Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda Maiti Zanzibar. |
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kupiga kura ya hapana kwa Rasimu ya katiba inayopendekezwa kutokana na kutozingatia maslahi ya Zanzibar.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda maiti mjini Unguja.
Akivizungumzia baadhi ya vifungu Maalim Seif amesema katiba inayo pendekezwa imepunguza mamlaka zaidi ya Zanzibar tofauti na ilivyoelezwa na wanaounga mkono katiba hiyo.
Amesema kuwa katiba inayopendekezwa imetoa mamlaka zaidi kwa Serikali ya Muungano kwa kusema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja yenye mamlaka kamili hivyo kuinyang’anya Zanzibar mamlaka iliyo nayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar toleo la 2010.
Maalim Seif amesema kuwa Katiba ya Zanzibar inampa uwezo Rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika Mikoa na maeneo mengine ya kiutawala ambapo kwa sasa mamlaka hayo yamewekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha amesema kuwa rasimu hiyo bado haijatoa uhuru kwa Zanzibar kushirikiana na Mashirika na Jumuiya za kikanda pamoja na Kimataifa kutokana na mashirika hayo kutoa uwanachama kwa nchi zenye mamlaka kamili ya kiuongozi jambo ambalo kwa Zanzibar bado halijapatikana.
“Shirika kama la Chakula duniani, UNESCO na mashirika mengine hatoi uanachama kwa nchi ambazo hazina mamlaka ya kujiendesha wenyewe na kwa Katiba hii inaqyopendekezwa bado Zanzibar haijapata mamlaka kamili” alisema Maalim Seif.
Aidha amesema kuwa Rasimu iliyotolewa na Tume ya jaji Warioba ilipunguza idadi ya mambo ya Muungano kutoka 22 hadi kufikia saba badala yake Rasimu inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba imeyaongeza kutoka saba hadi 14.
Pia amesema kuwa Rasimu inayopendekezwa bado imeifanya Ta nganyika kuendelea kuvaa koti la Muungano kutokna na mambo yake yasiyokuwa ya Muungano kuendelea kusimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia amesema kuwa katiba inayo pendekezwa imekosa uhalali wa kisheria kutokana na kutopatikana kwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar waliyoinga mkono rasimu hiyo wakati wa upigaji wa kura.
Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba Yahya Khamis Hamad wajumbe waliopiga kura ya ndio hawakufikia theluthi mbili badala yake matokeo yaliyotangazwa yalikuwa na lengo la kuipitisha rasimu hiyo kinguvu kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi.
Aidha amesema kuwa endapo katiba inayopendekezwa itapitshwa itasababisha mgogoro wa kikatiba kutokana na na katiba hiyo kukinzana na katiba ya Zanzbar hivyo kulazimisha kufanyiwa marekebisho katiba ya Zanzibar jambo ambalo halitawezekana.
Amesema kuwa ili kuifanyia marekebisho katiba ya Zanzibar kutahitajika theluthi mbili ya Wajuumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunga mkono ambapo wajumbe watokanao na chama cha CUF hawatakubali jambo hilo kutokea.
Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Mh, Nassor Ahmed Mazrouy amewataka Wazanzibar kuikataa katiba inayo pendekezwa pamoja na kuwakataa Wabunge na Wawakilishi wote waliopiga kura ya ndio kwa katiba inayo pendekezwa.
Naye Mjumbe wa kamati ya maridhiano Mansour Yussuf Himid amesema kuwa ataendelea kuitetea Zanzibar ipate mamlaka yake kamili hivyo ataendelea kupingana na mfumo wa Muungano wa CCM uliojaa ukatili dhidi ya Wanzibari.
Alisema kuwa kwa mujibu wa vitabu vya dini mbali mbali vinaeleza kila nafsi itaonja mauti je wao wanaogopa nini kilichobakia ni kuingia mitaani kuwambia Wazanzibar wasikubali kuipitisha katiba hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Maridhiano Zanzibar,Mzee Nassor moyo alisema kuwa Wazanzibar waliungana na Tanganyika kwa hiari yao hivyo hakuna mtu yeyote wa kuwalazimisha kufanya mambo yanayokwenda kinyume na matakwa ya Wazanzibar.
Mapema mkurugenzi wa habari na uenezi wa CUF, Salim Abdallah Bimani alisema kuwa rasimu inayopendekezwa sio ya wazanzibar na haitofika Zanzibar bali itaishia Kisiwa cha Chumbe .
Na aliwataka wazanzibari kuungana pamoja na kuikataa kwa nguvu zote rasimu ya Chenge na wenzake kwani imekuja kuangamiza Zanzibar.