machi mwaka huu na kuanzia Aprili, raia wengi wa China wamegundulika kuwa na homa hiyo, ingawa baadhi walitibiwa na kuruhusiwa.
Agizo la Rais Kikwete
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani huko Arusha, Rais Kikwete alisema: “Hili ni jambo la dharura la kitaifa lazima hatua muafaka zichukuliwe kudhibiti ugonjwa huu, ambao asili yake ni nchi za Asia na Bara la Amerika.”
Alisema dalili za ugonjwa huo ambao unasababishwa na mbu aina ya Aedes Egyptie anayeuma mchana ni homa kali ya kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na kutoka damu puani na kwenye fizi na kupoteza fahamu.
“Napenda kutoa wito mtu yoyote ambaye atapata dalili za ugonjwa huu, aende mara moja hospitalini ili afanyiwe vipimo badala ya kunywa dawa,” alisema.
Tayari Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetangaza kuanza kuchukua hatua za dharura kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na uelimishaji na uhamasishaji wa jamii kuchukua tahadhari.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Charles Pallangyo alisema jana kuwa wizara yake imetoa hadhari ya ugonjwa huo kupitia kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini na itatoa mafunzo maalumu kwa watumishi wa afya ikiwajumuisha madaktari na mafundi maabara ili kuwajengea uwezo.
Aidha, wizara hiyo itaanzisha vituo maalumu vya ufuatiliaji wa ugonjwa huo katika hospitali za Mwananyamala, Amana na Temeke.
Ugonjwa kutoka nje
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa Homa ya dengue katika Hospitali ya Mwananyamala, Dk Mrisho Lupinda alisema upo uwezekano mkubwa kuwa virusi hivyo viliingia nchini kutokana na mwingiliano na urahisi wa watu kusafiri kati ya Tanzania na nchi za Mashariki ya Mbali.
“Namna watu wanavyopata nafasi ya kusafiri kwa haraka kwenda sehemu moja na kurudi kwa shughuli mbalimbali ikiwamo biashara ndivyo namna maambukizi yanavyoenea kwa urahisi. Hii inawezekana kabisa kwamba mwingiliano wa kibiashara umechangia kwa kiasi fulani,” alisema.
Alisema ugonjwa huo ni wa kawaida katika maeneo ya kitropiki kwenye mabara yote, lakini umezoeleka zaidi kwenye nchi za Mashariki ya Mbali hasa bara la Asia.
Alisema mbu wanaoambukiza ugonjwa huo walikuwapo nchini kwa zaidi ya miaka 300 iliyopita lakini hawakuwa na virusi hivyo.
Hakuna unyanyapaa
Mkurugenzi wa Tiba katika Hospitali ya Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee alisema licha ya ugonjwa huo unaua na kuambukiza, wananchi hawapaswi kuwa na unyanyapaa kwa waliogua.
“Baada ya taarifa kuenea kwa kasi, kuna watu wameogopa na wanadhani wale waliopata hawapaswi kuguswa au kusogelewa lakini huu ni ugonjwa usioambukizwa kwa njia hizo kama ukoma,” alisema.
Alisema mgonjwa wa dengue anahitaji tiba ya dalili zinazojitokeza na ili asiambukize atahitaji kulala kwenye chandarua hata kama ni mchana,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI.

Lissu: Walipotelea wapi waasisi sita wa Muungano

Msemaji wa kambi ya upinzani Bungeni ofisi ya Makamo wa Rais muungano Mh, Tundu Lissu akisoma hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya makamu wa Rais Muungano bungeni jana.
Dodoma. Serikali imetakiwa kutoa maelezo bungeni, kuhusu sababu za kuuawa kwa waasisi sita wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wanaodaiwa kuzikwa katika handaki moja Zanzibar.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), msemaji wake, Tundu Lissu aliitaka Serikali kueleza waasisi hao walifanya makosa gani.
Aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdallah Kassim Hanga aliyekuwa Waziri Mkuu, Abdulaziz Twala aliyekuwa Waziri wa Fedha na Saleh Akida aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi, Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa ambao alisema waliuawa na kuzikwa handaki moja eneo la Kama, Zanzibar.
Lissu alisema hayo huku akinukuu kitabu cha ‘Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru’ kilichoandikwa na Harith Ghassany alichosema kilionyesha jinsi viongozi hao walivyouawa na kuzikwa katika kaburi moja.
“Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja,” alisema Lissu huku wabunge wakiwa kimya kumsikiliza.
Mgawo wa Zanzibar
Lissu pia aliibua mambo mazito kuhusu mgawanyo wa fedha za misaada na mikopo ya kibajeti kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Alisema Muungano ni kielelezo cha unyonyaji na ukandamizaji ambao nchi kubwa imeifanyia nchi ndogo ya Zanzibar kwa miaka mingi.
Alikwenda mbali na kuitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au Wazanzibari kwa umoja wao, kufungua kesi Mahakama za kimataifa kudai fedha zote ambazo nchi yao imeibiwa kwa kivuli cha Muungano.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alisema hadi Machi mwaka huu, Zanzibar ilikuwa imepata gawio la Sh27.1 bilioni badala ya Sh32.6 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge, sawa na asilimia 83.
Hata hivyo, alisema hilo linaweza lisiwe tatizo, kwani kwa mwelekeo wa takwimu hizo, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha, gawio lililoidhinishwa linaweza kuwa limelipwa lote.
Haya hivyo, alisema tatizo kubwa na la msingi ni kwamba, gawio lililoidhinishwa na Bunge si halali kwa Zanzibar, kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya ya Aprili 30, mwaka huu.
Lissu alimnukuu Mkuya akisema mapato halisi ya Serikali ya Muungano yanayotokana na misaada na mikopo nafuu ya nje kwa mwaka 2013/2014 yalikuwa Sh1.163 trilioni.
“Kama Zanzibar ingepatiwa asilimia 4.5 ya mapato hayo kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, kwa mwaka jana pekee, gawio halali la Zanzibar lingekuwa Sh52.335 bilioni,” alisema.
“Badala ya kupatiwa Sh52.335 bilioni ambazo ni fedha zake halali, Zanzibar iliidhinishiwa Sh32.62 bilioni au asilimia 52 ya fedha zake halali. Hii ni sawa na asilimia 2.8 ya fedha zote za misaada badala ya asilimia 4.5.”
Alisema kwa ushahidi huo wa nyaraka za Serikali, kwa mwaka jana pekee Zanzibar iliibiwa Sh25.145 bilioni sawa na asilimia 48 ya fedha zake halali za gawio la misaada na mikopo ya kibajeti.
Kutokana na hali hiyo, kambi hiyo imeitaka Serikali kueleza ni kwa nini fedha halali za Zanzibar kutokana na misaada na mikopo ya kibajeti hazijalipwa kwa mwaka jana wa fedha.
Pia kambi hiyo imeitaka Serikali kupeleka mbele ya Bunge, takwimu za fedha zote za misaada ilizopokea na mikopo ya kibajeti kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Katika takwimu hizo, kambi hiyo imeitaka Serikali kueleza katika fedha hizo, ni kiasi gani kililipwa kama kwa Zanzibar kama gawio lake katika kipindi hicho kwa fedha za misaada na mikopo ya bajeti.
Kuhusu misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti, Lissu alisema: “Ukweli ni kwamba hali ni mbaya zaidi kuhusu fedha za misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti. Hapa pia takwimu za Serikali hii ya CCM zinatisha na kusikitisha.”
Alitolea mfano kuwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 fedha za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikijumuisha misaada na mikopo zilikuwa Sh2.692 trilioni.
“Fedha hizi zote zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Tanganyika. Zanzibar haikupata kitu chochote,” alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.
Lissu alisema kutokana na Muungano, Zanzibar imenyang’anywa mamlaka ya kuomba mikopo au misaada kutoka nje bila kibali cha Wizara ya Fedha ya Muungano.
“Sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka kujua unyonyaji na wizi huu wa fedha za Wazanzibari utakomeshwa lini?” alihoji Lissu.
Waziri afafanua
Wakati Lissu akisema hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan alisema kati ya Julai Mosi, 2012 na Machi mwaka huu Zanzibar imepata gawio la Sh36.75 bilioni kutokana na Kodi ya Mishahara ya Wafanyakazi (Paye).
Waziri Hassan alisema hatua hiyo ni baada ya mawaziri wa pande mbili kukaa na kukubaliana kuwa SMZ inastahili kwa vile kodi ya mapato inayotokana na mishahara ya wafanyakazi ni suala linalohusu mapato ya Muungano.
Hata hivyo, alisema marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato kuhusu kodi ya mishahara yanahitajika ili kuweka utaratibu wa wazi zaidi.
Pia alisema kuanzia Julai, 2013 hadi Machi mwaka huu, SMZ imepokea kodi ya mshahara ya Sh15.75 bilioni na fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo Sh1.24 bilioni.
Kuhusu gawio la mapato ya misaada ya kibajeti, Waziri Hassan alisema SMZ imepata Sh27.19 bilioni kati ya Sh32.63 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2013/14.
Alisema Serikali pia iliichangia SMZ Sh600 milioni kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waasisi na Picha
Lissu alisema kuna jambo linalofikirisha sana kuhusu picha za miaka 50 ya Muungano, kwa kuwa baadhi ya watu wanaoonekana katika picha hizo wamefutwa katika historia wanayofundishwa watoto shuleni.
Alitolea mfano picha ya Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume wakisaini hati za makubaliano ya Muungano wakiwapo viongozi waliokuwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Kwa upande wa Tanganyika alikuwapo Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde, wakati kwa Zanzibar wanaoonekana ni Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo,” alisema.
Lissu alisema Ghassay katika kitabu chake ameonyesha jinsi waasisi hao walivyotoa mchango mkubwa katika kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
“Baadaye viongozi hao walifanikisha Muungano wa Zanzibar na Tanganyika Aprili 26 ya mwaka huo,” alisema na kuongeza kuwa hilo lilithibitishwa pia na aliyewahi kuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe.

Lissu alisema katika kitabu chake, Jumbe ameeleza kuwa Kambona, Munanka na Lusinde ndio waliompelekea Karume nakala za hati ya makubaliano na kusainiwa Aprili 22, 1964.
CHANZO: MWANANCHI.

Thursday, 8 May 2014

CAG abaini kasoro vyama vya siasa


Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya hesabu za serikali (PAC) Mh. Zitto Kabwe.
Dodoma. Ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), katika vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu umebaini madudu ikiwamo vyama vinne kutokuwa na akaunti benki.
Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma jana, CAG Ludovick Utouh alivitaja vyama ambavyo havina akaunti benki kuwa ni UMD, NLD, NRA na ADC.
“Katika hesabu walizotuletea kulikuwa hakuna ushahidi kwamba wanaendesha akaunti benki,” alisema huku akibainisha kuwa kitendo hicho ni kinyume na Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
Halikadhalika katika ukaguzi huo, vyama vya siasa 11 kati ya 21 vyenye usajili wa kudumu, havikuwasilisha taarifa za hesabu za mwaka kama Kifungu cha 14(1) cha sheria hiyo ya mwaka 1992 kinavyosema.
Alipoulizwa baadaye vyama hivyo, Utouh alivitaja CCK, UPDP, Tadea, Demokrasia Makini, Chausta, DP na AFP. Vyama vya Sauti ya Umma na Chauma viliwasilisha hesabu zao vikiwa vimechelewa.
Utouh alisema katika ukaguzi huo, taarifa za hesabu zilizowasilishwa na vyama 10 hazikufuata misingi ya mfumo wa utoaji wa taarifa za fedha za kimataifa.
“Tulibaini kuwa hakuna chama cha siasa hadi sasa kilichowasilisha kwa msajili wa vyama vya siasa tamko la mali zote zinazomilikiwa na chama husika jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” alisema.
Utouh alitumia mkutano wake huo na wanahabari kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto kwa kusimama kidete kuhakikisha vyama vya siasa navyo vinakaguliwa na CAG kama sheria inavyoelekeza.
Kwa upande wake Zitto, naye alimpongeza CAG kwa kukagua vyama vya siasa akisema ni kati ya maeneo yaliyokuwa na matatizo.
“Kwa kitendo chako cha kuamua kukagua bila hata ya kupewa fedha ni kitendo ambacho kinaonyesha uzalendo wako wa hali ya juu,” alisema Zitto na kuongeza:
“Kwa sababu tunachokitaka sisi ni kila senti ya mlipa kodi ikaguliwe na kama nilivyowahi kusema huko nyuma kwa miaka minne vilikuwa vimepewa ruzuku ya Sh69 bilioni.”
Zitto alihoji kama CAG anakwenda kukagua bodi za mazao nchini ni kwa nini vyama vya siasa visikaguliwe wakati ndivyo vinavyozalisha Serikali pale vinaposhinda uchaguzi?
CHANZO: MWANANCHI.

CUF yaonya kauli za kuvunja Serikali ya Umoja Zanzibar


Mwenyekiti wa Chama cha wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza jijini Dar es Salaam jana. Picha na Raphael Lubava 
Dar es Salaam. Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), limelaani kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliyoitoa katika mikutano yake Zanzibar na kusema kuwa ina lengo la kuvunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema jana kuwa, kauli hizo zilizotolewa na viongozi wa CCM kuhusu SUK ni za kichochezi zinazopandikiza mbegu za chuki na vurugu inayoweza kusababisha maafa makubwa.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa inatokana na maoni ya Wazanzibari wote na imesaidia kuleta amani na utulivu Zanzibar…. kauli za kuchochea kuivunja zinapandikiza mbegu ya chuki na vurugu,” Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari.
Alisema Baraza Kuu pia limelaani kauli iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd kuwa Mwakilishi wa Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa siyo raia wa Zanzibar na kuiita kuwa ya kibaguzi yenye lengo la kupandikiza chuki dhidi ya Wazanzibar na Watanzania wenye asili ya Kiasia.
Wiki iliyopita, katika mkutano wa hadhara wa CCM ulioongozwa na Kinana kwenye Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja, Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Salmin Awadh Salmin alisema wawakilishi wa CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza hilo ili kuwapa nafasi wananchi wahoji iwapo wanataka kuendelea na SUK au la.
Salmin alisema wajumbe hao wamefikia hatua hiyo kwa kuwa wanaona lengo na matumaini ya kuundwa kwake yamefutika na hayana dalili njema katika siku za usoni.
Katika mkutano huo, Kinana alinukuliwa akisema kuwa kwa miaka 20 tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad amekuwa akiwayumbisha Wazanzibari kutokana na tabia yake ya kubadilisha ajenda za kisiasa na kutikisa misingi ya umoja wa kitaifa nchini.
Alisema tabia ya kiongozi huyo imekuwa haifahamiki na haijulikani anatafuta jambo gani licha ya kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa mwaka 2010 na CCM na CUF.
Msimamo wa CUF kuhusu Ukawa
Profesa Lipumba alisema CUF inawahakikishia Watanzania wote kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka chama hicho hawatarudi katika Bunge Maalumu hadi pale litakapojadili na kuiboresha Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Tutashirikiana na wajumbe wote wa Ukawa katika mapambano ya kudai Katiba ya wananchi, tunawaomba wananchi waunge mkono juhudi hizi za kupigania kuheshimika kwa maoni yao katika kupata Katiba Mpya,” alisema.
Alisema Baraza Kuu la Uongozi la CUF, limeupongeza Ukawa kwa uamuzi wa busara wa kujiondoa kwenye Bunge la Katiba kwa kile walichoeleza kuwa lilipoteza mwelekeo na wajumbe walio wengi wakifuata maelekezo ya CCM ya kuacha kujadili rasimu iliyokuwapo na kujadili mpya yenye mfumo mpya ambao haukupendekezwa na wananchi.
Aliongeza kuwa, CUF inatoa wito kwa viongozi waliounda Ukawa kuendeleza umoja huo na kufahamu kuwa wananchi wamepata moyo na hamasa mpya baada ya kuanzishwa kwa umoja huo na kwamba wasikubali kugawanywa na CCM.
“Baraza Kuu la CUF linampongeza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kwa ukomavu wa kisiasa aliouonyesha wa kuvunja kambi rasmi iliyokuwa ikiundwa na chama kimoja na sasa kuvishirikisha vyama vingine, kikiwamo CUF.”
Bunge la Bajeti
Profesa Lipumba alisema CUF kimebaini kuwa nidhamu ya bajeti imeendelea kuporomoka na kutolea mfano wa bajeti ya 2013-2014 kwamba haikutekelezeka kutokana na makadirio ya mapato kuonekana makubwa kuliko hali halisi ya ukusanyaji.
Alisema CUF inalaani utaratibu aliouita mbovu wa misamaha holela ya kodi ambayo husababisha upotevu wa fedha za Watanzania. Alisema kwa mwaka huu wa fedha, zaidi ya Sh2 trilioni zimepotea kutokana na misamaha hiyo.
 CHANZO: MWANANCHI.

Upinzani watoa masharti Uchaguzi Mkuu 2015


Kiongozi wa kambi ya Upinzani Bungeni Mh, Freeman Mbowe.
Dodoma. Serikali imetakiwa kuandaa taratibu za mpito za kushughulikia Uchaguzi Mkuu ujao ili kunusuru nchi kuingia katika mtanziko unaoweza kuwa chanzo cha machafuko ya kisiasa, endapo utafanyika bila kupatikana kwa Katiba Mpya la sivyo Kambi Rasmi ya haitashiriki.
Hayo yalielezwa jana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alipokuwa akitoa hotuba ya kambi hiyo bungeni kuhusu Makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Hatuwezi kuingia uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa kwa utaratibu uliopo leo, hatuwezi kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani na Tume ya Uchaguzi kama ilivyo leo, hatuwezi tena kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani wakati matokeo ya uchaguzi wa Rais hayawezi kuhojiwa mahakamani.”
Aliongeza: “Hatuwezi kuingia kabla na hoja ya mgombea huru haijapatiwa majibu, tukiwa na daftari la wapigakura lililopo leo na hatuwezi kulikubali daftari jipya litakalotengenezwa kama wadau wote hatutashirikishwa kikamilifu.”
Kauli hiyo ya Mbowe imekuja siku moja tu baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwasilisha bungeni, Bajeti ya ofisi yake ambayo imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Mbowe alisema kama ilivyo kawaida, Serikali na CCM inaweza kupuuza tahadhari hizo na kulazimisha kwenda katika chaguzi hizo katika mazingira ambayo hayana mwafaka kama inavyoonekana sasa katika Mchakato wa Katiba Mpya.
Ukawa haitarejea bungeni
Katika hotuba hiyo iliyobezwa na wachangiaji wa CCM kuwa imezungumzia Katiba badala ya Bajeti, Mbowe alisema wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hawatarejea katika Bunge la Katiba mpaka watakapohakikisha kuwa maana halisi ya uwepo wa Bunge hilo unafuatwa.
Alisema kama lengo ni kutumia mwavuli wa Bunge Maalumu la Katiba ili kuendeleza mfumo wa kikatiba na muundo wa muungano uliopo sasa, wajumbe wa Ukawa hawatakuwa sehemu ya usaliti huo kwa Watanzania.
“Kama kitakachojadiliwa katika Bunge la Katiba kitalenga kuboresha matakwa ya wananchi kama yalivyodhihirishwa katika Rasimu ya Katiba na taarifa za tume, wanachama wa Ukawa watakuwa tayari kurudi kwenye Bunge Maalumu la Katiba ili kuendelea na mjadala wa rasimu,” alisema Mbowe.
Ofisi ya Rais
Mbowe alisema kati ya wajumbe 201 wa Bunge la Katiba walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, zaidi ya wajumbe 160 ni wanachama wa CCM.
Alisema hofu ya Kambi ya Upinzani kwamba CCM ingetumia mamlaka ya Rais katika uteuzi wa wajumbe wa bunge hilo, sasa imedhihirika wazi.
Alisema wajumbe hao walichomekwa kwenye Bunge Maalumu kwa kutumia kivuli cha waganga wa jadi, taasisi za kidini, asasi za kiraia, taasisi za kitaaluma na watu wenye malengo yanayofanana.
“Hatua hii imechangia kujenga mazingira ya kutokuaminiana na hivyo kuweka msingi mbaya wa mchakato husika,” alisema.
Alisema hata lilipoanza Bunge la Katiba, CCM iliendelea kufanya hila za kuchakachua kanuni za Bunge la Katiba ili kupitisha hoja zao kirahisi.
“Walipoona wamekwama walimtumia Mwenyekiti wao Taifa (Rais Kikwete) ambaye alitumia kivuli cha urais kusisitiza msimamo wa CCM na kutisha wajumbe wa Bunge la Katiba kwamba kama ukipita muundo wa serikali tatu jeshi litapindua Serikali,” alisema Mbowe.
Alisema Rais Kikwete ndiye aliyebariki uandikaji wa Katiba Mpya Desemba 2010, lakini hivi sasa anaongoza mawaziri wake, viongozi waandamizi, wabunge na wajumbe wa CCM kujadili Rasimu ya Katiba kwa kutukana, kudharau, kubeza, kuzomea na kushutumiana.
Alisema kitendo hicho kinathibitisha kauli zilizowahi kutolewa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kwamba Serikali ya CCM haioni haja ya kuwa na Katiba Mpya kwani iliyopo sasa inatosha.
CHANZO:MWANANCHI.

Wednesday, 7 May 2014

‘JK, Shein ndiyo wanaoweza kuirejesha Ukawa bungeni’

Rais wa Tanzania Dk Kikwete akiwa na Rais wa Zanzibar Dk Shein
Dar es Salaam. Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Juma Duni Haji amesema watu pekee wanaoweza kulinusuru kundi la Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa), kurejea bungeni ni Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Duni ambaye pia ni kiongozi wa CUF, alisema hayo jana kwenye mdahalo kuhusu Bunge Maalumu la Katiba tunayoitaka uliofanyika Dar es Salaam.

“Ngoma hiyo imeshakwama, kamwe haturudi bungeni kujadili mambo ya CCM kwani hayatuhusu. Kwa mazingira yaliyopo, ule sasa umegeuka kuwa mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM, wanaweka mambo yenye masilahi kwa chama chao, kamwe haturejei,” alisema.

Alisema kama viongozi hao hawazioni dosari zinazofanywa na wajumbe wa CCM, basi suala la kupata Katiba Mpya ni ndoto kwa sababu Ukawa hawako tayari kurejea katika Bunge hilo.

“Tunawaachia CCM waandae Katiba ya Watanzania, sisi hatutashiriki kwa sababu tumegundua rafu hiyo mapema,” alisema.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema hata kama Ukawa hawatarejea bungeni, vikao vitaendelea kama kawaida kwa sababu kanuni zinawaruhusu kufanya hivyo.

“Katika Bunge Maalumu la Katiba, wapo wabunge wa CCM na wale 201. Walioteuliwa na Rais ambao walitoka nje pamoja na Ukawa ni wajumbe 25 na wamebaki 176, hivyo watu wasiseme waliobaki ni wajumbe wa CCM,” alisema.

Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Humphrey Polepole alisema Bunge Maalumu la Katiba halina mamlaka ya kubadilisha rasimu hiyo, bali kuiboresha.


CHANZO: MWANANCHI.

Mvua ya Samaki Sri Lanka

Samaki waliotoka mtoni kutokana na upepo mkali
Wakaazi wa kijiji kimoja Magharibi mwa Sri Lanka wamesema kuwa wameshangazwa na pia kufurahishwa na tukio la 'kunyeshewa' na mvua ya Samaki wadogo.

Samaki hawa ambao walikuwa katika hali nzuri ya kuweza kulika wanaaminika kuwa walibebwa kutoka kwa mto kwa upepo mkali.

Wanakijiji hao wa wilaya ya Chilaw walisema kuwa walisikia kitu kizito kikianguka na wakapata samaki wengi wenye uzani wa kilo hamsini .

Hili si tukio la kwanza la aina hii kuwahi kutokea Sri Lanka- mwaka wa 2012, kulitokea kisa cha mvua ya viumbe vya baharini vijulikanavyo kama 'Kamba' ambavyo huliwa

Wanasayansi wamesema kuwa mvua ya Samaki hutokea wakati ambapo upepo mkali unazinga juu ya maji ya kina kifupi na hivyo kusababisha mzunguko wa maji unaovuta karibu kila kitu kilicho ndani ya maji ikiwa ni pamoja na samaki na hata Vyura.

Viumbe hawa wa majini wanaweza wakasafirishwa kwa masafa marefu kwa kushikiliwa na mawingu hata baada ya ule mzunguko wa maji kuisha.

Wanakijiji wanasema kuwa mvua hiyo ya Samaki ilinyesha Jumatatu huku viumbe wale wakianguka kwenye mashamba, barabara na paa za kijiji hicho.

Baadhi ya samaki hao wenye urefu wa kati ya sentimita tano na nane, walikuwa bado wako hai na walitiwa kwenye ndoo za maji na wanakijiji waliowatumia kama kitoweo badaye.

Hii ni mara ya tatu kwa tukio kama hili kufanyika Sri Lanka, ingawa katika eneo tofauti.

Kando na ile mvua ya ‘Prawn’ya mwaka wa 2012 kusini mwa Sri Lanka, mvua ya kimondo (meteors) nyekundu na manjano ilinyesha mwaka huo huo,tukio ambalo bado linachunguzwa na wanasayansi wa Marekani na Uingereza.

CHANZO: BBC SWAHILI
Rais Barack Obama wa Marekani aliyeamuru msaada wa kijeshi na vifaa kuwatafuta wasichana Nigeria.
Marekani imetangaza kwamba imetuma kikosi cha wataalamu nchini Nigeria kusaidia kuwatafuta wasichana takriban 200 wa shule waliotekwa nyara mwezi uliopita na wapiganaji wa kundi la Boko Haram.

Rais Barack Obama ameshutumu utekaji nyara wa wasichana hao na kusema kuwa mataifa yanapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kulikomesha Boko Haram.

"Tayari tumetuma kundi letu Nigeria. Wamekubali msaada wetu ambao unashirikisha wanajeshi, wadumishaji wa sheria na mashirika mengine ambao wanajaribu kutambua waliko wasichana hawa ili wawape msaada," Rais Obama alisema.

Rais Obama amesema kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kutumia utekeji wa kikatili wa wasichana hao kama msingi wa kuungana na kuangamiza Boko Haram.

Nchini Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan amekubali msaada huo kama alivyosema msemaji wake, Daktari Reuben Abati.

"msaada huo kutoka kwa Rais Obama uliwasilishwa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni John Kerry kama saa tisa alasiri hivi," Daktari Abati alisema.

CHANZO: BBC SWAHILI.
Edwin Mtei Kuzaliwa:  Mwaka 1932, Marangu Mkoani Kilimanjaro Kazi: Gavana wa Kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) •Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki •Waziri wa Fedha chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere  Elimu: Shahada ya Sanaa (Sayansi ya Siasa na Historia na Jiografia) Siasa: Mwanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Arusha. Kero za Muungano zimetokea kuwa msamiati maarufu katika siku za karibuni nchini, hasa pale ulipoanza mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.

Wengi wamekuwa wakieleza kuwa kero zipo lukuki katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umetimiza miaka 50 sasa.

Kero hizo zimetumika kama kete ya kutetea muundo unaofaa wa Muungano ingawa mjadala sasa umehamia kwenye  serikali mbili au tatu.

Hata hivyo, katika kero hizo, zipo ambazo zimeanza kupatiwa ufumbuzi na zipo ambazo zimeibuka upya tena kwa kasi.

Miongoni mwa kero ambazo ni ngeni kwa wengi, ni kutokujulikana zilipopelekwa fedha za Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika  Mashariki  (EACB) iliyonjika mwaka 1965.

Kero hiyo, ilikuwa ikizungumzwa chini chini na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na hata wanasiasa wa pande zote mbili za Muungano.

Kutokana na watu wengi kuhoji, fedha hizo, wakati wa uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba  mjini Dodoma, Rais Jakaya Kikwete naye alizungumzia kero hiyo na kuahidi kuwa itafanyiwa kazi.

Hata hivyo, ili kupata maelezo ya kina juu ya kero hii, gazeti hili linazungumza na Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei, ambaye pia aliyekuwa Waziri wa Fedha kati ya mwaka 1978 hadi 1981.

Mtei, ambaye pia aliwahi kuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) na ameshika nafasi mbalimbali katika jumuiya hiyo kabla ya kuvunjika, anaeleza historia ya akiba hiyo ya Zanzibar na wapi ilipo.

Anasema ni kweli kuwa baada ya kuvunjika kwa EACB mwaka 1965, Zanzibar ilikuwa na akiba ya fedha zake katika bodi hiyo.

Anasema Zanzibar ilikuwa na kiasi cha fedha kama asilimia 4, huku Kenya, Uganda na Tanzania (Bara) zikiwa na kiasi kikubwa cha fedha.
Je, zipo wapi fedha za Zanzibar?


Mwanasiasa huyo anasema fedha hizo  baada ya kuvunjika kwa bodi hiyo, fedha hazipo tena na anashangazwa na watu wanaoibuka leo na kudai sasa kana kwamba bado zipo BoT.

Anasema anakumbuka wakati huo, mara baada ya kuvunjika kwa bodi hiyo, ulifanyika mgawanyo wa fedha katika hazina za nchi hizo kuanzisha benki kuu.

Anasema fedha za Tanzania Bara zilifanya kazi mbalimbali  na zile za   Zanzibar  ziliingizwa katika kazi ya kuanzishwa kwa tawi la BoT Zanzibar kwani wakati huo kulikuwa na tawi moja  lililokuwa Dar es Salaam.

“Nakumbuka fedha za Zanzibar tulitumia katika ujenzi wa BoT, tawi la Zanzibar, ujenzi ambao ulikuwa na gharama kubwa ukihusisha kujengwa kwa eneo maalumu la  kuhifadhi fedha hizo,” anasema Mtei.

Anaongeza kuwa kabla ya hapo, Zanzibar ilikuwa haina tawi la Benki Kuu hivyo, fedha hizo ndizo zilitumika kuanzishwa tawi la kwanza.

“Ni kweli kulikuwa na malalamiko ya Zanzibar baada ya bodi  kuvunjika, lakini hatukuzitumia fedha hizi kwa mambo mengine, ila tulifungua tawi la Benki Kuu Zanzibar,” anasema.

Anaeleza kuwa anachokumbuka ni kuwa fedha za Zanzibar zilikuwa asilimia nne katika jumuiya hiyo na kwa jumla Tanzania ilikuwa na asilimia 35 katika bodi hiyo.

“Kuanzisha  BoT Zanzibar  haikuwa kazi ndogo kwani ilibidi tutafute majumba strong (imara). Tujenge mahali pa kuhifadhi fedha na ujenzi ni gharama hasa  strong room (chumba maalumu cha kuhifadhi fedha), ” anasema Mtei.

Anaongeza kuwa kwa kumbukumbu zangu, wakati huo, kwenye vikao vya uamuzi huo, Zanzibar ilikuwa inaongozwa na Katibu wa Wizara ya  Fedha aliyemtaja kwa jina moja la Sheha.

“Sheha ndiye aliyekuwa anahudhuria vikao, alikuwa akija na kukutana nami tunajadili,” anasema.
 Serikali moja  EAC

Akizungumzia mvutano wa kisiasa kwa sasa, kutokana na mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya, anasema ni vyema maoni ya wengi yafuatwe na kuheshimiwa.


Hata hivyo, anasema  baada ya  Muungano kudumu kwa miaka 50, angetaka ndoto iwe ni kuwa na nchi moja katika ukanda wa Afrika ya Mashariki.

“Mimi  kama mchumi nataka nchi kubwa moja. Tuache kuzungumzia mambo ya kutugawanya, inawezekana kuna nchi ndogondogo lakini lazima ziunganishwe na kuwa moja kubwa kupitia Shirikisho la Afrika ya Mashariki,” anasema.

“Nchi hii ni moja ambayo nadhani tuanze kuifikiria sasa iwe na Tanganyika, Zanzibar, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na hata  Zambia na  Malawi

“Mimi nimejifunza katika political science (sayansi ya siasa) kuwa nchi inapokuwa moja kubwa, basi uchumi wake unastawi na watu wanapata maendeleo ya kiuchumi kuliko kuwa nchi ndogo,” anasema.

Anaongeza, hata hivyo, kuwa ni vyema kujiuliza ni kwa nini miaka 50 ya Muungano sasa, bado Watanzania wengi ni maskini?

“Lazima, tufikirie mbele zaidi, kwenye vikao vya umoja wa mataifa, zinapozungumza nchi kubwa, utaona kabisa kila mjumbe anakuwa makini na hata kama yupo nje anarudi kusikiliza, lakini kama ni nchi ndogo wajumbe wanatoka kuvuta sigara nje ya ukumbi.”

 Anaongeza kuwa Watanzania na wakazi wa ukanda wa Afrika ya Mashariki wanapaswa kufikiria kuwa na nchi moja kubwa kama Marekani, Ujerumani  au Brazil kama kweli wanataka kukuza uchumi wao.

Muungano ni maridhiano.

Akizungumza muundo wa Muungano, Mtei  anasema ni muhimu kuwapo kwa Muungano ambao unaridhiwa na nchi zote wanachama.

Anasema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni lazima uendelezwe na kulindwa, lakini, kwa kuzingatia masilahi na maridhiano ya kila upande.

“Tuwapinge wote ambao wanataka kuvunja Muungano, pia tuondoe kero zote zilizopo kwani Muungano ni makubaliano ya watu wote kwa masilahi yao,” anasema.

Mtei ambaye ni muumini wa Kilutheri ana historia ndefu ya maisha ambayo yanafurahisha. Ni mtu ambaye alilelewa na mama yake mzazi na kukulia katika maisha ya umaskini, akichunga mbuzi baada ya kutoka shule ya Ngaruma iliyokuwa ikimilikiwa na Kanisa la Kiinjili la  Kilutheri Tanzania. Baadaye alikwenda  Old Moshi, Tabora, kisha Chuo Kikuu Makerere, Uganda.

CHANZO: MWANANCHI.